Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Judith Salvio Kapinga (9 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:-

Je, lini TANESCO watalipa fidia kwa wananchi wa Rorya waliopisha eneo la kupitisha umeme mkubwa toka mwaka 2011?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge ahsanteni sana na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa mbele, naomba nitumie dakika moja kwa ajili ya shukrani. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya rehema na baraka. Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyoiweka juu yangu na kuniteua niweze kumsaidia kama Naibu Waziri wa Nishati nikimsaidia Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Dotto Mashaka Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu. Napenda nimwahidi Mheshimiwa Rais imani hiyo aliyonijalia nitaitumikia kwa weledi na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, TANESCO tayari imekamilisha uthamini na uhakiki wa marudio ya mali zilizoathiriwa na mradi na kwa sasa ipo katika hatua za maandalizi ya malipo. Malipo hayo yanatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, tunawaomba wananchi wanaosubiri kulipwa fidia wawe na subira wakati maandalizi ya malipo yakiwa yanaendelea kufanyika.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini Vijiji vya Namikunda, Chipole, Machombe, Mtakateni, Machenje, Matawale, Mpekeso, Chakama na Kata ya Temeke vitapewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Masasi, Mkandarasi NAMIS Corporate Limited alipewa jumla ya vijiji 17 ambavyo havikuwa na umeme. Hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2023, vijiji 11 vimeshawashwa umeme na vijiji sita vitakamilika kabla ya mkataba wa Mkandarasi kwisha tarehe 31 Desemba, 2023. Aidha, vijiji vya Namikunda, Mtakateni, Matawale, Mpekeso na Chakama vimeshawashwa umeme. Vilevile, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2023, Vijiji vya Chipole na Machombe vitakuwa vimepatiwa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa zoezi la kusimamisha nguzo katika Kata ya Temeke bado linaendelea na nguzo tayari zimesimamishwa katika Kijiji cha Machenje na zoezi la kuvuta waya linatarajiwa kufanyika mwezi Septemba, 2023. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme wa uhakika katika Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa muda mfupi wa kujenga kituo kidogo cha umeme (Switching Station) kwenye eneo la Nyamirangano lililopo kwenye Halmashauri ya Ushetu. Kupitia kituo hicho kidogo, TANESCO itaongeza njia nyingine za umeme kutokea kwenye kituo hicho kwenda Ushetu, Msalala na Kahama ambazo zitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme. Mradi huu unategemewa kukamilika 2024 na unagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.2, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imechukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni pamoja na kufunga transformer yenye ukubwa na uwezo wa MVA 120 katika Kituo cha Msamvu. Kazi hiyo ambayo inagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 inatarajiwa kukamilika mwezi huu wa Novemba, 2023. Aidha, sambamba na hilo, TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya usambazaji wa umeme katika Manispaa ya Morogoro ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-

Je, lini Mkoa wa Rukwa utaunganishwa na Gridi ya Taifa ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Gridi ya Taifa, Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme Msongo wa Kilovolt 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma kwa Mradi wa TAZA, umbali wa kilomita 620. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, Wakandarasi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wameshapatikana na Wakandarasi wa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme wapo katika hatua za majadiliano. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2023 na kukamilika mwezi Desemba, 2025, ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme kwenye Kata za Kikeo, Kinda na MaskatI – Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mvomero ina jumla ya vijiji 129 ambapo kati ya hivyo, vijiji 92 tayari vimeshapatiwa umeme. Vijiji 37 vilivyosalia ambavyo baadhi vinapatikana katika Kata ya Kikeko, Kinda na Maskati vitapatiwa umeme na mkandarasi ambaye yupo maeneo ya mradi anaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu. Mkandarasi huyu anatarajia kukamilisha kazi ifikapo mwezi Juni, 2024, ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, wakandarasi wangapi kutoka Mkoa wa Kagera wamepata kazi katika mnyororo wa ujenzi wa Bomba la Mafuta la Hoima – Tanga?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi Wakuu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanga) wameendelea kushirikiana na Wakandarasi wadogo wajenzi pamoja na watoa huduma mbalimbali katika maeneo yote inayopitiwa na mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Kagera hadi sasa, jumla ya wakandarasi na watoa huduma 42 wamepatiwa kazi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa ujenzi wa mradi huu, zikiwemo uuzaji wa vifaa vya ujenzi, huduma za usafirishaji, ulinzi, usambazaji wa mafuta, huduma za umeme na hoteli, nashukuru.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inaielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati safi na vifaa sahihi vya kupikia. Kwa sasa Serikali inakamilisha kuandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha asilimi 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2033. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia, ahsante.