Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Judith Salvio Kapinga (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Rehema, kwa kutujalia wote kuweza kuwepo hapa siku ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo wangu…

NAIBU SPIKA: Samahani Mheshimiwa Mbunge kidogo. Waheshimiwa dakika ni tano na kengele itagongwa moja. Karibu Mheshimiwa Judith Kapinga.

MHE. JUDITH KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyotangulia kusema, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye Rehema kwa kutujalia kuwepo hapa siku ya leo. Kipekee na kwa dhati ya moyo wangu, napenda kumshukuru Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa maono makubwa aliyonayo kwa taifa letu la Tanzania. Namwombea afya zaidi, nguvu zaidi na hekima zaidi ili aweze kutuongoza katika utekelezaji wa maono haya kwa kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imeeleza nia ya dhati ya Serikali kuboresha mfumo wa elimu ili kuleta tija kwa wahitimu. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea katika sekta ya elimu, mfumo wetu wa elimu bado unalalamikiwa sana. Sababu kuu ni moja, bado haujaweza kumzalia matunda kijana wa Kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia taifa letu lina vijana wengi wenye talanta ambao iwapo mfumo wa elimu ungeboreshwa na kuzingatia teknolojia wangeweza kujiajiri, kuajiri vijana wengine lakini pia wangeweza kuchangia kikamilifu katika pato la taifa. Ndiyo maana leo napenda nijielekeze kuchangia ni kwa namna gani mfumo wa elimu unaweza kuboreshwa na kuzingatia teknolojia ili tuweze kufikia ajira milioni 8 ambazo tumeahidi katika Ilani yetu ya Chama Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tulipokaa hapa ukiangalia ulimwengu matajiri kumi wakubwa duniani saba kati yao wamepata utajiri aidha kwa njia ya mtandao (internet) ama kwa njia teknolojia bandia, sidhani kama ni Kiswahili sahihi ila wenzetu Wazungu wanasema artificial intelligence ama kupitia TEHAMA. Nikitoa mifano michache, ukimwangalia Jeff Bezos tajiri wa kwanza duniani amepata utajiri wake kupitia mtandao wa Amazon wa kununua na kuuza bidhaa anaingiza bilioni 127 kwa saa moja na ameajiri watu si chini ya laki moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia na matajiri wengine ambao ni wadogo, Mark Zuckerberg tajiri mdogo kuliko wote duniani ameajiri watu 52,000 anaingiza mamilioni ya shilingi kupitia mitandao ya jamii tunayoitumia hapa kama WhatsApp, Facebook na Instagram.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia matajiri wengine wadogo kabisa Larry Page, Sergey Brin wote wanaingiza mamilioni ya shilingi kwa saa moja na wameajiri siyo chini ya watu 135,000. Siwezi kuwaelezea wote lakini taswira hii inatuambia teknolojia ndiyo mwarobaini wa changamoto za ajira za vijana wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai kwa Serikali ya chama changu kuweza kuangalia upya mifumo yetu ya elimu ili kuboresha masomo ya sayansi. Ubunifu unaanzia kwenye kujua ABCs za computer. Lazima tuboreshe masomo yetu ya sayansi yazingatie mafunzo ya computer kuanzia elimu ya msingi kwa sababu huko ndiko ubunifu unakoanzia na siyo kusubiria kuwafundisha watoto vyuo vikuu wakati vichwa vyao tayari vimekomaa. Matajiri wote hawa walipata mafanikio kwa sababu mifumo ya elimu iliwaandaa, iliwakuza kiubunifu na iliwasaidia na ndiyo maana wengi wao walivyofika chuo kikuu waliweza kubuni program hizi ambazo zinatatua changamoto za dunia za teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia leo vijana wetu wanaomaliza form four na form six mfumo wa elimu umewasaidia vipi? Mfumo wa elimu unapaswa kumsaidia kijana kwa ujuzi wa kujitegemea kwa ngazi yoyote anayoishia. Kinachosikitisha zaidi vijana wetu wa chuo Kikuu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUDITH KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, napenda kuipongeza Serikali kwa commitment kubwa inayofanya katika sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kuzungumzia namna tunaweza tukaboresha mifumo ya kutumia huduma za fedha kwa njia za kimtandao. Kama tunavyofahamu, kutokana na changamoto kubwa ya ajira vijana wengi wamejielekeza katika kufanya ujasiriamali wa kimtandao ambao kwa kiasi kikubwa unatumia huduma za fedha za kimtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za fedha za kimtandao zimewekwa pamoja na sababu nyingine, ili ziweze kumrahisishia huduma mfanyabiashara. Nafahamu hizi huduma za kifedha za kimtandao zinahusisha tozo ambazo zina kodi ambayo ni muhimu sana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali. Pamoja na dhamira hizo ambazo ni njema sana tozo kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha kwa mitandao ni kubwa mno na hivyo inasababisha vijana wengi wasiweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Leo hii ukiwa unatuma pesa shilingi 5,000/= tu kwa mtandao wa simu gharama yake ni shilingi 750/=, unaweza ukaona ni ndogo lakini ni 15% ya pesa ya mtu. Anayetoa shilingi 50,000/= anakatwa shilingi 2,700/= ni 5.4%; anayetoa shilingi 200,000/= anakatwa shilingi 3,700/= ni 1.9%. Kwanza unaona yule ambaye ni maskini kabisa wa chini ametoa shilingi 5,000/= anakatwa 15% ya pesa yake, yule ambaye anatoa shilingi 300,000/= anakatwa 1.9% ya pesa yake. Sasa hawa vijana ambao wanaanza biashara wataweza vipi kupambana katika soko hili la kimitandao? Hawana ajira, wanaamua kujiajiri kwenye mitandao na gharama zinakuwa kubwa kiasi hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiamua kwa mfano leo unaamua kutuma ada kutoka Tigo Pesa kwenda NMB gharama yake kwa Sh.140,000/= unakatwa Sh.6,000/=. Kama una watoto watatu gharama yake ni Sh.18,000/=, kwa uchumi upi wa Mtanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ni kubwa mno, kijana anafanya kazi kwenye mtandao ili apate faida ya shilingi 10,000/= na shilingi 20,000/= lakini yote inaliwa kwenye tozo za huduma za fedha za kimtandao. Naomba Serikali iangalie upya hizi tozo ili ziweze kuleta unafuu kwa vijana ambao wanapambana kwenye mitandao ili kuweza kupata kula yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye huduma za internet, natambua tafiti zinaonesha Tanzania ndiyo ina tozo ndogo kabisa kwenye data, katika ukanda wote wa East Africa, lakini tatizo lipo kwenye upandishaji holela wa huduma za data (internet). Wiki moja iliyopita ukitoa shilingi 8,000/= kwa Tigo ulikuwa unapata GB 16, yaani kesho asubuhi watu wameamka wameweka 8,000/= wanunue GB 16 wanapewa GB tatu, hawajapewa taarifa kwamba huduma gharama yake zinaongezeka. Halafu sasa MB 300 unapata kwa Sh.1,000/= yaani kwa mfanyabiashara uki-post post mbili, hela imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 3,000/= unapata GB moja wakati shilingi 3,000/= ulikuwa unapata mpaka GB 5. Watanzania hawakupewa taarifa ya upandishaji wa gharama hizi yaani kampuni ya mawasiliano anaamka anaamua kupandisha gharama za mitandao kama anavyopenda. Pato la mtu mmoja-mmoja ni shilingi elfu moja na kitu, lakini unamfanya Mtanzania atumie gharama ya shilingi 3,000/= kwa siku kwenye huduma ya mawasiliano, sio sahihi. Naomba Serikali iangalie upya ili inusuri vijana hawa ambao wanatumia mitandao ya kijamii kujipatia kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la pili kutoka mwisho, sisi tunapolipa huduma, tunaweza kulipa huduma kupitia Master Card Visa pamoja na PayPal kulipia malipo nje ya nchi. Leo mimi kijana wa Kitanzania nikiamua kufungua website kutaka kutangaza bidhaa watu wa nje ya nchi waweze kununua kwenye website yangu hawawezi kulipa kupitia Master Card, PayPal, Visa au Credit Card hela iingie moja kwa moja kwenye benki yangu, lakini mimi nina uwezo wa kuwalipa wale wa nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vijana tunawahimiza ubunifu, lakini ubunifu wao hauwezi kuwasaidia kwa sababu watu wa nje hawawezikuwalipa kwenye akaunti zao za benki. Naomba BoT na Wizara ya Fedha iangalie suala hili kumnusuru kijana huyu wa Kitanzania na kumwekea mazingira mazuri ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia na mimi ningependa nijielekeze katika mambo mawili. Tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha ukuaji wa uchumi, na tunapohusisha ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa tunaongelea mambo ya msingi sita; yaani uendelevu, uzalishaji, uwekezaji, mashirikiano, usalama pamoja na usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kwenye usawa ndipo ambapo ningependa nijielekeze kwasababu ni suala ambalo linahusisha haki na utu wa watu. Na tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha utu na haki za watu. Yaani lengo kuu la maendeleo ya watu ni uhuru na haki za watu; huwezi kutofautisha hayo masuala mawili.

Mheshimiwa Spika, nazungumza haya kwasababu uhuru na haki ya mtu unahusisha uhuru wa kipato. Tunapojadili mpango huu ni muhimu sana kuweza kuweka baadhi ya mambo sawa, ambayo yanashika uhuru wa kipato cha mtu; na uhuru wa kipato cha mtu mara nyingi unalindwa na Sheria na taratibu za nchi.

Mheshimiwa Spika, ningependa nijielekeze hapa kwasababu zipo Sheria ambazo zinakandamiza uhuru wa kipato cha mtu, inawezekana kukawa na changamoto, na hapa ningependa nijihusishe specifical katika Sheria ya Uhujumu Uchumi, nafahamu imeongelewa sana lakini ningependa niweke mkazo hapa. Kwa ambao hawafahamu Sheria hii ya Uhujumu Uchumi na Utakatishaji Fedha ilikuja baada ya tukio la Septemba 11; pale ndipo ambapo Sheria hii ilisisitizwe iweze kuletwa katika mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla, ndipo na hapo sisi tukapata sheria hii. Lakini tulipokosea nchi nyingi za Afrika pamoja na Tanzania tulipata mapokeo ya sheria hii bila ya kuangalia mazingira yetu ya ndani.

Mheshimiwa Spika, na vile vile tulipopata sheria hii hatari zaidi hatukuwa na uzoefu na kujadili ama kuendesha mashtaka haya, na hivyo tukajikuta tunapokonya haki za watu za dhamana, lakini vile vile tukapoka mali za watu kwa kudhania, kwamba sheria inaruhusu ilhali kimsingi ilikuwa labda ni tafsiri mbaya ya sheria ama sheria hazikukaa sawa ama matumizi mabaya tu ya nafasi pamoja na madaraka ya watu waliodhaminiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu makosa mengi katika sheria zetu za Tanzania yana dhamana; ukiangalia wizi, ukwepaji wa kodi ni makosa ambayo yana dhamana lakini ilivyokuja sheria hii dhamana ikanyimwa. Hata hivyo, watafsiri wetu wa sheria wametufelisha sehemu moja, makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha ni matokeo ya makosa ya msingi yaani leo hii umeiba ama unatuhumiwa kwa ukwepaji kodi, mpaka ukwepaji kodi uwe- establish ndipo pale utaweza kujua, je, ukwepaji kodi ulisababisha utakatishaji wa fedha? Ndipo hapo unamhukumu mtu kwa kosa la kuhujumu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu makosa haya ya utakatishaji wa fedha ni vigumu sana kuya-prove wenzetu wa DPP wakaamua warahisishe Maisha. Moja, kwa sababu ni ngumu sana ku-prove sasa wanaamua pale kwenye kosa lako la msingi ambalo lina dhamana akuwekee na money laundering ili likose dhamana. Pili, kwa sababu halina dhamana utawekwa rumande sasa pale ndiyo wanakuja na negotiations (pre-bargaining) anakwambaia sasa hapa kuna shitaka hili na kwa sababu mashtaka haya yana sifa ya kukukalisha rumande miaka na miaka, mtu uko frustrated unawaza biashara zako, unawaza familia yako, unamuwaza mke au mume wako utakosa ku-negotiate ili uweze kutoka? Uta-negotiate tu na hapo ndipo ambapo watu wanapokwa mali zao kwa taratibu ambazo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema utaratibu huu ni unyang’anyi tu wa bila silaha, tunapokonya watu kwa taratibu ambazo zingeweza kutafsiriwa ili ziweze kurahisisha watu wetu walinde kipato chao na utu wao. Kwa hiyo, haya masuala ya hii sheria, naomba sana Serikali yangu sikivu iangalie upya na inawezekana sheria haina matatizo ila tafsiri ya sheria kwa watendaji wetu iangalie mazingira ambayo tutalinda utu na kipato cha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo napenda nijielekeze nalo ni kuhusiana na masuala la mawasiliano na teknolojia. Inawezekana nikaonekana kama mlalamikaji lakini napenda nisisitize hapa. Kwanza napenda niishukuru Serikali yangu Sikivu, tulipozungumza masuala ya mabando ilisikia ikatoa maelekezo na tunashukuru sana. Hata hivyo, bado naomba Serikali iangalie masuala ya mabando ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi. Vijana wengi wanatumia huduma hizi, toka mwezi wa kwanza tunalalamika huu ni mwezi wa nne masuala haya hayajafanyiwa kazi, tunapewa tu matamko lakini vijana wengi zaidi ya milioni 23 wanatumia mitandao ya simu kwa ajili ya shughuli zao, tunaomba tuangaliwe. Unapewa MB 300 kwa Sh.2000 unafanya biashara, vijana huku ndipo tulipokimbilia kwa sababu mfumo wa elimu haujaweza kutusaidia. Sasa kwa mantiki kama hizi tunasaidiwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TCRA imetoa tamko kwamba ikifika Mei Moja vijana zaidi ya 90,000 wanaosajili line wawe wana vibanda, leseni na TIN namba. Anasajili line kwa Sh.1000 na anapata wateja kwa kusambaa huku mtaani leo hii unamwambia awe na kibanda wateja atapata wapi? Airtel inawalipa vijana hao zaidi ya shilingi milioni 700 ikilipa kima cha chini lakini inalipa mpaka shilingi bilioni 1 kwa vijana 30,000 lakini wanaenda kukosa kazi hawa. Naomba Serikali yangu iangalie mambo kama haya ili vijana wa Taifa hili wasiwe frustrated na mazingira ya kibiashara. Naomba Serikali yangu ituangalie sisi vijana ambao tunalipenda Taifa letu na tunafanya kazi kwa juhudi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunivumilia na kunipa dakika za ziada. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa sasa hivi Tanzania na dunia nzima tumesimama katikati ya mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamebadilisha yataendelea kubadilisha namna tunavyoishi, namna tunavyofanya kazi na namna tunavyoshirikiana na watu wengine. Huko tunakoelekea, kwa namna ambavyo mabadiliko ya teknolojia yanatokea, haina shaka kwamba kwa ujumla maisha yetu yatabadilika kwa kasi ambayo tusiyoitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunakumbuka, tukiangalia hapa tulipo na tulipotoka, mapinduzi ya kwanza ya viwanda namna ambavyo yalikuwa yanaendeshwa, yalikuwa yanatumia njia ya maji pamoja na mvuke, yaani water na steam power. Mapinduzi ya pili yali-advance kidogo yakawa yanatumia electronic power; mapinduzi ya tatu yakaenda yakawa yanatumia electronics and information technology. Hapa tulipo sasa hivi yame-advance kiasi cha kwamba tunatumia mchanganyiko wa nguvu kazi yaani za mikono, kidijitali na mbinu za kibaiolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya ili niweze kueleweka kwamba hapa tulipo tuko katika nyakati ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya dunia na mabadiliko yanayoenda sasa hivi kwa kasi ambayo yanatokea haijawahi kuwa recorded toka dunia imeanzishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema pia ili tuone umuhimu wa kuwekeza katika masuala ya teknolojia, sayansi pamoja na uvumbuzi, lakini hatutaweza kufanikiwa kwa sababu masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia, uvumbuzi, mawasiliano na habari hayajawekwa pamoja katika nchi yetu, yaani yameparanganyika. Yapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini masuala ya information na communication na ICT yako kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu kama tunavyofahamu ni dubwana kubwa namna hii, masuala ya sayansi na teknolojia, hayawezi kuendelezwa pale kwa kasi ambayo sisi tunaitaka na ndiyo maana leo hii nataka nishauri Serikali yangu sikivu. Wakati umefika sasa tu-centralize masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia, uvumbuzi, habari na mawasiliano kwenye sehemu moja. Sehemu sahihi ni Wizara hii ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba kwa nini tu-centralize leo? Ni kwa sababu tunapaswa kujisuka upya ili tuweze kwenda na kasi ambayo dunia inaenda. Lazima tukae kwenye mstari ambao the rest of the world wapo. Leo hii tulipokaa hapa nchi 24 duniani zimeshaweka makubaliano ya kumaliza matumizi ya mafuta ya petroli kuanzia mwaka 2025, ina maana watakuwa wanatumia magari ya umeme ama magari ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tulitakiwa tuwe tuna mkakati wa kutuwezesha sisi kuungana na dunia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwekeza kwa wataalam ambao wanaweza kubadilisha mifumo yetu ya magari kwenda kwenye mifumo ya magari aina ya umeme na gesi. Haya yote hayawezekani kwa sababu mambo yote haya yamekuwa decentralized. Hakuna sehemu moja ambapo tunaweza tukajisuka kama nchi na kwenda katika kasi ambayo dunia yote inaenda leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni rai yangu kwa Serikali ya chama change, ni wakati umefika tu-centralize sayansi, teknolojia, uvumbuzi, mawasiliano na habari kwenda kwenye Wizara hii ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kasi ambayo sisi tungeitamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia kwa mfano leo, kuna nchi kadha wa kadha zinanufaika na startup program za vijana kwa sababu wamejisuka na system yote imekuwa centralized. Leo South Africa wanaingiza takribani 1.3 trillion kwa startup program 10 tu za vijana. Imagine pesa ambayo Serikali yao inapata kama wana startup programs 100. Kenya tu hapo wamewekeza kwenye startup programs na wanapata zaidi ya USD milioni karibia 300 kwa program 10 tu. Sisi tunaweza kufanya haya; startup programs chini ya COSTECH hazijipambanui zaidi kiuchumi kwa sababu hazijaweza kusukwa ipasavyo kwa mifumo ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema vijana wa Taifa hili watapata ajira zile milioni nane kwa urahisi kama tukiwekeza kwenye masuala ya teknolojia na hizi startup programs. Kwa sababu startup programs 10 tu zina uwezo wa kuajiri mpaka vijana 1,000. Sasa imagine una startup program 100. Ndio maana naendelea kusisitiza, ni wakati umefika kujisuka upya masuala yote yanayohusiana na sayansi, teknolojia na uvumbuzi yawe centralized hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya ICT iko chini ya Wizara ya Mawasiliano lakini Sera ya Sayansi na Teknolojia, tena ya siku nyingi, iko Wizara ya Elimu. Sera ya Uvumbuzi mpaka leo mwaka 2021 hatuna Sera ya Innovation kwenye Taifa letu. Ndiyo maana nazungumzia habari ya ku-centralize masuala haya ili yaweze kufanyiwa kazi katika sehemu moja na tuweze kupiga kasi. Trust me not, ikifika 2025 hapa tutatafutana kwa sababu dunia inaenda kwenye kasi ambayo haijawa recorded sehemu yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye masuala yanayohusiana na ma-bundle. Kumekuwa kuna malalamiko kwa walaji wengi kwamba ma-bundle wanayotumia yanaenda kwa kasi mno. Inawezekana ikawa ni matumizi, lakini kuna tatizo sehemu. Wizara ilielekeza haya makampuni ya simu yaweze kuweka mita zinazoonyesha utumiaji wa ma-bundle, lakini tatizo linakuja kwenye speed ya ma-bundle ambayo tunauziwa. Hizi zinaitwa MPDS hazijawekwa wazi. Kuna makampuni wanatutoa speed ya 3 - 5 MPDS, lakini sasa ma-bundle tunayouziwa, leo Vodacom akinipa mimi bundle la 2GB na Tigo akinipa bundle la 2GB inawezekana la Vodacom likaisha kabla ya Tigo kwa sababu haijawekwa kwamba bundle la 2GB ambalo ninapewa inabidi liwe la speed gani, MPDS ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana watumiaji wa mtandao mmoja wanalalamika kuliko watumiaji wa mtandao mwingine, kwa sababu hatuna hata kipimo na hatuwezi ku- trap matumizi ya mitandao yetu. Ndiyo maana leo unaweza ukanunua 2GB ikaisha. Ni haki kwa Mtanzania kulalamika kwamba bundle langu linaisha kama upepo, kwa sababu hatuambiwi speed ya ma-bundle tunayotumia ni MPDS ngapi; na ni vigezo gani vinatumika? Kwa hiyo, labda ifike kipindi tuuziwe ma-bundle kwa mantiki ya speed basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunaambiwa Watanzania ni nchi ya nne kwa ma-bundle rahisi Afrika; lakini sasa kama bundle langu nanunua kwa bei rahisi napewa GB1 sawa, baada ya saa moja, nanunua tena GB1, hiyo ni rahisi in terms of quantity or in terms of speed? Kwa hiyo, ifike mahali sasa Wizara ituangalie hapa; kuna jambo hapa kwenye masuala ya ma-bundle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wangu wa pili naomba nizungumzie kuhusu masuala ya matumizi ya internet. Naipongeza Serikali, watumiaji wa internet wameongezeka mpaka kufikia milioni 29, lakini nachelea kusema kwamba watumiaji hawa kwa kiasi kikubwa ni watumiaji wa mijini. Sisi kule kwetu Mbinga Kata 29 na vijiji 117 hatuna internet. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani vijiji vyote 117 tunahangaika, mpaka tufike mjini ndiyo tuweze hata kutuma document ama kufungua document kwenye simu. Naomba Waziri wakati anakuja hapa, atueleze sisi wananchi wa Mbinga Vijijini ni lini tutatatuliwa matatizo yetu ya internet? Leo hii kata zote 29 na vijiji 117, jamani naomba Waziri atuambie sisi wananchi wa Mbinga Vijijini tutafanyaje? Maana sasa tunakosa cha kufanya. Tunaomba tuangaliwe tupate na sisi 3G kwa sababu vijana wengi wako kule vijijini, siyo kwamba vijijini hamna vijana ambao wamesoma. Wanataka kuuza kahawa zao kwenye mitandao, wanataka kuuza unga wao kwenye mitandao, tuletewe na sisi kule ili tusije kufanya kazi mjini tukae kule kule kwetu tuuze biashara zetu kule kule tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunafahamu kwamba mawasiliano ya simu ndiyo maisha siku hizi, lakini kata saba hata kupiga simu huwezi. Kata hizo, naomba niweke kwa record; Kitura, Kipololo, Ngima, Mhongozi, Ukata, Amanimakoro, Kihangimauka; na hapa Mheshimiwa Waziri
nataka nikupe taarifa nitashika shilingi, naomba utuambie ni lini kata hizi zitapata mawasiliano ya simu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu vijana katika Taifa lolote duniani ndiyo wadhamini wa Maendeleo wa Taifa hilo yaani they are the trustees of prosperity in the nation. Lakini vilevile vijana katika Taifa lolote ni zawadi kwa Taifa hilo na ndiyo maana kuna msemo unaosema wazee watatangaza vita, lakini ni vijana watakaoenda mbele kupigana au kufariki yaani all the men declare war, but it is the youth must fight and die. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nusu ya watu wote duniani yaani asilimia 50.5 ni vijana chini ya miaka 30; nasema haya kwa sababu Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siyo Rais wa wastani hata kidogo, she is not an average president anafahamu na anatambua vijana wa Taifa hili ndiyo waliobeba mustakabali wa Taifa hili kwa namna moja ama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatambua makali yetu ya Taifa ya kesho yatazimwa na vijana wa Taifa hili na ndiyo maana juzi katika mkutano wake wa vijana aliahidi mkeka utakaokuja utasheheni na kupambwa na vijana wa Taifa hili. Ila sasa hapa tunamuomba Mheshimiwa Rais aharakishe kwa sababu wananchi mtaani wanalalamika kwamba nazi zimepanda bei (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema maneno haya kwa sababu Rais anafahamu nguvu ya vijana na ndiyo maana tarehe 15 alituita pale Mwanza kuongea na sisi na kutupa moyo na kutupa muelekeo wa Taifa hili. Ndiyo maana nasema kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan she is not an average president at all, anatambua kwamba vijana ndiyo walioikamata dunia hii, kwa hiyo, kwa mantiki hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mkutano ule, tunasema kwamba sisi kama vijana ametuthamini kweli kweli, sisi kama vijana ametupenda kweli kweli na sisi kama vijana ametujali kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama vijana tunamuahidi kufanya kazi kwa kuwa ametupa ari ya kufanya kazi, ametupa nguvu, lakini vilevile ametupa hamasa ya kuendelea kum-support kwa kila jambo atakalolifanya kwa sababu mambo anayotufanyia sisi vijana wa Taifa hili ni ya mfano na tunatiwa moyo kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba kwa bajeti hii ya Serikali ambayo ipo mbele yetu Rais wetu Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi kweli kweli na ninataka niseme hapa kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaenda na trend za dunia inavyoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani kwa lugha moja ama nyingine anaongea lugha moja na ulimwengu wote kwa ujumla na ningependa niwape mfano mmoja; wakati sasa hivi dunia inaenda kwenye deployment ya mtandao wa 5G ambao unaenda kuongeza global economic value ya USD trilioni 13.1 lakini inaenda kuongeza ajira takribani milioni 22.1. Juzi Mkurugenzi wa TCRA alifanya mkutano akatuambia Tanzania kwa mara ya kwanza tunaenda kwenye majaribio ya 5G; mtandao ambao kama leo ulikuwa una-download movie yako ya 20GB kwa zaidi ya lisaa limoja unaenda kui- download kwa sekunde moja mambo ambayo sisi kama Taifa tulikuwa hatufikirii kama tutafika huko, lakini Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan anatuonesha mfano wa namna ambavyo tunapaswa kuongea lugha moja na ulimwengu wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naongea haya Mheshimiwa Rais pia alijiuliza itawezekana vipi tukafikia malengo haya makubwa ya kimtandao kama Watanzania wengi kwa kiwango kikubwa hawana smartphone. Kodi ambayo imefutwa ya VAT labda kwa ambao hawafahamu ukileta simu hapa nchini kulikuwa kuna kodi tatu ambazo simu ilikuwa inatozwa; ya kwanza - custom processing fee; ya pili - railway development fee na ya tatu - VAT ambapo custom processing fee ilikuwa ni 0.6 percent, railway development fee ilikuwa ni 1.5 percent na VAT ilikuwa 18 percent. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani leo ukiingiza mzigo wako wa milioni 10 kodi ambayo ulikuwa unalipia ni asimilia 20.1, kodi ambayo imeondolewa ni asilimia 18 kwa hiyo, kodi ambayo imebaki kwenye simu ni asilimia 2.1 yaani labda niongee kwa lugha rahisi, ukiwa una mzigo wa milioni 10 kodi yako ilikuwa ni 2,010,000 yaani asilimia 20.1, lakini leo hii una mzigo wa milioni 10 kodi ambayo unachajiwa badala ya milioni 2,100,000 ni shilingi 210,000 ni zaidi ya asilimia 97 ya kodi katika hizi simu ambazo zinaingizwa yaani simu janja, vishikwambi na modem imeondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema kufikia asilimia 80 ya watanzania wanaotumia mitandao ifikapo 2025 siyo ndoto ni suala ambalo linatekelezeka na litatekelezeka kabla ya 2025 na sisi kama vijana wa Taifa hili tunamshukuru Mheshimiwa Samia kwa sababu hapa ndipo ambapo tumejiajiri kwa kiasi kikubwa sana. Kwa kweli ndiyo maana naendelea kusema bajeti hii Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tunashukuru kwa haya yote tungependa tuishauri Serikali masuala machache ambayo inabidi ifanyie kazi; moja, tunaomba Serikali ifuatilie masuala ya fedha za mtandao za simu kwa watu ambao wanafariki, yaani Tigo Pesa, M-Pesa, Halotel Money, Zantel Pesa zote hizo naona kwamba utaratibu haujakaa vizuri na tunaona kwamba kuna fedha zinapotea za watu waliofariki kwenye mitandao ya simu ambazo haziwi claimed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliopo sasa hivi tunatambua sheria inasema kwamba, ili uweze ku-claim fedha either katika mitandao ya simu au benki kuna utaratibu wa kufuata ule wa wasimamizi wa mirathi, lakini kwa dunia tunavyoenda sasa hivi tunaona huu utaratibu upo very complex kwa sababu ili uweze ku-claim hela za ndugu zako; kwanza huwezi kuambiwa salio mpaka uende na barua ya kuthibitishwa kama msimamizi wa mirathi na uende na viambatisho vingine ambavyo pamoja na hivyo. Lakini utaratibu huu wa kimahakama unachukua zaidi ya miezi mitatu au sita na sheria inasema kwenye mitandao ya simu line inafungwa baada ya miezi mitatu baada ya hapo hela inawekwa kwenye holding fee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi dunia inapoenda kwa nchi za wenzetu kama Uganda kuna mitandao ya simu ambayo mtu akienda next of kin wake yaani mnufaika wake pamoja na uthibitisho wa marehemu kwamba amefariki na cheti cha kufariki anapatiwa hizi fedha. Tunaomba kwenye suala hili utaratibu uimarishwe ili kuweza kuwalinda walaji, lakini vilevile kuhakikisha fedha hizi hazipotei na wanufaika wa makampuni ya simu hawanufaiki wao peke yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu pia hata line ikifungwa ndani ya miezi mitatu kuna fedha zinabaki kule, lakini hakuna utaratibu wa ku-claim fedha hizi kwa walaji ama kwa Serikali. Kwa hiyo, tunaomba suala hili fedha za watu wanaofariki kwa sababu siyo wote ambao wana-claim iangaliwe kwa namna moja ama nyingine ili hata Serikali iweze kuongeza fedha hapo ili makampuni ya simu wasinufaike wao peke yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Mheshimiwa Waziri alisema itakuja sheria ya Data Privacy and Protection Act, lakini tunaona suala hili ni la muhimu sana kuna fedha nyingi sana zinapotea hapa za waliofariki, tunaomba Serikali ifuatilie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa nishauri kuhusiana na charge za kwenye mitandao ya simu. Sasa hivi ukiwa unatoka kwenye simu unataka kuchukua hela benki yaani unatumia zile USSD code…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani naomba nimalizie kwa dakika moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano NMB *150*66# makampuni mengine yote ya simu una-dial nyota hiyo, yaani charge yako inaenda benki yaani uhitaji kuwa na salio ili uweze ku-access benki yako, lakini kwa Vodacom huwezi ku-access mpaka uweke salio la kawaida hata kama ukiwa na bundle hata kama ukiwa na bundle haikubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itusaidie Vodacom wabadilishe utaratibu huu ili sisi tuweze ku-access benki zetu na kama kuna ma-charge waende kwenye benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa asilimia 100 bajeti hii na ninakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Aliyekuwa Rais wa South Afrika Hayati Nelson Mandela, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, aliwahi kusema na nitamnukuu: “From the poorest of countries to the richest of nations, education is the key to moving forward in any society”. Kwa lugha yetu ya Taifa anasema kuanzia kwenye nchi masikini kabisa hadi mataifa tajiri kabisa elimu ndiyo ufunguo pekee wa maendeleo katika jamii yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maneno haya kwa namna moja ama nyingine yalielezwa na Rais wetu mpendwa na anayewapenda Watanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tarehe 6 Aprili, wakati wa hafla ya kuwaapisha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu na alisema napenda nimnukuu: “Lazima kufanya tathmini ya elimu itakayomsaidia Mtanzania. Tuangalie mitaala yetu tuone mtaala utakaotupeleka mbele na kukuza Taifa letu”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maneno haya ya Rais wetu mpendwa kwa namna moja ama nyingine yanatuonyesha umuhimu wa mfumo wa elimu katika kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa letu. Mfumo wa elimu kwa namna moja ama nyingine ndiyo unaoamua nguvu kazi ya taifa letu itasukuma vipi gurudumu la uchumi katika nchi yetu. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua ajira za wananchi wa Tanzania zitapatikana vipi na kwa kiasi gani. Mfumo wa elimu ndiyo unaoamua umaskini katika taifa letu utaondolewa ama utapungua kwa kiasi gani na kwa wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu mengi yameongelewa kuhusiana na kubadilisha mfumo wa elimu lakini mimi napenda kujikita katika namna ya kulinda mfumo wa elimu. Hata kama tutafanya mabadiliko ya mfumo wa elimu tusipolinda mfumo wa elimu ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kueleza namna gani tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, hapa ningependa nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako; kwa kipindi hiki ambacho amekua Waziri tumeona mabadiliko yasiyo na tija na ya haraka katika mfumo wa elimu, kidogo yameweza kuwa contained. Huko nyuma mabadiliko katika mfumo wa elimu yalikuwa yanaweza yakafanyika abruptly, muda wowote na ku-disturb walaji ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana wa Taifa hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa kipindi hiki ambacho amekuwa Waziri, amejitahidi sana kuwalinda walaji ambao ni vijana wa Tanzania. Hongera sana mama yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nijielekeze ni kwanini tunapaswa kulinda mfumo wa elimu, kwa sababu mabadiliko yoyote katika Mfumo wa Elimu yanaweza kuathiri vijana wa Taifa hili kwa kiasi kikubwa sana. Tunashukuru Mungu leo tuna Mheshimiwa Prof. Ndalichako, kesho hatutakuwa naye. Kwa mantiki hiyo, inatupasa kulinda mfumo wa elimu kwa kuweka taratibu ambazo zitalinda misingi ya mfumo wa elimu. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, hapa napenda kutoa mifano michache ili muweze kunielewa. Mwaka 1997 aliamka mtu akafuta UMITASHUMTA, lakini tunashukuru Serikali ilirudisha UMITASHUMTA mashuleni na sasa hivi inafanyika katika utaratibu mzuri tu. Hii ilikuwa hatari sana kwa sababu wote tunajua michezo namna ilivyo multibillion industry duniani.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa pili. Kuna kipindi pia kuna mtu aliamka akaamua akataka kuunganisha Chemistry na Physical; yaani kipindi kile somo hili lilitakiwa liitwe Physics with Chemistry. Tunashukuru mambo haya hayakuweza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa tatu, mwaka 2014, Kidato cha Nne waliwekewa alama zao za ufaulu kwa kutumia wastani wa point ama kwa lugha nyingine GPA. Vijana waliomaliza 2014 na 2015 waliwekewa kwa mfumo huu na sababu zilizotolewa kipindi kile, ni ili tuwe na system inayofanana. Mwaka 2016 tukarudisha mfumo ambao tumeuzoea wa division. Kwa hiyo, tuna wanafunzi katika nchi hii ambao kuna kipindi waliwekewa marks zao kwa mfumo wa GPA, baadaye ikabadilishwa ikarudisha division. Nasema haya ili mnielewe ni kwa nini inatupasa kulinda mfumo wetu wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, Serikali iliwahi kugharamika kupeleka walimu nje waweze kujifunza programme za re-entry, kuwasaidia watoto wa kike wanaopata ujauzito waweze kuwa accommodated tena katika mfumo wa elimu. Zoezi hili lilikuwa frustrated kwa sababu lilikuwa halilindwi. Baadaye ikaonekana halina mantiki, likawekwa kwenye kapu, lakini tayari tuligharimika kuwasomesha walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine, ilitokea programme ya voda fasta ya walimu kusomeshwa miezi mitatu. Walimu walisomeshwa na wakapelekwa kufundisha watoto wetu na kuambiwa kwamba wana-qualify. Miezi hii, mitatu! Naeleza haya ili kuonesha ni kwa nini tulinde mfumo wetu wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii mtoto wa miaka mitatu yuko boarding school. Mtoto wa miaka mitatu mama yake au baba yake amempeleka boarding school. Naeleza haya ili tuweze kuona hatari hizi na kuona umuhimu wa kulinda mfumo wetu wa elimu.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningependa sasa nilieleze hapa, leo hii kuna vijana katika nchi hii walisoma miaka mitatu chuo, walivyomaliza wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. Inawezekana sisi tukawa tumesahau, lakini wale vijana hawajasahau, wamelibeba hili kwenye mabega yao na kwa machozi zaidi ya miaka saba sasa wanatembea nalo bila kupata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mnakumbuka, Chuo kilikuwa kinaitwa Chuo cha Kilimo Mbeya (Mbeya Polytechnic College) kati ya mwaka 2013 mpaka 2016. Chuo hiki kilipewa usajili na NACTE, vijana walisajiliwa na kudahiliwa na walisoma pale miaka mitatu. Baada ya kusoma miaka mitatu, vijana hawa wakaambiwa vyeti vyao havitambuliki. NACTE wakasema Chuo chenu kilikuwa hakilipi ada za usajili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Jidith, muda hauko upande wako.

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini. Kwa nini Mkoa wa Ruvuma unaongoza ni kwa sababu tuliwaambia Wanaruvuma nendeni mkalime muongeze chakula katika nchi hii na walitumia jembe la mkono na mbinu duni za kilimo na mpaka mwaka jana wakaongeza tani 50,628 za mahindi kwa ajili ya akiba ya chakula cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tuliwaambia Wanaruvuma nyie ni kati kati ya mikoa mnayozalisha mazao ya chakula kwa wingi katika nchi hii. Mwaka jana waliongeza ziada ya chakula tani 877,048 kwa kuwa mahitaji ya chakula ya kimkoa yalikuwa tani 469,172 na wao Wanaruvuma kwa mikono yao walizalisha tani 1,346,220.

Mheshimiwa Spika, leo hii baada ya kuwapetipeti sana wazalishe mazao ya chakula kwa ajili ya akiba ya nchi hii, tumewasahau. Tumesahau jasho walilolitoa kwa dhati ya mioyo yao kulima, tumesahau nguvu waliotumia kwa mikono yao kulima na leo hii wanalala na mahindi yao ndani, wanahangaika na mahindi yao ndani, wanalia na mahindi yao ndani. Kwa takribani miaka mitatu hakuna soko la mahindi Wilayani Mbinga na Mkoani Ruvuma kwa ujumla huku tukijua Mkoa wa Ruvuma ndiyo unaozalisha kwa kiasi kikubwa mahindi na chakula cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa uchungu sana kwa sababu wana Ruvuma wamekuwa disparate. Mwaka jana akatokea tajiri tapeli anayejulikana kwa jina la Njako akaenda pale Mbinga Kigonsera akachukua mahindi ya wakulima yenye thamani ya shilingi bilioni 5 na mpaka leo hii tunapozungumza tunaenda kwenye mzunguko mwingine wa kuuza mazao mpaka leo wakulima hawajapata fedha. Vilevile mpaka leo hawana soko ambalo wataenda kuuza mahindi yao.

Mheshimiwa Spika, wakati haya yote yanafanyika NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana walikuwepo na hawajawahi kununua hata debe moja la mahindi Wilayani Mbinga. NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana, wameweka vituo kwenye miji wamegeuka ma-God father, wanasubiri mkulima atembee kilomita 60, 100, 200 aende kuwapelekea gunia zake 10 za mahindi. Mkulima huyu ataweza vipi kwa sababu mpaka aende kilometa 100 gharama zote za uzalishaji zimeisha pale. NFRA watuambie kama wao wamegeuka ma-God father sisi tunataka usuluhisho wa masoko ya wakulima kwenye nchi hii ikiwemo Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wamelima kweli kweli mahindi mwaka huu, wananchi wa Mbinga wamelima mahindi kweli kweli, kuna kizungumkuti mwaka huu wanaenda kuuza wapi? Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri leo hapa nitamkamatia shilingi yake. Mwaka jana tumetapeliwa, fedha zetu hazijarudishwa mwaka huu bila kutuambia tunaenda wapi kuuza mahindi yetu tunakamata shilingi yake hapa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nakupa taarifa kabisa uje na majibu yanayoeleweka kwa wananchi wa Ruvuma na Mbinga kwamba mahindi yetu tunayapeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais anazunguka nchi jirani kwenda kuongea na majirani zetu kuweza kujua mahindi yetu tunayauza wapi? Kinachotusikitisha wataalamu wetu wamekaa wanamshangaa Mheshimiwa Rais, yaani Mheshimiwa Rais kashatafuta masoko wanategemea mkulima atabeba gunia zake 10 aende akauze mahindi yake Malawi au Msumbiji, wataalamu wetu mnatuangusha. Haiwezekani mpaka tuje hapa tulalamike ndipo mtafute suluhu ya matatizo yetu, mlipaswa kuyaona mapema kabisa kwa sababu msimu wa mahindi sasa ndiyo umeanza. Sasa ndiyo tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie tunaenda kuuza wapi sisi mahindi yetu wananchi wa Ruvuma kwa sababu tumechoka na kutapeliwa na kwa muda mrefu sasa tunahangaika huku na huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasemaje kuhusiana suala la kilimo. Inasema: “Chama cha Mapinduzi kinatambua kwamba mageuzi ya kujenga uchumi wa viwanda ni lazima yaendane na mageuzi ya kuongeza tija kwenye kilimo”. Namkumbusha Mheshimiwa Waziri Ilani ya Chama chetu inasema nini kwenye masuala ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nimalizie kwa kumnukuu Mwalimu Nyerere alisema kama ifuatavyo: “Tarmac roads, too, are mostly found in towns and are of especial value to the motor-car owners. Yet if we have built those roads with loans, it is again the farmer who produces the goods which will pay for them”. Tutawalinda wakulima wa nchi hii Mheshimiwa Waziri tunaomba majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kuja na mkataba huu, kwa kuwa naamini kwamba mkataba huu una manufaa makubwa sana kwa nchi yetu ya Tanzania na nchi nyingine za Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba uanzishwaji wa maeneo huru ya biashara siyo jambo jipya duniani, ni jambo ambalo limeanza miaka mingi nyuma tangu miaka ya 1950; na mfano mzuri ni European Economic Community ambayo ilianza mwaka 1957 na baadaye kubadilishwa jina pale ambapo European Union iliundwa mwaka 1993. Kwa hiyo, inawezekana kwa sisi kama Bara la Afrika tumechelewa kutokana na changamoto mbalimbali na kuja na mkataba huu 2019 kwa sababu ni wazi kabisa sisi kama Afrika tumekuwa wahanga wa masuala ya ukoloni. Kwa hiyo, inawezekana tulichelewa kama Bara. hata hivyo, changamoto tulizonazo na ambazo tulikuwa nazo kama bara haziwezi kutunyima fursa ya sisi kama waafrika kuja na mbinu mbalimbali za kutuinua kiuchumi ikiwemo kuwa na soko huru la biashara kuelekea kutimiza malengo yetu ya ajenda 2063. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kwamba mojawapo ya hasara au changamoto ambazo tunaweza kuzipata kutokana na kuridhia mkataba huu ambao tumeelezwa na Serikali, moja ni kupungua kwa mapato ya kodi yanayotokana na ushuru wa forodha kwa bidhaa ambazo zitaondolewa kodi kwa takriban shilingi bilioni 41 ndani ya miaka 10, yaani wastani wa shilingi bilioni 4.1 kwa mwaka. Pia mojawapo ya changamoto nyingine ambazo tumeambiwa ni uwezekano wa kupoteza ajira kwa baadhi ya sekta hususan sekta za uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachelea kusema kwamba changamoto hizi zinafikirisha ukilinganisha kwamba sisi kama Taifa bado tuna changamoto ya ajira, lakini niseme kwamba kuna baadhi ya masuala ambayo kama Taifa tukifanyia kazi, changamoto hizi ambazo tunaweza tukazipata kutokana na kuridhia mkataba huu, tunaweza tukazipunguza kwa kiasi kikubwa sana na njia mojawapo ni kuendelea kujenga uchumi shindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi shindani una variables mbalimbali, lakini sisi kama taifa tukiendelea kujijenga tunaweza tukapunguza changamoto hizi kwa sababu tayari tuliishaanza. Mojawapo ya masuala ambayo tunaweza tukayajenga ili kuweza kuongeza uchumi shindani mojawapo ni kuendelea kuwa na miundombinu imara na wezeshi lakini vilevile kuendelea kuwa na taasisi imara, kuendelea kuwa na elimu ya juu inayotoa vijana ama watu ambao wanaweza kupambana kwenye soko la ajira la biashara, kuenzi mabadiliko ya teknolojia, kuenzi mabadiliko ya ubunifu na kuwa na masoko yenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini iwapo kama Taifa tutafanyia kazi masuala haya na kuwa na uchumi shindani, tunaweza tuka-penetrate kwenye masoko na vilevile athari ambazo tumeambiwa tunaweza tukawa nazo kama Taifa, tunaweza tukazipunguza ikiwemo suala la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia ripoti ya takwimu za biashara za benki yetu kuu kwenye kanda za kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine za jirani kwa mfano tukianzia biashara za bidhaa kati ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania tumekuwa tukifanya vizuri. Kwa mfano ukiangalia takwimu za miaka saba nyuma yaani kuanzia 2013 mpaka 2020 kwenye kuuza bidhaa tumekuwa tukifanya vizuri kwa sababu tumekuwa tukipanda, tulianza mwaka 2013 na US dola milioni 419, lakini mwaka jana 2020 tumeweza kupanda mpaka US dola milioni 812.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye kuuza bidhaa tumeweza ku- contained soko letu na kulinda soko letu kwa sababu tulianza na US dola milioni 394, lakini kwa mwaka jana tumeweza ku-contained na kushuka mpaka dola milioni 324. Kwa hiyo, inaonyesha kabisa sisi kama Watanzania tunafursa kwenye soko hili kwa sababu bidhaa zetu kwa uuzaji wa nje tumekuwa tukifanya vizuri sana na tumeweza kulinda soko letu la ndani kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye masuala ya ajira, ukweli ni kwamba ukipunguza kodi kwenye bidhaa unafanya makampuni yaweze kuzalisha zaidi, lakini generally hii ina-apply kote, ina-apply tu kwenye nchi ambazo gharama zao za maisha ni ndogo, ya kwamba kama gharama za maisha husika ni ndogo inamaana bidhaa zao zinaweza zika- penetrate kwenye masoko ya nchi nyingine kuliko nchi ambazo gharama za maisha ni kubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukachukulia mfano, wamarekani wakati wamejiunga na mkataba wa North America na free trade area, wamarekani viwanda vyao vingi sana vilikosa ajira kwa sababu Mexico ilikuwa na gharama za chini ndogo kuliko Marekani, lakini sisi kama Tanzania cost of living inakuwa approximated kwa dola 0.32. ina maana tunafanya vizuri kuliko nchi nyingine za Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukauza zaidi ni kuimarisha tu baadhi ya masuala ya kiuchumi ili tuweze kushindana zaidi na kufanya vizuri katika soko. Na hapa sasa inabidi tufanyie masuala ambayo ni ya msingi sana ikiwemo kujiongeza kiji-digital, yaani huduma ambazo zinatolewa kiji-digital sasa tunafanya kazi kwa uharaka na ziweze kuwa reliable. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumzia suala la taasisi imara liweze kutuvusha lazima taasisi zetu ziweze kubadilika.

NAIBU SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa kengele imeshangongwa.

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa mfano taasisi za kiserikali kama AFTC lazima zitoke kwenye kufanya kazi kwa mazoea ya finically na ziende kwenye biashara za mitandao kwenda kulinda walaji kwenye mitandao. Sasa hivi ukiwauliza hawana hata mkakati wa kulinda walaji kwenye mtandao ambapo biashara kubwa imeamia huko. kwa hiyo, mimi sina shaka kama Taifa tutafanya vizuri tukiendelea kufanya kazi tu kwa ajili ya variable sisi ambazo tukazifanyisha ukiwa na uchumi shindani basi tunaweza tukafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)