Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yahya Ali Khamis (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. YAHYA ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu kwa mara ya mwanzo, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na uwezo wa kusimama katika Bunge hili Tukufu, pia namshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa mama yetu Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa safari ya Dubai na kwa safari ya Marekani. Safari hizo zimefungua milango kwa Tanzania. Leo ukizunguka duniani Tanzania watu wanaielewa vizuri kwa mambo mazuri yanayokuja kwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde, Katibu na wengine katika Wizara ya Kilimo kwa kuweza kuleta mambo mazuri katika nchi yetu kwa mwelekeo huu wa bajeti unaokuja. Tunajua kwamba sasa Tanzania inafunguka kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika ni kidogo lakini nilikuwa nataka dakika 10 leo mimi kwa sababu leo nina mambo mahususi. Nina mambo maalum, nina mambo mahususi na muda maalum ya kuchangia kwa siku ya leo. Kwa mara ya mwanzo kabisa kuchangia katika Bunge hili dakika tano ni kidogo kwa sisi watu wa darasa la saba. Ilikuwa leo unipe kama dakika 10 hivi nichangie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya, kwa kuwa ni mara yako ya kwanza, nakuongezea dakika mbili, utumie dakika saba vizuri. (Makofi)

MHE. YAHYA ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tanzania tuna fursa kubwa ya mambo ya kilimo, tuna mashamba makubwa kwa ajili ya kilimo, lakini mashamba yale hayaendani na mfumo wetu wa kilimo cha sasa. Mashamba yale yamekuwa ni mashamba yapo tu, lakini mashamba ambayo hayaendani na kilimo tunachokwendanacho sasa. Na mashamba haya nitayataja; kwa sababu, mashamba kama yanafanya vizuri tutayataja na kama mashamba yanafanya vibaya tutayataja kwa sababu ni mali ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la mwanzo ambalo linafanya vibaya haliendani na mambo yetu ya kilimo ni Shamba la Madibila Kapunga. Shamba la pili ni shamba la Madibila. Shamba la tatu linakwendakwenda kidogo, la Ubaruku, linakwendakwenda kidogo. Mashamba mengine ni; West Kilimanjaro, Kilombero Morogoro, Dakawa Morogoro, Njombe, Kagera pamoja na Ruvu Mkoa wa Pwani. Mashamba haya hayaendani na wakati. Naiomba Serikali iwe karibu na mashamba yale kama kweli tunataka kuleta mfumo wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ni lazima mashamba yale Serikali iwe karibu na iyasimamie kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama huyu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefungua mipaka kwa ajili ya wawekezaji ili Tanzania tupate mafanikio. Sasa nikawa ninajiuliza Wabunge wanasema kwamba, mama anaupiga mwingi? Hili neno hili ikawa mimi nalitafsiri hii kuupiga mwingi ni nini? Lakini baadaye nikajua kumbe kuupiga mwingi ni uvumbuzi wa mambo. Ukae, upeleke akili yako ufikiri, ili ujue nini utasaidia Watanzania. Sasa kama tafsiri ni hiyo kwamba, mama anaupiga mwingi ni mvumbuzi basi na mimi namwambia leo Mheshimiwa Bashe kwamba, leo; mara ile nilimuona amevaa combat na mimi namwambia Mheshimiwa Bashe lile combat moja anipatie. Anipatie combat ili na mimi ni niwe mvumbuzi kwenye kilimo. Na kwa sababu tulimsikia siku ile mama anamuelekeza Mheshimiwa Bashe, kwamba na mikoa ya pwani ipate skimu kwa ajili ya mashamba ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uvumbuzi wangu na mimi nimezunguka Mkoa wa Pwani, kata baada ya kata na kijiji baada ya kijiji. Nimekwenda kwa baskeli, kwa miguu na mvua yangu; naanguka na pikipiki, lakini kwa sababu tunataka tumsaidie mama huyu anaupiga mwingi na sisi Wabunge tuupige. Tuzunguke katika mikoa yetu kila mahali ambapo tutajua kwamba, kuna vyanzo vya maji basi tupeleke mashamba kwaajili ya umwagiliaji. Hiyo ndiyo tafsiri yangu ya kuupiga mwingi, sasa na mimi nimeupiga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda katika Kijiji kimoja kinaitwa Maparoni kina eka 10,000. Nimekwendsa katika Kijiji kimoja kinaitwa Kwasalie kina eka 12,500. Nimekwenda katika Kijiji kimoja kinaitwa Msalala kina eka 7,000. Nimekwenda katika shamba moja Mbuchi A lina eka 8,200. Nimekwenda katika Kijiji kinaitwa Mbuchi B kina eka 4,600. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni mashamba ambayo kama tutapeleka skimu tukafanya mashamba ya umwagiliaji, basi Mkoa wa Pwani tunaitengeneza Mbarali nyingine. Kwa hivyo namuomba Mheshimiwa Bashe aanze na mashamba ya Mkoa wa Pwani na huko tutapata mashamba mkakati kwa ajili ya kupeleka mashamba ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona dakika saba sitazifika kwa leo, naomba nimuachie mwenzangu. Naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)