Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (8 total)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Barabara ya Kimara - Mavurunza – Kinyerezi ya kilometa saba maarufu kama Kikwete Highway iliahidiwa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2010 na ilikuwepo kwenye Ilani za Uchaguzi tatu; mwaka 2010, 2015 na 2020.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua, ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya vipaumbele vya Serikali ni ahadi za viongozi na hasa viongozi wa Kitaifa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara aliyoitaja ya Kimara kwenda Kinyerezi ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais tutaijenga kwa kiwango cha lami kadiri fedha zitakavyoendelea kupatikana. Tunajua baada ya kuwa na Stendi ya Magufuli, hii barabara ni muhimu sana kwa sasa kupunguza msongamano kwenye barabara zetu za Mji wa Dar es Salaam. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Wananchi wa mtaa wa Mavurunza Kata ya Kimara na mtaa Kibo kata ua Ubungo, tumechangishana tumejenga vituo 2 vya Polisi lakini hatujamalizia kwa sababu nguvu zimeisha. Je, Serikali inaweza ikaahidi kuingiza katika bajeti ijayo ili vituo hivi vikamilike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo Mbunge wa Jimbo la Ubungo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea tena azma ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanajengewa vituo vya Polisi ili lengo na madhumuni waweze kupata pahala pa kupeleka matatizo yao, lakini pia waweze kulindwa wao na mali zao. Nimwambie tu kwamba tupo tayari kuhakikisha kwamba tunaingiza fungu maalum kwa ajili ya ujenzi wa hicho kituo ili lengo na madhumuni wananchi wa Ubungo na maeneo ya Jirani waweze kunufauika na kituo hicho. Nakushukuru sana.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alifika katika Mtaa wa Ubungo Kisiwani tarehe 14 Mei, 2022 akafanya mkutano na wananchi pale na kulikuwa na mgogoro wa kiwango. Aliagiza kwamba wataalam wakafanye tena tathmini ili warudi kwa wananchi waelewani kuhusu kiwango ambacho kinastahili. Je, ni lini hiyo ripoti itapatikana?

Mheshimiwa Spika, la pili. Kwa kuwa muda mrefu umepita na wananchi pale hamna kinachofanyika na hata anuani za makazi hazijafanyika pale kwa sababu ya suala hili: Kwanini Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri msitoe tamko kwa sababu fidia hii haijulikani italipwa lini na wananchi wanaendelea na maisha yao kama kawaida? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili, Mthamini Mkuu alishamaliza kazi yake na alishasaini. Kwa hiyo, baada ya hili zoezi kukamilika, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, ni kutafuta fedha. Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba tutarudi kukaa na wananchi na kuwaeleza haya yote ambayo yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Waziri kwamba kauli ya Serikali ni kwamba bado tunahitaji kuendelea kulitumia lile eneo, na ndiyo maana tunatafuta fedha ili tuwalipe kwa wakati. Kama muda utakuwa umepita, maana yake kuna options mbili kwenye sheria. Moja, kurudia uthamini; na pili, kunaweza kukawa na interest ili kuhakikisha kwamba wale wananchi wanapata fidia stahili kutokana na kutoa eneo lao. Ahsante sana.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Wananchi wa Jimbo la Ubungo wameathirika sana na mafuriko ya mito Gide, Mto China na Mto Ng’ombe, ninavyoongea Mtaa wa Kibangu leo nyumba za wananchi 12 zimebomolewa na mto huo. Nauliza kwa nini Serikali isichukue hatua za dharula za kujenga gambiozi katika mito hiyo ili kuokoa maisha ya wananchi wakati tunasubiri mradi huo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Profesa Kitila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefika wakati na imeona athari ambazo zinajitokeza hasa zinazosababishwa na mito hii mikubwa na hasa kipindi cha mvua kubwa kama hiki ambacho tukonacho. Namwambia Mheshimiwa Profesa kwamba wazo na fikra alilolitoa ni jambo ambalo tayari tumeshakaa na tumeshalifikiria, lakini kwa heshima ya wazo lake tunalichukua na tunazidi kwenda kulifanyia kazi. Nakushukuru.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara ya Suka – Golani ambayo ilianza kujengwa mwaka jana, kilometa nane zimeshajengwa mita 400 lakini imesimama baada ya flow ya fedha kushuka.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akaahidi hapa kwamba mwaka huu flow ya fedha itakuwa nzuri kwa barabara hii ili wananchi wahakikishiwe kwamba barabara inakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, baraba hii ya Suka – Golani kama ambavyo nimeshasema hapa kwenye baadhi ya maswali niliyoulizwa, kwamba TARURA imeongezewa fedha sasa na tutaangalia kupitia Meneja wa TARURA katika Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Ubungo kuona ni namna gani katika bajeti ambayo ameitenga barabara hii itaweza kuendelea kufanyiwa matengenezo.
MHE. PROF. KITILA. A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa jibu hilo kwa umakini huo ambao ameonyesha Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye jibu lake.

Je, lini atakuja kwenye Mtaa wa Kibangu Kata ya Makuburi ili kushughulikia changamoto ya uchafuzi wa mazingira kutoka kwenye Viwanda vya EPZA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu swali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari kwenda kuona uharibufu ambao umefanyika huko na badala ya hapo kukaa na wamiliki wa viwanda hao na kuwaeleza namna bora ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa wananchi, nakushukuru.
MHE. PROF KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Barabara ya Kimara – Mavurunza mpaka Segerea imewekwa kwenye bajeti ya mwaka huu, lakini kwa sasa haipitiki, hali yake ni mbaya sana: Kwa nini Serikali isifanye matengenezo wakati tukisubiri ujenzi wa lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, barabara za Dar es Salaam nyingi ambazo siyo kwa kiwango cha lami ziko kwenye mazingira magumu. Nimwagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, aende kwenye barabara hii ambayo inaunganisha Jimbo la Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo na Mheshmiwa Bonnah, waende wakaiangalie ili waweze kuondoa hizo changamoto na waweze kurejesha usafiri kati ya hayo majimbo mawili, ahsante.
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, Serikali haioni haja ya kushughulikia mkanganyiko na mtanziko uliopo kuhusu dhana na mipaka ya Jiji la Dar es Salaam, na kama inaona haja hiyo lini itafanya hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ameainisha dhana ya kuangalia upya mipaka katika Jiji la Dar es Salaam kutokana na ukubwa wake na umuhimu wake kwa Taifa, sisi tumepokea jambo hilo na tutakwenda kushauriana na timu yetu tuone muda gani tunaweza tukalitekeleza ili tuangalie hivi vigezo ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameviainisha ahsante.