Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (8 total)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonyesha jitihada ya wazi ya Serikali kutatua kero ya miwa kwa kulima miwa katika Bonde la Kilombero. Lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri huduma zinaendelea. Kwa mfano, hivi tunavyozungumza, Vyama vya Ushirika vya RCG AMCOS ambavyo vilikuwa na DRD7 mwaka jana, wamepunguziwa kwenda 3. Chama cha Kitete AMCOS ambacho kilikuwa na DRD5 mwaka jana, mwaka huu imepewa 3. Chama cha KIDODI AMCOS ambacho kilikuwa na DRD4 mwaka huu kimepewa 2. Chama cha Mbwade, Msindazi na MIWA AMCOS vyote vimepunguziwa DRD, ambayo inapelekea kupunguza kiasi cha miwa ambacho kinapeleka Kiwandani.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana, tulilaza miwa tani 400,000. Mwaka huu wametupunguzia uwezo maana yake nini, maana yake wanajiandaa kuhujumu wakulima wa miwa kwa zaidi ya tani 400,000 ambazo tumelaza mwaka jana. Je, nini tamko la Serikali kwa vitendo hivi ambavyo vinafanywa na Kiwanda hiki? Lakini nini tamko la Serikali kwa makaburu hawa weusi ambao ni watanzania wenzetu wanaowasaidia wawekezaji kuumiza wakulima wetu? Naomba tamko la Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali inataka wawekezaji wote nchini, kufanya uwekezaji na shughuli zao zote kwa kuzingatia sheria. Na kama kuna hujuma kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, ni kinyume cha sheria na tutafuatilia.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, suluhu ya kudumu ya miwa ya wakulima wa Kilombero ni upanuzi wa Kiwanda hiki ambao nimeeleza. Kwa sababu, tukishapanua wakulima watauza zaidi miwa yao kwa sababu, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya mara tatu ya miwa ambayo wanachukua sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, kama nilivyoeleza wakati wa bajeti yangu, mwaka huu wenzetu wa SIDO tumewaelekeza na wameshakubali kufanyia kazi. Tutakuwa na mitambo midogo ya kuchakata miwa ya wakulima katika ngazi ya chini.

Kwa hiyo, kutakuwa na wajasiriamali ambao wanaweza wakauza miwa kwa wajasiriamali wadogo wa kuchakata miwa hiyo. Kwa sasa hivi tuna viwanda vikubwa peke yake, sasa tumeona kwamba kuna haja ya kuwa na wajasiamali wadogo wadogo, watasaidia sana kuchukua miwa hii ya wakulima wetu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuendelea kuzungumzia mradi wa Mchuchuma na Linganga kwenye Bunge letu bila utekelezaji dhabiti ni aibu, ni wa muda mrefu tangu enzi ya akinamama Mary Nagu wakiwa Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unasuasua kwa sababu mwekezaji hana mtaji wa kutosha, ndiyo maana ameshindwa kulipa fidia. Kwa nini Serikali inamkumbatia huyu mwekezaji, kwa nini isiachane naye kama mama Samia anataka mradi huu uendelee, ikamtafuta mwekezaji mwingine na Serikali ikawekeza vya kutosha?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nijibu swali nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi umechukua muda mrefu lakini lazima tukubaliane kwamba mwekezaji huyu Situan alikuwa na mkataba na Serikali kupitia NDC. Kwa hiyo mkataba wake lazima uhitimishwe kisheria, tukienda papara tutapata matatizo. Hata hivyo, nimpe taarifa kwamba leo hii wanakaa na tunaamini ndani ya mwezi huu mazungumzo yatakamilika. Baada ya hapo tuatajua ama twende naye au tuachane kisheria twende kwa mwekezaji mwingine, lakini tumesema kabisa kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais mradi huu lazima uanze ndani ya mwaka ujao wa fedha.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni bahati kubwa kuuliza swali la kwanza kabisa kwenye Wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Serikali imefanya utafiti gani mpya na upembuzi wa kina kufahamu fursa mpya za uwekezaji zinazoendana na sayansi na teknolojia? Kama imefanya hivyo, je ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuweka taarifa hizi zinazoendana na wakati kwenye tovuti za Wizara zinazotangaza masuala ya uwekezaji? Kwa sababu hata hao wawekezaji wanaangalia kwenye tovuti hizo. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji kila mwezi inatoa taarifa mpya ambayo inaonyesha fursa ambazo zimejitokeza. Pia inatoa taarifa kuhusu aina ya uwekezaji ambao umefanyika katika mwezi huo lakini tupokee ushauri wake kuhusu kuweka kwenye website ya Wizara. Nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndio kwanza ofisi hii imeanzishwa na tupo katika mchakato wa kuanzisha taasisi mbalimbali ikiwemo suala la website, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kulingana na fursa mbalimbali ambazo Mheshimiwa Waziri ameziainisha hapa zimepelekea kuwepo kwa wimbi kubwa la wawekezaji kutaka kuja kuwekeza nchini. Sasa nilitaka kujua, je, Serikali inatumia vigezo vipi kuweza kuwatambua wawekezaji wenye tija kwa Taifa hili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Nchi yetu kwa sasa inapokea idadi kubwa ya wawekezaji na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa mazingira mazuri ambayo anayaweka katika kuvutia wawekezaji. Lakini tunavyo vigezo maalum vingi vya kuweza kutambua ni mwekezaji gani tumpokee na tumpeleke wapi. Naomba nitaje vitano tu;

(i) Tunahakikisha kwamba tunapokea uwekezaji ambao hatimaye utasababisha kukidhi mahitaji ya bidhaa za ndani;

(ii) Tunapendelea sana uwekezaji ambao hatimaye utaongeza thamani ili kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ya vitu vyetu ikiwepo kwenye thamani ya mazao;

(iii) Tunaangalia uwekezaji ambao hatimaye utazalisha ajira kwa watu wetu. (Makofi)

(iv) Tunazingatia sana uwekezaji ambao utatusaidia kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi ili kuongeza fedha za kigeni na;

(v) Tunazingatia sana uwekezaji ambao utadhalisha utajiri kwa watu wetu kwa hivyo kuchochea uwekezaji ndani.

Mheshimiwa Spika, hayo ni baadhi ya vigezo ambavyo tunazingatia.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa ni mwaka wa 14 toka wananchi hawa wafanyiwe tathmini hawajalipwa, je, ni lini Serikali italipa wananchi hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Waziri yupo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kwenda kuongea na hawa wananchi kujua hatma ya malipo yao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maeneo yote ambayo yametwaliwa yanayostahili kulipiwa fidia huwa tunaingiza kwenye bajeti na hata katika bajeti ambayo tutawalisha mwaka huu tutayapangia. Baadhi ya maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja yatakuwemo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda Bagamoyo Mheshimiwa Mkenge anafahamu kwamba hata mwaka jana tulikuwa naye na mwaka huu pia tumepanga kutembelea eneo la Bagamoyo. Kwa hiyo, wakati wowote tukimaliza vikao vya Bunge tutakwenda Bagamoyo. Ahsante sana.
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali na naomba kuuliza swali la nyongeza, tukijua kuwa malighafi nyingi ndani ya nchi yetu inatoka katika vijiji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha sekta binafsi waweze kuwekeza hizo industrial pack ili wananchi waweze kunufaika katika Taifa lao hususani kwenye vijiji? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji pamoja na Mamlaka ya EPZA, tumeendelea kuhamasisha wawekezaji kupitia njia za makongamano na forum mbalimbali. Hivi ninavyozungumza wiki iliyopita tu, tulikuwa na wawekezaji wa ndani 200 na wawekezaji kutoka China 100, walikutana pamoja na kuweka mikakati ya kuweza kushirikiana kwenye kuwekeza katika haya makongamano makubwa. Kwa hivyo, niwakaribishe hata Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Toufiq ambaye ni mfanyabiashara muhimu kabisa katika nchi yetu, aweze kuwekeza katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kulingana na majibu ambayo yametolewa na Waziri, nataka kufahamu, ni upi mkakati maalum na wa haraka wa Serikali kuuingiza Mkoa wa Songwe kiujumla wake katika mpango wa uwekezaji wa kimkakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka kufahamu: Je, Serikali imeshafanya vitu gani katika kuongeza biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Songwe katika maeneo yafuatayo: eneo la madini, dhahabu na makaa ya mawe, kilimo cha mpunga, uvunaji wa chumvi na mazao mengine ya kibiashara yanayoendelea katika Mkoa wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maswali ya nyongeza yanahusu fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Songwe na ametaja maeneo specific; madini, chumvi na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, ninahitaji kumwandalia taarifa hizi kwa kina ili nisije nikatoa majibu ambayo ni ya kurukaruka. Kwa hiyo, naomba tupate nafasi kwa sababu kwa kweli ni swali ambalo ni jipya kidogo, ahsante.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilemela katika kuunga mkono uwekezaji ilitenga eneo la ekari 52 katika eneo la Nyamungoro, eneo lenye miundombinu yote; maji, barabara na liko kwenye main road ya kwenda Musoma kwa ajili ya kuweka industrial park na tayari andiko lilishafika katika Ofisi za Serikali; ni lini mradi huu utatekelezwa ili tuongeze ajira na kukuza TEHAMA kwa watu wa Mwanza na ukizingatia ni ukanda wa maziwa makuu ni hub katika eneo hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maendeleo ya Industrial Park tunafanya pamoja na Wizara ya Viwanda, ipo chini ya EPZA. Nalifahamu hili eneo na nilishafika na tayari lipo katika Taasisi yetu ya EPZA wakilifanyia kazi, linaenda kwenye bodi na baada ya hapo tutalitolea maelekezo maalum kwamba ni lini hasa ratiba itatoka ya utekelezaji. Naamini katika mpango na bajeti ambao tutawasilisha kwenye Mkutano ujao, tutaeleza mpango maalum kuhusu Industrial Park ya Manispaa ambayo Mheshimiwa Angeline Mabula ameieleza.