Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii na nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni yao mazuri sana kuhusu Sekta ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu baadhi ya hoja, naomba niseme mambo mawili ya kihistoria. Moja, naomba nichukue nafasi hii kukipongeza sana Chama cha Mapinduzi kwa kuadhimisha miaka 44 tangu kilipozaliwa na ukijumlisha na wazazi wake, miaka 60 leo mambo ambayo yanakifanya kuwa chama kikongwe kabisa Barani Afrika. Historia ya leo inakiweka Chama cha Mapinduzi kuwa chama ambacho kimekaa madarakani kwa muda mrefu kuliko vyama vyote Afrika. Mwaka juzi kulikuwa na chama ambacho kilikuwa kimekizidi sitaki kusema nchi gani lakini kimeondolewa madarakani kwa hiyo kimebaki Chama cha Mapinduzi na nakipongeza sana kwa historia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Bunge hili zimeshatolewa hotuba hapa za kufungua Bunge na hotuba za wakuu wa nchi zaidi ya 20 lakini zipo hotuba tano ambazo ni za kihistoria ikiwemo hizi hotuba mbili ambazo tunazijadili leo. Kwa ruhusa yako kwa haraka sana, hotuba ya kwanza ya kihistoria ambayo inajulikana katika nchi hii ndani ya Bunge hili ni hotuba ya Desemba, 1962 iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Hotuba hiyo ndiyo iliyozaa Jamhuri ya Tanganyika. Lengo lake kubwa ilikuwa ni kujenga Umoja wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya pili ni ya tarehe 25 Aprili, 1964 iliyotolewa katika Bunge hili. Lengo la hotuba hiyo Mwalimu alitumia kuomba ridhaa ya Bunge kuridhia Mkataba wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Hotuba hiyo ndiyo iliyozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya tatu muhimu ya kihistoria katika nchi hii ya tarehe 29 Julai 1985. Hotuba hii aliitumia Mwalimu Nyerere kuaga…

WABUNGE FULANI: Uwekezaji.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Tulia wawekezaji unakuja. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya nne ni ya tarehe 20 Novemba, 2015 iliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Hotuba hii lengo lake kubwa ilikuwa ni kujenga msingi wa kupambana na ufisadi na kuimarisha maadili ya utumishi wa umma na matokeo yake wote tumeyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya tano ya kihistoria ni iliyotolewa tarehe 13 Novemba, 2020. Lengo lake kubwa ni kulinda na kuendeleza status ya nchi ya uchumi wa kati. Hotuba hii imetoa mwelekeo wa kiuchumi wa nchi na imejengwa katika uwekezaji kama njia ya kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa nafasi kuwa sehemu ya Serikali yake ili kutekeleza maono makubwa ambayo yapo ndani ya hotuba hii ya tarehe 13 Novemba, 2020. Lengo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais ametuelekeza na ambalo tunalisimamia kwa bidii na kwa maoni ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyatoa ni mambo matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tuhamasishe uwekezaji wa ndani nan je ya nchi. Katika kuhamasisha uwekezaji Waheshimiwa Wabunge wanairudia ile kauli ya Mheshimiwa Rais, tunapozungumzia uwekezaji sio lazima moja, iwe kutka nje, lakini sio lazima uwe bilionea. Unatumia nafasi yako ndogo uliyonayo unaweka akiba, unapata mtaji, unawekeza unajenga uchumi, unaanza kujitengenezea mazingira kutoka kuwa elfunea kwenda milionea na hatimaye kuwa bilionea. Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani waende kuhamasisha katika halmashauri zao ili halmashauri zetu zitengeneze mazingira ya uwekezaji, ikiwemo kutenga maeneo ya uwekezajikwa wawekezaji wetu wa ndani, lakini pia wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumepewa kazi ya kuwezesha wawekezaji ndani ya nchi waliokwisha kuwekesha hapa kwa sababu, balozi mkubwa sana uwekezaji ni yule muwekezaji ambaye tayari yupo ndani ya nchi. Kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha halmashauri zetu ili ziweke mazingira mazuri ya kuhudumia wawekezaji ambao wapo. Pale ambapo kuna changamoto za wawekezaji tuzishughulikie kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho katika uwekezaji, ni muhimu sana kuwahudumia. Kwamba, pale ambapo mwekezaji ameshaweka, amewezeshwa, kiwanda kipo pale, ni muhimu sana mamlaka zilizopo kuanzia ngazi ya halmashauri wawekezaji hawa wahudumiwe kwa kupatiwa mahitaji muhimu. Tunafanya mawasiliano ya karibu na wenzetu katika Wizara mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, huduma muhimu zikiwemo umeme, maji na barabara zinapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, kwa sasa katika nchi yetu huduma za msingi za kufanya uwekezaji mkubwa zipo vizuri ikiwemo katika eneo la miundombinu. Kama ni barabara maeneo yote makubwa yameshaunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami. Kama ni usafiri wa majini karibu maziwa yetu yote makubwa ikiwemo na bahari tayari kuna vyombo vya usafiri vya kutosha, lakini pia usafiri wa anga umeimarika sana. Kama ni hali ya kisiasa ambayo ni ya msingi sana katika uwekezaji Tanzania ndio inaongoza kwa utulivu wa kisiasa Afrika. Kwa hiyo kwa kweli Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuhamasisha wawekezaji waje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tupo katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko Sheria ya Uwekezaji ili kuiboresha zaidi ikiwemo kuimarisha taasisi yetu ya TIC ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wametoa maoni mazuri namna ya kuiboresha. Pia tunatengeneza mkakati wa kuhamasisha uwekezaji katika ngazi ya kitaifa, lakini pia katika ngazi ya mkoa hadi katika ngazi ya halmashauri na ndio maana tumekuwa tukipita Mheshimiwa Waziri Mkuu akituongoza kwenda kuzindua Miongozo ya Uwekezaji katika ngazi ya mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwaalika sana Waheshimiwa Wabunge katika mikoa yenu. Pale ambapo tumekuja kuhamasisha na kuzindua miongozo hii naombeni sana mshiriki. Niwapongeze sana Mkoa wa Iringa, tulikuwa huko juzi, imefanyika kazi kubwa na nadhani mikoa mingi inaendelea kuzindua na hivi karibuni tutakwenda kuzindua katika mikoa mingine chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tumeaswa kila unapopata nafasi ushukuru watu ambao wamefanya tofauti katika maisha yako. Sasa nataka nichukue nafasi hii kwanza kukishukuru sana Chama Cha Mapinduzi kwa fursa kilichonipa ya kugombea nafasi ya ubunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana wananchi wenzangu wa Jimbo la Ubungo kwa kunipa nafasi ya kuwa Mbunge wao, hatimaye tukakomboa Jimbo la Ubungo lililokaa Misri kwa miaka 10 sasa lipo Kaanan, tumetoka Misri sasa tupo Kaanan. Niwapongeze sana, tutashirikiana sana kuhakikisha kwamba, mambo ambayo tumeyaahidi tunayafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi hii kuchangia maeneo haya mawili katika maazimio yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze mchango wangu kwenye hiba. Hiba ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hiba ni urithi au waingereza wanasema legacy. Hili naamini wasomi wataandika kwa muda mrefu ujao kwaajili ya kuweka kumbukumbu sawasawa; mchango ambao Mheshimiwa Rais wetu wa Tano alitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa duniani maisha yetu ni mafupi, na kifo cha Dkt. Magufuli kinatukumbusha kwamba hapa duniani Maisha yetu ni mafupi sana. Muhimu sana kwa kweli ni kwamba, sio kwamba tutakufa au la, kufa tutakufa, lakini tukifa tunapoondoka tutakumbukwa kwa lipi? Mwenzetu kwa kweli ameondoka akiwa ameacha alama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa duniani tunaambiwa kuwa kuna mambo mawili, kuna kutoa na kupokea. Wengi wetu huwa tunapokea, lakini tunapata baraka kwa kutoa, mwenzetu ametoa, ametoa maisha yake, ametoa kupitia mchango mkubwa wa kazi zake ambazo tutaendelea kuziishi kwa muda mrefu bila kuorodhesha mambo mengi ambayo ameyafanya ambayo watu wengi wameyasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, na uteuzi wa leo wa Makamu wa Rais ni jibu na ujumbe kwamba kazi inaendelea. Hilo ndilo jibu ambalo tunapewa kwamba, ni stability and continuity. Kwamba kitabu kinaendelea kuandikwa tunaendelea kwenye ukurasa mwingine. Tunashukuru sana kwa uteuzi ambao Mheshimiwa Rais ameufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kifo hiki kinatukumbusha miaka 20 iliyopita. Tarehe 4 Julai, 2001 nchi yetu ilikumbwa pia na msiba wa Makamu wa Rais Dkt. Omari Ali Juma. Mheshimiwa Mkapa alipomteua Dkt. Ali Mohamed Shein alitoa sababu kwa nini amemteua. Alitoa sababu sita ambazo kwa kweli ukizirejea, ndizo unazoziona leo kwa viongozi wetu wawili wakuu; kwa maana ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, lakini hata uteuzi wa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa ruhusa yako naomba nizirejee hizo sifa sita ambazo zilimuongoza Mheshimiwa Mkapa kumteua Mheshimiwa Ali Mohamed Shein. Yeye alisema kwamba, Watanzania wanatarajia sifa zifuatazo kutoka kwa viongozi wao; na ameandika pia kwenye kitabu chake kwamba ndivyo kigezo cha viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sifa ya kwanza ni utu na uadilifu. Yamesemwa hapa kuhusu utu na uadilifu wa Mama Samia lakini pia wa Mheshimiwa Dkt. Mpango. Upendo na heshima kwa watu wote. Kupenda kazi na kutumikia wananchi badala ya kupenda kutumikiwa na kukuzwa. Watu wengi wenye vyeo tuna shida moja. Ukiwa na cheo kuna mawili, unataka watu wakikuona wakuone nini? Wakimuona Kitila wamuone Kitila kwanza Waziri baadaye, ama Waziri kwanza Kitila baadaye? Watu wengi wanataka waonwe kwanza kwa vyeo vyao, halafu baadaye wao. Hapa Mheshimiwa Mkapa anasema, kiongozi mzuri ni yule ambaye anataka kwanza kabla ya cheo chake watu wamuone yeye, na hii ni sifa ya msingi ambayo viongozi wetu wawili wanayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naiweka vile vile namba nne, kuweka mbele maslahi ya taifa na Watanzania badala ya maslahi binafsi, viongozi wetu tunawafahamu vizuri. Unyenyekevu, limezungumzwa sana hili, viongozi wetu wawili Mheshimiwa Rais tangu aanze kazi hii; na watu wanaomfahamu kabla tuliopata nafasi na bahati ya kufanya naye kazi kabla tunafahamu unyenyekevu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho ni kuzingatia misingi ya Taifa; na aliitaja misingi tisa; utu, haki, usawa, fursa sawa, amani, umoja, upendo, mshikamano na hii ya mwisho aliandika kwa herufi kubwa MUUNGANO. Kiongozi yeyote katika nchi hii lazima tukimuona, tukimuangalia, tukimsikia tuwe na hakika kwamba Muungano wetu upo salama. Hakuna shaka kwamba kwa viongozi wetu wawili hawa Muungano wetu upo salama sana. Na hilo ni jambo la msingi mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni ukuu wa Katiba yetu. Watu wamelizungumza hili na limezungumzwa sana lakini sidhani ni kwa uzito ambao tunapaswa kuuona. Marekani wameshafiwa na Marais nane, wakiwa madarakani tangu mwaka 1841 na juzi 1993; na muda wote walikuwa na changamoto ya namna ya kumuapisha Makamu wa Rais, wamehangaika wameweza kufanikiwa kufanya mabadiliko 25 mwaka 1967. Sisi walioandika Katiba Mungu awabariki. Katiba yetu ina ukuu wa pekee, tumepita katika kipindi kigumu wala tusijue kwasababu Katiba yetu na misingi ipo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamtakia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais na viongozi wote neema na baraka na mafanikio tele katika uongozi wao. Mungu awabariki sana. Ahsante. (Makofi)