Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Irene Alex Ndyamkama (2 total)

MHE. IRENE A. NDYAMKAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, ni lini Serikali inawahakikishia wananchi wa Mkoa wa Rukwa itawatafutia wawekezaji na kuwekeza kiwanda hicho cha sukari mkoani hapo?

Mheshimiwa Spika, swali jingine, kwa kuwa, Mkoa wa Rukwa ni tatu bora kwa kilimo nchini Tanzania. Ni lini Serikali itaangalia tena mkoa huu kwa kuwekeza viwanda vingine?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunaendelea na kuhamasisha uwekezaji au viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mpango wa miaka mitano ambao umeuona moja ya maeneo muhimu sana ambayo tumeainisha ni kuhakikisha tunatafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, ikiwemo miwa na mazao mengine ambayo yanalimwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, na yeye ni mmoja wa wadau muhimu sana ambao tunaweza tukashirikiana ili kuhakikisha tunawekeza viwanda vidogovidogo vya kati na vikubwa kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Rukwa. Lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, muda wowote Wizara iko tayari kushirikiana na kukushauri na kushauriana na wawekezaji wengine, lakini pia kuangalia vivutio maalum ambavyo vitasababisha wawekezaji wengi kuwekeza katika mikoa yetu ikiwemo Mkoa wa Rukwa.
MHE. IRENE A. NDYAMKAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa meli hii imedumu takribani miaka 100 na ilikuwa mkombozi wa Wana-Ziwa Tanganyika, nikimaanisha Rukwa, Katavi na Kigoma. Je, ni lini sasa Serikali itakarabati meli hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Ziwa Tanganyika lina uchumi mkubwa na Serikali imetujengea bandari mbili, Bandari ya Kasanga na Bandari ya Kabwe. Ni lini Serikali itatujengea meli mpya Mkoa wa Rukwa kama mikoa mingine ili wananchi wa Mkoa wa Rukwa wafaidike na Serikali yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Irene Ndyamkama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba, tayari Mv. Liemba ipo kwenye hatua nzuri kwa sababu mkandarasi amekwishapatikana na mwezi ujao tuna-sign mkataba ili kazi iendelee. Kwa hiyo, katika hili la Mv. Liemba kama ambavyo Wabunge wengi wa Mkoa wa Katavi na maeneo ya jirani walizungumza wakati wa bajeti, tumezingatia linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili tumepokea hoja yake ya kupata meli ya Mkoa wa Katavi kama mikoa mingine. Tutalifanyia kazi kadiri ambavyo Serikali itapata fedha za kutekeleza hilo, ahsante.