Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. David Mwakiposa Kihenzile (2 total)

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, lakini pia swali hilo linafanana na hali ya kule Mufindi. Kwa kuwa Mufindi ni kitovu cha viwanda nchini na zaidi ya viwanda tisa viko pale na miundombinu imekuwa ni mibovu sana; na kwa kuwa barabara ya Nyololo - Mtwango na Mafinga - Mgololo zimeahidiwa kuanzia wakati wa Mwalimu Nyerere, pamoja na Rais Magufuli, zimeahidiwa na Mawaziri Wakuu, Mzee Pinda na Mzee Kassim Majaliwa, zimetajwa kwenye Ilani ya CCM karibu mara tatu…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuingiza kwenye bajeti barabara hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara zote alizozitaja zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji mkubwa sana ambao yanachangia fedha nyingi sana kwenye Mfuko wa Serikali na kama alivyosema barabara hizo zimeahidiwa na viongozi wengi wa Kitaifa, lakini pia barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizo kwa sababu ya umuhimu wake, kuanzia bajeti inayokuja zitaanza kutengewa fedha ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kwa kuwa Serikali inatambua jambo hili ambalo nimesema nataka kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini Serikali itamaliza kero ya maji katika ukanda huu wa baridi ambapo kuna vyanzo hivyo na hivyo kufanya tatizo la maji kuwa historia katika maeneo ya Kata za Migohole, Kasanga, Mninga, Mtwango, Idete pamoja na maeneo mengine ya Makungu, Kiyowela na Mtambula?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza, kwa kuwa suala la maji ni mtambuka na ni muhimu sana, katika eneo hilo la Mufindi Kusini kulikuwa na mradi ulikuwa unaitwa Imani, ni lini Serikali itakwenda kuufufua kwa kuboresha miundombinu ili wananchi waliokuwa wananufaika waweze kunufaika especially kwenye Kata za Ihoanza, Malangali, Idunda, Mbalamaziwa, Nyololo, Maduma na Itandula?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge David Kihenzile kwa namna ambavyo amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa matatizo ya maji katika Jimbo lake. Hii ni kawaida yake kwa sababu pia amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza tatizo la maji litakoma lini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama Ilani ya CCM inavyotutaka Serikali kuhakikisha kufika mwaka 2025 tuweze kukamilisha maji vijijini kwa 95%, kwa maeneo ya Mufindi tutahakikisha mwaka ujao wa fedha tunakuja kuweka nguvu ya kutosha ili libaki kuwa historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kufufua miundombinu, katika maeneo mbalimbali suala hili linaendelea kutekelezwa. Katika eneo la Mufindi, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha tutakuwa tumeshafanya kwa sehemu kubwa kuona miundombinu chakavu tunaitoa na tunaweka miundombinu ambayo inaendana na matumizi ya sasa.