Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. David Mwakiposa Kihenzile (15 total)

MHE. DAVID M. KIHENZILE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta Mradi wa Kuhifadhi Mazingira Mufindi katika chanzo cha maji cha Mto Ruaha na shamba la miti la Sao Hill?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya kuboresha hali ya upatikanaji wa maji nchini. Chanzo cha maji cha mto Ruaha Mdogo ni miongoni mwa mito inayomwaga maji nchini katika kidakio cha Great Ruaha. Kutokana na umuhimu wa Mto Ruaha Mdogo na kwa lengo la kuhakikisha mto huo unatiririsha maji kwa muda wote, Wizara kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji tayari imekamilisha kuweka mipaka ya vyanzo vya maji na taratibu za kuvitangaza katika Gazeti la Serikali zinaendelea. Hii ni pamoja na uanzishwaji wa Jumuiya ya Watumia Maji, utunzaji wa vyanzo vya maji, upandaji wa miti rafiki na maji pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi vyanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa shamba la miti la Sao Hill lililopo Wilaya ya Mufindi, shamba hili limehifadhiwa na Wakala wa Misitu (TFS) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoendelea.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Nyololo – Mtwango – Mafinga hadi Mgololo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyololo – Mtwango yenye urefu wa kilomita 40.4 na barabara ya Mafinga – Mgololo yenye urefu wa kilometa 81.14 zinasimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS). Barabara ya Nyololo – Mtwango ni barabara ya mkoa ya kiwango cha changarawe na barabara ya Mafinga – Mgololo ni barabara kuu ya kiwango cha changarawe na kiwango cha lami katika maeneo korofi. Barabara hizi zinapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara na chakula na pia zinahudumia viwanda kadhaa ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nyololo – Mtwango kwa kiwango cha lami. Aidha, inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mafinga – Mgololo kwa kiwango cha lami, ambapo kwa sasa kazi hii ipo katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, barabara hizi zitaingizwa katika mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi kwa kiwango cha lami, kwa sasa barabara hizi zinaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali kila mwaka ili kuhakikisha kuwa zinapitika katika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mgololo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mgololo kilipatiwa gari la kubeba wagonjwa mwaka 2018 ambalo linalotumika kwa sasa kuhudumia wagonjwa wa dharura kwenye kituo hicho. Hata hivyo, kutokana na udogo wa gari hilo na ugumu wa jiografia ya eneo husika, gari la kubebea wagonjwa lililopo Kituo cha Afya Kasanga hutumika kuhudumia wagonjwa wa dharura inapohitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na kwa kulizingatia hilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri imenunua gari ya wagonjwa kwa kutumia mapato yake ya ndani lenye thamani ya shilingi milioni 174.

Aidha, Halmashauri imefanya matengenezo ya magari mawili ya wagonjwa ambayo yalikuwa mabovu kwa muda mrefu na kufanya Halmashauri kuwa na jumla ya magari matano ya kubebea wagonjwa. Magari haya yanatumika kubeba wagonjwa mara tu dharura zinapotokea katika vituo vya afya vilivyopo Wilayani Mufindi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa ili kuboresha huduma za rufaa Wilayani Mufindi na nchini kwa ujumla, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mgololo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mgololo kilipatiwa gari la kubeba wagonjwa mwaka 2018 ambalo linalotumika kwa sasa kuhudumia wagonjwa wa dharura kwenye kituo hicho. Hata hivyo, kutokana na udogo wa gari hilo na ugumu wa jiografia ya eneo husika, gari la kubebea wagonjwa lililopo Kituo cha Afya Kasanga hutumika kuhudumia wagonjwa wa dharura inapohitajika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa magari ya kubebea wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na kwa kulizingatia hilo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri imenunua gari ya wagonjwa kwa kutumia mapato yake ya ndani lenye thamani ya shilingi milioni 174.

Aidha, Halmashauri imefanya matengenezo ya magari mawili ya wagonjwa ambayo yalikuwa mabovu kwa muda mrefu na kufanya Halmashauri kuwa na jumla ya magari matano ya kubebea wagonjwa. Magari haya yanatumika kubeba wagonjwa mara tu dharura zinapotokea katika vituo vya afya vilivyopo Wilayani Mufindi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa ili kuboresha huduma za rufaa Wilayani Mufindi na nchini kwa ujumla, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza Kodi kwenye Vifaa vya Mchezo ili Sekta ya Michezo iweze kustawi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakaposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 Serikali kwa kuona umuhimu wa Sekta ya Michezo nchini, imetoa msahama wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira vilivyopo kwenye Manispaa na Majiji.

Aidha, Serikali itaendelea kutoa msamaha wa VAT kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira vilivyopo kwenye Halmashauri baada ya kuridhishwa na matumizi ya msamaha uliotolewa kwenye Manispaa na Majiji. Aidha, katika kuendeleza Sekta ya michezo nchini Serikali imetoa msamaha wa VAT kwenye huduma za elimu zitolewazo kwenye vituo vya mafunzo ya michezo nchini.
MHE. DAVID M. KIHENZILE Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Kiwanda cha Parachichi Mkoa wa Iringa hususan Mufindi Kusini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara namba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na azma ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda katika nchi yetu. Moja ya mikakati ambayo Serikali imeweka ni pamoja na kutenga maeneo katika kila Wilaya na kuweka miundombinu wezeshi ili kuvutia uwekezaji wa viwanda kulingana na malighafi zinazopatikana katika eneo husika.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Mufindi, Serikali imetenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ikiwemo eneo la Igowole katika Jimbo la Mufindi Kusini. Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana Tanzania ikiwemo zao la parachichi Wilayani Mufindi, nakushukuru.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, kwa miaka kumi ni wawekezaji wangapi wa nje walionesha nia ya kuwekeza na kufanikiwa na upi mkakati kwa ambao hawajafanikiwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) jumla ya miradi 4,543 ilisajiliwa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2021 ambapo mitaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 53.1 ilitarajiwa kuwekezwa na kutoa ajira 654,260. Kati ya miradi hiyo, miradi 3,304 ilitekelezwa sawa na asilimia 72.7 ya miradi yote iliyosajiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kufanikisha uwekezaji ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA, dirisha moja la kuhudumia wawekezaji, kuboresha na kujenga miundombinu wezeshi, vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi na kutenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji. Nakushukuru.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI K.n.y. MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata ya Mwabuki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti Mbunge wa Jimbo la Misungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mwabuki ina jumla ya vijiji sita vya Lubuga, Mhungwe, Mabuki, Mwagagala, Mwanangwa na Ndinga. Kwa sasa vijiji hivyo vinapata huduma ya maji kupitia visima vya pampu za mkono ambapo hali ya huduma ya maji ni asilimia 39.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma ya maji Kata ya Mwabuki katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imekamilisha usanifu wa mradi wa maji kutoka bomba kuu la KASHWASA kupeleka katika vijiji vyote vya Kata ya Mwabuki. Kwa sasa taratibu za manunuzi zinaendelea na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Desemba, 2022 na kukamilika mwezi Desemba, 2023. Kukamilika kwa mradi huo kutaongeza huduma ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 39 hadi kufikia asilimia 100.
MHE. NANCY H. NYALUSI K.n.y. MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, lini skimu za umwagiliaji Ukanda wa joto Ihowanza, Malangali, Idunda, Mbalamaziwa, Itandulu, Nyololo na Maduma zitajengwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 itatenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu za Ukanda wa joto za Ihowanza, Malagali Idunda, Mbalamaziwa, Itandu, Nyololo na Maduma. Baada ya kukamilisha zoezi hili Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa skimu hizo.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga miradi ya umwagiliaji katika Tarafa ya Malangali ili wananchi waweze kushiriki katika kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Iringa unakadiriwa kuwa na eneo linalofaa kwa kilimo la hekta 54,000. Kati ya hizo hekta 20,017 zinamwagiliwa ambapo hekta 16,789 zinamwagiliwa kipindi cha masika na hekta 3,550 zinamwagiliwa kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na uhakiki wa maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya ya Mufindi ambapo hadi sasa skimu nne (4) zenye jumla ya hekta 1,800 zimehakikiwa na kuwekwa kwenye mpango wa umwagiliaji. Aidha, Tume inaendelea na uhakiki wa maeneo mengine yanayofaa kwa umwagiliaji ikiwemo Tarafa ya Malangali.

Mheshimiwa Spika, zoezi la uhakiki litakapokamilika, Tume ya Umwagiliaji itaandaa mpango kazi utakaoainisha kazi zitakazofanyika katika skimu hizo.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka magari ya kubebea wagonjwa katika Vituo vya Afya vya Mtwango na Mgololo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu na uhitaji wa magari ya kubebea wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kwa kutambua mahitaji yaliyopo, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi bilioni 35.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari 316 ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za manunuzi zinaendelea na magari hayo yatagawiwa kwenye halmashauri zote 184 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambayo itapewa magari 2 ya kubebea wagonjwa, ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa Shirikisho la International Federation of Cross and Crescent nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (International Federation of Red Cross and Crescent - IFRC) ni Shirika la Kimataifa linalounganisha vyama vya nchi mbalimbali vya Msalaba Mwekundu. Nchini Tanzania Chama cha Msalaba Mwekundu kilianzishwa chini ya Sheria Na. 71 mwaka 1962 kufuatia nchi yetu kuridhia mikataba ya Geneva yam waka 1949. Kazi kubwa ya Shirikisho hili ni kufanya shughuli za kusaidia wahanga wa maafa na kuimarisha uwezo wa wanachama wake katika kukabiliana na maafa. Kutokana na umuhimu wa Shirikisho hilo kwa nchi yetu, tayari Serikali imekamilisha majadiliano na uongozi wa IFRC na zoezi la kuwashirikisha wadau wote wanaohusika hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha mkataba na shirikisho hilo, hatua hizo zitakapokamilika mkataba utasainiwa na Ofisi za IFRC kufunguliwa nchini na kuanza kufanya kazi. Ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza:-

Je, lini Serikali italeta mradi wa kuhifadhi Mazingira katika chanzo cha maji cha Mto Ruaha na shamba la miti la Sao Hill?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo chanzo cha Mto Little Ruaha kilichopo kwenye Shamba la Miti la Sao Hill. Mto huo ni chanzo cha maji kwa wananchi wa Mji wa Iringa na viunga vyake na unatumika kwa shughuli za uzalishaji umeme, ufugaji na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada mbalimbali za kutunza vyanzo hivyo zinaendelea ikiwemo kuanzisha Jumuiya nne za Watumia Maji Wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa; kutoa elimu ya uhifadhi wa vyanzo; na kutekeleza program ya kupanda miti rafiki na maji ambapo miti 3,000 imepandwa katika halmashauri hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inaandaa Mpango wa Uhifadhi wa Vidakio wa mwaka 2021 hadi 2035. Kwa kupitia mpango huo, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imepanga kuweka alama ya mipaka ya kudumu katika chanzo cha Mto Little Ruaha ndani ya Shamba la Miti la Sao Hill; kuweka mabango yenye jumbe za katazo za shughuli za binadamu katika chanzo cha uhifadhi wa chanzo; kupanda miti rafiki na maji; kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi endelevu wa vyanzo vya maji na mazingira; na kuajiri walinzi wa kulinda vyanzo vya maji kwenye shamba hilo hususani kwenye maeneo yenye uharibifu.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mtwango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Sadan. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya na itapeleka fedha kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mtwango pindi fedha zitakapopatikana.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu ya mawasiliano katika Kata za Idete, Kiyowela, Maduma, Idunda, Makungu na Ihowanza?

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Idunda na Ihowanza, Wilayani Mufindi ambapo ujenzi wa minara unaendelea na utakamilika ifikapo Julai, 2022. Mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali itafikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Idete na Maduma. Aidha, Kata za Kiyowela na Makungu zitafanyiwa tathmini ya kiufundi kubaini changamoto halisi iliyopo ili kutatuliwa.