Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Simai Hassan Sadiki (10 total)

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yanaendelea kuathiri vyanzo na miundombinu ya maji kule kijijini Nungwi jambo ambalo limepelekea kuwa na kero kubwa kwa Watanzania wanaoishi maeneo yale. Napenda kusikia kauli ya Serikali ni lini mradi huo unaozungumziwa hapa unatarajiwa kuanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri ni lini atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda kuangalia moja kwa moja uhalisia wa athari ya mabadiliko ya tabia nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa idhini yako nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Simai kwa juhudi yake ya kufuatilia miradi mbalimbali katika Jimbo lake ikiwepo miradi ya maji kwa kweli ni mwanaharakati mkubwa kufatilia maendeleo ya maslahi ya jimbo lake na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara tu baada ya utaratibu wa kifedha utakapokamilika mradi huu utaenda kutekelezwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo katika harakati za kufatilia taratibu hizi za kifedha zikamilike ili kusudi kwenda kutekeleza mradi huo katika eneo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mara tu baada ya kumaliza kikao hiki mwishoni mwa mwezi huu tutafuatana mimi na yeye twende tukaone athari hiyo ambayo inajitokeza ndani ya jimbo lake, ahsante.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la moja la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga uzio kuzunguka eneo la Kituo cha Polisi lilolokuwepo Nungwi ili kuepusha uvamizi eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tutatathimini mahitaji ya gharama za ujenzi wa uzio huo ili kuweza kuanza mkakati wa ujenzi kupitia juhudi za mfuko wa tunzo na tozo kama ambavyo tumefanya kwenye maeneo mengine.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wabunge na baadhi ya wananchi kutokana na ucheleweshwaji na matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa na baadhi ya Halmashauri hasa kule Zanzibar: Je, Serikali haioni haja sasa kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kubadilisha utaratibu wa fedha hizi, badala ya kupitia Halmashauri sasa kupitia moja kwa moja kwenye account maalumu za Majimbo husika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kumekuwa na utaratibu usiokuwa rasmi kwa baadhi ya Halmashauri hasa kule Zanzibar, ukizingatia kwamba Jimbo la Nungwi hadi hii leo bado hivi tunavyozungumza hatujapata fedha za mwaka 2021/2022. Hii ni kutokana na hali ya sintofahamu iliyotokezea pale Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini A.

Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Jimbo la Nungwi kuhusiana na fedha hizo juu ya upatikanaji wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Sadiki Simai, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili la Mfuko wa Jimbo lipo kisheria na limeelezwa kabisa katika Sheria Na. 6 ya mwaka 2012 na katika sheria hii imeeleza wazi kwamba fedha zote za Mfuko wa Jimbo zitakuwa zinapitia kwenye Halmashauri. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa ameshauri hilo na kwa kuwa jambo hili lipo kisheria, basi atupe muda tuone namna ya kufanya kwa sababu inabidi twende kwenye sheria ili tuhakikishe kwamba fedha hizi zinakwenda kwenye mifuko ya Wabunge wenyewe. Hata hivyo tulilifanya hili, kwani ilifika wakati tukaona kwamba fedha nyingi zilikuwa zikitumika kinyume na utaratibu. Ndiyo maana Serikali iliamua sasa zipitie kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Halmashauri hiyo ama Jimbo lake kwamba mpaka leo fedha zile hazijapatikana na kwa sababu labda zilitumika kwa mambo mengine, tuseme tu kwamba lengo la Mfuko wa Jimbo ni kusaidia kuboresha miradi ya maendeleo katika Majimbo husika na hakuna lengo lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunataka tutoe wito kwa Halmashauri zote, Mabaraza ya Miji yote, kwamba fedha hizi zitumike kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jimbo na siyo vinginevyo. La kwanza, wahakikishe wanawajulisha Wabunge kwamba fedha zimeingia; la pili, wawape fedha hizi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo lake tutalifutilia na tutahakikisha kwamba fedha zake tutazipata kwa wakati. Nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Nungwi imebadilika hadhi kutoka kijiji kuelekea mji na kwa kuwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la watu pamoja na wawekezaji katika sekta ya utalii wa Kimataifa.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza majengo na watendaji ili kukiongezea daraja Kituo cha Polisi Nungwi kutoka daraja C kwenda B?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Nungwi kumekuwa na changamoto kubwa mno ya upatikanaji wa maji jambo ambalo limewapelekea maaskari wengi kuondoka kituoni kwenda sehemu za mbali kutafuta maji hayo.Je, Serikali haioni haja ya kuwachimbia kisima au kutafuta njia mbadala ili kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji ya kudumu katika eneo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja tunatambua kweli maeneo mengi ya vijijini ikiwemo Kijiji cha Nungwi kimekua na kuwa Mji Mdogo na watu wameongezeka, lakini kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, eneo hili ni dogo, kama tuna dhamira ya kupanua, basi Mheshimiwa Mbunge atusaidie kushirikiana na Mamlaka ya Wilaya pale ili tupate eneo la kutosha kuweza kujenga kituo kinachokidhi mahitaji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la upatikanaji wa maji, naomba nishauri kwamba, kazi ya Jeshi la Polisi sio kuchimba visima, lakini kule kuliko na polisi kama walivyo wananchi wengine mamlaka za ugawaji wa maji ziwafikie kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuwachimbia kisima. Tutawasiliana na wenzetu wa upande wa Zanzibar ili kuona uwezekano wa kuwapatia kisima wenzetu hawa ili wasiende umbali mrefu kutafuta maji. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa masuala ya badiliko ya tabianchi si masuala ya ki-Muungano lakini masuala ya mikataba ya kimataifa na masuala ya mikataba ya kikanda ni masuala ambayo yanahusika moja kwa moja na masuala ya kimuungano je mtaishirikisha vipi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika matayarisho ya mfuko huo wa mazingira?
WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimia Mwenyekiti, kwanza pamoja na majibu mazuri sana aliyoyatoa Comrade Chillo, Naibu Waziri wangu naomba kujibu swali la nyongeza la ndugu yangu Simai, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli suala la mazingira si suala la Muungano. Hata hivyo, katika kipindi chote, kwa sababu mazingira hayajali mipaka, tumehakikisha kutekeleza miradi mbalimbali upande wa Tanzania Bara na upande wa Visiwani. Ndiyo maana leo hii tuna mradi mkubwa wa ujenzi wa ukuta kule Wete Pemba, hali kadharika Kaskazini A kuna mradi unaendelea. Hata hivyo katika mradi wetu, na juzi mmeona tulikuwa na tukio kubwa sana la kupokea Mwana Mfalme katika nchi yetu katika mradi wa carbon credit, na kwenye jambo hili tumeshirikiana kwa kizuri zaidi. Kwa hiyo huku tunakokwenda sasa ushirikiano wetu unakuwa mkubwa zaidi; na hata katika vikao hivi vya awali ambavyo tumeendelea kuvifanya vyote tunashiriki kwa umoja na Ofisi ya Makamu wa Kwanza Zanzibar kule, kwa lengo la kuhakikisha kwamba mazingira tunayashughulikia wote kwa upana wake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kuweza kunipa nafasi hii kuuliza swali dogo la nyongeza.

Je, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mpango gani wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya kuandaa mradi utakaoenda kuzuia maji ya bahari kuendelea kumeza kingo kule maeneo ya Nungwi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai, Mbunge na mtumishi wa wananchi wa Jimbo la Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayompango ama ilishakuwa na huo mpango na ndiyo maana tayari kuna baadhi ya kingo kwa upande wa Zanzibar ambazo tayari zimeshajengwa na hii ni kutokana na athari kubwa ya kimazingira ambayo ilifika wakati maji ya bahari yanaingia kwenye vipando vya wananchi ikiwemo mihogo, migomba ambayo haihimili maji ya chumvi. Pia maji haya yalikuwa yanaingia kwenye maeneo ya makazi. Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakaona kuna haja ya kushirikiana katika suala hili. Tayari yako baadhi ya maeneo kwa mfano Kisiwa cha Pemba maeneo ya Wete, Micheweni na maeneo ya Unguja pia tumeanza. Namwambia Mheshimiwa kwamba katika bajeti ambayo tumeisoma juzi tutajitahidi tutenge fungu kwa ajili ya kulipa kipaumbele Jimbo lako kwa ajili ya kujenga hizo kuta. Nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, haki ya Kitambulisho cha Mtanzania ni haki ya kila raia wa nchi hii.

Je, Serikali haioni haja ya kuambatanisha kitambulisho cha Mtanzania na cheti cha kuzaliwa mara tu baada ya mtoto kuzaliwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi tumesema umuhimu huo upo lakini kuhusu cheti cha kuzaliwa hili litakuwa la kisheria lazima sheria yetu ya NIDA irekebishwe Sheria ya Kitambulisho cha Taifa kwa sababu sheria ile inatambua mtu anayestahili kupewa kitambulisho ni yule aliyefikisha miaka 18 na kuendelea, lakini anayezaliwa leo anastahili kupata kitambulisho cha kuzaliwa. Kwa hivyo tutajitahidi katika marekebisho hayo kuweza kulijumuisha suala ambalo Mheshimiwa Mbunge amelihoji. Nashukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa sasa ni mwaka wa tatu nimekuwa nikisimama katika Bunge hili kuulizia jitihada zinazochukuliwa na Serikali zote mbili katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Nungwi lakini majibu tunayopata leo ndiyo kwanza shilingi milioni 650 zimetengwa kwa ajili ya kufanya utafiti. Ninachotaka kujua ni lini utafiti huu utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, shughuli za utalii na uchumi wa bluu zimekuwa zikiathiri sana ukataji wa mikoko katika maeneo ya fukwe za Bahari ya Hindi kule Zanzibar. Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuhakikisha kwamba mikoko inarejeshwa katika uhalisia wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana kwa kuwa jambo hili amekuwa akilipigia kelele sana na hatimaye sisi kama Serikali tumeshaandaa fedha kwa ajili ya kuanza angalau tathmini ya awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha hizi zimeshapatikana naomba kumwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa utafiti unaenda kuanza muda wowote. Kama tulivyosema kwamba kuna kuta za aina nyingi, kwa hiyo ni lazima utafiti ufanyike ili tujue ni aina gani ya kuta. Kuna kuta za slope ambazo zinatoa maji mitaani zinapeleka baharini, lakini pia kuna kuta ambazo zinakinga kutoka baharini maji yasije mitaani. Kwa hiyo ni vyema utafiti ufanyike ili tuone ni aina ya kuta na pia tuweze kupima current ya maji ya sea breeze na land breeze, ni aina gani ya huduma ambayo wananchi wanatakiwa wapatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwa upande wa swali la pili, tumechukua hatua nyingi. Moja ni kuendelea kutoa elimu wasikate, wapande na wasichome mikoko ambayo ipo around ufukwe wa bahari. Kubwa zaidi tumeendelea kuhimiza kupitia ilani ambayo inasema kwamba kila Halmashauri kila mwaka lazima ipande miti milioni 1.5. Kupitia miti hii tumehimiza mikoko ipewe kipaumbele ili kunusuru fukwe zetu lakini zaidi kuendelea na ile sera yetu ya soma na mti. Tunataka wanafunzi wa sekondari, msingi, vyuo na vyuo vikuu wapande miti, lakini miti ambayo tumeipa kipaumbele hasa kwa shule za fukwe ni mikoko, nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Serikali, ikumbukwe ya kwamba mwaka 2020/2021 niliuliza suala hili hili. Mwaka 2021/2022 nikauliza tena suala hili hili na nikajibiwa kwamba katika bajeti ile litatengwa Fungu Maalum kwa ajili ya kwenda kujenga ukuta ule. Mwaka 2022/2023 nimeishauliza tena suala hili ndiyo kwanza milioni mia sita zimetengwa kwa ajili ya utafiti. Ninachotaka kujua ni lini Utafiti huu utaanza wakati ambapo milioni sita hiyo inauwezo wa kutosheleza kujengea huo ukuta? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili. Kwa kuwa Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, harakati zao za kiuchumi zimeegemea zaidi katika shughuli za uvuvi na utalii. Mambo ambayo yamekuwa yakitaja ni miongoni ambayo yanapelekea kuharibu na kupelekea athari za mabadiliko ya tabiachi. Je, Serikali ina mpango gani ya kuokoa mazingira ya bahari yaliyosababishwa kutokana na athari za uvuvi na utalii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, changamoto yetu kubwa katika ujenzi wa ukuta huu ulikuwa ni kuweza kuanza kupata fedha za kuanza kufanya tathimini ya awali. Kwa kuwa sasa fedha zimeishapatikana, tulichokifanya tayari tumeishawasiliana na tumeishawasilisha andiko letu kwa wenzetu Wakala wa Majengo. Kwanza kwa ajili ya kutufanyia Michoro ama Ramani kwa ajili ya aina ya ukuta ambao unatakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuna kuta za aina nyingi, kuna gabrion wall, kuna zile slope, kuna zile vertical, kuna blocks. Sasa tunataka tufanye utafiti tujue ni aina gani ya ukuta ambao wananchi wa pale utaweza kuwasaidia lakini pia umesema tuwatengenezee ukuta ambao utaweza kuwasaidia kuzuia maji lakini pia waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kama ambavyo Wananchi wako hivyo. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwa kuwa taratibu tumeishazianza sasa hivi tunakwenda kuanza hii tathimini ili lengo na madhumuni tuwapelekee ukuta utakao wasaidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli shughuli zetu za uvuvi lakini na shughuli za utalii zimekuwa zikiathiri mazingira hasa maeneo ya bahari na maeneo ya fukwe. Tayari tumeona kwamba shughuli za uvuvi haramu, shughuli za uvuvi usiyokuwa rasmi lakini shughuli za ulimaji wa mwani na shughuli nyingine zinazofanyika pembezoni ama ndani ya bahari zinaathiri mazingira. Lakini la kwanza tumeanza kutoa elimu kwa Wananchi ili lengo na madhumuni Wananchi wafahamu ni aina gani ya uvuvi ni aina gani ya shughuli ambazo wanatakiwa wafanye kwenye bahari?

Mheshimiwa Spika, lakini tumeanza kufanya doria, tunashirikiana na wenzetu wa Thumka, wenzetu wa Mji Mkongwe, wenzetu wa Mlemba Conservation na wenzetu wengine kupitia Wizara ile ya Uchumi wa Bluu. Lakini kikubwa zaidi tumeanza kuchukua hatua zikiwemo za kuangamiza nyavu na vifaa vyote vinavyoweza kuweza kuathiri mazingira ya bahari, nakushukuru. (Makofi)
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuwa mara nyingi nimekuwa nikisimama Bungeni hapa na kutaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuwaathiri kule Nungwi lakini majibu yamekuwa yakitofautiana katika swali moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanataka kujua je, eneo lile unalolizungumzia hapa kwamba bado halijakidhi vigezo na masharti vilivyowekwa ili kuweza kupewa kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa tafiti nyingi zimeshafanyika katika kubaini athari za mabadiliko ya tabianchi kule maeneo ya Nungwi katika maeneo ya jamii na maeneo ya fukwe.

Je, Serikali kupitia Wizara yako ina mkakati gani au inawahakikishiaje wananchi kutengewa fedha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika eneo lile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Simai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii nimpongeza Mheshimiwa Simai kwa kazi nzuri anayoifanya hasa kutokana na athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi na jinsi ambavyo anawasaidia na kuwasemea wananchi wake kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo linatakiwa lijengwe ukuta kwa upande wa Nungwi limekidhi vigezo na lina kila sababu ya kufanya hivyo na ndio maana tumeanza kufanya utafitii na ndio maana viongozi wa SMZ na SMT wameshafika pale na ndio maana tumeshaliombea bajeti kwa ajili ya kulifanyia kazi kwa sababu tumeona athari ya kwamba pale pana kila sababu ya kusaidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Msheshimiwa Simai kwamba kutokana na vigezo hivyo tulivyovitaja eneo lile lina kila sababu ya kushughulikiwa na kusaidiwa na kufanyiwa kazi kama ambavyo Serikali imeliahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Nungwi niwaambie kwamba athari ya kuingia maji ya chumvi kwenye mitaa ama kwenye makazi ya wananchi hili jambo niwaambie linaenda kuondoka na ukuta ambao wanaulalamikia unakwenda kujengwa. Kwa nini utajengwa? Kwa sababu kwanza Serikali imeguswa na jambo lile lakini utakwenda kujengwa kwa sababu tayari tumeshaanza kujenga kuta kama hizi, tumejenga kule Pemba, Sepwese na tumeanza kujenga kule Mtwara Mikindani maana yake na Nungwi tunakwenda kujenga ukuta huu, nashukuru. (Makofi)