Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Simai Hassan Sadiki (6 total)

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI Aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji ya African Adaptation Program (AAP) iliyojengwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi ili kuondokana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo la Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la UNDP ilitekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi kupitia African Adaptation Program (AAP) mwaka 2011 katika eneo la Nungwi, Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja na kufaidisha jumla ya watu 11,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa ipo haja ya kufanya mapitio ya kuimarisha miundombinu ya miradi ya maji kupitia mpango wa African Adaptation Program (AAP) ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya maji kutokana na ongezeko la watu katika Jimbo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaandaa mpango wa kuimarisha miondombinu ya maji katika maeneo mbalimbali Unguja ikiwemo eneo la Nungwi kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Usambazaji Maji Safi na Salama na Misingi ya Maji Machafu Zanzibar chini ya mkopo wa Benki ya Exim ya India. Katika mpango huo, matenki mawili ya zege yatajengwa, moja la lita 500,000 na lingine la lita 300,000 ambapo mtandao wa maji utakuwa na urefu wa kilometa
14. Ahsante.
MHE. HASSAN SADIKI SIMAI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya ucheleweshwaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo upande wa Tanzania Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Hassan Sadiki Simai Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua jitihada kuhakikisha kuwa fedha za Mfumo wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zinawasilishwa kwenye majimbo ya Zanzibar kwa wakati. Mtiririko wa uwasilishwaji wa fedha hizo umekuwa wa kuridhisha. Kwa mwaka 2022/2023 shilingi bilioni 1,400,000,000 zimepelekwa Zanzibar mwezi Septemba, 2022. Aidha, fedha za mwaka 2021/2022 zilipelekwa Zanzibar mwezi Oktoba, 2021. Nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya ukosefu wa magari na nyumba za Askari Polisi Kituo cha Polisi Nungwi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Nungwi ni kituo cha Daraja C na kipo Mkoa wa Kaskazini Unguja. Pamoja na kufanya kazi mbalimbali za kipolisi, hushughulikia pia na kusimamia majukumu ya utalii.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kinacho gari Na. PT. 3388, Toyota Landcruiser ambalo hutumika kwenye kazi za kila siku za polisi. Kutokana na udogo wa eneo la kituo, hakuna sehemu inayoweza kutosheleza kujenga nyumba za makazi ya askari polisi. Hivyo, Serikali inawashauri wadau wenye nyumba za kupangisha wapangishe askari wetu. Aidha, uongozi wa Mkoa Kaskazini Unguja unaombwa ushirikiane na uongozi wa jamii kupata eneo linalofaa kujenga nyumba za askari ili Serikali iingize ujenzi wa nyumba hizo katika mpango.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa dharura wa kunusuru athari za mabadiliko ya tabianchi - Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Jimbo la Nungwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zilizopo eneo la Nungwi. Tayari, Serikali kupita Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 650 kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ya kuzuia athari hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua hizo ni pamoja na kuelimisha wananchi kupanda mikoko pamoja na kuhamasisha ulimaji wa mwani usioharibu fukwe. Serikali zote mbili za JMT na SMZ zitashirikiana katika kutafuta fedha zaidi ili kudhibiti uharibifu unaotokea eneo la Nungwi, nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza:¬-

Je, sababu zipi zimekwamisha ujenzi wa ukuta maeneo yanayoathiriwa na Bahari Nungwi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-¬

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge na Mtumishi wa Wananchi wa Jimbo la Nungwi, najibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa fukwe wa Bahari ya Hindi. Lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha zoezi la ujenzi wa ukuta wa Nungwi umechelewa lakini kwa sasa Serikali imepata fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imetenga fedha jumla ya shilingi milioni mia sita na hamsini kwa ajili ya kufanya tathmini ya awali ili kuwa na usanifu wa miundombinu itakayosaidia kurudisha ufukwe katika hali ya awali.

Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kuwahimiza wananchi wa maeneo ya Pwani kuongeza jitihada za kupanda mikoko, kutofanya uchimbaji holela wa mchanga lakini pia kuhamasisha ulimaji na uvunaji wa mwani usiyoharibu fukwe. Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar zitaendelea kushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali, nakushukuru.
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI aliuliza: -

Je, sababu zipi zinasababisha eneo linaloathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kupewa kipaumbele cha utekelezaji wa Mradi ili kunusuru hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Simai Hassan Sadiki, Mbunge wa Jimbo la Nungwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya tabianchi yanazidi kusababisha athari katika maeneo mbalimbali ya nchini yakiwemo maeneo ya ukanda wa pwani nchini. Katika kubainisha maeneo yaliyoathirika na kuyaweka katika kipaumbele, Serikali inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na athari zilizojitokeza hii ni moja ya sababu mojawapo ya vigezo vinavyotumika katika kuweka kipaumbele maeneo yaliyoathirika katika mipango ya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kubaini maeneo mbalimbali yenye changamoto kubwa ya uharibifu wa Mazingira na kuyaweka katika kipaumbele ili kuyatafutia rasilimali fedha, nashukuru.