Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Janejelly Ntate James (15 total)

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi, lakini kumekuwa na nyaraka zitolewazo na miongozo na Menejimenti ya Utumishi wa Umma zinazokinzana kabisa na Sheria mama ya Utumishi wa Umma. Je, lini hizi nyaraka na miongozo vitafutwa ili sheria mama za kiutumishi zitumike?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, lazima nikiri kwamba tunapokuwa na nyaraka basi sheria ndiyo hufuata mkondo wake. Tunapokuwa na sheria ambayo inayokinzana na Katiba ni dhahiri Katiba inakuwa juu ya ile sheria, lakini tunapokuwa na nyaraka inakinzana na sheria basi sheria ndiyo inafuata mkondo wake.

Kwa kupitia swali lako kama ulivyoliuza nitapata fursa ya kukaa na watendaji na kuangalia zile nyaraka zote ambazo zinakinzana na sheria iliyopo na tutafanya maamuzi kutokana na namna. Lakini pia ikikupendeza nitaomba nipate nyaraka hizo ili niweze kuzipitia na kushaurina na watendaji katika Wizara yangu. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTANTE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa kwa sasa hivi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuboresha maisha ya watumishi lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hivi Serikali haioni kumshusha mtumishi mshahara ni mojawapo ya adhabu apewazo anapokuwa na utovu wa nidhamu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali mtatoa tamko la kwamba hawa watumishi wanaofanyiwa recategorization mishahara yao ikiwa chini ya vyeo vile wanavyoenda kuanzia watabaki na mishahara yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze kusema siyo adhabu kumshusha mshahara mtumishi ambaye ametaka kubadilishiwa kada yaani recategorization kwa job satisfaction kwa sababu bila kufanya hivyo utakuta mwalimu tayari alikuwa ameshapanda daraja juu na sasa ameomba kuwa Afisa Sheria, natolea mfano, ni lazima aende kuwa Afisa Sheria Daraja la II, entry point ili kutengeneza seniority katika eneo la kazi. Bila ya kufanya hivyo, tunaweza tukawa tunawabadili kada watumishi anakwenda katika idara husika anakuta tayari kuna watumishi wengine waliotumikia kada hiyo miaka mingi yeye akaenda kuwa senior zaidi yao kwa sababu tu alishatumikia cheo kingine na kada nyingine. Kwa hiyo, kwa ajili ya kulinda hiyo seniority ni lazima aende katika entry point ya kazi ile aliyoiomba.

Mheshimiwa Spika, lakini akiwa ametumikia cheo kikubwa zaidi kwingine atahamia kule na mshahara binafsi ataombewa na mwajiri. Akiombewa mshahara binafsi atabaki nao kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba baada ya kufikia cheo sasa tuchukulie Afisa Sheria labda kafika kuwa Principal basi atalipwa mshahara ule wa Principal na ataacha mshahara wake wa mwanzo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, utumishi wa umma unaongozwa kwa sheria, taratibu na kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa. Kwa wale wote ambao wanastahili kufanyiwa recategorization ni wajibu wa waajiri kwanza kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya recategorization. Mbili, ni wajibu wa mwajiri kumfanyia recategorization huyo mtumishi na kumwacha na mshahara binafsi endapo kada yake ni ileile ambayo amejiendeleza nayo. Hili si ombi ni kwa mujibu wa sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge kama kuna mifano maeneo mengine Waziri wangu pamoja na mimi mwenyewe tuko tayari kwenda kuweza kuwashughulikia hawa Maafisa Utumishi na waajiri ambao hawatekelezi sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nihitimishe kwa kusema hivyo, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali; na niwapongeze kwa kutenga hizo fedha na kuzipeleka kwa ajili ya kufanya malipo; lakini nina maswali mawili (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna watumishi ambao wamestaafu lakini walihusika kwenye zoezi hili, wengine wamepewa nafasi za uteuzi na walihusika kwenye zoezi hili: Je, Serikali mmejipangaje kuhakikisha hizi fedha zinafika kwa walengwa? (Makofi)

(b) Kwa kuwa ulipaji wa malipo ya Watumishi wa Afya ni endelevu, Serikali mmejipangaje kuwa mnawalipa kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nipokee pongezi zake nyingi kwa Serikali ambapo baada ya watumishi wale kufanya kazi hiyo, imehakikisha imepeleka shilingi bilioni tatu kwa ajili ya watumishi kupata haki zao. Pili, watumishi waliostaafu au watumishi waliopata teuzi mbalimbali ambao kwa wakati huu hawapo kwenye Halmashauri, bado taarifa zao zote za kiutumishi na haki zao zipo katika Halmashauri husika na baada ya kuchakata malipo hayo, watapata haki zao kwa sababu taarifa zote zipo kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa zao zote zipo na malipo watayapata pale walipo kwa kadri wanavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na utaratibu wa malipo kwa watumishi wa huduma za afya, ni zoezi endelevu na Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa kuhakikisha watumishi wanaofanya kazi masaa ya zianda wanalipwa kwa wakati. Kwa kweli hali kwa sasa inaendelea kuimarika na mpango huu ni endelevu, tutahakikisha kwamba tunatafuta fedha kwa wakati na kuhakikisha kwamba watumishi wale wanapata haki zao kwa wakati.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kata ya Kilungule, Jimbo la Mbagala wananchi wamejenga Kituo cha Polisi kwa nguvu zao, lakini sasa ni mwaka wa tatu Serikali haijafanya juhudi ya kufungua kituo hicho. Je, ni lini Wizara italeta watumishi ili kituo hicho kifanye kazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo hiki vilevile nakifahamu nakumbuka wakati ambapo tunaanza jitihada za kujenga hiki tulishiriki kufanya harambee. Niwapongeze sana wananchi walioshiriki lakini niwahakikishie kwamba juhudi hizo za wananchi hazitapotea bure kwa vituo vyote ambavyo wananchi wametoa nguvu zao, basi Serikali tutaangalia kadri itakavyowezekana, hali itakaporuhusu tuweze kuvikamilisha.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali; je, sasa kwenye Ajira Portal ni lini mtaongeza key ambayo itam-pick yule kijana ambaye amejitolea ikawa ni sifa ya nyongeza katika kuajiriwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA
UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kurejea tena kwenye maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wakati anafunga mjadala wa hoja ya Wizara yetu wakati wa bajeti. Alieleza na ninaomba ni- quote kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alieleza kuwa; Serikali imeyachukua maoni yote yaliyotolewa na Wabunge, na kwamba tunakwenda kuyafanyia kazi na utakapofika muda wa kuwashirikisha Wabunge kama wadau kwa kutoa maoni juu ya mfumo mzuri wa kutoa ajira kwa vijana wetu ambao mawazo mazuri kama haya anayoyatoa Mheshimiwa Mbunge yataingizwa ndani yake, tutakuja kulishirikisha Bunge lako na Wabunge watapata nafasi hiyo ya kueleza yale yote ambayo wanayataka yaingie katika mfumo.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali katika Bajeti yake ilipitisha posho ya Watendaji wa Kata ya kila mwezi, lakini posho hii imeonekana ni hisani. Baadhi ya Halmashauri zinalipa zingine hazilipi.

Je, Serikali mna tamko gani kuhusu posho hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, posho hizi zilipitishwa kwenye bajeti na Bunge hili Tukufu na tutaenda kuhakikisha kwamba linatekelezwa kwa sababu tayari zilitengwa ili Watendaji hawa waweze kupata posho hizi za madaraka.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, wale ambao walipewa namba za NIDA kabla ya tarehe ya GN Namba 96 ya Mwaka 2023, vitambulisho vyao vitatoka vikiwa na ukomo au vitakuwa havina ukomo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kuleta uelewa kwa wananchi ili wajue kwamba vitambulisho vyao ambavyo vimekaribia kuwa na ukomo na ambavyo vina ukomo havitawaathiri ili kupunguza taharuki iliyo kwa wananchi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitambulisho ambavyo vitakuja baada ya tangazo hili havitakuwa na ukomo lakini hata vile vitambulisho ambavyo vimekuja kabla ya tangazo wataendelea. Kwa sababu lengo la Serikali hii ni kuhakikisha kwamba vitambulisho haviwezi kuwafanya watu wakakosa huduma zao muhimu. Kwa hiyo ndio maana tukasema kwamba vitambulisho ambavyo vitakuja baada ya tangazo hili havitakuwa na ukomo, lakini hata vile ambavyo tunasema vimeshakwisha muda navyo vilevile vitaendelea kutumika kuwapatia wananchi huduma mpaka pale Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itakapotoa maelekezo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipi wananchi watafikiwa na taaluma hiyo. Kwanza kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Waziri ameshatoa tangazo kupitia vyombo vya habari kama vile televisheni, redio na magazeti. Nadhani wengi ambao wanakwenda kwenye mitandao huko wameona, lakini kikubwa tumeshatoa maelekezo na tupo tayari muda wowote tunaweza tukaanza mafunzo kwa watendaji wote wa NIDA kuwapa maelekezo na mafunzo ili sasa waanze kuwafundisha wananchi ili wananchi waweze kujua huu mchanganuo wa kipi kimekwisha ukomo na kipi hakitakwisha ukomo na kipi kitatumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali na niwapongeze kwa juhudi mnazofanya za TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona sasa hivi kuna utaratibu wa viongozi wa aina moja au Maofisa wa aina moja kufungua group na kutumiana document za kiserikali ndani ya group. Je, hiyo sheria mliyoitunga imejua na hiyo kwamba imo huo au haimo?

Je, kama haimo na hairuhusiwi mnafanya nini ili sheria i-accommodate ili kuwaepusha wanaotumia huo mtandao wasije kupatwa na matatizo ya kuhukumiwa na hiyo Sheria ya kuwa na Nyaraka za Serikali kwa sehemu zisizo husika. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly James Ntate, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inayosimamia nyaraka za Serikali inaelekeza wazi kwamba mawasiliano ya Serikalini yafanyike kwa njia ya barua lakini haielekezi vinginevyo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako kwamba haitokuwa sawa na ni marufuku ya Serikali kuwasilisha au kutumiana document za Kiserikali kupitia njia ya WhatsApp na njia nyingine zisizo rasmi isipokuwa kwa yale maelekezo ambayo yatakuwa yametolewa vinginevyo katika mamlaka.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tunajua mtumishi kabla hajastaafu ana miezi sita ya kumwandaa kustaafu. Je, ni nini sasa tamko la Serikali kuandaa mapema hayo malipo ya kusafirisha mizigo ya wastaafu ili wasiendelee kunyanyasika kama ilivyo sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama nilivyosema mwanzo ni kweli moja ya changamoto ambazo huwa zinakuwepo ni kwa wale ambao wanastaafu lakini bado kwenye bajeti yetu hatujaweka. Kwa sababu, ni kweli kwamba wanaostaafu wanajulikana, dhamira ya Serikali yetu ni kuhakikisha wote wanalipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunahakikisha kila unapotokea mwaka husika ambao wanaastafu wanawekwa kwenye bajeti za Serikali ili kulipwa kwa wakati bila kufanya ucheleweshwaji wowote kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itarejesha utaratibu wa mafunzo elekezi ya uongozi, utawala bora na uadilifu kwa watumishi ambao wamefikia ngazi ya Afisa Mkuu ili wanapopata nafasi za uteuzi waweze kutumika ipasavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma na Sheria ya Utumishi wa Umma pia Ibara ya 4 hadi Ibara ya 8 inampa mamlaka Katibu Mkuu Kiongozi kuweza kuhakikisha kwamba utumishi wa umma unakuwa ulio bora na ambao unakwenda na weledi lakini pia ambao unaweza kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, nataka kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako, kwamba Serikali imeendelea kufanya utaratibu wa kutoa mafunzo kwa watendaji wote au watumishi wote ambao wanakuwa katika ngazi za uteuzi ili kuweza kuwa katika viwango bora vya kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nataka kumhakikishia kwamba hilo jambo au maombi ya Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuyafanyia kazi na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunakuwa na utumishi ulio bora kama ambavyo sheria inamtaka Katibu Mkuu Kiongozi.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunajua wanaotakiwa kuajiri Serikali Kuu ni Menejimenti hya Utumishi kupitia Sekretarieti ya Ajira; je, ni lini Serikali sasa itachukua hilo jukumu badala ya kuachia idara zinazojitegemea? Kuachia Wizara nyingine kuajiri watumishi wa Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali iliamua kugatua baadhi ya mamlaka yake na kupeleka kwenye Taasisi na Wizara mbalimbali ili kupunguza lile lundo la watu wote kuja katika sehemu moja, lakini pia tukizingatia professional katika uajiri, lakini mawazo anayotoa Mheshimiwa Mbunge ni mawazo ambayo hata sisi ndani ya Wizara tunayaangalia, lakini nataka nikuhakikishie kwamba mambo yote haya yanakwenda kisera, kimkakati, na baada ya kujiridhisha kwamba tutakapoyachukua kuyarudisha Wizarani au kuendelea kufanya katika njia nyingine yatakuwa na tija kwa ajili ya kusaidia Watanzania inapofika kwenye jambo zima la ajira.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mawazo yako ni mazuri, na sisi kama Wizara tuyachukue na kuendelea kuyafanyia kazi na tutakuja kujulishana vizuri baadae. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali za kufungua kituo hiki siku nne zilizopita, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tishio la panya road waliojaa Dar es Salaam, Serikali haioni haja ya kituo hiki kufanya kazi masaa 24 kama jibu linavyosema, badala ya masaa nane ambayo kinafanya sasa hivi kuanzia saa tatu mpaka saa nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni haja Kituo cha Kiburugwa kwa kata ya jirani kukikarabati ili kiendane na mazingira bora ya watumishi wa Polisi kufanyia kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ntate Mbunge wa Viti Maalum Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; hili la kufanyakazi saa 24 ndiyo maagizo ya wizara na ni maagizo ambayo IGP ameyapokea na kuelekezwa kwa viongozi wa Polisi Kanda, Mkoa na Wilaya za Dar es Salaam. Kwa hiyo, nitasisitiza kwamba hili lifanyike kwasababu tayari kuna askari sita na mkaguzi mmoja ambaye ni Mkuu wa Kituo hicho hakuna sababu zozote za msingi za kufanya kazi chini ya masaa ishirini na nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukarabati kituo cha Kiburugwa kama alivyokwishasema Mheshimiwa Mbunge nakubaliana nae baadhi ya vituo vilivyo katika hali mbaya vinahitaji kukabaritiwa hii ni moja ya kuweka mazingira bora ya askari wetu kufanya kazi lakini pili kuwahudumia hawa ambao wanapelekwa vituo wawe katika mazingira bora zaidi. Kwa hiyo, nakubaliana na wewe Mheshimiwa tutatafuta fedha kwaajili ya kukabarati vituo vilivyochakaa kikiwemo hiki cha Kiburugwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuangoma ni Kata yenye mkusanyiko wa watu wengi sana na kata hiyo haina Kituo cha Polisi. Je, ni lini Mambo ya Ndani mtajenga Kituo cha Polisi pale Kata ya Tuangoma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tuangoma ni moja ya Kata za Jiji la Dar es Salaam ambao haina Kituo cha Polisi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na especially Mbunge wa Jimbo achangie kidogo na kuhamasisha wadau kushiriki ili Serikali ije isaidiane nanyi kukamilisha, kama ambavyo maeneo mengine wamefanyakazi hiyo. Nashukuru sana.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tuangoma ni Kata yenye mkusanyiko wa watu wengi sana na kata hiyo haina Kituo cha Polisi. Je, ni lini Mambo ya Ndani mtajenga Kituo cha Polisi pale Kata ya Tuangoma?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janejelly Ntate Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Tuangoma ni moja ya Kata za Jiji la Dar es Salaam ambao haina Kituo cha Polisi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na especially Mbunge wa Jimbo achangie kidogo na kuhamasisha wadau kushiriki ili Serikali ije isaidiane nanyi kukamilisha, kama ambavyo maeneo mengine wamefanyakazi hiyo. Nashukuru sana.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado kuna hela nyingi ziko pale kwenye hizi TRAT na TRAB. Kuna shilingi bilioni 600 zipo TRAB na shilingi trilioni 2.29 bado zipo TRAT.

(a) Je, Serikali mnatupa muda gani wa kuwa mmemaliza hizi hela zirudi kwenye Mfuko wa Serikali zikafanye kazi za maendeleo? (Makofi)

(b) Katika kuchelewesha huku na kusuasua, hamuoni kwamba tunaharibu mahusiano mema ya Serikali na wafanyabiashara ambao ndiyo tegemeo letu la mapato? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia jambo hili ambalo ni muhimu sana na amejenga hoja za Kibunge. Niliyaepuka haya maneno ya TRAT na TRAB lakini kwa kuwa ameshayasema ngoja niyasema tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja; fedha zile ambazo zipo zinabishaniwa kabla hazijaamuliwa haziwi fedha za Serikali ni fedha zinazobishaniwa, na katika kubishaniwa kwake na hivi sasa tumeanzisha Ofisi hiyo ya Msuluhishi, kimsingi Serikali inataka kujenga mahusiano mazuri na walipakodi, kwa sababu Serikali ingenyoosha mkono tu kwamba hapa tunachokadiria sisi ndiyo tunataka ulipe, hiyo ndiyo ingeharibu mahusiano na walipakodi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo zitakuwa fedha za Serikali mpaka pale ambapo mkono mwingine whether TRAB ama TRAT itakaposema kwamba hii sasa ni fedha ya Serikali, lakini ikiwa bado inabishaniwa Serikali inatoa fursa ya haki kutendeka na vyombo hivyo vinaongozwa na watu ambao ni maarufu katika tasnia ya sheria. Kwa hiyo, tunaamini haki itaendelea kutendeka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuharakisha ndiyo tumetengeneza utaratibu wa kuanzisha hizi sessions maalum ili haya mambo yasiwe yanakaa sana, kwa sababu yanaondoa utulivu katika ufanyaji wa biashara.

Mheshimiwa Spika, lingine kama ambavyo nimeweka kwenye jibu la msingi, uwepo wa ofisi hii ambayo wafanyabiashara wameitamani siku nyingi ya Msuluhishi wa Masuala ya Kikodi, tunaamini na yenyewe itaenda kupunguza mrundikano wa masuala yanayobishaniwa kwa sababu sasa maeneo ambako makadirio hawakuridhiana yataenda kwa mtu mwingine ambaye hayuko kwenye mfumo ule wa kukadiria.