Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Janejelly Ntate James (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JANEJELLY J. NTALE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa jicho lako kuniona, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kuwa mmojawapo wa Bunge la Kumi na Mbili. Lakini niwashukuru wakinamama wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam na Baraza Kuu la UWT Taifa na wajumbe wengine wako humu ndani ya Bunge kwa kuniamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nishukuru Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama pekee kinatupa nafasi watumishi wa Serikali ndani ya Bunge hili, ahsanteni sana. Lakini nimesoma risala zote mbili, Mheshimiwa Rais anaongelea maboresho ya watumishi na maslahi ya watumishi, tunashukuru sana alivyohamishia Serikali Dodoma ametekeleza kilio cha watumishi wa Serikali na vyama vyao ambavyo tulikuwa kila siku tukishauri hilo, tunamshukuru sana.

Lakini tumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye alisimamia zoezi hilo aliposema kila mtumishi kuondoka Dar es Salaam ahakikishe akaunti yake imesoma, tunakushukuru sana. Lakini tunampongeza Rais kwa jinsi alivyojenga mji wa Kiserikali Mtumba, mji huo umeleta mahusiano kazini kwa kufanya Wizara kati ya mtumishi na mtumishi kufahamiana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais kwenye risala yake anasema ataboresha maslahi ya watumishi, lakini niombe kushauri ili maslahi ya watumishi yaboreshwe turudi kwanza tuangalie sheria za kiutumishi, kuna baadhi ya sheria yatafanya zoezi hili liwe gumu. Kuna sheria moja inaitwa sheria ya re-categorization…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ntale ukae chini upokee taarifa, Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sababu ya muda nitaenda kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Ntale ningependa kukupa taarifa kwamba umesema Chama cha Mapinduzi ndiyo cha pekee kutoa fursa kwa watumishi wa umma, ujue kwamba tulikuwa tuna Mbunge anaitwa Dkt. Sware Semesi alikuwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu, alikuwa ni Mbunge wa CHADEMA, alikuwepo mama Lyimo alikuwa ni Chancellor wa Chuo Kikuu pale alikuwa ni Mbunge wa CHADEMA, mimi peke yangu nilikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni Mbunge, kwa hiyo usipotoshe, na wengine wengi.

SPIKA: Mheshimiwa Janejerry James Ntale unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JANEJELLY J. NTALE: Mheshimiwa Spika, naomba nisiipokee hiyo taarifa kwenye Chama cha Mapinduzi kimetenga nafasi mbili kabisa kwamba ni nafasi za watumishi wa Serikali kutoka kwenye vyama vya wafanyakazi na humu ndani tuko wawili mimi na Dkt. Alice, sipokei hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naongelea sheria ya re- categorization. Sheria hii kama haijaumiza mtumishi yeyote aliyehumu itakuwa imeumiza mtoto wako au mpiga kura, ile sheria mtumishi akijiendeleza, akiomba kufanyiwa re- categorization anashushwa mshahara na kwenda kuanzia kwenye cheo kile cha wale wengine waliopo.

Mheshimiwa Spika, binafsi sisi hatupingi mtu kwenda kuanzia pale wanapoanzia wataalam wale, lakini aachwe na mshahara wake. Kwa sababu nimefanyakazi Wizara ya Fedha kila mtumishi ana budget line yake ya mshahara huyu mtumishi hakuna anapoongeza bajeti, mshahara wake unakuwa ni ule ule, alichobadilisha ni kada, niombe hiyo sheria, Menejimenti ya Utumishi wa Umma mkaiangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Jenista ni shahidi tumekuwa tukikulilia kilio hiki cha sheria hiyo inaumiza sana watumishi. Lakini kuna na miundo ambayo siyo rafiki tena kwa watumishi, leo hii Mheshimiwa Rais tunamshukuru ameunda Wizara ya TEHAMA.

Lakini kwenye muundo wa ma-executive assistant ambao ndiyo wasaidizi wenu bado wamekamatwa na hati mkato.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANEJELLY J. NTALE: Mheshimiwa Spika, naona muda umeniiishia lakini nitalileta kama swali naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uweza wa kusimama hapa. Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sikumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyojipambanua kwamba yeye maendeleo kwake hayana itikadi za kivyama. Kama angefuata itikadi za vyama maendeleo tunayoyasema Dar es Salaam yasingekuwepo. Dar es Salaam tunajua fika ilikuwa ni ngome ya wapinzani lakini amefanya maendeleo ya barabara, maji, elimu iliyopelekea wananchi wa Dar es Salaam sasa nao kumlipa fadhila ya kuifanya Dar es Saalaam ya kijani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mpango, amekuja na Mpango kwelikweli kama jina lake. Hata hivyo, Mpango huu wanaohusika ni wataalam wake ambao ni rasilimali watu. Mimi nijikite kwenye rasilimali watu. Haya yote tunayoongea humu, yote tunayojadili humu, wanaoenda kuyatekeleza ni rasilimali watu, ni watumishi wetu, lakini kuna sehemu hawa watumishi hawatoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waheshimiwa Wabunge wamesema kuhusu kilimo, lakini ukiangalia nchi ina shortage ya Maafisa Ugani 6,000 badala ya 12,000. Sasa hawa 6,000 hawawezi kutumika kwa nchi kumfikia kila mkulima, suala hili tuliangalie kwa makini. Hata hao waliopo vitendea kazi walivyonavyo ni vichache sana. Tumesikia kuna Kata zina vijiji 15, lakini Afisa Ugani huyu hata baiskeli hana, atamfikiaje huyu mkulima? Kama kweli tunataka kilimo kiwe ni uti wa mgongo, tuwaangalie hawa Maafisa Wagani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajivunia GePG ambapo mtandao uliotengenezwa na watumishi wetu wa Serikali. Hii ni software tungekuwa tunainunua kwa wataalam wengine ingetumia bilioni za fedha. Kwa hiyo, tuwaendeleze hawa watumishi wetu kielimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi imefikia wakati watumishi wanaogopa kwenda kusoma kwa sababu ya nyaraka zinazotoka utumishi. Mtumishi sasa hivi akienda kusoma, anaambiwa muda wake alioenda shule hautahesabiwa kwenye promotion yake. Sasa tunaenda kuzalisha wale walioenda kusoma na aliyebaki akaendelea na ule muundo anakuwa mwandamizi, yule aliyetoka na elimu yake anakuwa junior kwake. Sasa hii inapunguza utendaji kazi ndani ya Serikali. Huyu mwenye elimu kubwa angemshauri huyu lakini sasa huyu ni mwandamizi kwake, atamshaurije na huyu ni senior wake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Utumishi niwaombe, tuangalie hizi nyaraka. Kuna sheria za kiutumishi, lakini nyaraka ndani ya sheria za kiutumishi zimekuwa nyingi mno, zinaleta mkanganyiko. Sasa hivi mtumishi ukimwambia nenda kasome ataleta sababu zisizo na msingi, lakini ukimfikia kwa karibu anakwambia ngoja kwanza nipande kwenye huu muundo nifikie daraja la uandamizi ndiyo nitaenda kusoma lakini sasa wanadumaa na utaalam unabadilika kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuiangalia hii miundo, tutabaki tunawalaumu wataalam hawafanyi kazi lakini kumbe kuna kitu kimewakwamisha. Naomba tuliangalie hili kwa umakini. Tuna vijana ambao ni wazalendo wa kweli. Mfano ni hii Wizara ya Fedha ambayo imekuja na huu Mpango, wanakesha, wanaumiza vichwa kuja na Mpango kama huu, lakini sasa miundo inawakamata. Tuliangalie suala hili na kama tunataka nchi hii iendelee, tuwekeze kwenye rasilimali watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ana utashi kabisa wa kuwekeza kwenye rasilimali watu. Ukiangalia Ilani ya Uchaguzi imesema hivyo; ukiangalia hotuba yake hapa imesema hivyo; Mpango umekuja unasema hivyo, lakini je, tunatekeleza sisi tunaomsaidia? Nizidi kuiomba Menejimenti ya Utumishi wa Umma, hebu angalieni nyaraka zenu za kiutumishi, zimekwamisha kabisa haya maendeleo na huu Mpango wanaoenda kuutekeleza ni rasilimali watu hii hii. Tukiyafanya hayo, Tanzania inaenda kubadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami kama wenzangu wote nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wote na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondokewa na Rais wetu kipenzi, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kuwa mwanamke wa kwanza kuvunja na kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Nchi kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Mwigulu kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kupewa Wizara nyeti; Wizara ya Fedha na Mipango. Hongera sana. Vile vile nampongeza kwa Mpango ambao ameuwasilisha leo yeye na timu yake yote ya waatalam pamoja na Mwenyekiti wake wa Bajeti. Kwa kweli inatoa matumaini ya Taifa letu, tunaenda wapi kiuchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita katika sehemu ya uvuvi na kilimo. Nikianza na uvuvi, Tanzania ni nchi iliyobahatika sana. Tuna maziwa ya kutosha, mito na bahari, lakini bahati hii bado hatujaitumia. Tumeenda na kudra ya Mwenyezi Mungu tu kuvua samaki walio ziwani na baharini; lakini kama tukijikita kwenye vizimba kufuga kitaalam Mheshimiwa Waziri atapata mapato ya kutosha na ugomvi kati ya Serikali na wananchi kwa uvuvi haramu utakuwa umekoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sehemu hii Serikali ijikite kutoa hela za kutosha, Wizara husika ndiyo itafute maeneo na kujenga vizimba. Vizimba hivyo wananchi wakodishwe kufuga. Nilikuwa napiga mahesabu, lakini mimi sio mtaalamu wa hesabu; ila tukiweka vizimba hivyo kila baada ya miezi sita tunavua Samaki, tena ambao siyo wa kupima na rula, kwa sababu amefikia kiwango kinachotakiwa. Vile vile hapa tutapata kodi, hapa tunawainua akina mama na vijana, watapata ajira kutokea pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi Jirani, Uganda nimetembelea mwenyewe vizimba vya akina mama. Mwanamama anakwambia kwa mwaka ana uwezo wa kutengeneza shilingi milioni 200 au shilingi milioni 15, lakini sisi Tanzania tumekaa tu. Naiomba Serikali, nakuamini Mheshimiwa Mwigulu na Waziri wa Uvuvi, tuchukue hatua, wakati ni sasa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba tunaukalia uchumi, nasi tumeukalia uchumi kwenye hili la uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wenyewe, ukiamua wewe mwenyewe kutafuta vizimba, kuna idara inaitwa ya Idara ya Mazingira; unaambiwa hapa mazingira hayafai, hapa hayafai, lakini kwa Waganda inafaa vipi? Tunakosea wapi hapa? Sasa sisi tunaiomba Wizara husika, yenyewe ndiyo ishirikiane na Idara ya Mazingira, wote ni Serikali moja, watuambie kwamba maeneo kama haya hamtaharibu mazingira, weka vizimba, fuga Samaki. Mheshimiwa Waziri utapata mapato ya kutosha pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri, kwenye bajeti ijayo Mheshimiwa Waziri tenga ruzuku, tupe akina mama na vijana tukaweke vizimba kule tukutengenezee mapato na tuinue uchumi wa Tanzania. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo, toka uhuru mpaka leo bado tuko kwenye kilimo cha jembe, hatujawahi kutoka hapo, lakini tunasema kilimo ndiyo uti wa mgongo, kilimo ndiyo asilimia 70 ya Watanzania tuko pale, kilimo ndiyo kinagusa kila Mtanzania, ndiyo tumekiweka mbali na Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Kilimo. Tumetembelea miradi kama Kilosa, lakini ukiangalia kidogo kwenye sehemu ya umwagiliaji waliyoijenga pale na mazao yanayotoka pale na tumebahatika maziwa na mito ya kutosha, lakini bado hatujaingia kwenye kilimo cha umwangiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kilimo hicho tukiingia, mbegu hakuna. Kilio cha mbegu kimekuwa kikubwa sana. Hakuna mbegu za kutosha, hakuna wataalam wa kutosha, kwa hiyo, kwenye kilimo tunakwama hapo. Ushauri wangu tu, niishauri Serikali sasa ijikite kwenye kilimo cha umwangiliaji, lakini ijikite kabisa kwenye uzalishaji wa mbegu, tena ambazo ni za kiwango kwa kutumia utafiti, tutenge bajeti ya kutosha ya utafiti wa mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuhakikishe tunaajiri Wagani wa kutosha, hawapo. Leo hii kuna Kata nyingine zina vijiji 15 na mgani ni mmoja; lakini kwa sababu yuko TAMISEMI, wanamwambia utakaimu Utendaji wa Kata. Tumeyaona haya. Sasa Ugani anaufanya saa ngapi? Akishaenda kwenye Utendaji wa Kata, kule kuna kusimamia kuuza mashamba na kadhalika, Ugani anaacha, anaomba recategorization akawe Mtendaji wa Kata, tunawakosa Wagani namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado hata yule ambaye amejitahidi kulima yeye mwenyewe, masoko hakuna. Kuna kipindi ilitangazwa hapa zikalimwa mbaazi Tanzania kwamba zitaenda India, lakini matokeo zilipelekwa mpaka kwenye vituo vya shule kuwapikia wanafunzi, India hazikuwahi kwenda. Sasa tunakwama wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo na uvuvi, vitu hivi tukivishika, tukaviwekea mkakati kama tulivyoweka kwenye miundombinu ya barabara, Tanzania tutafika mbali. Huo ndiyo ulikuwa ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)