Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwanakhamis Kassim Said (4 total)

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa wazee hawa walifanya kazi kwenye Serikali hii, walitumia vigezo gani kuwa walipwe kiinua mgongo na wasilipwe pensheni yao ya kila mwezi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Je, Waziri yuko tayari kwa ruhusa yako kuungana nami kwenda kuwaona wazee hawa kuwapa maneno mazima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. HAMAD HASSAN CHANDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said wa Jimbo la Magomeni kwa juhudi yake ya kufuatilia wazee kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo ambavyo tumetumia ni Kanuni, Taratibu na Sheria ambazo zimewekwa na kama hatukutumia vigezo hivyo, basi ingekuwa ni kinyume na taratibu. Hivyo basi, Serikali bado iko na usikivu. Serikali yetu ni sikivu, Mheshimiwa Mbunge anao uwezo wa kupeleka malalamiko tena na tutayazingia kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Swali la pili, niko tayari kabisa mimi na Waziri wangu kufuatana naye kwenda kushuhudia jambo hilo, Inshaallah. (Makofi)
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, majibu anayoyajibu Mheshimiwa Waziri, mimi sina, sijayaona kwenye swali langu. Hapa sikuuliza sheria kwa sababu sheria haina matatizo, wale watekelezaji wa sheria ndio wenye matatizo.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na jibu la msingi ambalo ni zuri kama alivyolieleza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wasimamizi wa sheria ni pamoja na Jeshi la Polisi, na huenda dhamana anazozikusudia ni zile ambazo zinatolewa na Jeshi la Polisi lakini watu hawatoki. Jambo la msingi ambalo tumelifanya Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia IGP ni kuwataka RPCs, OCDs na wale wakuu wa vituo (OCSs), kukagua mara kwa mara mahabusu zetu na kuona watu waliomo ndani na sababu gani zimesababisha awe ndani ili waweze kuachiwa kama hakuna sababu za msingi.

Mheshimiwa Spika, lakini tumebaini pia kwamba kuna baadhi ya watu wanawekwa ndani hata ndugu zao wanagoma kuwawekea dhamana, na hii ni kwa sababu ya matukio ya mara kwa mara yanayojirudia kiasi kwamba yanafedhehesha jamii. Kwa hiyo, niwaombe pia ndugu wawe wepese kuwadhamini kwa wale ambao dhamana zinakuwa wazi.

Mheshimiwa Spika, tumewasisitiza wakuu wa vituo pale inapowezekana kwa makosa yanayodhaminiwa waweze kutoa dhamana. Na kama Mheshimiwa Mbunge ana jambo specific, niko tayari kukutana naye baada ya kipindi cha maswali na majibu ili tuweze kuambiwa halafu tuone ni kitu gani kilichokwama, nashukuru. (Makofi)
MHE. MWANAKHAMISI KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kuna wananchi wanapata matatizo panapokuwa na kesi za jinai, lakini wanapokwenda baadhi ya vituo wanakuwa hawapati huduma hizi wanaambiwa pale hawahusiki, waende kituo kingine.

Je, Serikali iko tayari kukifuta kifungu hiki ili wananchi pale wanapopata matatizo wapate huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, hatuna kifungu chochote cha kisheria kinachozuia mwananchi aliyebaini uwepo wa kosa la jinai kuzuiwa kuripoti kwenye Kituo chochote cha Polisi.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuelekeza kwamba ikiwa itatokea raia au mwananchi anapewa majibu hayo na askari wetu yeyote, atoe taarifa kwa Mkuu wa Kituo au Ofisa Upelelezi wa Wilaya au Mkuu wa Polisi wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu nielekeze IGP atoe mwongozo kwa Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa ili kama kuna udhaifu wa namna hii uelekezwe kwamba kuondolewe msingi wa kuzuia mwananchi kutoa taarifa kwenye Kituo chochote cha Polisi, nashukuru.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha Ligi ya Muungano?

Swali langu la pili, je, ushirikiano wa ZFF na TFF unasaidia Soka la Zanzibar la Wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha Ligi ya Muungano inaanzishwa upya na tunafahamu umuhimu wake kwenye kuimarisha ushirikiano hasa kwenye upande wa michezo. Kwa hivyo, kwa nyakati tofauti TFF na ZFF wamekuwa wakikaa kuangalia namna bora ya kuianzisha tena Ligi ya Muungano, japokuwa wanapata changamoto kwenye kupata udhamini wa kulifanya hili lakini nikuhakikishie dhamira ipo na tutahakikisha Ligi ya Muungano inaanza tena.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Ligi ya Wanawake, TFF na ZFF zimekuwa zikiendesha program mbalimbali za kiutawala na makocha wanawake kwa Soka la Zanzibar na unaweza kuona miongoni mwa mafanikio ambayo yameshapatikana ni kwa timu za wanawake za Zanzibar kufanya vizuri kwenye mashindano ya CECAFA. Nakushukuru. (Makofi)