Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwanakhamis Kassim Said (5 total)

MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa waliokuwa Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano waliostaafishwa kwa maslahi ya Umma tarehe 30 Juni, 1996?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. HAMAD HASSAN CHANDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said wa Jimbo la Magomeni, Zanzibar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais ilipokea malalamiko ya wastaafu saba waliopunguzwa kazini kwa manufaa ya Umma mwaka 1996. Baada ya uchambuzi wa suala hili na kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango, ilibainika kwamba stahili zao zote zilishalipwa kipindi walipostaafishwa. Hivyo, hawastahili kulipwa pensheni kutokana na masharti yao ya ajira, bali walilipwa kiinua mgongo cha mkupuo ambacho ni stahili ya watumishi walioajiriwa chini ya masharti ya “Operational Services.” Hii ni kwa mujibu wa Kanuni Na. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi Serikalini za Mwaka 1994 na Sheria Na. 36 ya Mwaka 1964 (The National Provident Fund Act).
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzana na Wakazi wa Kijiji cha Dunga – Zanzibar?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la Kambi ya Dunga 141KJ limejumuishwa katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Wizara wa Kutatua Migogoro ya Ardhi wa 2020/2021 – 2022/2023 unaoendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, upimaji na uthamini katika eneo hili ulianza tarehe 19 Aprili, 2022 na umemalizika tarehe 25 Aprili, 2022. Hatua zinazofuata ni kuwasilisha kitabu cha uthamini kwa Mthamini Mkuu wa Zanzibar kwa ajili ya idhini na kisha kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa uhakiki na malipo ya fidia. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge avute subira, kwani mchakato umefikia hatua nzuri na Wizara imedhamiria kumaliza migogoro yote ya ardhi kati ya taasisi zake na wananchi.
MHE. MWANAHAMIS KASSIM SAID aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza tatizo la watuhumiwa kutopewa dhamana kwa makosa yenye dhamana?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dhamana katika kesi za jinai ni haki ambayo imewekewa utaratibu wa kisheria. Kwa mujibu wa sheria zetu yapo makosa yanayodhaminika na yapo makosa ambayo hayana dhamana. Kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura 20 kimeainisha makosa yote ambayo hayana dhamana. Hivyo, kwa makosa yote ambayo hayajatajwa na kifungo hicho yana dhamana ambayo ni haki ya mshtakiwa.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, kwa nini Jeshi la Polisi haliondoi zuio la kuwahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma kwenye vituo nje ya maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Namba 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kikisomwa pamoja na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) Namba 309, mtu yeyote aliyetendewa au anayefahamu jinsi kosa lilivyotendeka au linavyotaka kutendeka anatakiwa kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi kilicho karibu na taarifa hiyo itachukuliwa na kufanyiwa kazi. Hivyo, hakuna zuio lolote la kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za polisi kwenye vituo vilivyo nje na maeneo yao, nashukuru.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, TFF inashirikianaje na ZFF kupandisha hadhi Ligi ya Zanzibar na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Jimbo la Magomeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekuwa ikishirikiana na ZFF katika mipango mbalimbali kwa lengo la kuendeleza Soka la Tanzania. Kwa sasa Bodi ya Ligi ipo katika mchakato wa kuandaa mafunzo ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi ya Zanzibar ambayo kimsingi yatalenga namna ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi katika masuala ya menejimenti, ligi na masuala ya uwekezaji, udhamini na masoko.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kuibua vipaji, TFF imekua ikishirikiana na ZFF katika uteuzi wa wachezaji katika timu za Taifa za Vijana, ambapo vijana kutoka Zanzibar wamekuwa wakiitwa katika vikosi vya timu ya Taifa ya vijana na hatimaye kucheza katika timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars), ahsante.