Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwanakhamis Kassim Said (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Leo tunazungumza ni mwaka 57 wa Muungano wetu na tunasema Muungano huu tutaulinda na tutautetea na ndipo tunapozungumza tunasema mbili zatosha, tatu za nini. Leo toka tulivyoanza kuchangia Muungano huu Wazanzibar ndiyo tumepangwa kuchangia. Kwa kweli inasikitisha na inaumiza kwa sababu huu Muungano siyo wa Wazanzibar peke yetu ni Muungano wa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukizungumza hapa ukisema leo ni miaka 57 Muungano huu asilimia kubwa sisi viongozi wenyewe hatuujui na tunashindwa kuuzungumzia, zaidi tukizungumzia Muungano tutauzungumzia kisiasa, kumbe Muungano huu ni tunu ya nchi yetu; ni moyo wa nchi yetu; ni mishipa ya nchi yetu. Sisi tunasema tunatoka Zanzibar lakini na sisi vitovu vyetu vipo huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi baba ni Mpemba, mama ni Mzaramo. Tunapouzungumzia Muungano lazima tuuzungumzie Muungano wa Watanzania; tuzungumzie Muungano wa wanyonge na tumzungumzie mtu wa chini.

Leo unapokwenda mikoani; utamkuta mwananchi kutoka Mtambwe lakini yupo Shinyanga na Shinyanga kule amewekeza kiwanda cha mchele lakini kuuzungumza Muungano kusema hajui, kwa sababu gani? Ni kwa sababu hatupewi elimu, wala wananchi hawapewi elimu kuhusu Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo unapokwenda mikoani, utamkuta mwananchi kutoka Mtambwe, lakini yupo Shinyanga; na kule amewekeza kiwanda cha mchele, lakini kuuzungumza Muungano, kuusemea hajui. Kwa sababu gani? Kwa sababu hatupewi elimu, wala wananchi hawapewi elimu ya Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye utalii tunapeperusha vipeperushi vya utalii. Kwa nini na Muungano tusipeleke vipeperushi wananchi wakaufahamu Muungano huu? Tumenyamaza zaidi! Leo tunanyanyuka kuzungumza Habari za Muungano, tunashindwa. Tunazungumza zaidi kisiasa, lakini kuuzungumza ile ilivyo, tunashindwa. Wapi tunafaidika, hatupajui; wapi tunakosea, hatujui; wapi tunapokwenda, hatujui. Tutayazungumza yale madogo madogo, lakini na makubwa yapo yanaumiza.

Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu, Jimbo la Magomeni kuna wanawake hawana uwezo wa kwenda China, China yao ni Kariakoo, wanakwenda kuchukua madera, khanga, viatu wanaleta Zanzibar. Utakuta amekwenda na mwananchi kutoka Mwanza, atachuka mzigo wake ule atakwenda kuuza Mwanza, lakini mwanamke anayetoka Zanzibar Magomeni, anateseka akifika bandarini. Muungano huo, miaka 57, tunaomba mambo haya mdogo madogo yaondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi sisi ni wamoja, ni ndugu, ni wazaliwa wa damu moja na tumbo moja, wa baba mmoja. Wameshapita viongozi wengi katika nchi hii, lakini bado wanasema wataulinda na watautetea kwa nguvu zote. Nasi tunasema tutaulinda na tutautetea kwa nguvu zote. Tunasema mbili zatosha, tatu za nini? Hatuoni haya, hatuoni aibu wala hatujuti, tunasema Muungano utaendelea kwa yeyote atakayekuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, Mheshimiwa Marehemu Dkt. Omary Ali Juma alikuwa ni Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alikuwa Waziri Kiongozi miaka minane, akawa Makamu wa Rais miaka saba. Alizikwa vizuri, kwa heshima zote, tunashukuru; lakini leo ukienda kwenye kaburi la Marehemu Dkt. Omary, inauma sana. Kwa kweli inatusikitisha. Mheshimiwa Dkt. Omary aliitumikia nchi hii kwa nguvu zake zote, hakuna ambalo hakujua. Alikuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Dkt. Omary kaburi lake lina uzio wa waya toka laipozikwa hadi leo. Maana kaburi lile utasema siyo Makamu wa Rais, kama nililozikwa mie tu, nikaenda nikazikwa, nikawekewa kuti, watu wakaondoka. Kwa kweli inauma. Viongozi wetu waliopita tunawaacha. Tunawadhalilisha. Hii inauma, inakera. Wao wameanza, imefikia hivyo, wengine itakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina zaidi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mimi leo sitawapongeza, nitawaombea, namuombea Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mwenyezi Mungu awape nguvu na afya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. Pia nichukue nafasi hii kumuombea Mheshimiwa Sirro na Kamishna wa Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, askari wetu wanafanya kazi ngumu sana, kwa kweli ni kazi ya kusikitisha. Asilimia kubwa ya Askari wa Jeshi la Polisi wanaostaafu ni nadra kuwakuta ni wazima. Askari wetu hawa wanafanya kazi ngumu wakistaafu wengi wana- paralyze. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana na ngumu na maeneo yao ya kazi siyo rafiki.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye vituo vya polisi Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza vipo kwenye hali ngumu lakini hata mazingira yao ya kazi wanapokuwa barabarani ni magumu. Wewe ni shuhuda leo ukiondoka kuanzia Dodoma kufika Dar es Salaam ni askari lakini jua, mvua wanapigwa askari wetu. Kazi yao ni ngumu sana, tutakaa tutawalaumu lakini askari wetu wanafanya kazi ngumu na kipato chao ni kigumu sana. Wapo askari siyo wazuri lakini kuna askari ni wazuri sana akiwemo Kamanda Sirro na Kamishna wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushahidi tosha ni wakati tunapofanya chaguzi. Askari wetu wanafanya kazi ngumu sana ya kudhalilishwa, kutukanwa, ni nusu kujuta kufanya kazi hii lakini hawana lingine la kufanya kwa sababu waliiomba kazi hii. Namuomba Mheshimiwa Waziri wawaone askari wetu kwa posho zao lakini na vitendea kazi. Sasa hivi unakwenda kwenye vituo kuripoti kesi ya ubakaji lakini unaambiwa hakuna gari wala hakuna askari kutoka pale kwenye kituo akamfuata mtuhumiwa, unaambiwa wewe kama unayo pesa utoe mafuta upeleke kule akachukuliwe mtuhumiwa. Mimi nahisi yote haya ni kwa sababu bajeti ni ndogo. Sababu ya vituo vyetu kuwa chakavu bajeti ni ndogo kwa sababu polisi si maskini wa wafanyakazi; wana wajenzi, watu wa umeme, nafikiri wana kila design ya mafundi, kwa nini wasipewe bajeti kubwa ya kufanya kazi zao wanakuwa ni watu wanyonge sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, turudi katika wale wanaostaafu, askari wetu wengi wanastaafu hawapati haki zao mapema. Unakuta askari kastaafu kama mwaka au miezi sita unamkuta ni omba omba. Haipendezi, inakera, inauma na wao ni binadamu kama sisi na wao ni wafanyakazi kama sisi, lazima askari wetu watunzwe wana kazi ngumu kutulinda sisi na mali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bora aombe kuliko kuiba. Wengi tunasema askari wanapenda rushwa lakini mimi nasema wasiombe rushwa ila kuomba ni haki kwa sababu hawaibi. Wanaomba kwa sababu wapo kwenye hali ngumu lazima tuungane bajeti ya watu hawa iwe kubwa, ni haki yao. Mimi nasema pesa hizi angekuwa nazo Sirro angewapa askari wote wakaneemeka au angekuwa Kamishna wa Zanzibar anazo pesa hizi angewapa askari wake wote wakaneemeka kwa sababu hataki waombeombe wala waombe rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo unawakuta askari wapo kwenye …

T A A R I F A

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Taarifa, endelea

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji anayeendelea kuchangia kwamba kuomba ama kutoa rushwa ni mwiko na ni kinyume kabisa cha sheria bila kujali mazingira uliyopo. Naomba Mheshimiwa mzungumzaji awatetee askari lakini asitee rushwa. (Makofi)

SPIKA: Pokea hiyo taarifa Mheshimiwa Mwanakhamis.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, sitetei rushwa, natetea askari wetu. Wengi tumezungumza hapa, wamesemwa wana vitendo vibaya, wanabaka, wanakera, wanaudhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri ni mwaka wa ishirini au na zaidi nipo kwenye siasa lakini sijawahi kukamatwa kupelekwa kituo cha polisi wala sijapelekwa magereza. Suala la magereza mimi sijui najua utendaji wa kazi wa askari wetu, kwa sababu sote humu tunapogombea anatulinda askari polisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana muda umeisha.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu chetu cha Quran mwanamke ametajwa mara tatu, mwanaume ametajwa mara moja, kwa nini sasa? Wengi tunamzungumza Mama Samia, tunampongeza kwa kazi nzuri alivyoanza, lakini mimi ninasema Mama Samia tumuombee dua usiku na mchana, huyu ni mama, huyu ni mwanamke. Nilisema Kitabu cha Quran mwanamke ametajwa mara tatu kwa sababu mama ndiye aliyebeba mimba, mama ni mlezi, mama ana upendo. Kwa hiyo, naomba Watanzania, Waheshimiwa Wabunge, tumuombee Mama Samia afanye kazi kwa kuwatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumuombea dua Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri waliyoanza kufanya, Mwenyezi Mungu awape nguvu na afya kwa kuitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge niliyetokea Zanzibar. Bajeti imezungumza vizuri sana, lakini bado nitasema kuna mambo yanayotutanza Wabunge tunaotoka Zanzibar. Mimi leo nilileta gari langu karibuni na barua hii hapa. Barua hii nimepewa nije na gari langu kuishi nalo Tanzania Bara kwa mwaka mmoja, wakati mimi ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkataba wangu nikiwa hai ni miaka mitano, leo nimepewa barua hii nikae na gari langu huku mwaka mmoja.

Je, tunamuuliza Mheshimiwa Waziri hii ni sheria au ni haki au ni nini? ama ni sisi tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili niulizie kuhusu ma-agent kutoa gari Zanzibar kuja Tanzania Bara. Tuelezwe huyu agent ana mchango kwenye Serikali au ni nini? Tuelezwe kwa kweli imekuwa ni mateso ni maonevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa wafanyabiashara wadogo-wadogo. Tunapenda sana wafanyabisahara wadogo-wadogo, vijana, akina mama na wazee, lakini vijana na wazee sasa hivi biashara zao wanafanyia katikati ya barabara, kwa kweli hii ni hatari maana hata Serikali inakuwa mapato inapoteza. Unakuta leo sado za nyanya zimepangwa barabarani, pana ujororo tu wa barabara tunaopita na magari, kwa hivyo naomba suala hili lishughulikiwe. Kwa kweli, wapangiwe nafasi, sehemu nzuri ya kufanya biashara zao wao wapate, lakini na Serikali ikusanye mapato vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Ilipopita bajeti Wabunge wengi tulizungumza kuhusu maliasili, kama hatukulisimamia suala la maliasili basi maliasili nafikiri baada ya muda mdogo itakuwa wanyama wetu wengi watapotea. Leo Mheshimiwa Mbunge anasimama anasema yeye tembo hana faida nae, ng’ombe ndiyo wana faida nao. Mimi naiomba Serikali lazima Wabunge wale waliopo pembeni mwa hifadhi wapewe elimu pia na wafugaji wapewe elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema tembo hana faida kwa sababu tembo ni mnyama aliyeumbwa hifadhi yake ni kukaa kwenye hifadhi, hatembei, hata ukimfuata tembo unamfuata nyumbani kwake. Kwa hivyo, mtu yeyote anayemfuata mtu nyumbani kwake unakwenda kumtafuta ushari. Mimi nilikuwa naomba suala hili la hifadhi zetu lazima zilindwe, ziheshimiwe na sheria zifuatwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utalii. Tunasema sana utalii ni wa nje tulikuwa tunautangaza, lakini sasa tutangaze utalii wa ndani. Nani atatangaza utalii wa ndani? Kutangaza utalii wa ndani ni wananchi wenyewe wa ndani. Tuna wasanii wazuri, vijana, warembo, hawa tuwape ubalozi watangaze utalii wetu wasitafute watu wengine wa nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi hii kwa kuweza kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani. vitabu vya Mwenyezi Mungu vinasema siku zote kama mwanadamu mwenzio hukumshukuru anachokifanya kwa hivyo hutoweza kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye nchi yetu, tunamwambia aendelee awe na subra, awe na uvumilivu, awe na ngozi ngumu, lakini awatumikie Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite moja kwa moja kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Mimi ninazungumzia zaidi Zanzibar. Nchi yetu ya Zanzibar sasa hivi kumekuwa na magari mengi sana. Magari yanasababisha foleni kubwa sana, kama unatoka nyumbani saa tisa basi unaweza ukarudi saa 12 au saa moja. Lakini tunamshukuru Kamishna amepanga mipangilio mizuri kwa sasa, Askari wako barabarani wanafanya kazi ya Jeshi la Polisi na kuwasaidia wananchi. Ninasikitika kwa sababu ya Askari wetu hawana vitendea kazi, hili ni tatizo kubwa sana, Askari leo unamkuta ana simu ya mkononi ndiyo anawasiliana na Askari mwenziye aliyepo mbali. Hata misafara yetu kwa sasa ya Viongozi wetu Zanzibar ni mtihani, kwa sababu Askari wetu hawana vitendea kazi. Leo sisi wenyewe tunapigiana simu muda wote unaambiwa simu imezimwa au mteja yule hapatikani, je, Askari huyu Kiongozi anatoka anakwenda safari Askari ana simu ya mkononi anampataje?

Mheshimiwa Spika, hili limekuwa ni tatizo mimi limenikumba niliambiwa nataka kuvamia msafara wa Kiongozi, wakati msafara unakuja mimi niko njiani sipata kukaa popote, Askari akanisimamisha nataka kuvamia na niliwekwa kituoni muda mrefu sana. Kwa kosa la vitendea kazi la Askari wetu. Si barabarani si ofisini ni matatizo. Serikali lazima isimamie Jeshi la Polisi kuwapa vitendea kazi. Tutazunguka, tutazungumza, tutawasema Askari wetu hawafanyi kazi lakini Askari wanajitahidi kufanya kazi. Vitendea kazi hawana, muda wote, siku zote, tunawazungumzia Askari wetu vitendea hawana. Kwa nini Serikali hawatusikii? Tunakwenda kwenye vituo vya Polisi unavikuta viti vya plastic vile vya cello vimefungwa vilemba, vimefungwa kamba. Viwanda vya viti vile vipo hapa nchini, kweli Serikali haina wa kwenda kununua viti vya kupeleka kwenye Ofisi zile za Polisi? Kwa kweli hali hii siyo nzuri, hata wale wafanyakazi hatuwapi moyo wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna askari wazuri…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Mheshimiwa Mwanakhamis kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mwakagenda.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mwanakhamis. Amezungumzia kwamba Jeshi la Polisi halina vifaa ni kweli, kibaya zaidi sehemu za mipakani Kyela, Tunduma unakuta Askari hawana gari ya doria na tunajua kabisa hapo ni mpakani. Nilikuwa nampa tu taarifa kusisitiza kwamba anachosema ni sahihi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda siyo kazi yako kujua usahihi au makosa ya mchango wa Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mwanakhamis.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vituo vya Polisi sijafika Mikoa mingine au maeneo mengine lakini utasema vyote ni Baba mmoja Mama mmoja. Ukienda kile utafikiri kama nimetoka hichi, ukienda na kile kingine utasema nimetoka kule. Lakini hali ya Jeshi letu la Polisi ni mbaya sana! siyo ofisini si barabarani, ajali zimekuwa nyingi hata Zanzibar ajali sasa hivi ni nyingi, wananchi wetu ajali ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Askari barabarani wazuri na kuna Askari wengine hawako vizuri wana majibu mabaya wanayowajibu wananchi, wanatujibu hata sisi, hivyo suala hili lifanyiwe kazi! Askari wana majibu mabaya barabarani hawana kauli nzuri, ni nusu tunasema wanatunyanyasa, wanatuadhibu! Mimi siyo mara moja siyo mara mbili tena niko Jimboni kwangu, nimejibiwa na Askari Traffic majibu mabaya na Askari ninamjua.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia kwa jioni hii ya leo. Kama hukumshukuru binadamu mwenzio kwa analolifanya basi hata Mwenyezi Mungu huwezi kumshukuru. Katika vitabu vya Quran mwanamke ametajwa mara tatu. Nichukue nafasi hii kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya mambo makubwa sana. miaka miwili tu lakini ameitumikia nchi hii kwa nguvu zake zote kwa sababu anahofu ya Mungu, Mama Samia ni mcha Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia amefanya miradi mingi katika nchi hii kama vile barabara, skuli na miundombinu mbalimbali. Sisi hapa Wabunge tumetoka kwenye majimbo ambayo haya hatukuyaanza sisi, wapo wenzetu walipita. Sasa, kuna miradi walitengeneza Wabunge wenzetu waliopita lakini sisi hatukuiendeleza miradi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia mtangulizi mwenziwe aliyepita amefanya miradi mingi sana na miradi ile yote haikukamilika, lakini Mama huyu alivyokuwa ni mcha Mungu na ana hofu ya Mungu miradi hii ameisimamia kikamilifu na bado anapambana nayo, na Mungu ndiye atamlipa. Kwa nini akasimamia miradi hii, ni kwa sababu ni kodi za wananchi, ni pesa za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia anafanya mambo makubwa sana, hata mazungumzo yake anapoyazungumza ni maneno laini yanamtoka ndani ya mdomo wake. Ni mama mmoja mwenye sura ya tabasamu muda wote, hata akikasirishwa basi yeye bado ametabasamu, huyu ni mcha Mungu wa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hususani wanawake Rais wetu ni mwanamke. Tulikuwa tuna nyimbo tunaimba mwanamke kuwezeshwa, lakini sasa mwanamke hawezeshwi mwanamke anafanya mwenyewe. Mama Samia anakwenda kila pembe kila na kwenye kila kichochoro. Mama huyu ni mcha Mungu, hata ukimtazama kwenye kipaji chake cha uso, ni mcha Mungu. Anapokwenda popote hatoki mtupu lazima atakuja na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia Miradi aliyoiacha Mheshimiwa Magufuli ameiendeleza. Sisi Wabunge humu tuseme Wabunge wangapi miradi tuliyoikuta ya wale Wabunge wetu watangulizi waliopita tumeiendeleza? Tukifika tunaanza miradi mingine mipya lakini ile tumeiacha. Mcha Mungu huyu ameendelea kufanya kazi, kuwatumikia Watanzania. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanawake tusimame na Mama Samia Suluhu Hassan, tumuimbe Mama Samia Suluhu Hassan, tumpigie makofi Mama Samia Suluhu Hassan, tumwombee dua Mama Samia Suluhu Hassan. Vile vijineno vijineno tuachane navyo, tuvipuuze, hususani wanawake Mama Samia ametubeba, ametupa uhuru, muda huu mwanamke tulikuwa tunaidai asilimia 50 sasa imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wanawake tumsafishie njia Mama Samia Miaka mitano, miaka miwili amefanya mambo haya miaka mitano ijayo atafanyaje? Nakuombeni Watanzania maneno yanayozungumzwa mengine yapuuzeni, Mama anapambana, ni mwanamke, amezaliwa na mwanamke, lazima tumuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia anapokwenda kuzunguka anachokileta anakileta kwa maendeleo ya Watanzania sote. Hawaletei watu wachache kama wakitumie wao peke yao, ni cha kwetu sote, lazima tumuunge mkono, tumpe nguvu Mama yetu, tumpe nguvu Rais wetu, tumpe nguvu Shujaa wetu hususan wanawake. Wanawake huu ni muda wetu, huu ni wakati wetu, wanawake lazima twende kifua mbele. Mama ni shujaa, Mama ametuwezesha, anaposafiri kwenda nje haendi kuzungumza na makapuku, anazungumza na wanaume, walioshiba, anazungumza nao na wanamwelewa akirudi anarudi na chochote. Nawaomba Watanzania Mama Samia amefanya mambo makubwa, ni mwanamke lakini anapambana, anaitetea nchi na kumtetea mwanamke. Mama Samia anamtetea mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze suala lingine kuhusu mwanamke. Mwanamke ni nguvu kazi ya Taifa letu, leo mwanamke huyu tunayesema ni nguvu kazi ananyanyasika, anadhalilika, wanawake wamekuwa wanauliwa kiholela, Ofisi ya Waziri Mkuu walisimamie suala hili. Wanawake wanauliwa sana. Hivi karibuni tuliona mwanamke, mumewe ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, baba ametoka nyumbani, anarudi mke wake ameuliwa. Juzi mwanamke ni Mhasibu amepigwa mpaka amechomwa moto. Kwa kweli inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke ni Taifa kubwa, mwanamke ni kila kitu, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ilisimamie suala la haki za mwanamke. Mama yetu anatutetea sana wanawake, lakini bado mwanamke hatujamsimamia. Waheshimiwa asilimia kubwa Wabunge humu waliopita walikuwa ndugu zetu albino wanateseka, wananyanyasika, lakini Serikali hii ilisimama na kuwatetea ndugu zetu wale albino na liliisha. Kwa nini lisiishe suala hili la mwanamke kunyanyaswa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini lisiishe mwanamke kuuliwa? Kwani sasa hivi wanawake wengi tunasoma kwenye mitandao wanawake wanapata matatizo, wanauliwa wengi sana. Je, wale waliokuwa hawatangazwi kwenye mitandao, ni wangapi? Naomba sana Serikali, chonde chonde tusimame na mwanamke, Rais wetu ni mwanamke na sisi wanawake ni jeshi kubwa, tumpambanie Mama Samia miaka mitano tena ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Ofisi hii ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kunijalia kupata nafasi hii. Nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazozifanya katika nchi yetu. Nichukue nafasi hii kumpongeza Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuisimamaia nchi yetu lakini pia kwa kuusimamia Muungano wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru watangulizi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Marehemu Aman Abeid Karume, kwa kweli walikaa wakafikiri suala kubwa sana kuungana na kutufanya sisi kuwa ndugu. Wao waliunganisha udongo au walichanganya mchanga, lakini Muungano wetu kwa sasa sisi tumechanganya damu. Kwa kweli sisi sasa hivi ni ndugu hatuwezi kutengana na hatuwezi kugombana; mambo mengine madogo madogo yatakayotokea hayo ni mambo ya kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumpongeze mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuusimamia Muungano huu. Kuna watangulizi wake walipita, yeye ni Rais wa Sita lakini amefanya mambo makubwa sana, na shahidi ni Mheshimiwa Waziri ambaye amezungumza kuwa kero nyingi za Muungano zimetatuliwa. Hilo tulijua litafanyika kwa sababu Muungano huu sasa hivi umetufanya sisi kuwa ndugu, hatutakiwi tugombane, tuzozane wala tuoneane, lazima tuwe pamoja, na mama yetu hilo ndilo analolitaka. Mimi bado nitashikilia, kung’ang’ania kushikilia na kusema kuwa Mama Samia ni mcha Mungu, Mama Samia ni mkweli, bado nitaendelea kuzungumza suala hilo Mama Samia ni mkweli na ni mcha Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu watangulizi walitangulia walizungumza kuhusu kero za Muungano. Mimi nasema kero zipo na zitaendelea kuwepo madhali sisi ni binadamu; lakini nasema kwa kipindi cha Mama Samia mambo mengi yatatatulika; yametatuliwa lakini ataendelea kuyatatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu walizungumza kuhusu kero ya Bandarini. Bandarini pana matatizo makubwa sana; kuna wanawake wanaotoka Zanzibar wakati wa hizi Sikukuu wanakuja kununua vitu vyao vidogo vidogo Dar es Salaam, na tunasema nchi yetu ni moja, ni Tanzania, wakifika pale bandarini wanaadhibiwa sana na suala hili tulishalizungumza sana. Sisi ni ndugu, Mheshimiwa Waziri tunamwomba afike bandarini kama wale watu wa bandarini hawana elimu wakapewe elimu. Sisi tunazungumza ni ndugu lazima tukubaliane, kuna mambo mengine hayana haja ya kujitokeza sisi kuja kulizungumza humu. Ni sisi wenyewe tujue hiki hakikubaliki, hili halikubaliki, lakini kumekuwa na unyanyasaji mkubwa bandarini wenzangu wamezungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mtu anakuja na TV yake moja, TV moja kweli ni ya kufanya biashara anakwenda kuzungumza na Watoto wake sasa hivi azam Alhamdulillah makero mengi mengi ma-stress yanaondoka kwa Azam tu, anakuja mtu TV ile ailipie kodi, tena anaambiwa ondoka, nimeshuhudia anaondoka. Ukienda kusema jamani mwachieni hayo matusi utakayoyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutakuwa tunavuruga Muungano na tunamvurugia mama yetu. Yeye ana nia nzuri kuutetea Muungano huu na bado anautetea na anaulinda kwa maslahi ya nchi yetu. Kwa hiyo na sisi tuliopewa nafasi lazima tuzisimamie kwa kuzitetea nafasi zetu na kuwatetea wananchi wetu. Wanawake wengi wanaofanya biashara ndogo ndogo wanadhalilika, wanateseka bandarini, biashara zao zinapotea, inauma sana. Hawa ndio wapiga kura wetu; na mwanamke tunasema sasa hivi ndiye mtetezi wa nchi hii, lazima tupewe kipaumbele. Muungano wetu ndio kama ni kioo chetu, kwa hiyo lazima muungano huu tuulinde, tuutetee, na msimamizi sasa hivi ni Mama, hakutuacha nyuma. Sisi tunasema hatuna malalamiko makubwa ya kuzungumza kuhusu Muungano huu maana yake tunasema sasa tumechanganya damu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,asilimia kubwa ya Wabunge wa Zanzibar wanaokuja miaka mitano lazima anaacha watoto huku. Huku wanaacha Watoto, ndiko kuchanganya damu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,Kwa kweli Mheshimiwa mambo ya hizi kero, mambo madogo madogo yaondoke. Sisi kila siku tunazungumza tunapiga kelele tunazungumzia hayo kwa hayo yale kwa yale, hayapendezi. Muungano wetu nchi nyingi wanatuonea choyo au wanatuonea husuda, kwa kweli ni jambo la kusikitisha.

MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, taarifa.

TAARIFA

MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa dada yangu anaye changia hapa sasa hivi. Si kwamba wanaacha watoto tu, mimi mwenyewe hapa ni mtu wa Morogoro Mama yangu ni Mtu wa Zanzibar. (Makofi)

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, umeyasikia maneno. Muungano huu hatukuchanganya udongo peke yake. Udongo bado utabakia kwenye kumbukumbu lakini sasa hivi tunasema Muungano huu tumechanganya damu. Tukizungumza hapa tukijifafanua asilimia kubwa tunasema sisi ni ndugu wa baba mmoja. Kuna mambo lazima tuyazungumze kiudugu, lazima tukubaliane isiwe kila siku tunapiga kelele Muungano Muungano. Muungano huu hakuna yeyote wa kuweza kuutengua kwa kusema huu haufai kwa sababu ukisema haufai mimi nikirudi Zanzibar huku na acha dada yangu, naacha bibi yangu, naacha shangazi yangu. Siwezi kwenda kule lazima huku nitarudi. Sisi sasa hivi tunakwenda free Zanzibar na Bara kwa sababu sisi ni ndugu.

Mheshimiwa Naibu Spika, utazunguka bara yote lazima utamkuta Mzanzibar yupo kazaa amejukuu kwa hiyo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Wizara hii ya Maliasili.

Mheshimiwa Spika, leo ni siku ya jumatatu ni siku tukufu ni siku nzuri sana kwa hivyo nakuombea dua kwa Mwenyezi Mungu akujalie kwa jambo lako hilo unalokwenda kulifanya la huko Duniani ufanikiwe. Kufanikiwa kwako ni kufanikiwa watanzania, kufanikiwa kwako ni kufanikiwa Wabunge, kufanikiwa kwako ni kufanikiwa Wanawake hususani wa Jimbo lako la Mbeya Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan bado kuendelea kupambana na nchi yake lakini kuiletea maendeleo nchi yake. Nimpongeze Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa Zanzibar kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini nirudi kumpongeza Dkt. Hussein na Mama Samia Suluhu walivyotangaza Royal Tour walitangaza jambo hili kwa upendo mkubwa, kwa ukakamavu mkubwa na kwa kuwa na moyo wa dhati wa nchi zao au wa nchi yao ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi walitangaza utalii wa fukwe, walianza huko wa Bahari halafu wakaja kwenye zetu za utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini jambo hili Viongozi wetu wa nchi kutangaza utalii? Kwa sababu hizi ni rasilimali za nchi yetu na ndizo tunazozitegemea na rasilimali zetu hizi ikifika miaka kumi, kumi na tano basi Mheshimiwa zitapotea. Kwa hivyo, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mama Samia walisimama kidete kutangaza utalii wa nchi zetu mbili hizi iliyobaki Watanzania nasi lazima tuwaunge mkono Viongozi wetu waandamizi wa Nchi kwa juhudi kubwa waliyofanya kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, kwa kweli wanakazi kubwa sana kwa sababu Mheshimiwa kila aliyenyanyuka alimzungumza tembo. Sasa siye kama kazungumzwa tembo kwa kweli tunasema ni jambo kubwa sana hili kuzungumzwa tembo kama amekuwa anapiga watu sasa ni hatari! Namuomba Mheshimiwa Waziri hii tembo aidhibiti kwa nguvu zake zote pamoja na Naibu Waziri. Kwanza ana Naibu Waziri mkakamavu, muelewa, mchapakazi na Waziri umeingia kwenye Wizara ni Wizara ngumu sana, lakini Mungu atakusaidia. Kwa vyote anavyochakatwa huyo tembo lakini bado uendelee kupambana tembo wasiathiri wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwakweli ni hatari tena hii ni hatari kubwa sana, tembo wasiumize. Unao Askari wakakamavu, unao Kamati yako nzito, madhubuti na Waziri Mkuu anasaidia sana kutatua migogoro, sasa hii migogoro ya tembo sasa ataitatua vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwakweli Mheshimiwa Waziri ni mchapakazi, Wizara hii ni Wizara ngumu, nzito sana ni Wizara iliyo na mambo mengi sana, lakini sisi tunasema unaweza, kwa sababu kule utamaduni ulifanya vizuri Alhamdulillah. Kwa hivyo na hapa tunataka uendelee kuchapa kazi, una Naibu Waziri ni Mwanamke lakini mwanamke shujaa sana, mtume Naibu wako Waziri anatumika usimuogope.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Askari wetu kwa kweli wanazungumzwa sana wao ni wanyonge, wamezaliwa kama sisi kila mmoja mwenye mama yake naye anao mama yao. Leo askari imekuwa wapo kwenye matatizo makubwa sana, tunakuomba Mheshimiwa Waziri uwasaidie askari wetu, wapambane lakini uwasaidie kwa nguvu zako zote. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana, kengele imeisha gonga.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kuna msanii Zanzibar alisema, “Mungu akitaka kukupa hakuletei barua, hukupa usingizini pasipo mwenyewe kujua.” Kuna msanii mwingine akasema, “Mpewa hapokonyeki, aliyepewa kapewa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nikasema hivi? Nafasi ya uongozi ikiwemo Rais na viongozi wengine nafasi hizi hupangwa na Allah Subhannah Wataala. Mwenyezi Mungu kama hataki uwe Rais basi utavaa makoti kila siku ukajitazama kwenye vioo mimi nitakuwa Rais lakini huwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan cheo hichi alitangazwa na Mwenyezi Mungu ndiye aliyempa. Vyeo hivi kuna leo kutenda kuna kesho kuulizwa lakini Mheshimiwa Samia ni mcha Mungu. Mheshimiwa Samia anafanya mambo makubwa kuwatumikia Watanzania na Watanzania wote ni mashahidi na sisi Wabunge ni mashahidi. Siku zote binadamu tunapofanya mazuri tunakuwa hatusifii na lile zuri halisifiwi baya ndiyo linasifiwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamzungumza Dkt. Samia tunampigia makofi sana muda wote nafikiri Wabunge wote wanamzungumza Mama Dkt. Samia kwa imani yao na imani ya Mama Dkt. Samia anayafanya lakini Mheshimiwa Dkt. Samia ana jeshi lake. Ana jeshi linalomsaidia kazi ya kumpongeza Mama Dkt. Samia na miaka miwili aliyoifanyia kazi na jeshi hili ni Mawaziri wetu na Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu na Wakurugenzi. Hilo ndiyo jeshi la Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni lakini Mawaziri wetu wanapambana. Wanafanya kazi kubwa sana kuwafanyia Watanzania na kazi hizi zinaonekana. Kwa nini tusiwapongeze, kwa nini tusiwaombee? Mawaziri hawa wakiongozwa na Kamanda wao Waziri Mkuu kwa kweli wanastahili sifa zote. Tumpigieni makofi Rais wetu lakini na Mawaziri wetu wanafanya kazi kubwa sana, wanastahili sifa. Kuna jeshi la ardhini na jeshi la angani. Naibu Mawaziri ni majeshi wa ardhini, Mawaziri wenyewe ni majeshi ya angani wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliposoma Bajeti yake aliisoma kwa madaha lakini kwa uelewa mkubwa na tulimuelewa tukamfahamu hata Watanzania waliifahamu Bajeti hii. Sasa basi kazi iliyobakia jeshi la Mama Samia wakaitekeleze bajeti hii ifanye kazi kwa weledi zaidi. Miradi hii ikakamilike fedha zifike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nimuombe Ndugu yangu Comrade Waziri wa Fedha kwa kweli kwenye makusanyo huko kumechafuka sana bado kazi hii hatujaifanyia kazi. Tuendelee kupambana na ukusanyaji wa kodi. Tunapokwenda kukusanya kodi, wale tunaowafuata ni binadamu na binadamu siku zote ana mbinu nyingi. Kwa hivyo twende kwa nasaha, kwa maridhiano tukawashauri lakini tuwaambie. Tusiende kwa vishindo kuwatukana, kupambana nao itakuwa hatufanikiwi. Letu tunalotaka itakuwa hatufanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sehemu za makusanyo rushwa ni nyingi, kunanuka rushwa. Udanganyifu ni mwingi, unakwenda kununua kitu anakwambia unataka cha shilingi 100,000 ukimwambia nakitaka nipe risiti anakwambia basi shilingi 150,000, itakuwa hatufiki. Mimi naomba jeshi la Mama Samia tushirikiane na Wabunge tukafanye kazi ya makusanyo jamani ndiyo tutapata maji, barabara na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja suala la Muungano. Viongozi wetu Hayati Karume na Hayati Nyerere walipoungana Muungano huu waliungana kwa makaratasi wakatiliana saini lakini hawakuridhika, ukachukuliwa udongo wa Zanzibar na udongo wa Tanganyika ukaja ukachanganywa. Leo udongo ule nadhani hakuna Mtanzania wala mzungu atakayekuja kuubagua udongo ule kwa muda huu uliofika kwa awamu hii, sisi hatukuungana tena kwa karatasi wala kwa udongo, tumeungana kwa damu. Sisi tumeshachanganya damu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uduvi unaupekecha pekecha Muungano huu lakini tunawaambia ole wao jeshi litakuwa ni la Mama Samia lakini wanawake tu ndiyo tutakaopambana nao. Hatuwezi ukavunjika Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja kwenye maliasili. Wabunge wengi wanawake, wanaume wanalia kuhusu tembo. Tembo huyu anatupatia faida, tunapata fedha za kigeni lakini tembo hii pia ni dawa kwa binadamu. Niiombe Serikali tembo sasa hivi anaua watu ni hatari. Tusiachie hii tembo ikawa inaua watu ni hatari na hatuwezi kuwaua tembo hawa kwa sababu tunapata faida nyingi sana. Nadhani hili janga liwe la Kitaifa wa kuisimamia hii tembo isiue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la maadili ya nchi yetu. Kuna watu kama ni kutoka ughaibuni, kama ni kutoka Afrika, kama Ulaya wamekuwa wanawadhalilisha viongozi wetu wanawatukana kwenye mitandao. Tunasema hii haikubaliki wala hatukubali na tunashangaa leo mwanamke utachukua simu utamtukana mwanamke mwenzio, iweje na lipi unalomtukania? Kama uko Ulaya basi shuka uje huku Afrika tukutane uso kwa uso tutukanane sisi na wewe na kama wewe unatukana uko Ulaya hayo matusi unayoyatukana basi yawe yako mwenyewe siyo ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi hii kuweza kuchangia jioni hii ya leo. Mimi nichukue nafasi hii kwanza kumuombea Mama yangu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya nchi hii Mwenyezi Mungu ampe nguvu ampe afya, ampe uzima lakini ampe uvumilivu ampe na Subira, Mwenyezi Mungu tunasema Alhamdulillah basi Mwenyezi Mungu anakuwezesha kwa mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja nimpongee Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Viongozi wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuitumikia nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite moja kwa moja kwenye Wizara hii ya Ardhi, wenzetu hawa Wizara ya Ardhi wanafanya mambo makubwa, mimi ni Mjumbe wa Kamati hii tumezunguka maeneo mengi wanafanya kazi kubwa sana, migogoro hii itaendelea kuwepo na itakuwa ipo madhari sisi binadamu bado tupo kwenye dunia hii. Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imeandikwa kuwa ardhi itapimwa nchi nzima na sisi tunatarajia ni hivyo kwa sababu nia ipo na sababu ipo ya kupimwa ardhi ya nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza migogoro, migogoro ni binadamu, sisi ndiyo tunayoitengeneza lakini na wale wanaosimamia kwenye kitengo hiki cha ardhi, pale wamefanya neno lililokuwa zuri basi tusema Alhamdulillah tuwashukuru tuwapongeze na Mama yangu, Dada yangu wanafanya kazi kubwa sana. Kwa kweli ardhi ilikuwa mahtuti iko ICU lakini leo ardhi inazungumzika, migogoro mingi imetatuliwa, mambo mengi yamefanywa, kwa hivyo tuseme tu tuwaombee wenzetu waendelee na kazi hii kazi hii ni kubwa, kazi hii siyo ya mtu mmoja ni yetu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu letu sote Wabunge kusimamia ardhi na kusimamia wananchi wetu tusiipe nguvu migogoro, kwa sababu tunalaumu migogoro lakini kuna migogoro mingine inatengenezwa, na watengenezaji ni wanasiasa. Hapa tunapigia kelele lakini mimi ni Mjumbe wa Kamati tumezunguka sana, hatujamaliza lakini tulikoenda kote ni kuzuri watu wanapewa hati zao wanapokea kina mama, baba, vijana, kwa kweli wenzetu wanafanya kazi kubwa, mimi nasema Alhamdulillah Mwenyezi Munge awawezeshe waendelee kuwatumikia watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia ardhi usimsahau Mheshimiwa Lukuvi. Mheshimiwa Lukuvi alifanya kazi kubwa sana ya nchi hii, alipewa Wizara ya Ardhi iko mbovu, huwezi kufanya ziara kamati ikienda kwenye sehemu ya ardhi kama utapokewa, ilikuwa ni matatizo makubwa lakini Alhamdulillah unapokwenda wananchi wanakuelewa wanaweka vikao wenyewe wanakuita mnazungumza mnapaga wanataka kupimiwa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mie niombe Serikali na Waziri wa Fedha yupo Wizara ya Ardhi hii iongezewe pesa, pesa ni ndogo wanayopewa hata tukiwalalamikia waje watupimie au watusikilize watu wanataka kupimiwa ardhi pesa ni ndogo wanayotengewa, kwa hiyo mimi nilikuwa naomba Serikali lazima isimamie ardhi. Ardhi ni kila kitu na wananchi sasa hivi ni waelewa wanajua kila kitu, kwa sababu ardhi ndio kila kitu, kilimo ardhi, ukienda kwenye maji ardhi, ukienda sehemu zote lazima tuwe na ardhi nzuri safi iliyokuwa haina migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lukuvi alifanya mambo makubwa sana, sisi tumekwenda Kigamboni tulipokewa kwa mapanga na kama Mbunge wa Kigamboni yupo ananisikia, alitupigia simu tulifika kwenye Pantoni hatukushuka lakini wananchi walituzonga, lakini leo nenda Kigamboni utapokewa na ngoma utapigiwa kwa sababu ardhi imepimwana ambayo haijapimwa lakini itapimwa kwa sababu ni ilani ya Chama cha Mapinduzi na Waziri wetu ni wa Chama cha Mapinduzi na Naibu Waziri ni wa Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo ni lazima ardhi itapimwa lakini tunaomba pesa Wizara ya Ardhi iongezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite moja kwa moja kwenye National House, National House pia walifanya kazi nzuri. Ndugu yangu Mchechu alifanya mambo makubwa sana, huyu kijana alifanya mambo makubwa sana, kwa hivyo tumpongeze na tumuombee kwa Mwenyezi Mungu amerudi pale pana viporo tele alivyovianzisha sasa aviendeleze viporo vile lakini nimuombe Mheshimiwa Mchechu arudi Kigamboni, tulisema tutaupanga Mji uwe wa Kisasa kwa hivyo warudi pale waende wakaupange Mji wa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri nisema naunga mkono hoja. (Makofi)