Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abeid Ighondo Ramadhani (14 total)

MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya vituo vya afya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata za Makuro na Ngimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Singida shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati Minyeye, Mnung’una na Msikii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini zikiwemo Kata za Makuro, Ngimu na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE K.n.y. MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara za Singida Kaskazini zinazounganisha Vijiji ambazo hazipitiki kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Singida Kaskazini ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 811.68 ambao umekuwa ukifanyiwa matengenezo pamoja na kujenga na kukarabati vivuko. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Singida ilifanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 78.55 na vivuko 22 kwa gharama ya shilingi milioni 739.39.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka fedha 2020/2021, barabara zenye urefu wa kilometa 67.8 na vivuko 20 vimetengenezwa kwa gharama ya shilingi millioni 711.08 ambapo hadi Machi, 2021 barabara zenye urefu wa kilomita 45 na vivuko 15 vimekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 barabara zenye urefu wa kilomita 62.5 na vivuko 24 vitajengwa kwa gharama ya shilingi millioni 711.08.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Halmashauri ya Wilaya ya Singida itafanya tathmini ya barabara zote za Singida Kaskazini ili kuandaa mpango wa namna bora ya kuweka vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itavipatia huduma ya maji safi na salama Vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Matumbo, Itamka na Msimihi katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21 imekamilisha miradi ya maji katika vijiji 7 ambavyo ni Mughamo, Mgori, Ngimu, Sefunga, Ghalunyangu, Kijota na Malolo hivyo, huduma ya upatikanaji wa maji kufikia asilimia 66.4 katika Wilaya ya Singida Vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 utafanyika utafiti wa kina kwa ajili ya kuainisha maeneo yenye maji ya kutosha chini ya ardhi. Hivyo vijiji vya Kinyamwenda, Igauri, Itamka na Msimihi vitapata maji baada ya kukamilisha uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji.

Aidha, kijiji cha Matumbo kitapata huduma ya maji ya uhakika baada ya ukarabati wa mradi wa maji kukamilika mwezi Julai, 2021.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Vijiji na Kata katika Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo havijapata umeme vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji 26 vya Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo havijapata umeme kati ya vijiji 84 vitapelekewa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza mwezi Machi, 2021. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2021 na gharama ya mradi ni shilingi bilioni 26.6.
MHE. ABEID I. RAMADHANI aliuliza: -

Barabara ya kutoka Singida kupitia Mji Mdogo wa Ilongero – Mtinko hadi Hydom ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Singida, Manyara na Simiyu.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Ilongero – Mtinko hadi Hydom kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Ilongero – Mtinko hadi Hydom yenye urefu wa kilometa 93.3. Mkataba wa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulisainiwa mwezi Oktoba, 2021 na kazi inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022. Mara baada ya kazi ya Usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Wananchi wa Kata za Mgori, Mughungu na Ngimu Jimbo la Singida Kaskazini wapo tayari kukabidhi Msitu wa Mgori kwa Serikali kuwa Hifadhi ya Taifa: -

Je, mchakato wa Serikali kukamilisha zoezi hilo umefikia wapi na faida gani wananchi watazipata kwa msitu huu kuwa hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kupongeza jitihada zote zilizochukuliwa na Serikali katika ngazi ya Vijiji, Wilaya na Mkoa pamoja na Mheshimiwa Mbunge katika kuhakikisha Msitu wa Mgori ambao ni makazi ya wanyamapori wadogo na wakubwa hususani tembo unahifadhiwa.

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikia mpaka sasa ni mchakato wa kupata Tangazo la Serikali ili kuutambua msitu huo kama hifadhi. Rasimu ya kwanza ya Tangazo la Serikali imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 4 Februari, 2022. Tangazo hilo litadumu kwa siku 90 kabla ya kutolewa tangazo la mwisho ambalo litatoa idhini kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kusimamia msitu huo.

Mheshimiwa Spika, faida za kuhifadhi msitu huu wenye ukubwa wa hekta 49,000 ni pamoja na: -

(i) Kuweka hali ya hewa nzuri kwa Mkoa wa Singida wenye misitu michache sana ya hifadhi na kuwezesha upatikanaji wa mvua hivyo kusaidia kwenye ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, ufugaji na maji;

(ii) Lakini vilevile utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji;


(iii) Lakini pia uwepo wa baioanuai nyingi za mimea ya asili na makazi ya wanyamapori kama tembo na wengine hivyo, kuchochea shughuli za utalii;

(iv) Sambamba na hilo kuwepo kwa fursa za ufugaji nyuki kwa wenyeji ili kuwaongezea kipato.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa kufua umeme wa upepo na jua wa MW 100 utaanza rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhan, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwekezaji aitwaye Upepo Energy alifanikiwa kushinda zabuni ya kuendeleza miradi miwili ambapo Megawatt 100 za umeme zitazalishwa kwa nguvu ya upepo na Megawatt 45.08 zitazalishwa kwa nguvu ya jua.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa majadiliano baina ya TANESCO na Mwekezaji kuhusu bei ya kuuziana umeme (PPA) yamekamilika. Majadiliano kuhusu mkataba wa utekelezaji (Implementation Agreement-IA) yanaendelea. Ipo changamoto ya mwekezaji kuhitaji “Government Guarantee” kinyume na Sera ya Serikali na masharti ya zabuni kama ilivyotangazwa. Iwapo mwekezaji atakubali kutekeleza mradi huu bila masharti mapya aliyoweka, mradi huu utaanza kutekelezwa mwezi Januari, 2023.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhudumia wananchi katika kudhibiti uhalifu. Katika tarafa ya Ilongero eneo la Kinyagigi Jimbo la Singida Kaskazini kunajengwa kituo cha Polisi cha Daraja C na kimefikia hatua ya umaliziaji. Kazi iliyobaki ni kuweka miundombinu ya umeme, maji safi na taka, milango na madirisha, dari, sakafu na kupaka rangi. Kiasi cha fedha shilingi 46,000,000 kinahitajika kumalizia ujenzi, na fedha hizo zinatarajia kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Vifaa Tiba katika Hospitali ya Ilongero pamoja na Vituo vya Afya vya Msange na Mgori Wilayani Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilipeleka Bohari Kuu ya Dawa Shilingi Bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa Tiba. Tayari Vifaa Tiba vimeanza kusambazwa kwenye Hospitali 67 za Halmashauri ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambayo imekwishapokea vifaa vya aina 17 vikijumuisha vifaa vya upasuaji na maabara.

Mheshishimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/ 2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyopelekwa kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizokamilika.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, lini Miradi ya Umwagiliaji katika Vijiji vya Msange na Mnghamo – Singida Kaskazini itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ighondo Ramadhani Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa Mughamo na kuanza ujenzi wa bwawa na miundombinu mingine ya umwagiliaji katika Skimu ya Msange.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Singida – Ilongero hadi Haydom?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANROADS tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Singida – Ilongero – Haydom yenye urefu wa kilometa 93. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga soko na stendi ya kisasa eneo la Njiapanda Merya Halmashauri ya Wilaya ya Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida imeanza utekelezaji wa hatua za awali za ujenzi wa Stendi ya Njiapanda ya Merya. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi milioni 10 na kufanya upimaji wa eneo la stendi, kufanya usafi na kusawazisha eneo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inakamilisha tathmini ya gharama za ujenzi wa stendi hiyo na kuanza kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi. Halmashauri inaendelea na maandalizi ya andiko la mradi wa soko na litakapokamilika litawasilishwa Serikalini kwa ajili ya uchambuzi na endapo litakidhi vigezo litatengewa bajeti na kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kufanya mageuzi ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali wa kuleta mageuzi ya kilimo. Mikakati hiyo inatekelezwa kwa lengo la kubadili kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kuwa kilimo biashara, chenye tija, himilivu kinachoratibiwa na kusimamiwa na Serikali na kushirikisha sekta binafsi ili kuwa na mifumo endelevu ya chakula na kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi hiyo ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 inatekeleza vipaumbele mikakati yenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji; kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo; kuimarisha usalama wa chakula na lishe; kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya nje ya nchi na kuimarisha maendeleo ya ushirika.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya vituo vya polisi vya Ilongero, Ngamu, Ngimu, Msange na Mtinko katika Jimbo la Singida Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Abeid Ramadhan Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa vituo vya polisi vya Ilongero, Mtinko na Ngamu. Tathmini iliyofanyika imebaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 46,480,000 zinahitajika ili kugharamia ukarabati wa vituo hivyo. Katika maeneo ya Ngimu na Msange hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vituo vya polisi. Napenda kutumia fursa hii kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Singida itenge maeneo yenye ukubwa stahiki pamoja na kutoa hatimiliki ili kuwezesha Serikali kupanga na kutelekeza kazi ya ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau. Nashukuru.