Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zuena Athumani Bushiri (9 total)

MHE. ZUENA A. BUSHIRI Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme katika Vijiji na Vitongoji kupitia REA III hasa katika maeneo ambayo nguzo zimetelekezwa barabarani zaidi ya miaka miwili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini - REA na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), inaendelea kutekeleza mpango wake wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu, mzunguko wa pili katika vijiji vyote nchini. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mradi huu unalenga kufikisha umeme katika vijiji 1,956 kati ya vijiji 12,268 ambavyo havijafikiwa na umeme. Kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu inayoendelea kutekelezwa kupitia TANESCO na REA ikiwa ni kazi ya kuendelea kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mawenzi litakamilika na kuanza kutoa huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbuge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto ambalo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha dhilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya vifaa na vifaatiba. Aidha, huduma zitaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukamilishaji usimikaji wa vifaa ifikapo Januari, 2022.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makanya kwenda kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi Wilayani Same ina urefu wa kilometa 40.9. Kipande cha kilometa 4.5 cha barabara hii kimeinuliwa kwa kujengwa tuta kati ya kilometa 14.5 zinazotakiwa kujengewa tuta kwa kiwango cha changarawe. Kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika muda wote na ndiyo maana imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara.

Katika mwaka wa fedha 20219/2020, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Same umefanya matengenezo ya barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 3.54 kwa gharama ya shilingi milioni 77.36.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Same imefanya matengenezo ya barabara hiyo kipande chenye urefu wa kilometa mbili kwa kiwango cha changarawe kwa gharama ya shilingi milioni 49.4. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 61.25 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita moja pamoja na ujenzi wa makalavati 14.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Makanya hadi kwenye Machimbo ya Jasi na itaendelea kuifanyia matengenezo ili kuhakikisha inapitika. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika bajeti zijazo ili kuiboresha na kurahisisha usafirishaji wa Jasi.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga uzio na uwanja wa michezo katika Shule Maalum ya Watoto wa kike Asharose migiro iliyopo Wilayani Mwanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athuman Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa michezo na utamaduni katika ukuaji na maendeleo ya wanafunzi na kutazama michezo na sanaa kwa mlengo wa ajira na stadi muhimu zinazochangia ukuaji wa kiuchumi na kijamii, Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika Shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila mkoa.

Mhesahimiwa spika, Shule ya Sekondari Asharose Migiro haipo kwenye mpango wa shule za sekondari zilizochaguliwa kuwa za michezo hivyo, inashauriwa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kutenga fedha kwenye Bajeti yake ya mapato ya ndani ili kuanza ujenzi wa uzio katika viwanja hivyo.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kununua magari ya Polisi kwa ajili ya vituo vya Polisi nchini?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na uhitaji wa kulipatia Jeshi la Polisi magari kama nyenzo za kutendea kazi. Kupitia mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Ashok Leyland ya nchini India, Serikali inategemea kupokea magari 369 kutoka nchini India ifikapo Septemba, 2022 ambapo mwishoni mwa mwezi Aprili, 2022 tunatarajia kupokea magari 78 yameshakaguliwa na kuthibitishwa. Magari hayo yatakapofika yatagawiwa kwenye Vituo vya Polisi vyenye uhitaji mkubwa.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga skimu katika vijiji vya Maore, Mpirani, Kadando na Mheza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu zilizopo katika vijiji vya Maore, Mpirani, Kadando na Mheza ili kupata gharama halisi za ujenzi. Baada ya zoezi la upembuzi yakinifu kukamilika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -

Je, ni lini umeme utafungwa kwenye mnara wa halotel uliopo kata ya Ngujini Wilayani Mwanga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jukumu la kuunganisha umeme kwenye minara ya mawasiliano ya simu nchini, ikiwemo ile iliyojengwa kwa ruzuku ya Serikali, ni jukumu la watoa Huduma, hii ni pamoja na gharama za kuunganisha umeme na kuendesha minara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia huduma za mawasiliano nchini kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi matakwa ya leseni zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya ukarabati wa nyumba za makazi ya polisi Moshi Manispaa?
NAIBU WAZIRI, MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 147 za makazi ya askari polisi zilizoko Manispaa ya Moshi imeonesha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 3.6 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajika kutengwa kwa awamu kuanzia kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo ukarabati wa nyumba 15 unatarajiwa kuanza kutekelezwa, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaboresha Madaraja ya Kampimbi na Mgandu Wilayani Same?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Madaraja ya Kampimbi yapo kwenye Barabara ya Same – Kisiwani hadi Mkomazi yenye urefu wa Kilometa 98. Mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Same – Kisiwani hadi Mkomazi yenye urefu wa Kilometa 98 umepangwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023. Ujenzi utajumuisha barabara na madaraja hayo na utaanza katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.