Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zuena Athumani Bushiri (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa Bungeni, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali hiki kwa siku hii ya leo na niwashukuru wapiga kura wangu wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kunichagua kuingia katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niko katika ukurasa wa 34 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020. Kwanza niipongeze Serikali kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maji, 1,423. Hii ni katika sera ya kumtua mwanamke ndoo ya maji. Katika Mkoa wa Kilimanjaro, tunazo wilaya ambazo zina matatizo ya maji na wilaya hizo ni Wilaya ya Mwanga, Same pamoja na Wilaya ya Rombo. Wilaya hizi mbili zimetolewa majibu na Waziri wa Maji asubuhi na bahati Mbunge wa Jimbo la Same aliongozana pamoja na Waziri wa Maji kwenda kuongea zaidi kuhusu mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu Mradi wa Maji wa Ziwa Chala ambao ni mradi mkubwa ambao uko katika mipango ya kutekeleza katika Wilaya ya Rombo. Wilaya ya Rombo ina changamoto kubwa sana ya maji, mwanamke anaweza akatoka asubuhi nyumbani kwake, akatumia masaa sita kwenda kutafuta ndoo moja ya maji. Katika kutatua suala hili la maji, kuna mradi mkubwa ambao unatekelezwa katika Wilaya ya Rombo, Mradi wa Ziwa Chala, lakini mradi huu hauna fedha za kutosha. Hivyo, niiombe Serikali iwasaidie akinamama hawa, akinamama ambao wameifanya kazi kubwa sana katika uchaguzi huu kuhakikisha kwamba Chama Cha Mapinduzi kinaongoza Wilaya ile ya Rombo. Tuiombe Serikali ifanye haraka ili mradi huu ukamilike ili tuwatue akinamama ndoo ya maji katika Wilaya ya Rombo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichangie katika ukurasa wa 19 kuhusu sekta ya viwanda, Manispaa ya Moshi Mjini ina viwanda vingi ambavyo vimefungwa amejaribu kuchangia Mbunge wa Jimbo, lakini kama mkazi wa manispaa ile na kama mwanamke ambaye naiangalia Serikali ya chama changu kwamba inao uwezo wa kufufua viwanda vile. Viwanda vile vimefungwa kwa muda mrefu na ni viwanda vingi ambavyo vimekosesha ajira kwa vijana, akinamama na wananchi wa Moshi kwa ujumla. Tuiombe Serikali sasa iwasaidie Manispaa ya Moshi, angalau ajira ziweze kupatikana, viwanda hivyo viweze kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika Wizara ya Afya, kwanza niipongeze Serikali kwa kujenga vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya, lakini wilaya zetu hizo zinakuwa bado hazina dawa za kutosha. Tuiombe Serikali na Wizara ya Afya ijaribu kufuatilia na kupeleka dawa katika hospitali zetu za wilaya na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza ya hiyo, kuna changamoto katika Wizara ya Afya, kuna huduma ya mama na mtoto, huduma hii katika maeneo machache ya vijiji watumishi wetu wamekuwa sio waadilifu, kwa kuwa tunavyotambua kwamba huduma hii ya mama na mtoto chini ya miaka mitano inatolewa bure.

Hata hivyo, baadhi ya watumishi wetu wanakuwa wakiwatoza akinamama hata wanapopeleka watoto wao kliniki na hata wanapoenda katika masuala ya kupima uzito tunaiomba Wizara ya Afya, ifuatilie ili iweze kubaini watu hao, watendaji hao ambao wanaichonganisha Serikali yao na wananchi kwa kuwa Serikali inatambua kwamba huduma hii inatolewa bure, wananchi wanakuwa wanajenga chuki na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Rais. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili nami nichangie kuhusu hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu 2021/2022. Mimi nitajikita zaidi katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na kazi ambazo amezifanya katika Taifa hili la Tanzania. Pia niipongeze Serikali kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya afya katika nchi nzima ya Tanzania. Pia niipongeze Serikali kwa kutoa dawa na vifaa tiba katika maeneo mengi ya zahanati zetu pamoja na hospitali zetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango mizuri ya Serikali tumeweza kujenga miundombinu mingi katika nchi yetu. Kwa mfano, tumepata vituo vya afya vya kutosha, zahanati za kutosha na hospitali za rufaa nyingi nchini Tanzania. Hata hivyo, kila lenye mafanikio lazima tukubali kuwa litakuwa na changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika zahanati hizi ambazo zimejengwa zimekuwa na uhaba wa madaktari pamoja na wauguzi. Utakuta maeneo mengine hasa maeneo ya vijijini zahanati moja inahudumiwa na daktari mmoja wakati wanaoitumia ni zaidi ya vijiji viwili au vitatu. Niiombe Serikali sasa ione umuhimu wa kuongeza bajeti katika sekta hii ili zahanati na hospitali zetu ziweze kupata watumishi stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna upungufu wa dawa. Nadhani Wabunge wenzangu wote wanakiri kwamba hospitali zetu zimebakia madaktari kwa professional zao ambazo wakishakuandikia dawa unaenda kutafuta hela ili ukanunue wewe mwenyewe, maeneo mengi dawa hazipatikani. Niiombe sasa au niishauri Serikali iweze kuongeza bajeti katika sehemu hii ambapo dawa zinahitajika sana ili wananchi wetu waweze kupata haki stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba ugonjwa wa COVID-19 umetingisha sana nchi yetu, kumekuwa na upungufu wa mitungi ya gesi. Wananchi wengi wanaoishi vijijini wanaopata magonjwa yale wanakosa oxygen na hivyo kuhatarisha maisha yao kwa sababu unapotaka kupata mitungi ya oxygen ni lazima uende katika hospitali kubwa za mikoa, halmashauri au rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali sasa, ili kuwasaidia wale wananchi ambao wapo vijijini, Serikali itenge fedha za kutosha ili iweze kupeleka mitungi hii hata katika ngazi ya zahanati ili kuokoa wananchi wetu walioko vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijatendea haki wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro kama nitakuwa sijachangia hospitali ya Rufaa ya Mawenzi katika Jengo la Mama na Mtoto. Hospitali ya Mawenzi ina jengo la Mama na Mtoto ambalo limejengwa tangu 2008. Ni takribani miaka 13 sasa jengo hilo halimaliziki. Hospitali ya Mawenzi inatibu wilaya saba za Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa hiyo, ukienda katika wodi ya zamani ambayo pia ni chakavu kwa majengo, unakuta wanawake wanalala wawili wawili; mmoja anageuzia kichwa huku na mwingine kule na vitoto vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika hili Serikali iweze kutenga fedha ili iweze kumalizia jengo lile na wanawake waweze kujifungua salama na katika maeneo ambayo ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kunipa nafasi hii kuchangia katika Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kuwapongeza Waziri wa Wizara ya Kilimo, Naibu Waziri na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri sana wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika kilimo cha umwagiliaji, umwagiliaji wa mpunga pamoja na tangawizi. Kilimo cha mpunga ni kilimo cha chakula na biashara, kilimo cha mpunga kinaingizia kipato sana wafanyabiashara, kilimo cha mpunga ni kilimo ambacho kinahitaji maji ya kutosha, lakini kwa tabia ya nchi mvua zimekuwa chache sana hivyo mazao ya kilimo cha mpunga yamekuwa machache sana.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Serikali imejipanga mipango mizuri sana ya kuweza kuwezesha kuweka miundombinu endelevu katika sekta ya umwagiliaji. Nitoe mfano katika kilimo cha umwagiliaji wa mpunga katika Lower Irrigation Moshi, Lower Irrigation Moshi ilianza na hekta 2300 lakini hadi sasa hivi zinalimwa hekta 1100 hii inatokana na miundombinu chakavu ambayo imejengwa tangu mwaka 1987. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama kweli Serikali nia yetu ni kuboresha miundombinu hii katika skimu zetu ni vizuri tukaelekeza nguvu ili tuweze kufanyakazi ya kusaidia wakulima wale ambao wametengeneza mabwawa yao ili Serikali iongeze nguvu ya kutengeneza mabwawa ya kutosha ili kilimo cha umwagiliaji kiwe kilimo endelevu.

Mheshimiwa Spika, nije katika suala zima la kilimo cha tangawizi, wote tunatambua kwamba kwa kipindi hiki cha Corona tangawizi imekuwa ni kilimo ambacho kimeleta tija sana nje na ndani ya Tanzania, hakuna familia ambayo inaweza ikalala bila kukosa kipande cha tangawizi. Kule Same Mashariki katika Mkoa wa Kilimanjaro wilaya ambayo inalima sana zao hili la Tangawizi, wakulima wamekuwa wakilima kilimo hiki kwa shida sana kwa sababu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilimo cha tangawizi kinahitaji maji ya kutosha, wamejaribu kujisukuma wao wenyewe na kutengeneza miundombinu ya maji kwa maana ya kutengeneza mabwawa Wapare wanaita ndiva. Ndiva ni mabwawa madogo.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ili kusaidia kilimo hiki kiweze kukua iweze kusaidia wakulima wale kuwatengenezea mabwawa ambayo yatavuna maji kipindi cha mvua ili kilimo hiki cha tangawizi kiwe kilimo endelevu na kiweze kuwaingizia mapato wakulima wetu pamoja na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nije katika zao la vitunguu, zao la vitunguu linalimwa mkoani Kilimanjaro ni biashara kubwa sana kwa akina mama kule Kilimanjaro ukienda utakuta akina mama wamebeba makarai wanauza vitunguu, vitunguu vinalimwa Himo, vitunguu vinalimwa Hai, vitunguu vinalimwa Ruvu, vitunguu vinalimwa katika Kijiji cha Gonja, Mahore, Mpirani, Kalung’oyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakulima wanatumia nguvu nyingi sana katika kilimo hiki, lakini nguvu zao zote zinaishia pale ambapo maji yanakuwa hayapatikani ya kutosha. Bado niendelee kuiomba Serikali ili kilimo hiki kiweze kushamiri na kuwapatia mapato wananchi. Naomba iendelee, hoja yangu iendelee ile ile ya kuomba Serikali itengeneze mabwawa, na kilimo hiki kimeleta manufaa sana kule Kilimanjaro kwa sababu vitunguu vingi vinauzwa Kenya, soko la Himo ndipo wafanyabiashara wanaotoka Kenya wanapovuka pale na kununua vitunguu hivi, kwa hiyo, ni zao ambalo linawaingizia mapato. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Zuena Bushiri.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuibadilisha historia ya Tanzania kwa kuwa Rais wa kwanza Mwanamke katika nchi yetu, pia nimpongeze Mama yetu kwa kutuletea bajeti ya kihistoria, bajeti ya mwanamke katika Taifa letu la Tanzania. Kule Kilimanjaro wanasema bajeti hii ina mshiko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mawaziri, nimpongeze Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na Watendaji wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi nianze kuchangia katika Sekta ya Nishati. Nimpongeze Rais wetu kwa kusikiliza kilio cha Watanzania wengi ambao Wawakilishi wao ambao ni Wabunge wakaja kulia kilio hiki katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu suala la zima la umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kutoa tozo la nguzo la umeme kuanzia shilingi 327,000 hadi 27,000, Tanzania bila giza inawezekana. Wote tunaelewa kwamba umeme ndiyo chachu ya maendeleo, Tanzania bila umeme hakuna Tanzania ya Viwanda, vijana wetu wengi wamefanya kazi nyingi sana katika nchi hii lakini mara nyingi sana wamekuwa wakikimbilia mijini kwenda kutafuta ajira. Baada ya Sera ya umeme vijijini vijana wengi wamepata ajira katika vijiji, wamejiajiri na hata wengine wameajiri wenzao tuipongeze Serikali katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunao wanawake wengi ambao wanajishirikisha katika biashara za mama lishe, wanawake hawa nao wamefaidi umeme vijijini kwa kuwa wameweza kutengeneza mazingira ya kuboresha biashara zao kama vile kutengeneza juisi na hata kuwa na friji kwa ajili ya kuhifadhi vyakula vyao. Niipongeze sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuipongeza Serikali kupitia nishati nije suala zima la Madiwani. Wote tunatambua kwamba Madiwani wana kazi nyingi sana katika Kata zao nani wawakilishi wetu ambao wanafanya kazi nyingi sana katika maeneo yao. Niipongeze Serikali kupitia Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha Madiwani ambao sasa fedha zao zitakuwa zinatoka Serikali Kuu badala ya Halmashauri zao. Hii itawaletea nguvu sana kwa kuwa watakuwa wanapata fedha zao kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi niiombe Serikali yangu sikivu tunatambua kazi nyingi wanazozifanya Madiwani katika maeneo yao ikitokea misiba wataombwa majeneza, ikitokea shughuli wataombwa hiki na kile, kukiwa na wagonjwa wataombwa usafiri ni hela hizi hizi, posho hii hii ambayo ndiyo wanayoitumia. Niiombe Serikali yako sikivu iwaongezee posho Madiwani hawa, naungana na wenzangu wote waliochangia hili kwamba ni vizuri Serikali ikawatazama sasa na wao waweze kuongezewa posho ili angalau waweze kuendesha shughuli zao vizuri na kwa amani katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije suala la TARURA, niipongeze Serikali Wabunge wengi sana hasa wa Majimbo wamekuwa wakilia kilio cha TARURA humu ndani tukiwepo na sisi wanawake wa Viti Maalum. Wengi wameongea mengi kuhusu suala la barabara, bila barabara hakuna maendeleo, wakulima kilimo kinahitaji barabara, wananchi wenyewe tunahitaji barabara, wameongea wengi wakasema kwamba hata akina mama wengine wakati wakijifungua wanajifungulia njiani kwa sababu ya barabara zetu kuwa mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi wa mwanamke siku zote mwanamke huwa anaangalia mtoto analia nini, mama ameweza kuangalia nini watanzania wanacholilia akajaribu kuleta bajeti hii katika Bunge hili ambalo kila Mbunge amefurahia bajeti hii na kwa kupitia Bunge hili Watanzania wengi kila mtu amefarijika na bajeti hii. Niseme kwamba tozo kwa ajili ya barabara ya TARURA ambayo zaidi ya shilingi milioni 222 zikipatikana nakutekeleza malengo kama ilivyokusudiwa naamini kwamba 2021/2022 ifikapo mwishoni tutakuwa barabara zetu zote zinapitika kipindi chote cha mwaka. Niiombe Serikali ipeleke pesa hizi zikafanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo mimi niunge mkono hoja. Nasema ahsante sana kwa bajeti hii nzuri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuchangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wetu Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anazozifanya katika Taifa hili Mungu aendelee kumlinda na kumbariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Makamu wa Rais, nimpongeze Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri, Spika na wewe Naibu Spika kwa kazi nzuri mnazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi nianze kuchangia katika Sekta ya Maliasili na Utalii. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu yake ya Royal Tour nakuiingizia nchi yetu mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio tunayoyapata, tunapata lakini pia tuna changamoto za wanyamapori. Kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa wananchi wanaoishi kwenye mipaka ya hifadhi. Kumekuwa na matukio makubwa mawili ya Tembo kuua wananchi na Tembo kuharibu mazao ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kilimanjaro tunazo wilaya tatu ambazo ni Wilaya ya Rombo, Mwanga na Same ambazo zinaathirika sana na wanyamapori. Katika Wilaya ya Same vijiji vya Mahore, Muheza, Kihurio, Bagamoyo, Kalamba na Kadando vimekuwa vikiathirika sana na wanyamapori hawa kwa kusababisha vifo kwa wananchi pamoja na uharibifu wa mazao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa fidia, fidia inayotolewa na Serikali ni Sh.25,000 endapo mwananchi atakuwa ameharibiwa zao lake kwa hekari moja. Hivi tunavyoongea nimepata malalamiko kutoka kwenye Kijiji cha Mahore, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mahore ametuma meseji kwamba tuombe msaada kwa kuwa askari wa wanyamapori wamezidiwa na tembo na hivyo wananchi wa maeneo hayo wameacha kazi zao na kwenda kulinda tembo ili kuhakikisha kwamba mazao yao yanakuwa. Naomba sana Serikali iangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo Serikali inatoa Shilingi Milioni Moja kama kifuta machozi kwa mwananchi ambaye ameuawa na tembo. Kulingana na hali ya maisha ambayo tunayo sasa hivi na kupanda kwa vitu, viwango hivi tukiviiangalia haviendani na hali ya maisha. Baba huyu au Mama huyu ambaye atuuawa na tembo, ameacha familia ambayo yeye ndiye alikuwa akitegemewa kiasi cha Shilingi Milioni Moja hakiwezi kusaidia chochote. Naiomba Serikali yangu sikivu, iangalie kwa makini fidia hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote Serikali hii sasa hivi tunayokwenda nayo ya Mama Samia Suluhu Hassan, ni lazima tumpongeze kwa kuwa anajaribu sana kutatua matatizo ya Hifadhi za Wanyama. Tushirikiane Serikali pamoja na wananchi ili tuangalie ni nini ambacho kinaweza kuzuia wale wanyama wasisogee katika makazi ya wananchi ili kulinda mali zao pamoja na uhai wao. Niiombe Serikali kupitia Bunge hili Bajeti ya 2022/2023 iongezwe katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango huo naomba sasa niende katika sekta ya barabara. Niendelee kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri ambayo imefanya, kwa kujenga barabara zetu nchini kote. Niiombe Serikali imalize barabara ambazo zimejengwa vipande vipande ili ziweze kumalizika na wananchi waweze kufaidi katika shughuli zao za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee barabara ambayo imejengwa vipande vipande barabara ya Same – Mkomazi. Hivi karibuni Kamati yangu ya Uwekezaji Mitaji ya Umma tukiwa kwenye ziara tulitembelea Hifadhi ya Mkomazi. Katika mojawapo ya mambo ambayo wameomba Serikali iwasaidie ni barabara ya Mkomazi - Same. Wamedai barabara ile ni fupi kwa wale ambao wanatokea Tanga na Dar es Salaam wanaifahamu, lakini wamesema watalii wengi wanaotokea Dar es Salaam na Tanga wanapenda barabara ile kwa kuwa ni fupi, lakini barabara ile imejengwa vipande kwa vipande, imeanza Kiurio kipande, ikaachwa Ndungu kipande, Maore kipande, Kisiwani kipande.

Mheshimiwa NaibU Spika, hivyo wanaiomba Serikali Hifadhi ya Mkomazi Game Reserve imetuma Kamati ya PIC, Mwenyekiti wangu yupo pale atathibitisha kauli hiyo. Tuiombe Serikali ili watalii wale waweze kupita njia iliyo rahisi kufika katika hifadhi na barabara ile ikiboreshwa kwa madai yao watalii wetu watapata urahisi wa kufika katika hifadhi vizuri na kwa usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana inazofanya na niendelee kuiomba Serikali iangalie yale matatizo ambayo yanawagusa sana wananchi wa Tanzania, kama vifo na kuharibiwa mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)