Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Kassim Hassan Haji (3 total)

MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza, kituo hiki kina miaka 13 hakijamalizika, je, Waziri atakuwa tayari kuongozana nami kwenda kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa uhalifu umeongezeka katika Jimbo la Mwanakwerekwe, sasa hivi kuna vibaka na waporaji wengi lakini hata miundombinu ya Serikali nayo imekuwa ikiharibiwa kwa makusudi.

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na kadhia hii wanayoipata wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu rafiki yangu Mheshimiwa Kassim niko tayari kuambatana naye kwenda katika kituo kile na kukiona. Nimuambie kwamba kituo kile nakifahamu na kipo kwa muda mrefu ni kweli, lakini niko tayari kuambatana naye kwenda kukiangalia kituo kile na kuona namna ambavyo tunaweza tukawasaidia wananchi ili kuimarishiwa hizi huduma za ulinzi na usalaama katika eneo lao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lingine ni kuhusu vitendo hivi vya uhalifu ambapo vijana wanafanya vitendo vikiwemo vya uvunjifu wa miundombinu na uharibifu wa vitu vingine. Ndani ya jimbo lake kuna kituo kingine kikubwa cha Mwanakwerekwe na hicho kinafanya kazi muda wote, hasa kupitia kituo hiki tutajitahidi tuwe tunafanya doria za mara kwa mara ili kuweza kuwakamata na kuwashughulikia wale wote ambao wanavunja amani ama wanafanya vitendo vya uhalifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine tuko tayari kuendeleza na kuimarisha ulinzi shirikishi ili wananchi na wao waweze kutoa mchango wao katika kulinda amani ya wengine. Kikubwa, tuko tayari kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu wale wote ambao watakuwa wanafanya vitendo hivi. Nakushukuru.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa kuna ucheleweshaji mkubwa wa malipo ya watu wanaomiliki maduka hayo na hospitali.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweka njia nzuri ya kuwafanya wamiliki wa maduka yale waweze ku-invest au kuingia katika uwekezaji huu wa kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa mfumo uliokuwepo kabla wa kuandika karatasi na kujaza fomu za kawaida umekuwa ukichelewesha hayo malipo ambayo imekuwa ni sababu mojawapo ya wamiliki wengi wa vituo na maduka kusita kujiunga na Bima ya Afya, lakini sasa bima ya afya imeshatengeneza mfumo mtandao ambapo sasa malipo hayo yanaweza moja kwa moja yakaingizwa kwenye mtandao siku hiyo na akaweza kulipa mapema kila baada ya mwisho wa mwezi.

Kwa hiyo, tunaielekeza Bima ya Afya sasa waweze kufikisha hiyo huduma Zanzibar mara moja ili hilo tatizo liweze kuondolewa. (Makofi)
MHE. HASSAN HAJI KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Hata hivyo, kwa kuwa utaratibu uliokuwepo sasa hivi, wa abiria ambao wanasafiri wanasubiria sana nje kabla ya kuingia ndani. Je, ni lini Serikali hii itatoa maelekezo ya wale abiria ambao tayari wana tiketi, wasisimame pale nje, waingie ndani moja kwa moja na kusubiria usafiri ndani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba eneo ama jengo lilipo la kusubiria abiria pale Dar es Salaam Kwenda Zanzibar lina uwezo wa kubeba abiria 150 na jengo ambalo tutajenga litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 400.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hatua ambayo Serikali inachukua tunaweza ratiba maalum, mahususi kwa boti zote mbili ambapo boti ya kwanza kama ambavyo iko inaondoka saa moja asubuhi, boti ya pili itaondoka saa tatu na nusu, boti ya tatu itaondoka saa sita, nyingine saa nane mpaka saa kumi na mbili. Kwa abiria wote ambao wanakuwa nje na wana tiketi, hawa ndio wanatakiwa waingie kwenye jengo hili ili kuruhusu wasafiri kuliko mwingine yeyote kwa sababu eneo lile bado ni dogo. Kwa hiyo, ni maelekezo kwa Serikali kwa abiria wote, lakini pia wale wote wanaosimamia eneo hili.