Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Kassim Hassan Haji (3 total)

MHE. KASSIM HASSAN HAJI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe ambacho kiliwekwa jiwe la msingi mwaka 2008 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Mwanakwerekwe kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Naibu Spika, Mwanakwerekwe kuna Kituo cha Polisi cha Daraja ā€œCā€ ambacho kinatumika hadi sasa na kinafanya kazi kwa saa ishirini na nne, na eneo hilo lilitolewa na Serikali baada ya kuhamisha Idara ya Maonyesho Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la Magogoni Amani kwa Mabata ndiko kuna jengo la kituo kidogo cha polisi, ambacho kinajengwa kwa nguvu za wananchi na jiwe la msingi liliwekwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka 2008 na ujenzi wake umefikia kwenye hatua ya renta. Serikali kupitia Jeshi la Polisi inatafuta fedha ili kumalizia ujenzi wa kituo hicho kiweze kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuongeza maduka ya kutolea dawa kwa kutumia Bima ya Afya ili kuondoa usumbufu wanaopata wananchi wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba idadi ya maduka na vituo vinavyotoa huduma za Bima ya Afya Zanzibar ni vichache ambapo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni, 2021 hadi Desemba 2021 idadi ya vituo vimeongezeka kutoka 19 hadi 65.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha wamiliki wa vituo vya kutolea huduma za afya na maduka ya dawa kujiunga na huduma ya bima ili kuwafikia wananchi wote. Ahsante.(Makofi)
MHE. HASSAN HAJI KASSIM aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuitanua sehemu ya kusafirishia abiria wanaokwenda Zanzibar katika Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TPA imetenga kiasi cha Sh.1,500,000,000 kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya abiria katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa sasa ni manunuzi ya Mkandarasi kwa ajili ya maboresho ya eneo la kusafirisha abiria kwenda Zanzibar. Maboresho yatahusisha ukarabati wa miundombinu ya gati la kuhudumia abiria ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la abiria ili kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria, kuweka mkanda wa mizigo (conveyor belt), ukarabati wa kingo za gati, maboresho ya sehemu ya abiria mashuhuri (VIP), sakafu na vyoo. Aidha, Mkandarasi anatarajiwa kupatikana na kuanza kazi mwezi wa Desemba, 2022.