Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Ally Juma Makoa (13 total)

MHE. ALI J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante sana; kwa kuwa tatizo la Mji wa Mpwapwa linafanana na Mji wa Kondoa, Halmashauri ya Mji wa Kondoa ina tatizo kubwa la muda mrefu la maji na tatizo ni uchakavu wa miundombinu.

Ni lini Serikali itapeleka fedha kutatua tatizo la miundombinu chakavu ya maji iliyojengwa miaka ya 1970?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Makoa kutoka Kondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ambayo muda wake wa uhai umekwisha kwa maana ya lifespan imesha- expire sasa hivi tayari tumeshaanza mchakato wa kuona namna gani mwaka ujao wa fedha kukarabati labda kwa kubadilisha mabomba kama yamechakaa sana au kuongeza mabomba kwa maana ya mtawanyo wa miundombinu au kuona kwamba kama kipenyo kilikuwa kidogo tutaweka mabomba makubwa kulingana na idadi ya watu namna ilivyoongezeka na uhitaji wa maji safi ulivyoongezeka hivyo nipende kumwambia Mheshimiwa Ali Makoa kuwa Kondoa napo tunakwenda kupaletea mapinduzi makubwa kuondoa changamoto ya maji.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza, nina swali moja tu. Sasa kwa sababu zoezi la ukamilishaji wa ujenzi litachukua muda mrefu kwa kuzingatia majibu ya Mheshimiwa Waziri. Sasa je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga japo daraja la dharura kwa kupitia vyombo vyetu vya jeshi ili kunusuru kesi za vifo pamoja na upotevu wa mali za wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia changamoto za wananchi wake wa Jimbo lake waliompigia kura kumleta hapa Bungeni. La pili, naomba nimwambie kwamba jambo hili tumelipokea, kabla ya kwenda kuomba vyombo vyetu vya Jeshi kuna taratibu zake, naomba nimwelekeze Katibu Mkuu Ujenzi atume mtaalam wetu katika eneo hili ili tuone kama kuna haja ya kujenga daraja la dharura kwa wakati huu na tuweze kulifanyia kazi wananchi wetu waendelee kupata huduma kama ilivyo matarajio ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa barabara hii ya Iboni-Bolisa – Bobali inakabiliwa na athari za mazingira inaendelea kubomoka na kuliwa na maji ambayo yanapita katika mito hii ambapo patakwenda kujengwa vivuko na daraja. Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kulinusuru daraja hili japo kwa kuweka fedha za dharura ili isije ikapata gharama kubwa zaidi ya kujenga daraja badala ya vivuko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, barabara zetu na madaraja haya ambayo yanakabiliwa na athari za kimazingira kama mmomonyoko wa udongo kutokana na maji yote yanafanyiwa tathmini na kuandaliwa mpango kwanza wa kudhibiti madhara haya yatokanayo na athari za kimazingira, lakini pia yanatengewa fedha kwa ajili ya kujenga vivuko au madaraja kuhakikisha barabara hizi zote zinapitika vizuri.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwanza tathmini imefanyika ikiwemo ya kudhibiti mmomonyoko ili barabara ijengwe na kupitika wakati wote. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa wananchi wa Kondoa Mondo, walikuwa wanasubiria ujenzi wa barabara hiyo, sasa hivi inaonekana kwamba imekwepeshwa. Sasa Serikali ina mpango gani juu ya kuijenga barabara hiyo hiyo ambayo imeandikwa kwenye Ilani kutokea Mondo kwenda Kondoa - Bicha – Guseria kwenda kwa Mtoro?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi walikuwa na matumaini, kwamba kilomita hizi 400 zingepita kwenye Daraja la Mto Bubu, je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuharakisha ujenzi wa lile daraja ambalo litaunganisha barabara hii iliyokuwa inategemewa ili kuondoa kero na kuokoa maisha ya wananchi na mali zao vinavyopotea kila mwaka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Barabara ya kuanzia Goima – Mondo - Kondoa – Bicha, ipo kwenye Ilani na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha barabara hii pia itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa daraja katika Mto Bubu, Daraja la Mungui, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Kondoa kwamba tunajua changamoto ambayo ipo, upembuzi yakinifu wa daraja hili umeshakamilika na sasa hivi tutakamilisha usanifu wa kina. Meneja wa Mkoa ameshapewa kibali aandae pia na documents za kutangaza daraja hilo kuanza kujengwa. Kwa hiyo, litaanza kujengwa tu mara baada ya kukamilisha usanifu wa kina.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Moja; kwa kuwa kiwango wanacholipwa wakulima walioharibiwa mazao na wanyama ni kidogo sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kubadili sheria, ili kuweza kuwalipa wananchi kulingana na thamani ya mali zao zinazoharibiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, pamekuwa pakitokea matukio haya ya tembo mara kwa mara katika maeneo hayo hususan Kijiji cha Chemchem, ni lini Serikali sasa itatujengea kituo cha Askari wa Hifadhi, ili kuweza kuzuia athari zaidi katika mzao ya wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza mawili, ya Mheshimiwa Ally Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wananchi wamekuwa wakilipwa kiwango kidogo. Na kiwango hiki cha kifuta machozi ama kifuta jasho ni ile tu kutoa pole kwa wananchi na kuweka mazingira ya ushirikiano baina ya uhifadhi na wananchi, lakini tulipata maelekezo katika Bunge lako hili Tukufu wakati wa bajeti kwamba, tupitie kanuni za sheria hizi na tayari Wizara imeshaanza kuzipitia kwa ajili ya kurejea upya kanuni hizi, ili kifutajasho basi kiweze kuongezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge wa Kondoa Mjini, Mheshimiwa Ally Makoa kwamba, katika bajeti hii ya 2022/2023 tumeoanga kujenga vituo 13, vituo hivi vitapelekwa katika Jimbo lake ili tuweze kupeleka Askari waweze kuendelea na zoezi la kuzuia wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza la nyongeza. Kata ya Suruke imeshajengwa mnara wa TTCL, lakini leo una mwaka mzima haufanyi kazi. Je, ni lini Serikali itawasha mnara ule wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa minara una hatua, hatua ya kwanza ni kuhakikisha kwamba tunajenga ile passive equipment maana yake kusimamisha ule mnara. Hatua ya pili ni kuweka vile vifaa vya kurusha mawimbi maana yake active equipment. Hatua ya kwanza katika minara yote ya TTCL nchi nzima tumeshamaliza na hatua inayofuatia ni kuhakikisha kwamba sasa tunaweka zile active equipment. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kazi hiyo imeshaanza na vifaa vimeshaingia, nina uhakika kwamba kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha hatua zitakuwa zimeshakamilika za utekelezaji katika kusimika hizo acturial equipment. Ahsante sana.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, katika tengo la fedha hizi, je, Serikali itaweka pia na huduma ya taa za barabarani kwa sababu, barabara hii imekatiza katikati ya mji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ni mpango sehemu tunapojenga barabara za lami mijini tunaweka na taa. Na Mbunge atakuwa shahidi kwamba, mpaka sasahivi tumeshaanza kuweka taa za barabarani katika mji wa Kondoa.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Pamoja na majibu ya Serikali, Kondoa Girls hii ilikuwa ni Shule ya Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne, lakini Serikali ilifanya maamuzi ya kuibadilisha kuwa Kidato cha tano na sita na ikawaondoa wale wa O’level. Sasa Kondoa bado tuna uhitaji wa Sekondari ya Bweni ya Wasichana: Je, ni lini Serikali itairudishia sekondari ambayo waliichukua kujengea sekondari ya wasichana ya bweni ya O’Level?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wananchi wa Kata ya Bolisa wana hamu ya kuona sekondari yao ya kata inaazwa kujengwa, na tayari kama Halmashauri ya Mji tulipokea barua ya mapokezi ya fedha: Sasa ni lini Serikali italeta fedha ili wananchi wa Bolisa waanze kujenga sekondari yao ya kata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Makoa, kwanza kutokuwa na shule ya bweni ya wasichana katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Serikali kwa sasa inaweka nguvu katika kuhakikisha kila mkoa unapata shule moja ya wasichana ya bweni ambayo ni kubwa itakayoweza kuchukua watoto katika mkoa husika na tayari shilingi bilioni 30 ilikuwa imeshatengwa, ambapo shule 10 katika mikoa 10 zimeshajengwa na tunaenda kwenye Phase II ambapo tutajenga tena shule tano. Vilevile tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuona Kondoa nao wanapata shule ya bweni ya wasichana ya Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne kadiri ya bajeti itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la Kata ya Bolisa kupata shule yao ya sekondari, nilijulishe Bunge lako Tukufu kwamba tayari Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeshakamilisha michakato yote ya kuweza kupeleka fedha katika Halmashauri zote 184 nchini kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari. Muda siyo mrefu Halmashauri hizi 184 zitapata fedha hii kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ikiwemo Kata ya Bolisa kule Halmashauri ya Kondoa Mjini.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, ninakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yenye kuridhisha ya Serikali nataka kujua sasa, Je, hizo shilingi milioni 300 ambazo zilitengwa kwa kufanya kazi zilizotajwa na Mheshimiwa Waziri hapo, zilitolewa na zikafanya kazi iliyokusudiwa ama walifanya tafiti tu za awali?

Swali la pili, kwa kuwa Serikali ina makusudio ya kufanya kuanza ujenzi mwaka ujao wa fedha, kwa kazi ya kuhuisha sasa hii skimu na hizi ripoti na tafiti, Wizara safari hii imetenga kiasi gani kwa ajili ya kazi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu matumizi ya fedha shilingi milioni 300 kama zilitoka au la. Madhumuni makubwa ya fedha hizi zilikuwa ni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nimesema katika kupata tathmini halisi, tumetenga fedha tena mwaka huu kuhakikisha ya kwamba tunalipitia eneo lote ili kupata taarifa sahihi na kuanza ujenzi wake kwa sababu tumepata changamoto miradi mingi ilipata changamoto kubwa, kwa sababu usanifu wa kina haukufanyika na imekuwa siyo ya kudumu muda mrefu na hivyo kuleta athari kubwa kwa sababu mara kwa mara imekuwa ikibomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunakwenda kurudia kufanya kazi hii kubwa katika umakini mkubwa zaidi na ku-involve wataalam wengi zaidi ili tupate kitu ambacho kitaleta tija kwa wananchi wa Kondoa Mjini.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kuhusu fedha kama zimetengwa. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba tunajiandaa kufanya zoezi hili katika mwaka wa fedha 2023/2024 ili ujenzi uanze katika mwaka wa fedha unaokuja 2024/2025. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia namna ya kuweza kulifanikisha kwa uharaka kwa sababu tunajua wananchi wa Serya na eneo la Mongoroma ni wakulima wazuri hatutaki kuwachelewesha, tutafanya kwa uharaka ili wafanye kilimo cha umwagiliaji katika eneo lao. (Makofi)
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanz; Mji wa Kondoa Mjini una hali mbaya sana hasa kipindi cha mvua kwa kuwa na mafuriko katikati ya mji. Je, Serikali inaweza ikatupa fedha kwa ajili ya kujenga mitaro kuzuia yale mafuriko kutokea mitaa ya Uwanja wa Puma mpaka katikati ya mji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tuna barabara ya kilomita kama moja kutoka barabara kuu kwenda katika Ofisi za Mkurugenzi maana yake majengo ya halmashauri . Je, Serikali ipo tayari kusaidia fedha kwa ajili ya kuweka lami kwa sababu ya ule muundombinu uliowekwa pale, jengo zuri la thamani kubwa lakini barabara ya tope?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba katika bajeti ambayo tumepitisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, sehemu ya fedha ambazo tumeziweka ni pamoja na Jimbo la Kondoa na sehemu ya fedha hiyo itahusika katika ujenzi wa mitaro ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Kwa hiyo nimwondoe shaka tu kwamba kwa kuwa tumeshapitisha bajeti, basi tutakwenda kutekeleza kama ambavyo yeye amehitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusiana na mahitaji ya kilomita moja kutoka barabara kuu ya lami kwenda katika jengo lao la halmashauri, niseme tu ombi hili tumelipokea japo tunatambua kwamba Mradi wa TACTIC sehemu mojawapo ni kutekeleza mradi huu ambao Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba nimeuliza swali ni lini, nilitegemea ningeambiwa mwezi ujao maana yake imekuwa ni story ya muda mrefu; nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, vituo vya afya vilivyopo Kata ya Suruke, Kingale pamoja na sasa tunajenga Kolo vitakuwa miongoni mwa orodha ya mgao huo?

Mheshimiwa Spika, la pili; kumekuwa na hofu kubwa kwa wananchi wa Kondoa wanaopata huduma katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji hasa wanapopata kesi ya kufanyiwa operation, sasa pamoja na ahadi hiyo ya kupatiwa ambulance wamekuwa wakipata rufaa kwa tabu sana kuletwa Hospitali ya Mkoa lakini hata hivyo, wananchi wamekuwa na mashaka makubwa.

Je, Serikali itakuwa tayari lini kwenda kujiridhisha na uwezo wa madaktari pamoja na vifaatiba vilivyopo katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatayo: -

Mheshimiwa Spika, fedha ambazo zinakwenda kununua magari haya ya wagonjwa 195 ambazo zinatoka kwenye mpango wa UVIKO-19 zitakwenda kununua magari haya na yatapelekwa kwenye Halmashauri zote 184 lakini ni maamuzi ya halmashauri kuona uhitaji mkubwa katika ngazi ya hospitali au katika kituo cha afya ambako gari litapelekwa. Kwa hiyo, ni maamuzi ya halmashauri kuona kipaumbele kwa wakati huo gari hilo litakwenda kwenye kituo cha afya au kwenye hospitali ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tunapanga kununua magari haya na UNICEF kuna uwezekano mkubwa magari ya wagonjwa yakaongezeka zaidi ya 195. Kwa hiyo, tunauhakika vituo vyetu pia ambavyo vimekamilika vitapata magari ya wagonjwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uhakika wa huduma katika Hospitali ya Mji wa Kondoa kwa maana ya uwezo wa madaktari na vifaatiba; madaktari wote wanaoajiriwa kwa ngazi zao wanakuwa wamesajiliwa na Serikali imejiridhisha juu ya uwezo wao wa kutoa huduma. Kwa hiyo, niwatoe hofu wananchi wa Mji wa Kondoa kwamba madaktari waliopo pale ambao wamepelekwa na Serikali wana uwezo unaotakiwa, wanatoa huduma ambazo zinatakiwa, lakini kama kuna mapungufu Serikali tutafuatilia na kuchukua hatua katika maeneo hayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa fidia aliyoitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ililipwa mwaka 2014 wakati barabara ilikuwa na upana wa mita 22. Mwaka 2017 walipokamilisha ujenzi wa barabara ile waliongeza mita nane kufika 30 na yenyewe ikachukua madarasa na nyumba ya malimu, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mbarawa alifika akaiona ile hali na akatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kutoa michoro pamoja na gharama na Mkurugenzi akafanya hivyo.
Napenda kujua sasa ni lini Serikali itatekeleza kupitia TANROADS ujenzi wa ile Shule ya Msingi Unkuku kwa sababu imeliwa sana na barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari niambatane naye pamoja na wataalam wake tukaione hii Shule ya Msingi Unkuku ilivyo katika mazingira hatarishi kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja. Ni kweli kwamba Serikali ililipa fidia wakati huo barabara ikiwa na upana wa mita 22.5. Kama alivyosema kwa sababu mimi mwenyewe sijaenda, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Kondoa na Dodoma ni karibu, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaongozana, tutafute siku mimi pamoja na wataalam ili twende eneo la shule tukaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umetolewa mwongozo kwamba pale ambapo miundombinu ya shule, zahanati ama hospitali zinakuwa zimepitiwa na barabara kwa maana ya kuifuata, hatutakuwa tunatoa fidia badala yake tutakuwa tunajenga ile miundombinu yote iliyoathirika. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakwenda na haya yote yatajibiwa ikiwa ni pamoja na kuona uwezekano kama kuna haja ya Serikali kujenga hiyo shule upya ama kutoa fidia, basi tutafanya hivyo baada ya kufika site, ahsante.
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, kuuliza maswali ya nyongeza. Nina maswali mawili, kama Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, nimewauliza wenzangu kule Kondoa, kwamba yapo majengo yaliyokamilika na mitambo na vitu vingine kama hivi vimejengwa Kondoa, lakini sifahamu huo mradi mkubwa namna hiyo umefanywa halafu Mwakilishi wa Wananchi na hata Mkuu wa Wilaya hana habari. Sasa ninataka kujua, je, majengo haya yamejengwa wapi? Na mitambo hii imejengwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, majibu ya kusema tathmini itaanza, ninapenda kufahamu hapa nyuma tumeambiwa Serikali imetoa minara mingi sana kwenye nchi hii karibu wilaya zote. Hapa ninapokuambia jimbo langu si vijiji ni mitaa, kwenye minara mitano iliyokwenda Kondoa hakuna mnara hata mmoja ambao unakwenda kwenye Mtaa wa Jimbo la Kondoa Mjini. Wewe ni shahidi ukitoka Dodoma kilomita 30 tu, kuelekea huko tayari mawasiliano yote yanakatika barabara hii ni kubwa. Sasa ninataka nijue Serikali inawaambia nini Wananchi wa Kondoa Mjini na Mitaa yake ambayo haina mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli alivyoingia tu Bungeni hoja yake ya kwanza ilikuwa nikuhakikisha kwamba Kondoa wana Mtambo ambao utaenda kuhudumia Wananchi wa Kondoa, ili TBC iweze kusikika kwa ajili ya wananchi wake. Serikali ilipokea ombi lake na tayari Serikali imeshajenga, imejenga mnara imejenga jengo na pia, imeshaweka jenereta. Eneo gani mtambo huu umejengwa? Ukiwa unaelekea Arusha upande wa kulia pale ambapo majengo ya halmashauri yanapojengwa pale, kwenye kona pale na ndio mtambo wetu upo na mnara wetu upo pale. Mimi mwenyewe ninaufahamu na nilishafika pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoweza kusema ni jambo moja kwamba ninawaomba TBC wanapoenda kutekeleza miradi ya maendeleo ndani ya Majimbo ya Waheshimiwa Wabunge wahakikishe wanawashirikisha Waheshimiwa Wabunge pamoja na Madiwani na Ofisi za Halmashauri ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa nishirikishi. Kwa hiyo, hayo ni maelekezo yangu kwa TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kweli tumeshafanya tathmini. Tunapofanya tathmini hatua ya pili nikupata fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano. Maeneo yetu bado ni mengi ambayo bado yana changamoto. Kipaumbele cha Mheshimiwa Rais, ilikuwa ni kuhakikisha maeneo ya mipakani, kuhakikisha maeneo ambayo yapo vijijini. Vile vile, kuhakikisha tunawashawishi watoa huduma wakawekeze katika maeneo ya mjini ili kuhakikisha kwamba haya maeneo yote yana huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninampa matumaini Mheshimiwa Mbunge, kwamba jambo lake la Kondoa ni jambo la Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na tunalipokea tutaenda kulifanyia kazi na kuchukua hatua stahiki ili wananchi wa Kondao wapate huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)