Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Ally Juma Makoa (6 total)

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. ALLY J. MAKOA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri ambayo kwa kweli imezidi kutuimarisha na ninadhani Serikali imesikia. Ninawashukuru Mawaziri waliochangia lakini kipekee kabisa nimshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo yake mazuri ambayo ameyatoa hapa mbele ya Bunge, ni matumaini ya Kamati kwamba sasa Serikali itakwenda kuyafanyia kazi mawazo ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, pamekuwa na hisia kubwa sana kwa upande wa Ngorongoro lakini lazima na Bonde la Kilombero na lenyewe litiliwe mkazo kama jinsi ambavyo Ngorongoro inavyotiliwa mkazo kwa sababu Bonde lile na lenyewe likiachiwa yatakuja kutokea madhara makubwa pengine kama haya yanayoweza kutokea Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, sasa ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali kupoipokea taarifa yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ALI J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dokta John Joseph Pombe Magufuli, Mama Samia na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Pia nitoe shukrani kwa Mawaziri wa Awamu iliyopita kwa kazi kubwa waliyomsaidia Rais wa nchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri yaliyofanyika awamu iliyopita, pia mimi mchango wangu katika mpango huu ni kama ifuatavyo, moja nitagusa sehemu ya kilimo. Kama tunataka tufikie malengo ya kilimo katika nchi yetu ni lazima kwanza mambo yafuatayo yafanyike. Moja, tuhakikishe ile migogoro mikubwa ya mashamba kati ya wananchi na taasisi za Serikali inamalizwa mapema ili kutoa nafasi kwa wananchi kuendelea kufanya kilimo. Iko migogoro kati ya wananchi na Jeshi la Magereza kuhusiana na mashamba na imechukua muda mrefu kiasi ambacho imekuwa ikisimamisha shughuli za kilimo kwa wananchi hasa maeneo ya Kingale kwa kule kwetu Kondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tujikite katika mbegu. Soko la jana nilikwenda katika maduka ya mbegu, mfuko wa kilo mbili wa alizeti unauzwa kati ya Sh.15,000 mpaka Sh.16,000. Kwa hiyo, Mpango ungejiwekeza katika maeneo ya uandaaji wa mbegu ili kurahisisha upatikanaji wa mbegu kwa bei nafuu kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kuhusu viwanda. Tumekuwa na viwanda vingi sana katika nchi hii. Nimekuwa Mkoa wa Pwani, tumekuwa tukiuita Mkoa wa Viwanda kwa sababu viko viwanda ambavyo vinaonekana, ni kazi kubwa iliyofanyika katika Serikali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne, Mpango huu unatakiwa uendane sambamba na kuweka tahadhari ya kuilinda miundombinu pamoja na mali za wenye viwanda. Nimewahi kushuhudia kiwanda kinaungua moto mpaka kinamalizika hakuna zimamoto. Kwa hiyo, nashauri kwenye Mpango huu wakati tunaandaa mipango ya viwanda tujaribu na Wizara nyingine ziwe zinashirikiana katika kufanya ulinzi. Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti Kondoa kiliungua mpaka kikamalizika hakuna zimamoto. Walipofanya juhudi ya kutafuta zimamoto Babati, Manyara, zimamoto linapatikana kiwanda kimeungua mpaka kimeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wawekezaji wa mabasi, muda mfupi badaye basi la abiria pia likaungua mpaka linamalizika, hakuna zimamoto. Kwa hiyo, tunaomba katika Mpango huu pia, Wizara ya Ulinzi iangalie maeneo yale ambayo yanakosa zimamoto yatufanyie mpango wa kupata zimamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, Mpango huu tunaomba uimarishe uwajibikaji, uadilifu na uaminifu katika sekta zote ambazo watu wamepewa majukumu ya kumsaidia Mheshimiwa Rais ikiwepo kwenye eneo la TRA. Bado kuna mianya mingi sana ya kodi kupotea na yako maeneo mengi kabisa kodi hazilipwi. Kwa hiyo, Mpango huu uendelee kuweka mkakati kwa ajili ya kuhakikisha kodi ya Serikali inaingia hasa kwa kutumia zaidi TEHAMA katika ukusanyaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ALI J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kuniona. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake mbalimbali anazotujaalia, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuumba mja wake Dkt. John Joseph Pombe Magufuli na akamjaalia kuwa Rais wa nchi hii na yeye akaitendea haki nchi hii kwa kufanya mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ndiyo mara yangu ya kwanza pia kusimama katika Bunge lako hili,nikishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua na kunifanya kuwa Mbunge. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini kwa kuniamini na kunipa kura nyingi za kishindo na mimi kuwa mwakilishi wao.Ahadi yangu kwao ni kwamba tutafanyakazi kwa bidii kubwa kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi. Vile vile niishukuru familia yangu mama Hashim na watoto wangu wawili kwa kuendelea kunipa nguvu katika kufanyakazi za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepitia hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais ile ya 2015 na hii kwa kweli hotuba zote mbili hizi zimejaa kila aina ya miongozo kwa ajili ya kuliletea neema Taifa hili. Ukweli ni kwamba pamoja na michango yetu yote tutakayochangia bado haitoi maana ya kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano, imefanya mambo makubwa sana katika Taifa hili. Hivyo basi, katika kuchangia mimi nitakwenda ukurasa wa 10, Wizara ya Afya. Serikali ya Awamu ya Tano imepunguza kwa kiwango kikubwa sana vifo vya mama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano. Kama tutamsaidia Mheshimiwa Rais kikamilifu basi tutaendelea kupunguza vifo hivi, lakini kama tutazembea, hatutaweza kumsaidia Mheshimiwa Rais, bado vifo hivi vitaendelea kupanda.

Mheshimiwa Spika, kwenye hiki kifungu cha akinamama wajawazito kumekuwa na malalamiko makubwa sana kwa wananchi kwamba sera za afya na Ilani ya CCM, utekelezaji wa sera unakinzana na Ilani ya CCM, Ilani ya CCM inaelezea kwamba tutaendelea kutoa huduma bure kwa akinamama wajawazito na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano,lakini uhalisia haupo hivyo. Akinamama wamekuwa wakitozwa gharama katika kujifungua na akinamama wengi katika ziara zangu wamekuwa wakizungumza wengine wameamua kusimamisha kujifungua kwasababu ya gharama kubwa za afya.

Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali za kupunguza vifo zinaweza zikawa zinamikwamo kwasababu wapo akinamama ambao wameamua kujifungulia majumbani kwasababu wanaogopa kwenda kujifungua hospitali wakiogopa gharama. Sasa kama hili litaendelea na wakahamasishana akinamama basi juhudi za Serikali za kupunguza vifo hivi zitakuwa zimekwama.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kondoa Mjini linaeneo ambalo limetengwa naMto Bubu. Miezi miwili iliyopita tumepata kesi za vifo, mama mjamzito akisubiria maji yapungue aende hospitali kujifungua maji hayakupungua akajifungulia upande wa pili wa barabara, mtoto akafariki,mama wakawa wanamkimbiza wampeleke Hanang, yule mama pia akafariki.

Kwa hiyo kutokana na hali hii iko haja ya Serikali kuona namna gani wanaweza wakasaidia ng’ambo ile ya Kata ya Serya ambayo haina kituo cha afya wala zahanati na wakati huo huo hawana uwezo wa kipindi cha masika kuja mjini kwaajili ya kutafuta huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kero kubwa sana katika maeneo hayo ambayo yanazungukwa na huo Mto Bubu. Kwahiyo ombi letu watu wa Kondoa tunaomba aidha yafanyike mambo mawili katika moja; kulijenga lile daraja ili watu waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi pamoja na kupata huduma za afya au kujenga kituo cha afya katika maeneo yale ya Serya.

Mheshimiwa Spika, eneo la kilimo wako wananchi ambao mashamba yao yaliharibiwa na tembo na wakaahidiwa muda mrefu sana watalipwa kifuta jasho. Mpaka leo watu wale wanadai, hawakulipwa fedha zao, lakini wananchi wa Kondoa wanalalamikia suala la kulipwa kifuta jasho.

SPIKA: Mheshimiwa Makoa, tembo walifika Kondoa Mjini?

MHE. ALI J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, jimbo langu lina maeneo ya mjini na vijijini. Ipo Kata ya Kingale na Kata ya Serya ipo pembezoni mwa Hifadhi ya Swagaswaga. Kwa hiyo, tembo wale waliharibu mashamba ya watu lakini vifuta jasho wanavyopewa haviendani na thamani ya mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunataka kupata mabilionea kupitia wakulima basi Wizara ione haja sasa ya kuangalia uwezekano wa kudhibiti tembo wale na kuwalipa wananchi fidia ya maeneo yao na siyo vifuta jasho. Kwa sababu kifuta jasho analipwa pesa ndogo sana ni bora alipwe fidia ili ile dhana ya kuwa na mabilionea kutokana na kilimo basi ipatikane.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni ajira kwa vijana. Serikali yetu imefanya vizuri sana kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vijana. Hata hivyo, katika sera ya mfuko ule nashauri kwamba akaunti ya mikopo ya vijana ingetofautishwa na akaunti zingine za halmashauri ili wakati wa kupanga bajeti ya kuviwezesha vikundi asilimia 10 ya bajeti ya mwaka huu iwe inaendana na zile asilimia 10 zilizopita ambazo zimerejeshwa. Tofauti na ilivyo sasa asilimia 10 inayofanyiwa hesabu ya current year lakini yale marejesho yanaingia kwenye akaunti ya maendeleo. Kwa hiyo, tunashindwa kujua uhalisia hasa marejesho yamekuwa ni kiasi gani na asilimia kumi ya safari hii ni kiasi gani ili kuwawezesha wale vijana, kinamama na walemavu kuweza kupata fedha ambazo zitawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaona vikundi vingi ambavyo vinapewa mikopo utakuta watu kumi wanapewa shilingi milioni 10, ukipiga hesabu ni shilingi milioni moja moja unashindwa hata kuwashauri wale vijana wafanye biashara gani. Mikopo hii maeneo mengi imekuwa siyo neema kwa vijana, wengi wamekimbia nyumba zao, wameshindwa kulipa madeni kwa sababu wanapewa mikopo kabla ya kupewa elimu ya kuifanyia kazi mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa namna ambavyo imefanya juhudi kubwa ya kujenga miundombinu ya barabara. Hata hivyo, kilio kilekile cha wananchi ni kwamba kipindi hasa hiki cha masika barabara nyingi hazipitiki. Kwa jimbo langu eneo ambalo linashughulikiwa na TANROADS mpaka sasa ni kilomita kama 0.8. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwa miaka yote mitano TANROADS wanaweza wasitie mkono au mguu katika jimbo langu. Eneo kubwa linachukuliwa na TARURA, uwezo wa TARURA ni mdogo kwa maana hiyo, tunaomba TARURA waongezewe nguvu kwa sababu barabara nyingi sasa hivi zinashikwa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ALI J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara lakini pia mimi nichangie katika eneo la elimu. Niikumbushe Wizara ya TAMISEMI kwamba Serikali ilichukua Shule ya Wasichana ya Kondoa na kuifanya shule ya Advanced Level na hivyo ikawa ni shule ya kidato cha tano na cha sita, lakini shule ile ilikuwa ni ya O-Level. Baada ya Serikali kuibadilisha hatukupata tena sekondari ya bweni ya wasichana ya Kondoa. Kwa hiyo, naomba katika mpango wa Wizara wa ujenzi wa sekondari kumi za bweni za wasichana, basi waende wakaifidie ile sekondari katika Jimbo la Kondoa Mjini ili mabinti zetu wa kidato cha kwanza hadi cha nne waweze kuendelea kupata masomo katika mazingira mazuri.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa elimu, tuna shule yetu shikizi ambayo sasa hivi imekwisha mature. Shule ile wananchi walijenga, sasa tuna madarasa manne, wako wanafunzi 300 ina mwalimu mmoja. Kwa hiyo, naiomba Wizara watusaidie kujenga majengo matatu ikamilishe majengo saba ili wanafunzi wale waendelee kusoma na isajiliwe iwe shule kamili ya msingi. Tukisema kuwarudisha katika shule mama itakuwa ni vigumu kutokana na mazingira magumu na umbali wa kutoka Chang’ombe hadi shule mama ilipo eneo la Tumbelo.

Mheshimiwa Spika, naishauri na kuiiomba Serikali kwamba walimu waliojitolea ni wengi, basi walimu wale katika ajira hizi wapewe kipaumbele kwa sababu wametumia muda wao mwingi kujitolea kufundisha katika sekondari hizo. Pia nishauri, wapo vijana wengi waliomaliza masomo ya ualimu, hawana kazi wako mitaani wakati Serikali inafanya mpango wa kuwaajiri basi watoe tamko la wale vijana waendelee kwenda kuzisaidia shule zetu kwa kujitolea angalau wawekewe fungu hata la kupata fedha ya nauli na sabuni kwa ajili ya kujikimu.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa afya, tunafahamu Hospitali yetu ya Wilaya ya Kondoa ilijengwa miaka mingi sana. Leo vituo vya afya vinavyojengwa kwenye kata ni bora kuliko Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ni hospitali kongwe sana. Naomba sasa katika ule mpango wa Wizara wa kujenga hospitali mpya, wafikirie namna gani sasa ya kupeleka fedha pia Kondoa kwa ajili ya kujenga hospitali mpya ukizingatia sasa Kondoa ni Halmashauri ya Mji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga barabara nzuri sana Kondoa, kwa hiyo, mazingira ya barabara ile yanavutia ajali nyingi. Mara nyingi zinatokea ajali, majeruhi wanapopelekwa kwenye hospitali ile wanakosa huduma na hivyo wanapewa transfer kuja Dodoma. Wakati huohuo, hospitali ya mji haina hata ambulance, kwa hiyo, wanaanza kuhangaika kutafuta ambulance kuwaleta watu Dodoma. Kwa hiyo, naomba mambo mawili hayo kwamba katika mpango wao waweze kusaidia kuijenga Hospitali ya Halmashauri ya Mji lakini pia basi wapeleke ambulance kwa ajili ya kusaidia watu wanapotakiwa kupewa transfer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine kwenye hospitali hii tunayo X-ray ya kisasa kabisa lakini watu wanakwenda kupimwa pale wanapewa CD wanakuja kusomewa majibu Dodoma. Tunaomba basi papelekwe mtaalam kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, cha ajabu zaidi ni kwamba hospitali kongwe haina chumba cha maiti. Juzi imetokea ajali watu karibu nane wamefariki lakini hatuna mortuary. Kwa hiyo, tunaomba watusaidie kujenga mortuary kwa ajili ya kuhifadhi maiti wetu.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa miundombinu, matatizo ni kama yalivyo katika Halmashauri nyingine; barabara zetu ni mbovu. Tulikuwa tunaomba, Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Kondoa itenganishwe wapatikane Mameneja wawili wa TANROADS ili mmoja afanyie upande wa Kondoa DC na mwingine Kondoa Mjini ili kuwapunguzia mzigo maana eneo ni kubwa sana. Izingatiwe Kondoa ni kubwa imetoa wilaya mbili na majimbo matatu. Kwa hiyo, ni wilaya kubwa sana, tunaomba tupate Meneja wa tofauti kati ya Wilaya ya Kondoa na Kondoa Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa wakati huu. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii lakini niwapongeze Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Chande kwa wasilisho lililo zuri kabisa kwenye bajeti yao. Nilikuwa naomba nichangie eneo dogo la mazingira wewe unafahamu mji wa Kondoa umekatiza mto mkubwa pale, sasa mto ule umehama kutoka njia yake ya asili kwenda mto mkondo mdogo.

Mheshimiwa Spika, huu ni msimu wa pili madhara yanayotokea kwenye mto ule ni makubwa sana nilikuwa naomba Wizara iweke fungu kwa ajili ya kuurudisha ule mto kwenye mkondo wake wa asili. Kwasababu madhara ambayo yanatokea kwa hivi sasa kwanza maji ni mengi yana-force kuingia kwenye mkondo mdogo, mashamba ya watu yanaendelea kumegwa na maji yanaelekea kwenye nyumba za watu, kama hatujaudhibiti kwa kwa wakati mto ule maeneo ambayo yanakwenda kuathirika ni pamoja na shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shule ya msingi Mpalangwi eneo lote la kanisa la Katholic makaburi yaliyopo kule pamoja na Chuo cha Bustani, kwasababu mto wenyewe ule ni mdogo sana maji yanatafuta njia mbadala ya kupita, kwa sasa kwasababu ni mkondo mdogo maji yanaingia mashambani yanakwenda kuharibu mazao ya wananchi. Lakini sio hiyo tu miundombinu ya TANESCO pia ipo mashakani kwasababu zipo nguzo ambazo tayari na zenyewe zimekwisha kufikiwa na maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba watenge fedha kwa ajili ya kurejesha ule mto katika chanzo chake cha asili. Aidha, Mheshimiwa Waziri aagize watu wa NEMC waende wakafanye tathmini mapema ili kuweza kuurejesha ule mto katika chanzo chake cha asili. Hasara nyingine inayojitokeza barabara ile inayotoka Iboni kuelekea Bolisa mpaka Gubali inakuwa haipitiki kwasababu Serikali itakuja kuingia gharama kubwa ya kujenga madaraja makubwa.

Mheshimiwa Spika, msimu wa mvua uliopita daraja ambalo lilijengwa na gharama kubwa na Serikali lilisombwa na maji zima zima kama lilivyo likahamishwa zaidi ya mita 200, kwa hiyo, pale fedha ya Serikali ilipotea kabla daraja halikuanza kujengwa, ni kwasababu ya nguvu ya maji ambayo ilikuwa inatoka kwenye mto mkubwa kwenda kwenye mto mdogo. Nilikuwa naomba tu eneo hili ili kuokoa hata shughuli za kiuchumi za wananchi wa kata ya Kondoa Mjini na Kata ya Bolisa kuelekea kata ya Kolo Gubadi zile barabara ili ziwe salama inabidi mto huu urejeshwe kwenye mkondo wake wa asili.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo ninakushukuru sana kwa nafasi hii ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini niwapongeze Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na hata Kamishna Mkuu wa Ardhi kwa kazi kubwa wanazozifanya. Pia nisiwe mchoyo wa fadhila kumpongeza Kamishna wa Mkoa ndugu yangu Kabonge kwa majukumu makubwa anayohudumia Mkoa wa Dodoma, katika kuhakikisha wananchi wanapata hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, niendelee na mchango wangu kwamba ardhi ni bidhaa pekee ambayo kama tutaitumia vizuri Taifa letu litaendelea kupata kipato endelevu. Ni kipato ambacho hakiyumbi kwa sababu hatutegemei kwamba kuna mwaka mapato yanayotokana na ardhi yatapungua kwa sababu kila mwaka tunapima ardhi na watu wanaendelea kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni chanzo pekee cha uhakika cha mapato ya Taifa letu ni lazima sasa kuiwekea miundombinu rafiki Wizara hii ili kuhakikisha mapato yanayotokana na ardhi kila mwaka yanaendelea kupanda. Nyenzo mojawapo ni kusaidia Wizara hii kupata watumishi wa kutosha katika zoezi la kuhakikisha kwamba upimaji wa ardhi unafanyika kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri nyingi hazina Maafisa wa Ardhi. Unakuta halmashauri ina afisa mmoja huyo ndio apime, huyo ndio aandae ramani, maana yake utagundua kwamba hatuwezi kufikia malengo ya upimaji wa ardhi kama tunavyohitaji. Kwa hiyo Serikali iangalie, katika ajira ni vyema kuipa kipaumbele Wizara ya Ardhi kuajiri watendaji wa ardhi ili kuhakikisha kwamba zoezi hili la upimaji linakwenda kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyo Mezani ni ardhi. Watanzania wengi vipato vyao ni vya chini sana. Mifumo ambayo inatumika kumilikisha ardhi ni mifumo ambayo si rafiki kwa Watanzania wengi ambao vipato vyao ni vya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, naweza nikasema kwamba, ardhi inaweza ikawa inauzwa milioni nne kwa kima cha chini na mnunuzi anatakiwa alipe kwa muda mfupi sana; miezi mitatu. Unajiuliza, ni Mtanzania wa aina gani huyu ambaye amelengwa kununua ardhi kwa bei kubwa kiasi hicho, hali ya kuwa kipato chao ni kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nashauri sasa Wizara ya Ardhi ikishirikiana na TAMISEMI, kwa maana ya halmashauri, watafute miundombinu, watafute njia rahisi za kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anamiliki ardhi kutokana na kipato chake alichonacho. Wanaweza wakaenda kupata wawekezaji. Mfano, wanaweza kuingia kwenye mabenki wakawa wanatoa hati, hati zinakwenda benki, Watanzania wenye kipato cha chini kidogo wakawa wanagomboa hati zao mabenki kwa kipindi hata cha miaka mitatu mpaka mitano, lakini kwa miezi mitatu Watanzania wachache sana wataweza kumiliki ardhi. Nina ushahidi; vijana wengi wamerudisha ardhi baada ya kushindwa kukamilisha malipo kwa sababu wameshindwa kutekeleza mkataba walioingia wa kulipa ardhi kwa kipindi cha miezi mitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hilo la wananchi wengi kushindwa kununua ardhi linakwamisha mapato ya ardhi kwa sababu kama ardhi hainunuliwi maana yake hati hazitaandaliwa. Kama hati hazitaandaliwa maana yake Serikali itapoteza fedha nyingi kutokana na hati, lakini kama hati nyingi zitanunuliwa, Serikali itapata fedha nyingi sana. Kwa hiyo tuweke mfumo rahisi wa wananchi kupata hati mapema. Ikiwezekana, wananchi wauziwe hati na siyo wauziwe maeneo. Maandalizi ya hati yatangulie halafu ndipo watu watangaziwe kuuziwa viwanja ambavyo tayari vimekamilika hati. Hapo Ardhi itaendelea kupata fedha kupitia hati zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na migogoro; nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wanashughulika kikamilifu sana kutatua migogoro ya ardhi. Sasa pale kwetu, nilizungumza na Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna migogoro mitatu ambayo inawasubiri wao tu ili iweze kukamilika. Hapa nimekubaliana na usemi wake wa kusema kwamba, maeneo yote ya wananchi yaliyochukuliwa hayakulipwa fidia, warejeshewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna mgogoro ambao upo baina ya wananchi na halmashauri na wamiliki. Halmashauri imechukua maeneo ya mtu, ya wananchi, haikulipa fidia. Lakini imeyapima yale maeneo na maeneo yamekwishauzwa kwa wananchi na wananchi wamekwishalipa fedha zao. Sasa wananchi wenye maeneo hawakulipwa fidia, wamezuia shughuli yoyote ya maendeleo kama matamko ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo namwomba ile nia yake ya kwenda Kondoa kwa ajili ya kusaidia kutatua huu mgogoro kila mmoja apate haki yake, aendelee kuwa nao. Naomba baada ya zoezi hili tufuatane naye kwa ajili ya kwenda kutatua mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mgogoro mwingine wa ardhi wa wananchi, kijiji pamoja na Hifadhi ya Swagaswaga. Wananchi wa Mongoroma na maeneo yanayopitiwa na hifadhi ile wao wanalalamikia mipaka. Najua siku atakayokuja Waziri, tutakwenda kutembea na kuwasikiliza wale wananchi. Zoezi hili la migogoro ya ardhi inayohusiana na mipaka ni matumaini yangu kwamba tutakwenda kulimaliza kama tutafika kwa wananchi kuwasikiliza halafu sisi wenye mamlaka, Mheshimiwa Waziri, viongozi pamoja na wananchi na mimi Mwakilishi wao, tukae tuone namna gani tunakwenda kuitatua hii migogoro ili wananchi waendelee na shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro namba tatu upo kati ya wananchi wa Iyoli na maeneo yanayohusiana na mgogoro Kata ya Kingale kati ya wananchi na Magereza. Waliotoa viwanja kukaribisha Gereza la King’ang’a wapo. Wenye kumiliki gereza hilo wapo. Viongozi tupo na sisi wawakilishi pia tupo; tunashindwaje kwenda kumaliza mgogoro huu ili wananchi waendelee na shughuli za kilimo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nina matumaini makubwa sana. Ahadi ya Waziri ya kwenda Kondoa kumaliza migogoro hii ikikamilika wananchi watakwenda kufanya shughuli zao za kujiongezea kipato na migogoro hii ambayo inaendelea itakuwa imekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)