Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Alexander Pastory Mnyeti (5 total)

MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kusikitika sana kwamba majibu anayoandaliwa Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam mengi ni ya uongo. Anaposema kwamba kule Nyanhomango maji yapo milioni ngapi sijui, ni uongo mtupu.

Mheshimiwa Spika, nataka nikwambie mimi ile Ihelele tunayoisema ndiyo chanzo kikubwa cha maji kinachopeleka maji Tabora, Nzega, Kahama, Shinyanga na maeneo mengine. Sisi hatuna tatizo na maji yanakwenda wapi; sisi shida yetu ni tupate maji kwenye kijiji hicho na maeneo yanayozunguka. Ni chanzo kikubwa lakini leo ni zaidi ya miaka 15 wananchi bado wanahangaika na maji kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, sasa kinachosikitisha ni hao wataalam wetu walioko huko. Mimi nimemaliza ziara juzi pale; hakuna hata tone la maji. Hizo DP anazozisema Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba ma-DP yamewekwa zaidi ya miaka 10 yanakwenda Mbarika halafu hayatoi hata maji. Sasa majibu haya Wanamisungwi wajue tu kama hamtaki kupeleka maji, lakini majibu haya yametolewa miaka 15 iliyopita yanaendelea kutolewa hayohayo, hatuwezi kufurahishana kwa staili hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hawa wataalam wanaoandaa haya majibu kwenda kwa Naibu Waziri, ni majibu ya uongo na wanatakiwa kuchungwa.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Mbunge lakini nataka nimhakikishie kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa sana katika Jimbo lake la Misungwi. Hivi karibuni tulikuwa na Mheshimiwa Rais na tumezindua mradi wa bilioni 12 katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji hayana mbadala na sehemu kwenye chanzo toshelezi, maelekezo ambayo tumeyatoa sisi kama Wizara ya Maji ni kuhakikisha kwamba kabla hatujapeleka maji maeneo mengine, wananchi wa maeneo husika lazima wapate huduma ya maji.

Kwa hiyo, ninachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, nimuombe saa saba tukutane na mimi niko tayari kuongozana naye kufanya ziara ili kwenda kujionea uhalisia na kuweza kutoa msaada katika eneo lile ili wananchi waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Majibu haya anayonipa Naibu Waziri wa Maji ni majibu ambayo yametolewa mwaka 2002 swali lilipoulizwa na Mheshimiwa Dalali Shibiliti, majibu hayo hayo; miaka kumi baadaye akauliza Mheshimiwa Charles Kitwanga akapewa majibu hayo hayo; nami nauliza miaka kumi baadaye napewa majibu haya haya.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua, maji Usagara yanakwenda lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnyeti Mbunge wa Misungwi. Awali ya yote Mheshimiwa Mnyeti pamoja na wananchi wote wa Misungwi poleni sana kwa adha hii ambayo imewapata kwa muda mrefu. Mheshimiwa Mbunge kama anavyofahamu Awamu hii ya Sita, ni awamu ambayo inakwenda kumaliza kama sio kupunguza kwa sehemu kubwa tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tulivyomsikia Mheshimiwa Rais, yeye mwenyewe akiwa hapa ndani kwa kutumia Bunge lako hili Tukufu aliahidi kuweka nguvu kubwa ya kuona kwamba matatizo ya maji yanakwenda kutatuliwa. Hivyo kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, kwenye bajeti yetu ya mwaka 2021/2022, tunakuja Misungwi kuhakikisha tatizo hili sasa linabaki kuwa historia. (Makofi)
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nasikitika sana kwamba majibu haya, ndiyo haya haya ambayo huwa yanatolewa kila mwaka. Unajua kinachouma ni kwamba, vyanzo vya maji vyote vikubwa unavyovijua vinavyopeleka maji Tabora, Nzega, Igunga, Kahama na Shinyanga vinatoka Misungwi, lakini wana-Misungwi hawapati fursa ya kupata miundombinu ya maji. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri: Ni lini Chuo cha Ukiriguru na Kituo cha Utafiti kitapata maji? Kwa sababu, majibu haya, ni haya haya ya miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, hiki nilichokijibu ndiyo mpango mkakati wa Wizara. Kama mnavyofahamu Wizara ya Maji tuko kwenye mpango mkubwa sana wa mageuzi. Hivyo, tuache kuangalia mambo yaliyopita, tuangalie ya sasa hivi na utekelezaji wetu sisi ambao tuko, nafikiri mnauona. Kwa hiyo, napenda tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, suala hili la maji katika hiki chuo mwaka ujao wa fedha kazi zinakuja kutekelezwa kadiri ya mipango ilivyo ndani ya Wizara.
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Barabara hii tunayoizungumzia hapa ni barabara ambayo imekuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa mihula mitatu mfululizo, 2010, 2015 mpaka 2020; na Mheshimiwa Rais alipokuja Misungwi aliahidi barabara hii ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami haraka iwezekanavyo na Mheshimiwa Waziri tulikuwa naye pale, maelekezo ya Rais yalitoka hadharani kuwa barabara hii itengenezwe. Sasa anaposema kwamba anatafuta fedha sijajua yeye ni TRA ama ni nini, kwa sababu mwenye TRA ambaye ni Mheshimiwa Rais amesema barabara ianze kutengenezwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kwamba, ni lini Wizara itaanza kujenga barabara hii? Kwa sababu imekuwa ikikarabati vipande vidogo vidogo ambavyo havina tija yoyote kwenye barabara hii. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pastory Mnyeti, Mbunge wa Misungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari jitihada za Serikali zimeonekana, tumeshafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Pia ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatumika tumeshaanza kujenga madaraja ambayo mara nyingi yanafanya barabara hii isipitike.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine wa barabara hii tayari tumeshaanza kujenga kilometa tano upande wa Kahama, ambayo ni barabara hiyo hiyo. Kwa hiyo Serikali ina nia njema na mara fedha itakapopatikana yote barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kama ahadi za viongozi wa kitaifa walivyoahidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo langu siyo kubishana na Mheshimiwa Waziri kuhusu asilimia zinazopatikana pale Misasi. Kwa mtizamo wangu kwa sababu naishi huko, kutoka asilimia 40, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba upatikanaji wa maji Misasi ni chini ya asilimia Nne hakuna maji, watu wanatafuta maji, hakuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mkandarasi aliyetekeleza mradi huu naweza nikasema ni kandarasi ya kitapeli, na Wizara imerithi miradi mingi ya kitapeli ya sampuli hii kwenye Taifa letu. Wakandarasi wanachukua fedha, lakini hawatekelezi miradi iliyokusudiwa kulinga na mkataba. Mradi huu tangu mwaka 2013 leo ni miaka tisa, kupeleka maji kilomita 15 kutoka chanzo cha maji, imekuwa ni stori za hapa, stori za pale, stori za kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ni lini upo tayari twende Misasi ukawaeleze hizi stori wananchi wa Misasi wewe mwenyewe kwa sababu Wabunge tumeshachoka, tumeshayaeleza mambo haya kila siku, mradi huu umesimama, Mkandarasi haeleweki, fedha ameshachukua, hakuna kinachoendelea site.

MWENYEKITI: Haya ahsante.

MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, ni lini mtaanza kuyafuta makandarasi ya namna hii kwenye Taifa letu, kwa sababu tumejaribu kufuatilia, Mkandarasi huyu kote alikotekeleza miradi hii yote ni feki, hakuna anachokifanya anachukua fedha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Alexander Mnyeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza lini kufuatana na mimi mara baada ya Bunge hili tutakwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Wakandarasi feki, tayari Wizara imeshughulika nao ipasavyo, huyo unayemuongelea tutaendelea kumfuatilia pia tufanye kama tulivyofanya kwa wengine. (Makofi)