Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maimuna Salum Mtanda (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa ridhaa yako kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa ridhaa ya kupeperusha bendera katika Jimbo la Newala Vijijini. Pia nipongeze na kuishukuru familia yangu kwa support wakati wote wa uchaguzi hadi sasa. Kipekee pia niwashukuru wapigakura wa Jimbo la Newala Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa Novemba, 2020 pamoja na ile ya 2015. Ni hotuba ambazo nimepitia zote, hotuba ambazo zina maono, hotuba ambazo kwa namna ya kipekee, hasa ile ya 2015, ilipotekelezwa pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilikifanya Chama Cha Mapinduzi kutembea kifua mbele wakati wa Uchaguzi wa Mwaka 2020. Nina imani hotuba hii ambayo ameitoa 2020 tukiitekeleza hivi inavyotakiwa 2025 itakuwa ni kuteleza kama kwenye ganda la ndizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mambo mengi, tumeyaona. Amesimamia vizuri miundombinu katika nchi hii kuanzia afya, barabara, elimu na sekta nyingine zote. Tunampongeza sana kwa kile ambacho amekifanya kwa kusaidiana na wasaidizi wake ambao ni Mawaziri wetu. Hata hivyo, zipo changamoto kadhaa ambazo zikisimamiwa na kutekelezwa ipasavyo nadhani nchi hii itasonga mbele sana zaidi ya hapa ambapo tupo sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanazalisha kwa kiasi kikubwa zao la korosho, zao ambalo linaipatia nchi hii uchumi na fedha nyingi za kigeni, lakini kuna changamoto ya barabara yetu ya kiuchumi, barabara ambayo inatumika kupitisha zao la korosho kutoka kwenye maeneo ya wakulima kuelekea bandarini. Barabara ile imeshaombewa muda mrefu lakini haikamiliki. Ni barabara ya kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi hadi Nachingwea. Barabara ile hadi sasa imekamilishwa kwa kiwango cha lami kwa kilometa 50 tu. Niombe wenzetu wa Ujenzi kuharakisha ukamilishaji wa barabara ile ili mazao ya wakulima yapate kusafirishwa kwa urahisi kuelekea bandarini, lakini pia kuvinusuru vyombo ambavyo vinasafirisha mazao hayo kuelekea bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Newala ambayo ipo Jimbo la Newala Vijijini imehamia mwaka jana katika eneo lake jipya la utawala. Eneo lile halina jengo la utawala na kwenye hotuba tumeelezwa na kusisitizwa suala la utawala bora. Utawala Bora ni pamoja na kuwepo na maeneo ya watumishi kutendea kazi, lakini Halmashauri ya Wilaya ya Newala haina jengo la Utawala. Niombe wahusika na wasimamizi wa masuala ya utawala kwa maana ya TAMISEMI watuangalie kwa jicho la pekee ili watumishi wale wapatiwe jengo la utawala nao wafanye kazi katika mazingira yaliyoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Newala Vijijini kuna changamoto ya maeneo ya kutolea huduma ya afya. Zipo kata 22 lakini ni kata tatu tu ndizo ambazo zina vituo vya afya. Naomba Mheshimiwa anayesimamia afya atuangalie kwa jicho la kipekee tupate vituo vya afya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana kwa kupunguza kiasi kikubwa cha migogoro iliyokuwa na Maafisa Ardhi wasio waaminifu ambao walikuwa wanagawa ardhi moja kwa zaidi ya watu wawili, changamoto hii ilikuwa kubwa sana katika baadhi ya maeneo ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo bado kuna baadhi ya changamoto za ardhi ikiwemo moja, mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kati ya eneo la Mpanyani karibu na Nangoo. Kutokana na mgogoro uliopo ambao haujapata suluhisho, msimu wa korosho unapowadia Halmshauri hizi mbili hugombania wapi kwa kwenda kuuza korosho zao, kila Wilaya huvutia kwake ili wapate mapato. Mgogoro huu umechukua muda mrefu tunaomba utatuliwe.

Pili, katika Kijiji cha Chilangala eneo la Mbwinji, watu wa Mamlaka ya Maji (MANAWASA) wamechukua ardhi ambayo wanakijiji walikuwa wamelima mazao yao ya chakula na biashara bila kulipa fidia kwa wananchi husika wa Chilangala kwa ajili ya mradi wa maji. Changamoto hiyo imezua mgogoro mkubwa kwa wananchi wa Chilangala ambao hawajajua hatma ya ardhi yao iliyochukuliwa. Tunaiomba Wizara ya Ardhi iingilie kati ili wananchi wa Chilangala walipwe fidia ya ardhi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Serikali imeanza kufanya sensa ya utambuzi wa nyumba vijijini zenye hadhi angalau ya kudumu kwa miaka 15, nyumba zilizojengwa kwa udongo, saruji na kuezekwa kwa bati ili ziweze kulipa pango la nyumba. Pamoja na lengo zuri la Serikali la kudhibiti mapato lakini malalamiko yaliyopo kwa wananchi wa kipato kidogo ni namna watakavyopata fedha za kulipia pango kwa kuwa wapo baadhi yao wamejengewa nyumba hizo na watoto wao au ndugu zao. Lakini wapo wanaolalamika kwa kuwa walijenga nyumba hizo kipindi bei ya zao la korosho ikiwa nzuri, lakini kwa hali iliyopo sasa wanapata wakati mgumu ni namna gani watakwenda kulipia pango hilo katika mazingira ya sasa ambapo bei ya mazao haijatulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu 2011 - Ofisi ya Ardhi Mtwara ilijiwekea mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria mbalimbali za ardhi katika Halmashauri tisa za mkoa huo kufikia Juni, 2021. Hadi kufikia Mei 15, 2021 Ofisi ya Ardhi Mkoa imefanikiwa kutoa elimu kwa Halamshauri za Masasi, Nanyamba na Nanyumbu pekee huku muda uliobaki ni mwezi mmoja tu. Je, ni nini kimekwamisha zoezi hilo kusuasua ukizingatia kuwa muda wa mpango umebaki mwezi mmoja tu? Je, upo uwezekano wa Ofisi ya Ardhi Mkoa kumaliza zoezi la utoaji wa elimu katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022?
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia naishukuru Wizara ya Fedha kwa uwasilishaji mzuri wa Mpango wa Miaka Mitano inayokuja kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Mpango huu, tuna maana kwamba ni mwelekezo wa Serikali kwa miaka mitano ijayo. Sasa ili kuutendea haki Mpango huu na yale matarajio tunayoyatarajia yaweze kupatikana vizuri, kuna mambo lazima yaboreshwe ikiwemo rasilimali watu, lazima iwepo, miundombinu iboreke na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza wenzetu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa sababu wametuwezesha na kutuelewa sisi Wananewala kwa kuwaendeleza na kuchukua majengo ambayo yalikuwa ya NDF ili kuwa VETA. Sisi Wananewala tuna kiu kubwa ya kupata ajira kwa vijana wetu, kwa hiyo, tukawakabidhi wenzetu wa Wizara ya Elimu majengo ili yatumike kama VETA na vijana wetu wakapate ujuzi, waweze kujiajiri wenyewe na kisha maendeleo ya watu yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema, lakini majengo yale yatatumiwa na Wilaya zaidi ya moja kwa maana ya Tandahimba, hakuna VETA, ni majirani zetu, watatumia pale; Masasi kwa maana ya Lulindi, hawana VETA, watatumia pale na Wananewala. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ituongezee au itujengee mabweni ili wanafunzi watakaoenda kusoma pale wapate elimu na ujuzi unaotosheleza bila kuhangaika, mwisho wa siku wakapate wao wenyewe kujiajiri na maendeleo ya nchi yaweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili maendeleo yaweze kupatikana, lazima miundombinu iboreshwe hasa barabara. Wananewala Vijijini wana barabara yao ambayo inaunganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara kwa maana ya Wilaya ya Lindi Vijijini na Newala; barabara ya kutoka Mkwiti – Kitangali hadi Amkeni. Barabara ile ni ya vumbi, lakini ikiboreshwa kwa kiwango cha lami, tuna uhakika kabisa kwamba mawasiliano yatakuwa rahisi, watu watafanya biashara, watakuwa wanasafiri kutoka eneo moja na kwenda eneo lingine na kujipatia fedha ambazo wataenda kuendeleza maisha yao na kuachana na hali ambayo wanayo kwa sasa. Kwa hiyo, naiomba Wizara ambayo inasimamia ujenzi, kwa sababu tunataka kuboresha au kuleta maendeleo ya watu, basi itujengee barabara ile kwa kiwango cha lami ili nasi maendeleo yetu yaweze kupatikana kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mchangiaji ambaye amezungumzia suala la utafiti kwa vyuo vyetu vya kilimo, ni muhimu sana. Utafiti wa mazao ni muhimu sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze fedha kwenye vyuo vya utafiti ili waweze kufanya utafiti wa mara kwa mara ambapo watakuwa up to date na hali ya mabadiliko ya mazao yetu kwa kadri inavyojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanamtwara tunalima korosho ambazo zina magonjwa mbalimbali; ni kama binadamu, magonjwa yanabadilika kila leo. Kwa hiyo, tusipowekeza kwenye utafiti wakulima wetu wakapata kujua aina ya magonjwa ambayo yanajitokeza kwa wakati huo kupitia watafiti wale wa TARI Naliendele, nadhani tutakuwa hatufanyi chochote na uzalishaji wa zao la korosho utakuwa unapungua kadri ya siku zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niunganishe na Maafisa Ugani. Tunaomba Maafisa hawa wawepo kwenye vijiji vyetu, kwa sababu sasa hivi tunavuna lakini kiholela…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja, lakini tunaomba tupatiwe Maafisa Ugani ili wakawasimamie wakulima wetu ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa mara nyingine naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na wale wote waliosaidia kuandaa hotuba ile. Nimeipitia hotuba yake, lakini naomba nami nichangie baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la watumishi, ambao ni walimu. Nilipata kusikia kuhusu ajira mpya za walimu kwamba sasa hivi Wizara imeweka mpango kwamba anayeomba ajira ya walimu anataja sehemu ambako anatakiwa kwenda kufanya kazi. Yaani kwenye application, katika maombi yake anaandika, mimi nataka kwenda sehemu fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo ni zuri, lakini linaweza kuwa na changamoto kwa upande mwingine kwamba kuna maeneo hali yetu, maeneo yetu tunayafahamu, kuna maeneo miundombinu ni hafifu kiasi kwamba hayatapata watu wa kuomba moja kwa moja. Katika mazingira hayo kuna maeneo yatanufaika, yatapata watu wengi na kuna maeneo yatakosa kabisa watu wa kuomba kutokana na hali ya kijografia. Kwa hiyo, naomba tuangalie upya, wazo ni zuri kwamba litapunguza ile hali ya mtu akishapangiwa eneo, anakwenda kuomba abadilishwe, lakini italeta athari kwa upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la uhaba wa walimu katika maeneo yetu. Sasa hivi nchi yetu iko kwenye uchumi wa kati, lakini tunataka tutoke hapo. Katika hali hiyo ni lazima kujiimarisha kuwekeza katika elimu ili hivyo ambavyo tunavitarajia viweze kwenda vizuri. Kuna uhaba mkubwa sana wa walimu katika shule zetu hasa za msingi pamoja na sekondari. Maeneo mengi ambayo yameadhirika ni yale ambayo yapo remote sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukija kwenye Jimbo la Newala Vijiji, kutokana na umbali kati ya kijiji na Kijiji; na sera yetu ni kwamba kila kijiji kiwe na Shule ya Msingi, unakuta jumla ya wanafunzi katika Shule ya Msingi kwenye shule fulani iliyopo katika kijiji fulani haizidi 100. Hesabu zinazopangwa kwa ratio ya mwalimu na mwanafunzi ni mwalimu mmoja na wanafunzi 45. Kwa hiyo, unakuta shule hiyo; mathalani shule yenye wanafunzi 80 au 90 inakuwa na walimu wawili tu, lakini ina madarasa kuanzia awali mpaka la Darasa la Saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu hao wana mzigo mkubwa sana. Kwa hiyo, naomba tuangalie, sawa ratio ni hiyo, lakini naiomba Wizara na kuishauri iangalie upya maeneo yale ambayo yako mbali lakini yana uchache wa wanafunzi ili angalau walimu waweze kuongezwa kwenye maeneo hayo na watoto wapate stahiki yake ili Tanzania ya viwanda iweze kuendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naiu Spika, ukienda kwenye afya, kuna uchache pia wa watumishi katika maeneo hayo. Unaenda kwenye Dispensary unakuta mtumishi ni mmoja, anahudumia watu wote; wajawazito awapime yeye, wagonjwa wa Malaria awatibu yeye, kila kitu ni yeye.

Mheshimiwa Naiu Spika, kama binadamu anachoka, wakati anapochoka, anakuja mgonjwa ambaye anatakiwa apatiwe huduma ya haraka, naye ana mlundikano mkubwa wa wagonjwa, anashindwa. Anaposhindwa, mgonjwa analalamika kwamba sijapata huduma ipasavyo; lakini siyo kwamba kwa matakwa ya yule ambaye yuko pale anatoa huduma, ni kwa sababu ya uchache wa watoa huduma katika eneo lile, wagonjwa hawapati matibabu stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara iangalie eneo hili ili wananchi wapate huduma ipasavyo. Ukienda kwenye Jimbo la Newala Vijijini hali ya Watumishi wa Huduma za Afya ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ukosefu wa bei za uhakika kwenye mazao mchanganyiko hasa Mbaazi, Njungu pamoja na Mihogo. Wananchi wanajitahidi sana kulima, lakini mazao hayo hayapati bei. Matokeo yake kule kwangu Newala vijijini wanaamua kuhama makazi yao, wanaenda mikoa ya jirani kulima ufuta angalau ambao una nafuu ya bei. Matokeo yake, maendeleo ya Newala Vijijini yanazidi kuzorota; na kwa sababu wazazi wamehama, wanaondoka na watoto wao na kwa hiyo, kunakuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi na mimba zisizotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo iangalie suala la bei ya mazao mchanganyiko kwa jicho la kipekee ili wananchi watulie kwenye maeneo yao waweze kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la TARURA ambalo jirani yangu Mheshimiwa Cecil ameliongea. Hali ya barabara zinazohudumiwa na TARURA kule kwetu siyo nzuri sana. Hatuwalaumu wao, lakini tatizo ni fedha chache ambazo zipo katika mfuko huo. Barabara nyingi hazipitiki. Wakulima ambao wanazalisha mazao yao pembeni au walioko pembeni mipakani mwa Newala na Wilaya jirani wakati mwingine wanashindwa kusafirisha hasa zao la Korosho kutoka kule wanakolima kuleta kwenye maeneo yao ili wauzie kwenye vyama vya msingi ambavyo viko kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake Jimbo la Newala Vijijini kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu ya barabara nzuri, linajikuta linapoteza mapato kwa sababu wanalazimika kwenda kuuza mazao yao kwenye wilaya na vijiji vya jirani hatimaye tunakosa mapato. Hasa ukienda Kata ya Mikumbi; barabara ya Mikumbi - Mpanyani haipitiki, barabara Namdimba - Chiwata haipitiki, barabara Mkoma - Chikalule haipitiki na barabara nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana suala la TARURA liongezewe mapato ili barabara ziboreshwe na Jimbo la Newala vijijini liweze kupata kile ambacho kinatarajiwa kutokana na mazoa yanayolimwa na wananchi wa jimbo hilo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Nianze kuwapongeza Waziri na timu yake lakini pia nimpongeze Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa hotuba yake. Kipekee, niishukuru Serikali pamoja na Wizara kwa kutupatia fedha shilingi bilioni moja sisi Newala Vijijini kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, Wizara ya Afya inakabiliwa na changamoto nyingi sana hasa kwenye maeneo yetu. Nianze na suala la ukosefu wa nishati ya umeme katika yale maeneo ambayo huduma za afya zinatolewa lakini hawajafikiwa bado na miradi ya umeme au pia mradi wa REA nao haujafika, kuna changamoto kubwa sana katika utoaji wa afya katika maeneo hayo. Katika maeneo mengi unakuta kuna zahanati zinatumia solar ambazo hazikaguliwi kiasi kwamba zinakufa matokeo yake wagonjwa wanaokwenda kupata huduma pale wanakosa huduma ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, akina mama wajawazito muda wa kujifungua haupigi hodi au hauchaguzi wakati mwingine wanakwenda kupata hizo huduma nyakati za usiku matokeo yake kituo kina giza lakini mama mjamzito anatakiwa ajifungue hapo. Inambidi mama mjamzito pamoja na uchungu alionao awashe tochi yake ya siku ammulikie mtoa huduma anayemsaidia kwa wakati huo. Mimi ni mzazi najua uchungu ulivyo, napata shida sana wakati mwingine wa kutambua namna gani mama huyu anaweza kumulika tochi amsaidie mzalishaji wakati yupo kwenye maumivu makali. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara iangalie kwa jicho la kipekee maeneo kama hayo ili ufumbuzi upatikane akina mama wapate huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dunia sasa hivi imekumbwa na magonjwa mengi ya milipuko ikiwemo suala la Corona. Wanaotoa huduma katika maeneo yetu ni madaktari wetu tunatambua lakini sijaona mkakati wa Serikali wa kutafuta PPE ya kuwakinga madaktari wanaokwenda kutoa huduma kwa wagonjwa. Matokeo yake madaktari wana-risk maisha, wananunua PPE wenyewe, kama hana uwezo anaingia kichwa kichwa kwenda kutoa huduma. Hii ni changamoto kubwa na tunawakatisha tamaa. Namuomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja yake aje na mpango mkakati wa namna gani atawasaidia madaktari kuwapatia PPE ili waweze kuwahudumia wagonjwa bila kupata shida au kuwa na hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nami niungane na wenzangu kuongelea yale makundi yaliyobainishwa katika Sera ya Afya kwamba watapatiwa huduma za afya bure. Hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imebainishwa kwamba wazee zaidi ya miaka 60 watapata huduma bure, akina mama wajawazito pamoja na watoto chini ya miaka mitano. Hata hivyo, suala hili limekuwa ni kinyume kila ukienda kwenye mikutano sijui kama ni kwangu peke yangu unakutana na kero hiyo. Wazee wanalalamika hawapati vitambulisho matokeo yake wanashindwa kupata huduma ya afya. Sasa hawaelewi wapo kwenye dilemma, je, kilichoongelewa katika Ilani ilikuwa ni kwa ajili ya kuombea kura au kweli Serikali ilikuwa na nia thabiti ya kuwasaidia wazee hawa? Niombe sana Serikali pamoja na Wizara ijipange vizuri wazee wabainishwe wapewe zile kadi wapate huduma za afya kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilivyoeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la akina mama wajawazito limekuwa ni changamoto kweli kweli, kuanzia kadi za kliniki wanatakiwa wanunue wao wenyewe. Kadi ya kliniki ambapo ndiko tutaona maendeleo ya ukuaji wa mimba yake anatakiwa anunue lakini tumeshaji nasibu sisi kwamba tutawapatia huduma za afya bure. Kwa hiyo, inaleta mkanganyiko sana kwa sababu akina mama hawapati hizo huduma bure wala Watoto. Kwa hiyo, tunapokwenda tukasema kwamba huduma zinatolewa bure tunakuwa hatueleweki. Niungane na wenzangu Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha hoja tunaomba uje na mpango mkakati utueleze namna gani au nini kauli ya Serikali kuhusiana na kundi hili la wanufaika wa huduma bure za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niungane na wale walioongelea suala la CHF Iliyoboreshwa. Mkakati ulikuwa mzuri lengo la Serikali lilikuwa zuri lakini wale waliokata kadi kwa ajili ya kupata hizo huduma hawapati …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imegonga.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi, awali ya yote niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kwa uwasilishaji pamoja na timu yake yote. Lakini pia Kamati; lakini kipekee kabisa niipongeze Serikali kwa mwaka huu wa 2021 kwa kupeleka michezo ya UMITASHUTA pamoja na UMISETA katika Mkoa wa Mtwara kwa sababu kwa kufanya hivyo inafungua milango ya fursa kwa Wana Mtwara, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye mchango, Tanzania wote tunatambua kwamba imekuwa ikishiriki mara nyingi kwenye michezo mbalimbali ya kitaifa pamoja na kimataifa. Kuna wakati huwa tunafanya vizuri, lakini kuna wakati hatufanyi vizuri sana. Lakini ukiangalia ni kwa nini hatufanyi vizuri sana kuna sehemu kuna gap.

Mheshimiwa Spika, Tanzania pamoja na Serikali yake kwa ujumla imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika maandalizi ya michezo ya UMISETA, pamoja na UMITASHUTA jambo ambalo ni jema kwa sababu tunataraji wanamichezo hawa ambao wanaenda kucheza michezo ya kimataifa watokane na maandalizi ambayo yanafanyika katika michezo ya UMISETA pamoja na UMITASHUTA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukianglaia Serikali inatenga shilingi 600 kwa wanafunzi wa shule za msingi kila mwanafunzi mmoja kwa ajili ya maandalizi ya UMITASHUTA na shilingi 1,500 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari, ni jambo jema tunawashukuru na kwa kweli wanafunzi wanahamasika na wanafanya vizuri. Niwapongeze TFF kwa sababu wakati wa michezo hiyo wamekuwa wakiwabaini wanafunzi wanaofanya vizuri wanawaweka kwenye database yao pamoja na CHANETA na watu wa basketball.

Mheshimiwa Spika, lakini pale michezo ambayo inashindanishwa ni mingi ipo pia michezo ya ndani wale wa michezo ya ndani sijaona mkakati madhubuti wa Serikali kuwashirikisha au kuwachukua katika database yao ili waweze kuwatumia baadaye. Nishauri sana Serikali kwamba michezo ya ndani ni sehemu ya michezo na yenyewe ichukuliwe kwa uzito wake Watoto wale nao wapate kushiriki katika michezo mingine hapo baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wale wanafunzi wanaomaliza wanaoshiriki michezo ya UMISETA pamoja na UMITASHUTA wakishamaliza shule hakuna wanakoelekea, wamejitahidi wamefanya vizuri, wamemaliza masomo yao wanarudi wanakaa nyumbani hakuna muendelezo wa michezo kwa wanafunzi wale. (Makofi)

Sasa swali la kujiuliza ni kwamba Serikali iliwekeza kwa kiasi kikubwa, wanafunzi wakajitoa, maandalizi yakafanyika, lakini mwisho wa siku fedha za Serikali ambazo zimeenda kuwekeza katika michezo hiyo hazileti tija kwa sababu wanafunzi wanapomaliza hakuna wanakoelekea tena ukiondoa wale wachache wa football, netball pamoja na basketball.

Kwa hiyo, niombe Serikali sasa iwe na mkakati madhubuti wa kuhakikisha wale wanafunzi wanaomaliza shule wanachukuliwa au wanaendeleza michezo yetu mbalimbali ili baadaye iweze kutuletea tija katika Taifa katika fani hiyo ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niongelee pia suala la utamaduni; hii ndiyo Wizara ambayo inasimamia kwa ujumla masuala yote ya utamaduni, utamaduni kwa maana ya vyakula, maadili na mambo yote yale ambayo yanakusanyika huko, lakini tumeona mmomonyoko mkubwa sana wa kimaadili sasa hivi katika nchi yetu. Niiombe Wizara kwa sababu ni Wizara ambayo ina vyombo vya habari; ina television pamoja na magazeti na redio kwa kupitia vyombo vyake vya habari waanze kurejesha au watoe elimu kuhusiana na suala la maadili katika nchi hii, hali iliyoko ni mbaya hata Mheshimiwa Rais alisema wakati anaongea na wazee wa Dar es Salaam, mwanafunzi au kijana amekaa kwenye kiti, lakini hampishi mama mjamzito wala wazee na hiyo inatokana na mmomonyoko wa maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutumie vyombo vyetu tulivyo navyo kutoa elimu ili suala la maadili liweze kuendelezwa katika nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna Mtanda.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Nishari.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nitoe pongezi nyingi kwa Waziri mwenye dhamana ya Nishati pamoja na watendaji wake wote. Pia niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuasisi suala la mradi wa umeme vijijini kwani umepunguza kwa kiasi kikubwa sana kero ya umeme ambayo ilikuwa inavikumba vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jimbo la Newala Vijijini. Wote tunajua kwamba umeme ni ajira, biashara, ulinzi lakini pia ni afya. Jimbo la Newala Vijijini lina jumla ya vijiji 107, kati ya vijiji hivyo ni 54 tu ndiyo vyenye umeme, vijiji 53 havina umeme sawa na asilimia 49.53. Kuna Kata sita katika hivyo vijiji 53 ikiwemo Kata ya Chitekete ambayo Mbunge mimi natoka haina umeme niko gizani. Kata nyingine ni Nakahako, Mpwapwa, Nandwahi, Mkoma 2 na Nambali, kata hizi hazina kabisa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ujazilizi wa vijiji vile ambavyo mradi wa REA umepita. Mheshimiwa Waziri una kazi kubwa ya kufanya kwa sababu kama walivyotangulia kusema katika vijiji ambavyo umeme umepita vingi wanauona umeme umekaa kama kamba ya kuanikia nguo, haujashuka kwenye nyumba za wananchi. Ukienda Kata ya Mdimba inahesabika kwamba ina umeme lakini Mdimba pale ambapo ndipo Makao Makuu ya Kata umeme haujashuka kabisa na ni kero kubwa wanasumbua kila siku. Tunashukuru tumepata mkandarasi, niombe sana Mheshimiwa Waziri msimamie kwa karibu kwa sababu hali iliyopo inahitaji usimamizi otherwise ile miaka miwili ambayo tumejipangia kwamba vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme kwa hali iliyopo Newala Vijijini tunaweza tusifanikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtwara sasa ameshusha neema ya madini. Tumesikia kuna graphite kule Chiwata ambayo na mimi pia inanigusa kwa namna moja au nyingine. Ili mradi ule uweze kufanyiwa kazi vizuri tunahitaji umeme wa uhakika. Kulikuwa na mpango ule wa kujenga power station ya megawatt 300 pale Mtwara, tunaomba wakati unakuja kuhitimisha hoja yako utuambie mpango hule umefikia wapi kwa sababu kupitia mpango ule tutakuwa na uhakika kwamba umeme wa kutosha utapatikana na miradi mingine mikubwa ya maendeleo kama viwanda pamoja na machimbo vitaendeshwa bila bugudha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia na mimi niongelee suala la kukatikakatika kwa umeme, hali ilikuwa mbaya sana kwa Mkoa wa Mtwara lakini niishukuru Serikali ilifanya juhudi kubwa sasa hivi umeme unakatika lakini nafuu hipo. Watu wa TANESCO Makao Makuu, watu wa Kanda, TANESCO Wilaya waliweka kambi kuhakikisha kwamba tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Mtwara linapata ufumbuzi.

Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba tulikwambia suala hilo na wewe ukalifanyia kazi na tunashukuru ulikuja ukaona ile hali ukatuma hiyo timu ikaja kuhakikisha kwamba suala la kukatikakatika kwa umeme basi linaisha Mkoani Mtwara. Niendelee kukuomba juhudi ziendelee kufanyika ili kukomesha kabisa suala la ukatikaji wa umeme ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia chochote kuhusiana na bajeti ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya pamoja na wasaidizi wake wote. Kwa kweli, ametuheshimisha sana wanawake wa nchi hii, wanawake sasa hivi wamekuja juu, wamepata ujasiri mkubwa, lakini yote hayo ni kutokana na mwongozo wake vile anavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri na timu yake yote, kwa namna ambavyo wameandaa bajeti. Bajeti ni nzuri, bajeti ambayo inawagusa wananchi wote wa nchi hii, kuanzia wakulima, wafanyakazi, wafugaji, pamoja na watumishi wote. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa namna ambavyo mmepokea maoni ya Wabunge, hatimaye mmeweka kwenye bajeti suala la fedha za Madiwani pamoja na Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa, kulipwa moja kwa moja katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muhanga wa Madiwani. Katika Jimbo langu la Newala Vijijini, Madiwani waliomaliza muda wao wanadai Halmashauri posho zao, mpaka leo hawajapata. Kwa hiyo, sasa hii ni tiba, tunashukuru na tunatumaini kwamba Madiwani sasa watafanya kazi kwa moyo, watakuwa na ari kubwa kwa sababu wanajua unapofika mwisho wa mwezi watapata posho zao bila shida. Sasa katika hilo, nami nashauri kwamba tuangalie pia zile posho angalau ziongezeke kidogo kwa sababu kiasi kile kwa kweli ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye masuala muhimu, masuala ya ukusanyaji wa mapato. Natambua kabisa nchi hii ina miradi mikubwa ya Kitaifa inayotekelezwa ambayo inahitaji fedha nyingi. Pia ipo miradi katika Halmashauri zetu ambayo nayo inahitaji fedha za kutosha, lakini kuna Madiwani ambao watalipwa posho kupitia Serikali Kuu, kuna Maafisa Tarafa, kuna Watendaji wa Kata, fedha hizi ukiangalia zinatakiwa zikusanywe ili hii miradi pamoja na hizi posho ziweze kupatikana. Kama hazitakusanywa vizuri, kwa usimamizi imara, haya ambayo yamewekwa kwenye bajeti yanaweza yasitekelezeke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tuweke namna nzuri ya ukusanyaji wa mapato ili yasivuje, tuweze kutekeleza miradi yetu kwa ufanisi mkubwa. Naomba nitoe mfano mdogo. Kupitia Ripoti ya CAG hii ambayo ameitoa ya mwaka 2019/2020 kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.2 ambazo zilikusanywa nje ya mfumo kupitia katika vyanzo mbalimbali vya mapato. Sababu ambayo CAG ameitoa ni kwamba fedha hizi zilipita nje ya mfumo kwa kukosekana kwa mashine za POS. Pia kulikuwa na fedha nyingine ambazo zilikuwa zinatumika, zile fedha mbichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana haya, matatizo ya POS tujiimarishe sasa, tuhakikishe tuna vifaa vya kutosha ambavyo vitaenda kutumika kila eneo linalohusiana na ukusanyaji wa mapato yetu ili malengo yetu yakapate kutimia vile ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, naipongeza sana Serikali kwa kuamua kwa dhati sasa kuanza mpango wa utoaji wa huduma za afya kwa maana ya Bima ya Afya kwa wananchi wote. Ni jambo jema kwa sababu Taifa ambalo litakuwa na wagonjwa wengi, basi halitaweza kuzalisha vile ambavyo tunatarajia. Kwa hiyo, kupitia mpango huu ni matumaini yangu kwamba wananchi watakuwa na afya bora, watafanya kazi zao vizuri na hatimaye Taifa litaweza kujipatia fedha nyingi katika kutekeleza miradi. (Makofi)

Mheshiiwa Mwenyekiti, sasa hapa naomba nitoe rai kwamba, kwa sababu tumeshaweka huo mkakati, tuandae namna ambayo wale wanaokwenda kukusanya fedha za Bima ya Afya au watakaosimamia ujazaji wa fomu za Bima ya Afya wapatiwe mafunzo maalum, kwa sababu sasa itasambaa nchi nzima tofauti na ilivyo sasa hivi kwamba wanaopata huduma ya Bima za Afya ni wachache kuliko tunavyotarajia kama Taifa kwamba sasa watu wote wanakwenda kupata hizi huduma za Bima ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naongea hivyo? Naongea hivyo kwa sababu ukienda kwenye Ripoti ile ya CAG, alibaini madai ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1 ambayo Bima ya Afya yanaidai Serikali kwa sababu tu ya changamoto ya zile kasoro za ujazaji wa fomu. Sasa ukiangalia wanaopata hizo huduma sio wengi kiasi hicho, lakini fomu ambazo zina shida ya kulipwa fedha zake ni zaidi ya shilingi bilioni 2.1. Je, Watanzania wote watakapoingia kwenye huo mfumo, ni kiasi gani cha kasoro kitasababisha upotevu wa dawa kwa kiasi kikubwa? Kwa hiyo, naomba sana mafunzo yatolewe, watu wawe na ujuzi wa kujaza zile fomu ili changamoto hizi zisije zikajitokeza kule tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza tena Serikali, kwa kweli katika bajeti hii imeweka mambo mengi sana kuhusiana na masuala ya kilimo. Ukienda kwenye kilimo cha mihogo wameweka namna ambavyo watasimamia mazao ya mihogo, lakini pia hata kwenye korosho. Sasa changamoto yangu ni viwanda. Katika nchi hii kuna baadhi ya viwanda havifanyi kazi sawasawa. Kule kwetu Newala ambako tunazalisha korosho kati ya tani 20 hadi 30 kwa mwaka hatuna kiwanda cha uhakika cha kubangua korosho ili kuithaminisha korosho hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kiwanda cha Agrofocus, hiki kimebinafsishwa, lakini tuna kiwanda cha Micronox; kiwanda hiki kimepewa mtu ambaye uwezo wake tunadhani ni mdogo kwa sababu, kwa mfano msimu uliopita hakuwa na malighafi. Inaonekana hakuwa na fedha, kwa hiyo, yale ambayo tulitegemea tuyapate kutokana na kiwanda hiki yanashindwa kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vile wakati vinafanya kazi kule Newala, zaidi ya asilimia 80 ya waliokuwa wanafanya kazi pale ni wanawake. Sasa hivi viwanda havifanyi kazi, wanawake wamekaa chini, wanashindwa kuwasaidia akina baba, wanashindwa kutimiza majukumu yao. Naiomba sana Serikali, nimeangalia pia kwenye bajeti sijaona mkakati wa dhati wa namna ya kuinua viwanda vile vikaweza kufanya kazi kuanzia msimu unaofuata. Kwa hiyo, changamoto hii maana yake bado ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna taarifa kwamba kulikuwa na mnunuzi kutoka nje alitaka kununua kiwanda kimojawapo na Serikali ina taarifa hiyo. Naomba basi Mheshimiwa Waziri wakati unakuja kufanya majumuisho utuambie hatima ya ununuzi wa kiwanda kile imefikia wapi? Hii itawasaidia wananchi wa Newala kujiajiri kupitia ubanguaji wa korosho wanazozizalisha kwa wingi katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo linaleta changamoto kubwa katika Mikoa au Wilaya ya Newala kwa ujumla ni suala la barabara. Wilaya ya Newala ipo Kisiwani, haina hata barabara moja ya lami kati ya wilaya na wilaya au wilaya na mkoa inayofika Wilaya ya Newala. Barabara zote ni za vumbi, lakini ni wakulima wazuri sana wa korosho na mihogo. Kwa hiyo, usafirishaji wa mazao yao ni changamoto kubwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Serikali ilikuwa kuunganisha barabara za mkoa na mkoa kwa kiwango cha lami. Wilaya ya Newala inaunganisha Mkoa wa Lindi kupitia Mtama kwenda Mtwara, lakini barabara ya kutoka Amkeni – Kitangali mpaka Mtama yenye kilometa 74 ni ya vumbi. Tunaishukuru Serikali imeshajenga kwa kiwango cha lami kilometa 22. Tunaomba Serikali iboreshe barabara hii, ijengwe kwa kiwango cha lami sasa ikamilike ili wananchi wa Newala ambao wanapata huduma zao nyingi katika Jiji la Dar es Salaam nao waweze kutumia barabara hii ikiwa katika mazingira mazuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.