Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Twaha Ally Mpembenwe (20 total)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Nyamisati – Bungu ni muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti hasa wakazi wa Kata za Mwambao, Maege, Mlanzi, Waluke na Kata ya Salala.

Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha ili shughuli za awali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ziweze kufanyika, barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bungu – Nyamisati ni barabara ambayo inaunga kwenye barabara ya Dar es Salaam – Lindi – Mtwara na ambayo ina kilometa takribani kama 43 na bahati nzuri nimeitembelea barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kati ya barabara muhimu sana kwa sasa kwa sababu ndiyo baada ya kujenga bandari ya Nyamisati na kuwa na kivuko ambacho kinafanya kazi kati ya Nyamisati na Mafia, kwa hiyo Wizara inatafuta fedha ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu sasa ndiyo barabara inayotumika sana na wananchi wa kutoka Kisiwa cha Mafia kuja Nyamisati na kwenda sehemu nyingine za Tanzania.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mpembenwe kwamba barabara hii tunatafuta fedha ili wananchi hawa waweze kufanya shughuli zao kwa uhakika zaidi na hasa tukizingatia kwamba ndiyo barabara muhimu inayounganisha watu wa Mafia na watu wa huku bara. Ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, wananchi wa Jimbo la Kibiti na wajomba zangu wa Rufiji wamekuwa wahanga namba moja sana wa bei za mazao ya Korosho pamoja na Ufuta katika kila msimu katika kila mwaka: Je, Serikali sasa iko tayari kutoa tamko ni msimu gani kutakuwa na mnada wa aina moja katika maeneo yote ambayo yanauza au yanavuna mazao haya?

Swali la pili; bei ya Korosho huwa itegemea sana na…

SPIKA: Hebu rudia swali lako la kwanza.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, Swali langu la kwanza ni kwamba, Serikali iko tayari kutoa tamko kwamba ni lini au msimu upi wataanza kufanya minada inayolingana katika maeneo yote yanayokuwa yanavuna mazao hayo kwa wakati mmoja? Kwa sababu mfumo wa TMX...

SPIKA: Nilisema urudie kwa sababu inaonekana, si ndiyo swali lako la msingi uliuliza?

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, hili halikujibiwa ipasavyo kwa sababu mfumo wa TMX ni mfumo ambao huwa unafanyika kwa kupitia Kanda moja na Kanda nyingine...

SPIKA: Haya endelea.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, Ahsante.

Swali langu la pili: Je, Serikali ina mpango gani; kwa kuwa suala la Korosho huwa linategemea sana na grade ya Korosho; Grade A huwa inauzwa kwa bei ya juu sana, lakini wananchi wa Jimbo la Kibiti pamoja na wajomba zangu wa Rufiji wamekuwa wahanga sana wa bei ya Korosho hasa grade A kwa sababu katika kila msimu Korosho Grade A inayouzwa katika Mkoa wa Pwani bei yake inakuwa chini sana ukilinganisha na Korosho Grade A inayouzwa katika maeneo mengine ambao wanavuna katika msimu unaofanana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kuhusu minada kufanyika kwa wakati mmoja, Waheshimiwa Wabunge watakuwa mashahidi kwamba toka msimu huu umeanza, tumeanza ku-introduce mfumo wa TMX. Mfumo huu umeanza kufanyiwa majaribio katika baadhi ya maeneo na tumeona upungufu wake na tunafanyia marekebisho ili uweze kujenga mazingira ya kuwa na online platform na kuongeza uwazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mfumo wa TMX utakapokuwa umekidhi vigezo tunavyovitarajia, utatumika katika maeneo yote ya kuanzia Pwani, Lindi, Mtwara mpaka Ruvuma ambako kuna uzalishaji wa Korosho lakini minada itaendana na mambo makubwa yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, ya kwanza ni Ikolojia. Kwamba wakati mazao yanazalishwa eneo A na kama eneo B wakati huo huo mazao hayo yamezalishwa, basi minada itafanywa kwa pamoja ili kuongeza transparency.

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi timu yetu ya wataalam iko katika
Mkoa wa Pwani ikifanya tathmini kubwa mbili; moja, tatizo la ubora ambalo linasababisha Korosho ya Pwani ikose bei sawa sawa na Korosho ya Tandahimba. Kuhusu suala la changamoto iliyoko katika Mkoa wa Pwani, ambayo Waheshimiwa Wabunge na wenyewe wanaifahamu, kwamba, kwa kuwa Mkoa wa Pwani unakabiliwa na uwepo wa mvua nyingi kuliko maeneo mengine, wakulima wa Pwani wamekuwa wakikumbwa na tatizo la Korosho yao kuwa na unyevu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo imeiagiza Bodi ya Korosho sasa hivi kuangalia namna gani tutavisaidia Vyama vya Msingi na Vyama Vikuu vya Ushirika vya Mkoa wa Pwani hasa CORECU ili viweze kuondokana na tatizo la unyevu na kuwapatia vifaa vya kuweza kuanikia Korosho yao ili iweze kukidhi viwango vinavyostahili.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, wiki ijayo Ijumaa tutakuwa na Mkutano mkubwa utakaoongozwa na Waziri wa Kilimo hapa Dodoma na Waheshimiwa Wabunge wa Korosho tutawaalika, tutagawa vifaa katika baadhi ya Vyama vya Ushirika ili kuongeza ubora wa Korosho katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge watupe muda, tathmini inaendelea na minada itafanyika kwa pamoja. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Maswa ina umuhimu sana sawasawa na barabara ya watu wa Kibiti kutoka Kibiti Dimani kwenda Mloka kule ambako kuna ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, na kwa kuwa Mheshimiwa Rais mama yetu Samia wakati anainadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi aliahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa kiwango cha lami.

Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili shughuli za awali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zianze mara moja katika barabara hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Kibiti ni moja ya barabara muhimu sana ambayo ni moja ya njia inayofika kwenye Bwawa la Nyerere, na barabara hii ni ahadi ya viongozi wetu wa Kitaifa.

Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Kibiti, kwamba barabara hii ipo kwenye mpango na itajengwa kwa kiwango cha lami kama viongozi ambavyo wametoa ahadi na kama ambavyo inaonekana kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nimpongeze kwasababu Mheshimiwa Naibu Waziri ni mtaalam sana katika mambo ya uvuvi na ni imani yangu kwamba majibu yake yamesikilizwa kwa makini na watu wa Mkuranga pamoja na Kibiti. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kibiti hasa katika maeneo ya Delta kuna kata kama tano kuna Kata ya Kihongoroni, Kata ya Mbochi, Kata ya Maparoni, Kata ya Msara na Kata ya Salale vile ni visiwa shughuli zao kubwa wanazozitegemea ni uvuvi wa hawa Kambamiti hatuna shughuli nyingine yeyote ya kilimo. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka umefika kuweza kutoa Muarobaini wa tatizo hili la muda wa uvuvi kwamba wananchi hawa waruhusiwe kuanzia kipindi cha mwezi wa 12 mpaka mwezi wa tano? hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili tunajua Kambamiti wanapatikana Kibiti na sisi kama watu wa Kibiti tunapenda sana kuona rasilimali ile inawanufaisha vile vile Watanzania wengine yaani kuchangia pato la Taifa. Je, Serikali ina mkakati gani ili sasa kuweza kuhakikisha Kambamiti wale wanawanufaisha sio tu wananchi wa Kibiti Halmashauri lakini vile vile kuongeza pato la Taifa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la ndugu yangu Mheshmiwa Mbunge wa Kibiti Comrade Twaha Mpembenwe. Kwanza naomba nikiri swali hili ni la muhimu sana kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti na wale wa Jimbo langu la Mkuranga, anataka kujua ni mbinu na mkakati gani muarobaini tutakaokuwa nao wa kuhakikisha kwamba wanachi hawa wa maeneo ya kisiju maeneo ya Mdimni, maeneo ya Nganje, maeneo ya Kifumangao, maeneo ya Nyamisati, maeneo ya Mfisini, maeneo ya Kiasi, Mbwera mpaka kule mpakani na Kilwa kwa maana ya Marendego.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maana Wizara imejipanga vyema tumeshaelekeza mahsusi kabisa kwamba Shirika letu la utafiti la TAFIRI kwa kushirikiana na idara yetu kuu ya uvuvi ifanye mapitio ya utafiti tuliokwisha kuufanya na sasa tutakwenda kufanya zaidi kwa kushirikiana na wananchi wenyewe na wadau katika maeneo yote haya ili tupate suluhu ya kudumu ni ukweli usio pingika, kwamba wananchi wa maeneo haya wao wamekuwa wakihifadhi maeneo haya Samaki wanapokuwa wamekuwa wanaondoka Bahari kuu na sasa matokeo yake hawana uwezo wavuvi wale wa kuwafikia Samaki wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeelekeza pamoja nami Mheshimiwa Waziri kwamba tufanya kazi ya kutoka nje kuondokana na yale mazoea ya kuwazuia tutafuta alternative ambayo itawafanya wananchi hawa sasa wawe na uwezo wa kuweza ku-enjoy rasilimali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ametaka kujua juu ya mkakati wetu, ni namna gani tutawasaidia. Wananchi hawa hawana jambo jingine la kufanya hakuna kilimo kinachoenea kikakubali katika eneo lile isipokuwa uvuvi tu wa Prawns kwa maana ya Kambamiti, ni maelekezo tuliyoyatoa pia tutafute njia mbadala za kuwasaidia waweze kufanya uzalishaji zaidi katika miaka mitano iliyopita wananchi wa Mkuranga na Kibiti wamezalisha tani 1,200 zenye thamani ya shilingi bilioni 16 na zikaingiza Serikalini Milioni 600 sasa tunataka tutoke hapo tuongeze uzalishaji zaidi ili na wao waweze kuondokana na umaskini ambao ulioenea katika eneo hili wakati wamekalia rasilimali kubwa sana. Nashukuru sana.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wananchi na wawekezaji katika Kata ya Mtunda kwenye Jimbo la Kibiti katika miundombinu ya umwagiliaji ukizingatia kwamba kuna uwekezaji mkubwa sana wa kilimo cha mpunga umefanyika pale na unaendelea wa ekari zisizopungua 20,000?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tukisema hapa tunatambua kwamba Bonde la Rufiji ni kati ya mabonde muhimu katika kilimo cha umwagiliaji hapa nchini Tanzania na ndiyo maana katika mkakati wetu wa mwaka huu katika bajeti yetu, tumeamua kuyapitia mabonde yote 22 likiwemo Bonde la Rufiji kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili baadaye tuje tutekeleze miradi mikubwa ya umwagiliaji ambayo pia itawagusa wananchi wa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kibiti kwenye Kata ya Bungu tuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kutupa shilingi milioni 250 kumalizia kituo cha afya. Ni lini Serikali italeta fedha hizo ili tuweze kumalizia kile kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tulishatoa fedha awamu ya kwanza shilingi milioni 250 katika vituo ambavyo asilimia kubwa ya Wabunge walipata, ikiwemo katika Jimbo la Kibiti ambalo Mheshimiwa Mbunge ameainisha. Nimhakikishie tu kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tutatoa fedha nyingine shilingi milioni 250; na katika awamu ya kwanza tayari vituo vya afya 100 tumeshapeleka shilingi milioni 250 kumalizia ile shilingi milioni 500 na bado vituo vya afya kama 123 ambavyo tutamalizia kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha watapata hiyo fedha, shilingi milioni 250 ili waweze kumaliza vyote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kibiti inafahamika maarufu sana kwa jina la Kanda Maalum, sasa ni upi mpango wa Serikali kujenga Kituo cha Polisi ambacho kina hadhi ya Kanda Maalum katika Wilaya ya Kibiti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ulianzishwa Mkoa wa kipolisi Kanda Maalum ya Kibiti, ukaanza kwa utaratibu wa dharura kwa kutumia ofisi ya OCD zilizokuwepo miongoni mwa Mikoa mipya ya kipolisi ambayo itajengewa majengo yake ni pamoja na Mkoa huu wa Kanda Maalum ya Kibiti. Kwa hivyo Mheshimwia Mbunge asubiri kadri tutakapokuwa tunapata fedha, Kibiti itapewa msisitizo maalum. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kibiti tumepatiwa fedha shilingi bilioni 6.2, tumejenga daraja zuri sana pale Mbochi ambalo linaunganisha wananchi wa Mbwela na Mbochi na kuja Kibiti Mjini. Hata hivyo, kuna kipande cha kilometa 35 ambacho ikinyesha mvua kinakuwa kipo katika hali mbaya sana.

Je, ni nini tamko la Serikali ili kuweza kuhakikisha kwamba tunakwenda kutengeneza kipande kilichobaki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Jimbo la Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi sana ambazo amezileta katika majimbo yetu ikiwepo Jimbo la Kibiti. Nimhakikishie kipande cha kilomita tatu ni kipaumbele kwa sababu kama tumepeleka billions za fedha katika daraja lazima tukamilishe kilomita tatu ili hilo daraja liweze kuwa na tija. Kwa hiyo namhakikishia kwamba tutatafuta fedha kuhakikisha kilomita hizi tatu zinatengenezwa ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwakunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Kibiti – Dimani – Mloka iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM); je, lini Serikali wataanza mchakato wa kuitengeneza barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpenbenwe Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ipo kwenye Ilani na Serikali kwakweli inaendelea kutafuta fedha kwa barabara hii ili iweze kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Bungu – Nyamisati imekuwa kilio cha muda mrefu sana kwa wananchi wa Jimbo la Kibiti; je, ni lini Serikali mtaitengeneza barabara hii katika kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii tayari tumeshakamilisha usanifu wa kina na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuijenga barabara hii yote kwa kiwango cha lami kuanzia Bungu mpaka Nyamisati. Ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza;

Je, ni nini mpango au Mkakati wa Serikali kujenga scheme ya umwagiliaji katika ukanda ule wa delta kule kwetu Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha tunayatumia mabonde yote makubwa nchini kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Tarehe 30 mwezi wa tatu mwaka 2023 mbele ya Mheshimiwa Rais, wakandarasi 22 walisaini mkataba wa mabonde yote ya kimkakati likiwemo bonde la Rufiji, Mto Ngono, Mto Manongawembele, Ziwa Victoria, Mto Luhuhu, Mto Songwe, Mto Ruvuma, Ifakara Idete na mpaka Litumbandio kwa Mheshimiwa Benaya Kapinga.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Tuna ahadi ya Waziri wa TAMISEMI katika Wilaya ya Kibiti kutoa fedha kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kibiti Mjini kwenda kule kwenye Halmashauri yetu ya Kibiti.

Je, ni lini Serikali itatoa fedha hizo kukamilisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri ya Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutakaa na wenzetu wa TARURA kuona ni namna gani wamejipanga katika kutekeleza ahadi ya hii ya Mheshimiwa Waziri ya kuweka barabara ya lami kutoka Kibiti Mjini mpaka ambapo wamejenga halmashauri yao. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: -

Je, ni lini sasa mchakato huu wa Serikali utakwenda kukamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa maeneo haya ni maeneo ya asili ya makazi ya wananchi, kwa mfano, maeneo ya Mtunda, Moyoyo, Nyafeja Pamoja na Nguwalo.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa kuweza kuhakikisha wakati wa kugawa maeneo haya wananchi hawa wanakwenda kupewa kipaumbele, kupata maeneo ya kulima ili waweze kuendesha maisha yao na vilevile kuchangia Pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni lini mchakato huu unakamilika? Tarehe 23 Mei, 2023 tunategemea taratibu zote za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ziwe zimekamilika na tutaanza ujenzi katika mwaka wa fedha unaoanza 2023/2024, kwa maana kuanzia tarehe 1 Julai mwaka 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili la kuhusu maeneo haya kugaiwa kwa wakazi wa maeneo hayo. Ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanufaika wa kwanza wanakuwa ni wakazi wa maeneo hayo. Kwa hiyo nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wake watapata maeneo katika mashamba haya.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Sensa ya Watu na Makazi iliyokuwa imefanyika hivi karibuni, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuweza kutoa tamko kwamba irudi tu katika mfumo ule wa zamani wa vijiji kuliko hivi sasa kuweza kusubiri kwa sababu imekuwa ni muda mrefu, tangu mwaka 2009?

Swali la pili, pale kwenye Jimbo la Kibiti, Kata za Kibiti, Dimani na Mtawanya ilitangazwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo tangu mwaka 2014, shughuli za maendeleo, vikao vya kisheria, mali zimekuwa haziwezi kumilikiwa ipasavyo.

Je, Serikali ina tamko gani kuhusiana na suala hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la kwanza la tamko la kurudisha kuwa na vijiji badala ya Mamlaka ya Mji Mdogo. Nirejee kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba vigezo vya kupandisha Mamlaka za Mji Mdogo kuwa Halmashauri za Mji zimewekwa wazi kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa na Mamlaka nyingi za Miji Midogo hizi bado hazijakidhi vigezo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuna Mamlaka za Miji Midogo asilimia 67 ambazo haziwezi kufikia malengo yao wanayojiwekea ya kibajeti na ni asilimia 33 tu ambazo zinafikia malengo yao ya kibajeti kwa asilimia 100, ikiwemo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo. Serikali itaendelea kuliangalia hili na pale tutakapokuwa tumeboresha miundombinu katika maeneo ya kimamlaka yaliyopo sasa tutaendelea kufanya review na kuona ni namna gani tunakwenda kuzipandisha hadhi mamlaka hizi.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la Kibiti. Vivyo hivyo kama nilivyotoa majibu yangu kwenye swali la nyongeza namba moja, kwamba tunaangalia vigezo vya mapato vilevile na kuweza kufanya huduma mbalimbali za kijamii, wao wenyewe kupitia mapato yao ya ndani. Mji Mdogo wa Kibiti tutafanya tathmini kama unakidhi vigezo vile vya kimapato basi tutaona ni namna gani ambavyo unaweza kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo katika Mji wa Kibiti.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la mawasiliano katika Kata ya Mchuki pamoja na Mbuchi kwenye Jimbo la Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kibiti kuna maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano. Vilevile kuna maeneo ambayo tayari Serikali imeyaingiza katika ile miradi 758. Kama kuna maeneo ambayo yatabaki kuwa na changamoto Serikali inayapokea ili iwatume wataalam wake wakafanye tathmini na tujiridhishe ukubwa wa matatizo yaliyopo pale then tupate fursa ya kupeleka huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Kibiti wamenituma niulize kwa mara nyingine tena, ni nini mpango au mkakati wa Serikali kuhusiana na barabara ya Kibiti – Dimani mpaka Mloka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii sasa hivi tunairudisha tena kuifanyia review ya usanifu, lakini naamini ndiyo barabara ambayo tayari tunajenga lile Daraja kubwa la Mbambe kuhakikisha kwamba tunaondoa hiyo changamoto. Mpango ni kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, ambayo pia ni barabara fupi sana kwenda Bwawa la Nyerere ukitokea Pwani, ahsante.

MHE TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye kata ya Salale Kijiji cha Nyamisati tuna shida kubwa sana ya kituo cha afya ukizingatia zahanati ya pale inahudumia wilaya mbili…

SPIKA: Mheshimiwa Twaha, uliza swali.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, je, lini Serikali mtatujengea kituo cha afya pale?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali ina vigezo vyake vya kuanza kujenga vituo vya afya. Hivyo, basi tutauma timu kwa ajili ya kwenda kule katika Kijiji cha Nyamiisati, kata ya Salale, Jimboni Kibiti kuweza kufanya tathimini na kuona kama vigezo vile vimefikiwa vya kuweza kujenga kituo hiki vya afya.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushurukuru sana. Katikakatika ya umeme Jimbo la Kibiti, Rufiji, Mkuranga imekuwa ni donda sugu. Nini mkakati wa Serikali kukomesha tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani ni Mkoa wenye viwanda vingi sana na unao-consume umeme mwingi zaidi, lakini tunahakikisha kwamba katika mradi wetu wa Gridi Imara tunautizama kwa karibu ili kuhakikisha wanapata umeme wa kutosha na wa uhakika na katika eneo lake la Kibiti tatizo hilo litakwisha.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Kibiti kata ya Mtawanya kuna vijiji vya Bumba, Msola na Makima vina shida kubwa sana ya maji. Ni nini tamko la Serikali kuhusiana na kuweka maji katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Twaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kata hii anayoiongelea tumeshazungumza mara kadhaa na Mheshimiwa Mbunge na tayari tunaiweka kwenye utaratibu wa kuona kwamba tunawaletea wananchi maji bombani yakiwa safi na salama.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naipongeza Serikali kwa majibu mazuri. Pamoja na hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweza kujenga shule mpya katika Jimbo la Kibiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba kuuliza: Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuweza kukarabati Shule ya Msingi ya Mchukwi pamoja na Shule ya Msingi ya Nyanjati iliyopo katika Kata ya Mahenge?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, hili la kwanza la mpango wa Serikali kujenga shule mpya katika Wilaya ya Kibiti, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mradi wa Boost, imejenga shule mbili mpya katika Jimbo lake la Kibiti. Jumla ya shilingi milioni 821 zilipelekwa katika Halmashauri ya Kibiti kujenga shule hizo ambazo ipo ya Itonga Kata ya Bungu na vilevile kuna shule inaitwa Mpembenwe ambayo imejengwa, ilipelekewa shilingi milioni 306 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye swali la pili sasa. Mheshimiwa Twaha Mpembenwe amekuwa akiifuatilia sana juu ya ujenzi wa shule hizi za Mchukwa na nyingineyo ambayo imetajwa. Namtoa mashaka, Serikali hii itatafuta fedha na kuweza kupeleka kwa ajili ya ukarabati wa maeneo haya ambayo ameyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kule Kibiti kuna shule mpya ya Sekondari ambayo sasa fedha imepelekwa kwa jitihada zake Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa fedha kwa ajili ya kujenga shule katika Kata ya Kibiti.