Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Twaha Ally Mpembenwe (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuwa mchangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Naomba tu kidogo nifanye marekebisho hapo jina langu naitwa Twaha Mpembenwe, Seif Mpembenwe alikuwa mzee wangu na tayari ameshatangulia mbele ya haki.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi, wapiga kura wa Jimbo la Kibiti kwa heshima kubwa sana waliyonipa mimi na familia yanguna leo hii niko hapa mjengoni nawashukuru sana. Sambamba na hilo, naomba vilevile nichukue fursa hii kuwashukuru watu muhimu sana katika maisha yangu hasa rafiki yangu mpenzi ambaye ni mke wangu mama Sabrina; wanangu Sabrina, Leyla, Naima na Najma. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoweza kutoa shukrani za dhati kwa aliyekuwa Mkuu wangu wa Wilaya lakini sasa hivi ndiye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Joseph Joseph Mkirikiti pamoja na Katibu Tawala wangu wa Mkoa, mama yangu Rehema Madenge wakati nafanyakazi chini yao walikuwa viongozi wazuri na waliweza kuniongoza vizuri na mpaka leo nimekuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Pwani ni wakarimu sana, halafu tuna desturi ya kuweza kushukuru. Sasa kabla sijaanza kuichangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ningependa kuanza kumshukuru Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mambo makubwa na mazuri aliyoweza kutufanyia watu wa Jimbo la Kibiti.

Mheshimiwa Spika, katika sekta nzima ya afya katika kipindi cha mwaka 2015 - 2020 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliweza kutupatia fedha takriban shilingi 4,021,493,500,fedha hizo ziliweza kutumika katika kuweza kujenga hospitali ya wilaya, vituo viwili vya afya, zahanati tisa na vilevile tumeweza kukarabati kituo chetu cha afya kikongwe cha pale Kibiti. Tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya elimu,Mheshimiwa Rais aliweza kutupa fedha takriban shilingi 4,243,607,588.99, fedha hizi zimeweza kutumika katika kuweza kujenga vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za Walimu na kuweza kukarabati vilevile shule yetu kongwe ya Kibiti Sekondari ambayo ninauhakika kabisa baadhi ya Wabunge hapa wamepita na kuweza kusoma katika shule ile.

Mheshimiwa Spika,kama hivyo haitoshi Mheshimiwa Rais ametufanyia lingine kubwa ameweza vilevile kutupa fedha takriban shilingi bilioni 14.3 katika Kata ya Salale katika Wilaya ya Kibiti pale katika Kijiji cha Nyamisati limejengwa Gati zuri ambalo kwa namna moja ama nyingine limeweza kuturahisishia sisi watu wa Kibiti pamoja na ndugu zetu wa Mafia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili vilevile naomba ku- declare specialinterest, katika gati lile limeweza kuturahisishia sana sisi watu wa Kibiti kwasababu kule Mafia kuna akinamama kule wa kiarabu arabu na sisi watu wa Kibiti tunakwenda kule kwenda kuoa sasa kuweza kuchanganya mbegu zile. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hilo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Rais ameweza kutupa fedha takriban shilingi 4,021,850,786.38 fedha hizi zimeweza kutumika katika kuweza majengo ya utawala majengo yale ni mazuri jengo kubwa la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji, bado kuna fedha kama shilingi milioni 700 tumeweza kuziomba kwa Serikali Kuu ili tuweze kumalizia katika miundombinu masuala mazima ya umeme na maji ili wananchi wale sasa waweze ku-enjoy kuweza kumchagua Mheshimiwa Raisna kuweza kuwa na Mpembenwe kama Mbunge wao.

Mheshimiwa Spika, shukrani hizi bado zinaendelea katika Jimbo letu la Kibiti limegawanyika katika sehemu kubwa mbili kuna sehemu ya geta na sehemu ya juu huku. Katika sehemu ya geta kule Mheshimiwa Rais aliweza kutupa fedha takriban shilingi bilioni 2.5, fedha zile katika kujenga daraja, kuna mambo mambo yaliweza kutokea lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ndugu yangu Mheshimiwa Selemani Jafo aliweza kutia mguu, sasa hivi ninavyoongea wakandarasi wako site, mkandarasi aliyekuwa amejenga gati la Nyamisati ndiyo yuko kule shughuli zinaendelea na vijana wetu pale vilevile wameweza kufunguliwa fursa za ajira, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais katika hilo.

Mheshimiwa Spika, kubwa kuliko yote tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuturudishia amani ambayo ilikuwa imepotea katika Jimbo la Kibiti. Jimbo la Kibiti amani ilikuwa ni bidhaa adimu sana. Nataka nieleweshe tu kwamba kuku walikuwa na uhuru mkubwa sana kuliko mwanadamu wa kawaida katika kipindi cha mwaka 2018/2019, lakini Mheshimiwa Rais aliweza kusimama katika nafasi yake kama Amiri Jeshi Mkuu na kuweza kuturudishia amani hiyo. Tunamshukuru sana katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa shukrani hizo katika Bunge hili la Kumi na Mbili tumefarijika sana kwasababu tuna kiongozi vilevile wa Chama Cha Mapinduzi naye siyo mwingine ni komredi Humphrey Polepole. Nataka niombe vile vile nichukue nafasi hii dakika moja kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Jimbo la Kibiti katika kipindi cha uchaguzi mpaka hivi sasa. Hivi ninavyoongea baada ya kuweza kuwasiliana na wadau mbalimbali nimeweza kufanikiwa kupata fedha shilingi milioni 175 kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kununua ambulance. Fedha hizi zipo sasa hivi katika akaunti ya Mkurugenzi Mtendaji, tukimaliza session hii tu nitamwona Waziri wa Fedha ili tuweze kuweka mustakabali mzima wa masuala ya exemption tuweze kuleta ambulance ile na wananchi wa Kibiti sana waweze kufurahia kuwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli lakini vilevile kuwa na Mbunge mbunifu ambaye ni Mpembenwe.

Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi wakati tukiwa vilevile katika suala zima la kampeni, nilipita huko vichochoroni, nimeweza kuhangaika kwa wadau wangu mbalimbali kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji ninavyoongea tumeweza kupata fedha shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa dispensary fedha hizo zipo kwa Mkurugenzi Mtendaji wakati wowote kuanzia sasa hivi dispensary ile itajengwa kwa kupitia force account. Hilivilevile linafanyika.

Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi vile vile naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu pamoja na kiongozi wetu komredi Humphrey Polepole, madawati 100 tayari yalishasambazwa katika Jimbo la Kibiti na hivi ninavyoongea kuna madawati mengine 500 wiki tatu zijazo yatasambazwa katika shule za msingi vilevile pamoja na shule za Sekondari.

Mheshimiwa Spika, pia naomba tu niseme tutaanza ujenzi wa kituo cha Polisi haraka iwezekanavyo kwa kutumia nguvu zetu za ndani.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais mimi sitaki kwenda mbali nasema machache tu.

SPIKA: Mheshimiwa Twaha sasa hotuba ya Rais sasa. (Kicheko)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sanakatika kuichangia hotuba ya Mheshimiwa Rais mimi nagusa sehemu tatu muhimu. Kwanza katika suala zima la kilimo, najua Wizara ya Kilimo inafanyakazi nzuri sana. Napenda vilevile kumshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Bashe kwa hotuba nzuri sana ambayo aliitoa siku alipofanya mkutano kule Tabora you realkneeled down,nilijaribu kumpigia simu lakini hakuweza kupatikana. Nampongeza sana kwa hotuba nzuri na mikakati mizuri ambayo Wizara ya Kilimo sasa hivi wanaendelea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo kuna shida kubwa sana katika suala zima la bei ya korosho. Bei ya korosho na ufuta kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani hususan katika Jimbo la Kibiti imekuwa ni mtihani mkubwa. Sisi tuna watoto wetu wa asili Wamwera, Wamakonde na Wayao kule, wao wanauza kilo moja ya korosho gredi A shilingi 2,700 wakati mwingine, lakini inashangaza sana kuona kwamba baba zao sisi watu wa Kibiti, kilo hizo za korosho gredi A inauzwa shilingi 800. Kwa hiyo naomba niishauri Serikali sasa tuweze kuangalia mustakabali mzima katika kuweza kuangalia minada hiyo wakati inafanyika, ifanyike kwa pamoja kwasababu minada ikiwa inaanza kule kusini halafu baadaye inakuja huku katika Mkoa wa Pwani, inakuwa shida sana, ndiyo wale wanunuzi wanaanza kufanya illegal price fixing, wakati mwingine wanakuja kununua korosho kwa bei ya chini. Mpaka hivi ninavyoongea sasa hivi bado kuna korosho chungu nzima za wananchi wanahangaika nazo kule.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nichangie katika sekta nzima ya mambo ya elimu. Tuna wajukuu zetu hawa sasa hivi wana miaka sita elimu bila malipo imeweza kuonyesha kwamba watoto wengi sana wameweza kusajiliwa kuingia Shule ya Msingi, ikifika mwakani tayari watoto hawa watakuwa wamesha-mature miaka saba imetimia. Kwa tafsiri hiyo tusipokuwa makini elimu bila malipo inaweza ikageuka ikawa timing bomb.

Naomba sasa kuishauri Serikali, tuweze kwa namna moja ama nyingine kuwaongezea nguvu watu wa Halmashauri turudishe baadhi ya makusanyo, vyanzo vya mapato viende kwao, hivi sasa wawe na mpango mkakati wa kuweza kutengeneza vyumba vya madarasa. Tukifanya hivyo tafsiri yake pana ni kwamba tutakuwa na uwezo mkubwa sana wa kuweza kufanikisha watoto hawa kuingia Sekondari na bila ya crisis ya namna yoyote.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo naomba nilichangie ni katika sekta nzima ya masuala ya uvuvi, nashukuru kwa kengele lakini bado dakika zinaendelea. Katika sekta hii ya uvuvi ..

SPIKA:Ahsante sana.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Delta.

SPIKA: Ooh,muda hauko upande wako Mheshimiwa Twaha.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE:Mheshimiwa Spika, nashukuru nanaunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji katika mpango huu. Lakini awali ya yote kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Wabunge wenzangu ambao wameteuliwa katika portfolio mbalimbali nataka niwaahidi tu kwamba sisi tutaendelea kuwapa ushirikiano katika nafasi zao walizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kama hivyo haitoshi vile vile nilikuwa naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Fedha kwa uwasilishaji wake mzuri ambao ameweza kuuwasilisha katika suala zima la mpango huu.

Mheshimiwa Spika, lakini kama hivyo vilevile haitoshi nimshukuru mwenyekiti wetu wa kamati ya bajeti kwa vile vile kuweza kuwasilisha na kuweza kutoa maoni mazuri zaidi kuhusiana na suala la mpango huu.

Mheshimiwa Spika, kubwa kuliko lote nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu mama yetu mama Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri sana kwa kuweza kuwatia matumaini watanzania ambao walikuwa tayari wameshapoteza matumaini na walikuwa na vilio ndani ya nafsi zao. Lakini mama ameanza vizuri sana na naomba tu nipite katika kauli yake niseme wale ambao wanakusudia kumzingua mama basi tutakwenda kuzinguana nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba ni nichangie mpango huu katika maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni suala zima la tax base na eneo la pili ni suala zima la performance of the projects hizi kubwa kubwa ambazo tunaendelea nazo sisi kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la kuchangia kwenye tax base kuongeza wigo wa tax base nilikuwa naomba kidogo nitoe ushauri hapa kwa Serikali. Hizi tough decision kuzichukua wakati mwingine kuzichukua zinakuwa ni ngumu lakini they are wealth taken mimi nilikuwa naomba niishauri Serikali tuangalie uwezekano wa ku-reduce cooperate tax rate tukifanya hivyo tafsiri yake ni nini tutakwenda kutengeneza kitu kinachoitwa multiply effects tunapo reduce cooperate tax rate tunawa-encourage cooperate citizen siyo tu wale kutoka nje lakini hata hawa wa local investors wale wenye mitaji iliyokuwa iko ndani sasa watatoka na watakwenda ku-invest maeneo tofauti.

Mheshimiwa Spika, sasa tunakwenda kutengeneza multiply effect kwa kufanya hivyo. Tafsiri yake pana ni kwamba anapokuja mtu aka-invest, mndengereko kama mimi nikawa na hela yangu ya mkopo nikachukuwa, nikaenda ku-invest kwenye kiwanda, ni kwamba nitaajiri watu. Ninavyoajiri watu, kinachofuata maana yake ni kwamba tunakwenda kuongeza wigo wa tax; na wale watu wanaokwenda kuajiriwa pale, tuta-improve their standard of living.

Mheshimiwa Spika, hii ni very basic economics ya form four sijui form five na nafikiri Mheshimiwa Waziri you know better than this. We have to reduce the corporate tax rate, lazima tucheze na fiscal policy ili sasa tuweze kuwa- encourage investors waje waweze ku-invest. Mama yetu alisema hii katika hotuba zake katika mambo aliyokuwa anazungumza, kwamba lazima tutumie fursa mbalimbali ili kuhakikisha kwamba hatuwakumbizi wawekezaji, tunawavuta ili tuendelee kuwa nao. Kwa kufanya hivyo, tafsiri yake ni kwamba lazima tuchukue tough decision. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna nchi ambazo zimeweza kufanya hivyo. Marekani katika miaka ya nyuma huko waliweza ku-reduce tax corporate rate na athari yake ni kwamba, kukawa na viwanda vingi, wawekezaji wakawa wengi waka-increase vilevile rate employment. Tukifanya hivyo, ile corporate tax base tunaiongeza.

Mheshimiwa Spika, wale watu ambao tunawakamua; nakumbuka kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja; mwanangu mmoja kutoka Mtama aliwahi kuzungumza kwamba ng’ombe tunamkamua mpaka inafikia hatua sasa hakuna cha kumkamua. Tafsiri yake ni kwamba we do have to expect kwamba hawa larger tax payer ndio watakuwa wao tu peke yao wanaweza waka- finance hizi fedha ambazo tunaenda kuzikusanya kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ndani ya nchi.

Nilikuwa naomba nishauri katika eneo hilo. Eneo la pili katika suala lazima la kungoze hii tax base…

SPIKA: Mheshimiwa Twaha, mwanao anakuangalia.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, mwanangu ananiangalia!

SPIKA: Mh! Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Sawa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, vile vile katika suala la kuongeza hii tax base nilikuwa naomba niishauri Serikali tuongeze wigo, tumefanya vizuri sana katika suala zima la electronic stamp, tumefanya vizuri sana kule kwenye wine katika mambo ya spirit tumefanya vizuri sana kwa sababu tumeweza ku- increase ile collection. Kwa mfano tumeweza ku-increase domestic collection 74.4 percent katika quarter ya kwanza ya 2020.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Value Added Tax ilikuwa imeongozeka 22.8 percent, vile vile tumeweza ku- increase suala nzima la makusanyo ya soft drinks kwenye asilimia 11.7. Hapa tumefanya vizuri. Sasa ni muhimu vile vile Serikali tukaongeza ile electronic stamp katika point of production kwenye maeneo mengine. Kwa mfano katika sekta nzima ya uzalishaji wa cement, kule bado hatujakugusa.

Mheshimiwa Spika, watu wengi sana wanatumia cement na action ambayo inafanyika kule, we can not control it. Katika maeneo mazima ya mambo ya nondo, mabati, we cannot control it. Kwa hiyo, ili sasa ili tuweze ku- extend ile tax base, mambo ya namna hii lazima tuweze kuyashungulikia. Tumefanya vizuri, lakini naomba kuishauri Serikali tuendelee kuweka msisitizo katika maeneo hayo mengine ili sasa tusije tu tukawabana wale larger tax payers peke yao. Wanatukimbia, wanaondoka.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mama yetu wakati anahutubia Taifa, watu wengi sana waliweza kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. Wakati nikiwa hapa, Wandengereko wenzangu kutoka Kibiti walikuwa wanapiga simu na kutuma message kedekede wakisema kwamba sasa jembe limekuja na tunakwenda kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni lazima tuangalie, hii tax burden tuweze kui- balance. Tukifanya hivyo, nafikiri tutafanya vizuri sana, collections zetu za ndani zinaweza zikaongezeka.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo nilikuwa naomba niichangie ni katika suala la zima la PPP. Mimi ni mgeni hapa Bungeni, lakini I know for sure, kwa kupitia paper works nilijua kuna Sheria ya PPP ililetwa hapa na ikaja mwaka 2018 kufanyiwa some amendments. Nilikuwa naomba niishauri tena Serikali, kama kuna upungufu katika sheria ile, basi iletwe tena tuweze kuishungulikia, kwa sababu miradi mikubwa mikubwa hii ni lazima tuifanye kwa kupitia PPP. Tukifanya hivyo, tafsiri yake ni kwamba haka kasungura kadogo, fedha zetu hizi za ndani tunazozikusanya zinaweza zikaenda kutusaidia ili kuweza kuendeleza huduma za jamii.

Mheshimiwa Spika, mfano katika Sekta za Afya na katika mambo mengine fedha hizi zinaweza kutumika. Kwa hiyo, miradi mikubwa mikubwa hii ili tuweze kuiendeleza vizuri zaidi, basi ile idea ya PPP tuilete tena hapa kama ile sheria ina upungufu. Kwa sababu tunapozungumzia PPP, tunazungumzia mifano tunayo pale ndiyo, tumejenga mabweni, lakini tuzungumzie substantial, ile miradi mikubwa mikubwa kama Serikali. Tunakwenda kutengeneza pale mradi wa Mwalimu Nyerere. If not, twendeni kwenye PPP. Najua tunatumia fedha zetu za ndani, ni suala la busara zaidi.

Mheshimiwa Spika, kama hivyo haitoshi, siyo vibaya vile vile, tukiona kwamba mazingira siyo rafiki and of course it has to be so, twendeni tukatumie PPP ili sasa kwa namna moja ama nyingine, miradi hii iende sambamba na iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, uliweza kutoa hapa maelezo kidogo kwamba mabehewa siyo lazima tu yashughulikiwe na watu wengine, sisi wengine tuliwahi kupata bahati kukaa kwa Wandengereko nchi za nje huko, tuliona. Ukienda pale UK utakuta zile British reli zinazokuwa zinazunguka, siyo zote zinakuwa controlled na British Government. Unaweza ukakuta kwamba kuna tajiri tu mmoja anashughulikia eneo fulani, tajiri mwingine anashughulikia eneo fulani lakini mambo yanakwenda.

Mheshimiwa Spika, when you talk about infrastructure in UK it is superb, ipo namba moja. Sisi twendeni tukaige mambo haya, wakati ndiyo huu. Mama tunaye, Mheshimiwa Samia anatupa sana uwezo sisi Watendaji. Ameweza kutupa fursa kusema kwamba tumieni vipaji mlivyonavyo ili tuweze ku-extend tax base tuweze kuongeza maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana nichangie katika haya maeneo mawili. Hata hivyo, katika suala hili la tax base nitakwenda kwa Mheshimiwa Waziri kwa wakati maalum kumpa takwimu ambazo ni research ambayo nimeweza kuifanya kwenye Commercial City pale Dar es Salaam. If you look at the number from 2015 to date, the number of corporate citizen ambazo tayari zimeshafungwa they are so many.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia amount of tax tunazo- collect zina-increase katika decreasing rate, iko pale Dar es Salaam. Mheshimiwa Waziri akiniruhusu, mimi nitakwenda, nitamfuata, nitampa research ambayo tulikuwa tumeifanya. Sasa ni lazima tuchukue maamuzi magumu ili tuweze kusonga mbele na tuweze kum-support mama yetu katika kuweza kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuwa mchangiaji siku ya leo. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kukupa pole wewe pamoja na Bunge letu Tukufu kwa kuondokewa na mwenzetu, kipenzi chetu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia Muswada huu, naomba niseme neno moja tu kama siyo mawili. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati anaingia madarakani mwaka 2015, kauli yake kubwa sana ilikuwa ni kwamba yeye ndiye Rais wa wanyonge na hayo yamethibitika. Ameweza kulipigania hilo katika kuhakikisha mwananchi wa kawaida anakwenda kutetewa hali yake ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la mambo ya kisheria sisi kama Wawakilishi wa Wananchi yanatukuta kule chini katika Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya. Lugha inayotumika kule ni Kiingereza. Anakuja mwananchi ameshinda kesi, lakini hajui kama ameshinda kwa sababu lugha iliyokuwa imetumiwa mle ni “yes”, “no”. Kwa hiyo, hii inakuwa ni shida kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu Muswada huu ulioletwa umeletwa hapa, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Vilevile nampongeza Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mwenyekiti na timu yake nzima ya Kamati ya Sheria. Muswada huu ni sahihi, umekuja katika kipindi kinachofaa kabisa ili sisi Wawakilishi wa Wananchi twende kule chini tukawatetee wananchi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, Kiswahili ni lugha ambayo inastahiki iendelee kutumika kwa sababu kubwa moja ya kulinda tamaduni zetu. Watoto wetu hawa sasa hivi wanaingia katika mitandao hii, kuna mambo mengi yanafanyika kule. Tutakapokuwa tunaitumia lugha yetu ya Kiswahili, ndiyo tutakapoweza kulinda tamaduni zetu hasa mambo haya ya kisasa; ndoa hizi za wenyewe kwa wenyewe, sijui rika moja, mwanaume kamuoa mwanaume, mwanamke inakuwa shida. Mambo haya yanarithiwa kwa sababu ya kutumia lugha za watu. Mheshimiwa Rais ameonyesha uzalendo na amepambana sasa hivi Kiswahili kinatumika kule SADC kama moja ya lugha ambayo inatumika katika mikutano yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nishukuru, lakini nimpongeze tena Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Kamati yote kwa ujumla, kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)