Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rwegasira Mukasa Oscar (18 total)

MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha na ni muhimu sana Watanzania wakapata ufahamu kwa takwimu kuhusu ukubwa au udogo wa tatizo hilo kuliko kupata taarifa ya tukio moja moja:-
(a) Je, ni zipi takwimu sahihi na mchanganuo wa matukio ya ujambazi unaohusiana na uporaji wa fedha ikiwa ni pamoja na vifo na majeruhi ya matukio hayo kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 Kitaifa?
(b) Je, ni mikoa gani miwili inayoongoza na mikoa gani miwili yenye matukio hayo machache?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya ujambazi yanayohusisha uporaji wa fedha kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 yalikuwa kama ifuatavyo:-
Mwaka 2013 matukio 1,266; mwaka 2014 matukio 1,127; na mwaka 2015 yalikuwa 913. Jumla ya matukio yalikuwa 3,306 yaliyosababisha jumla ya vifo vya watu 91 na majeruhi 189.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa inayoongoza kwa matukio hayo katika kipindi hicho ni Dar es Salaam iliyokuwa na matukio 733, yaliyopelekea vifo vya watu 65 na majeruhi 43. Mkoa uliofuata ulikuwa ni Mara uliokuwa na matukio 375 ya uporaji yaliyosababisha vifo 11 na majeruhi sita. Aidha, Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na Kusini Unguja haukuwa na matukio ya uporaji wa fedha kabisa.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Mgodi wa Stamigold, Biharamulo uko kijijini Mavota katika Wilaya ya Biharamulo na wananchi wa Kijiji cha Mavota kwa sasa hawana fursa hata kidogo ya kufanya uchimbaji mdogo mdogo licha ya kwamba mgodi huo upo kijijini kwao, hali ambayo imekuwa chanzo kikubwa cha migogoro inayosababisha uvunjifu wa amani:-
(a) Je, Serikali iko tayari kuwa na mazungumzo ya kimkakati na wananchi wa Kijiji cha Mavota kupitia Mbuge wao kwa manufaa ya uwekezaji na wanakijiji wa Mavota?
(b) Kama Serikali haiko tayari kufanya mazungumzo hayo, je, ni kwa sababu zipi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kuwa na mazungumzo na wananchi wa Kijiji cha Mavota kwa lengo la kuwawezesha wananchi hao kutumia fursa zilizopo katika Mgodi wa Stamigold karibu na Mavota. Mgodi huo kwa sasa unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia STAMICO ambapo Stamigold kampuni tanzu ya STAMICO ndiyo inayofanya shughuli za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo muhimu yatakayozingatiwa ni pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji hao wadogo, kuwaelimisha namna ya kupata mitaji ya uchimbaji ikiwa ni pamoja na kutumia fursa za kuomba ruzuku Serikalini. Kadhalika, pamoja na kuwapa elimu na kuwahamasisha kuunda vikundi vya uchimbaji ili waweze kusaidiwa kwa pamoja. Aidha, Mgodi wa Biharamulo utawapatia mafunzo ya utaalamu wa kuchimba madini pamoja na kuwafundisha kanuni za usalama, afya na utunzaji wa mazingira katika migodi yao. Lakini pia watapewa mafunzo kwa vitendo katika mgodi wa Stamigold pale itakapohitajika kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mgodi huo uko tayari na ulishaanza kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Mavota. Kati ya tarehe 26 na 30 Juni, 2015, Mavota Gold Mine Group kilipewa ushauri wa namna bora ya kuendesha shughuli za uchimbaji na utafiti wa dhahabu katika eneo walilomilikishwa leseni. Kikundi hicho kilimilikishwa leseni ya uchimbaji mdogo yenye Namba PL 001493WLZ iliyotolewa tarehe 23 Februari, 2015. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 9.43.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi umetoa fursa za ajira kwa vijiji vya jirani. Vijana wenye ajira za muda mrefu kutoka vijiji vya jirani ni 15 na wafanyakazi wenye mikataba ya muda mfupi ni 54.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mgodi umetoa fursa za kibiashara kwa vikundi vitatu kutoka vijiji vya Mavota pamoja na Mkukwa ambapo wanavikundi hushirikiana kutafuta mazao ya kuuza mgodini kwa kuwasilisha mazao hayo kila wiki. Mazao hayo ni pamoja na viazi vitamu, mihogo, mboga za majani pamoja na matunda. Kutokana na kufanya biashara na Stamigold kati ya kipindi cha Julai 2014 na Disemba 2015, vikundi vyote vitatu vimeweza kujipatia zaidi ya shilingi milioni 200.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Wananchi wa Kijiji cha Busiri, Wilayani Biharamulo ni miongoni mwa Watanzania wanaoendesha maisha yao kwa shughuli za uchimbaji mdogo mdogo ambazo zinahitaji kuungwa mkono na Serikali kimkakati.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaunga mkono wachimbaji wadogo wadogo wa Busiri?
Je, Serikali iko tayari kuwatembelea wananchi wa Busiri na kuwaelewesha ni namna gani na ni lini itaanza kutekeleza mkakati huo wa kuwaunga mkono wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mikakati ambayo Serikali imechukua kwa wachimbaji wadogo wa madini hasa katika eneo la Busiri ni kuwatafutia maeneo ya uchimbaji wa madini. Wizara imetenga eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 11,031 lililoko chini ya leseni za utafutaji wa madini namba 3220 ya mwaka 2005 iliyokuwa inamilikiwa na Ndugu Daudi Mbaga. Kadhalika katika eneo hilo la leseni ya utafutaji wa madini namba 5853 ya mwaka 2009 iliyokuwa chini ya kampuni Meru Resource Limited ambazo zote zimemaliza muda wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwisho wa mwezi Machi mwaka jana na mwisho wa mwezi Machi mwaka huu Wizara imegawa kwa wananchi wa Busiri leseni 81 zenye uchimbaji mdogo wa madini ambazo kwa ujumla wake zinachukua hekta 810 kati ya hekta 11,031 za eneo hilo. Aidha, Wizara imegawa leseni nyingine 30 za uchimbaji mdogo katika eneo lililoko katika karibu na eneo hilo takribani kilometa moja tu kutoka eneo la uchimbaji mdogo wa madini la Busiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine ni kuendelea kulitumia eneo la Shirika la STAMICO kutoa huduma za ugani kwa wachimbaji madini wadogo hasa wa kijiji cha Busiri na maeneo mengine nchini. Mkakati mwingine ni kuwapatia ruzuku pamoja na kuwapatia elimu endelevu itakayoendelea kutolewa pamoja na shirika la STAMICO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiwatembelea wachimbaji hawa mara kwa mara hasa kwa kutumia Maafisa na wataalam wa ofisi ya Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi na Afisi Madini Mkazi wa ofisi ya Bukoba. Tarehe 11 Machi, 2016 Afisa Madini Mkazi wa Bukoba alifika na kufanya mkutano na kikundi cha Busiri Mining Co-operative Society Limited chenye leseni ya uchimbaji mdogo. Aidha, ili kutekeleza sasa ombi la Mheshimiwa Mbunge Wizara yangu itamtuma tena Afisa Madini kutembelea eneo hilo na kuwaelimisha wananchi juu ya uchimbaji mzuri mdogo wa madini katika eneo hilo.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kwa miaka ya hivi karibuni vifo vya Watanzania kutokana na ajali za barabarani vimekuwa vingi na kuleta hisia kwamba hali hii sasa ni janga la Kitaifa, ni muhimu Watanzania wakafahamu kwa takwimu kuhusu ukubwa wa tatizo la vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani badala ya kusikia taarifa ya tukio moja moja:-
(a) Je, takwimu ni zipi na mchanganuo wa matukio kuanzia mwaka 2013 hadi 2015 Kitaifa na Mikoa miwili inayoongoza na yenye ajali chache?
(b) Je, mfumo gani endelevu kama upo, wa wazi ambao Serikali inatumia kutoa takwimu hizi kwa Watanzania badala ya taarifa moja moja pindi inapotokea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 zilitokea ajali 23,842 zilizosababisha vifo karibu 4,002 na majeruhi 20,689. Mwaka 2014 kulitokea ajali 14,260 zilizosababisha vifo 3,760 na majeruhi 14,530 na mwaka 2015 zilitokea ajali 8,337 zilizosababisha vifo 3,464 na majeruhi 9,383.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa ambayo imeongoza kwa ajali kwa mwaka 2013 ni Mikoa ya Kipolisi ya Kinondoni, ambao ulikuwa na ajali 6,589 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ambao ulikuwa na ajali 3,464 na mkoa ambao ulikuwa na ajali chache ilikuwa ni Simiyu ambao ulikuwa na ajali 67 na Tanga ajali 96. Mwaka 2014 mikoa iliyoongoza kwa ajali ni Mikoa ya Kipolisi Kinondoni ambapo ajali zilikuwa ni 3,086 na Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ulifuata kwa kuwa na ajali 2,516. Mikoa ambayo ilikuwa na ajali chache kwa mwaka huo ilikuwa ni Kagera ambayo ilikuwa na ajali 29 na Simiyu ajali 55. Mwaka 2015 Mkoa wa Kipolisi ya Ilala ajali 1,431 na Temeke ajali 1,420 ambayo ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa mwaka huo. Mikoa ambayo ilikuwa na ajali chache kwa mwaka 2015 ni Mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa na ajali 53 pamoja na Mkoa wa Arusha ambao ulikuwa na ajali 53.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo endelevu wa wazi uliopo wa kutoa takwimu za kupitia taarifa za mwaka za Jeshi la Polisi (Police Annual Reports) ambapo kila Mtanzania anaweza kupata taarifa hizo za ajali.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Tanzania imekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa sasa, ambapo Watanzania wamekuwa wakijulishwa na Serikali juu ya namna ya ushiriki wa Taifa katika mtangamano huo; ushiriki bora na wenye tija hauwezi kutokana na ushiriki mzuri wa Serikali pekee na mihimili mingine ya utawala bali pia ushiriki wa wananchi kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na kwa namna ya pekee Mikoa inayopakana na nchi za Jumuiya hiyo ukiwemo Mkoa wa Kagera.
(a) Je, kuna mkakati gani wa Serikali kumjengea mwananchi mmoja mmoja na taasisi mbalimbali kushiriki katika Jumuiya hiyo?
(b) Kama mkakati huo upo; je, ni kwa vipi wataufahamu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba jina la Wizara sasa limebadilishwa na imekuwa ni Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatambua umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika kujenga Jumuiya yao ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 7(1)(a) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inabainisha kuwa Jumuiya ni ya wananchi, hivyo nchi wanachama zina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanajengewa uwezo ili waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mtangamano wa Afrika Mashariki kwa kuzitumia fursa za Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hilo, Wizara iliandaa Mkakati wa Mawasiliano kwa Umma ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2012. Mkakati huu unatoa mwongozo wa utoaji elimu kwa Umma kuhusu Mtangamano wa Afrika Mashariki kwa makundi mbalimbali na pia ni nyenzo ya kupata mrejesho kutoka kwa wadau.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwa Mkakati huo, wananchi wamefahamishwa kufahamu mkakati huu kupitia ziara za mipakani, vipindi vya televisheni na redio, vipeperushi, machapisho, makala, mikutano na wafanyabiashara, semina, maonesho mbalimbali kama vile Wiki ya Utumishi wa Umma, Saba Saba, Nane Nane, Maonesho ya Wafanyabiashara Zanzibar na Siku ya Mara pamoja na kuweka mabango kwenye mipaka ya Namanga, Horohoro, Holili, Sirari, Mutukula, Rusumo na Kabanga.
Aidha, mkakati huu ambao upo katika mfumo wa kitabu, umesambazwa kwa wadau kwenye shughuli mbalimbali za elimu kwa Umma zinapofanyika na unapatikana katika tovuti ya Wizara, pamoja na Kituo cha Habari cha Wizara kilichopo katika jengo la NSSF - Water Front, ghorofa ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sote ni wadau wa mtangamano wa Afrika Mashariki, Wizara inaomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha wananchi katika Majimbo yao pindi wanapoongea nao ili waweze kuzitambua na kuzitumia fursa zitokanazo na mtangamano huo, kwani ni eneo mojawapo linaloweza kuwaongozea kipato na kupunguza tatizo la ajira lililopo nchini.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Biharamulo ni moja ya Wilaya za Mkoa wa Kagera zilizoathirika sana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba na hivyo ustawi wa zao hilo kuu la chakula upo mashakani.
Je, Serikali inatoa kauli gani isiyo nyepesi na inayolingana na uzito wa suala hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ugonjwa wa unyanjano unasababishwa na bakteria aitwaye Bacterium Xanthomonas Campetris pv. Musacearum. Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuudhibiti na kuzuia ugonjwa huu nchini kwa kutoa elimu sahihi juu ya unyanjano kwa wadau wote, madhara, ueneaji na udhibiti wa ugnjwa huu. Maeneo ambayo yamezingatia maelekezo ya udhibiti yamefanikiwa kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huu. Hata hivyo katika kipindi cha ukame ugonjwa wa black sigatoka umejitokeza Wilayani Biharamulo na kuleta athari kubwa katika zao la migomba. Ugonjwa huu unasababishwa na Fungi. Ugonjwa huu umejitokeza kuanzia mwezi wa Juni mwaka 2016 baada ya kuanza kipindi cha jua. Maeneo yaliyoathirika ni Nyamahanga vijiji vinne, Bisibo vijiji vinne, Ruziba vijiji vinne, Rusahunga vijiji vinne na Biharamulo vijiji vinne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia kituo chake cha utafiti kimeelekeza wataalam wa kilimo Wilayani Chato kuwashauri wakulima, kuondoa migomba yenye dalili kali za ugonjwa huo na kupanda mbegu aina ya FHIA zinazovumilia ugonjwa huu ambazo kwa sasa mbegu hizi zinapatikana kwa wingi Wilayani humo. Wakulima wakizingatia ushauri huo utasaidia kupunguza usambaaji wa ugonjwa huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, magonjwa ya unyanjano na black sigatoka yanaweza kutokomea iwapo wakulima watafuata kanuni bora za kilimo. Aidha, watafiti wetu na wa nchi za Kanda za Afrika Mashariki wanaendelea kutafiti aina ya migomba yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa huu.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Matumizi yasiyo sahihi ya lugha ya Kiswahili kwenye vyombo vya habari hayatoi fursa ya kukua kwa lugha yetu na badala yake yanachangia kurithisha lugha yetu kwa watoto kwa namna iliyo mbovu; mathalani, Mtangazaji wa runiga au redio anasema “hichi” badala ya “hiki” au nyimbo hii badala ya “wimbo huu” na kadhalika.
Je, Serikali ina mpango gani wa kimkakati wa kuvifanya vyombo vya habari kuwa mawakala wa kulinda usahihi wa lugha ya Kiswahili badala ya kuwa miongoni mwa wabomoaji wa lugha yetu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kusimamia na kuratibu matumizi ya Kiswahili fasaha kwa vyombo vya habari. Hivi sasa inaandaliwa Sera ya Lugha ambayo itabainisha majukumu ya vyombo vya habari katika matumizi na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili. Aidha, kwa sasa hatua mbalimbali zinachukuliwa katika kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vinakuwa mawakala wa kulinda lugha ya Kiswahili, ambapo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na wadau wa Kiswahili limeendelea kuendesha semina, warsha, makongamano na kutoa elimu inayohusu matumizi fasaha ya Kiswahili kwa waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali pamoja na kuandika makala na vijitabu maalum na kuvisambaza kwa wanahabari kuhusu matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lugha ya Kiswahili ni utambulisho na utamaduni wa Taifa letu na vile vile ndiyo lugha ya Taifa, waandishi wa habari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha lugha hii inaendelezwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi.
Aidha, mifano iliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge ya “wimbo huu” na “hiki” ni mada za nomino na sarufi ambazo hufundishwa katika somo la Kiswahili katika shule za msingi na upili. Hivyo, napenda kutoa wito kwa wanafunzi ambao miongoni mwao ni wanahabari watarajiwa kujifunza masomo yote kwa bidii ikiwa ni pamoja na Kiswahili.
Vilevile wamiliki wa vyombo vya habari wazingatie ufaulu wa somo la Kiswahili kama moja ya sifa kwa waombaji wa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashauri wanahabari kutumia zana kama vile kamusi na vitabu vya miongozo ya uandishi na kuhudhuria makongamano ya Kitaifa na ya Kimataifa ya lugha ya Kiswahili, kwa mfano, Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) ambayo hufanyika mwezi Septemba kila mwaka. Katika makongamano hayo, masuala ya kisarufi na ya kifasihi huwasilishwa na kujadiliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itawasaidia kuongeza ujuzi na weledi wa lugha ya Kiswahili, kujua pia istilahi za kisayansi na kiteknolojia na hivyo kuandika na kutangaza kazi bora na zenye maudhui lengwa kwa jamii na kuepuka upotoshaji wa maneno ya Kiswahili usio wa lazima.
MHE.OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Ibara ya 57(b) ya Ilani ya CCM inaahidi kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyote vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali nchini. Kwa kuwa kundi la waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa abiria maarufu kama bodaboda ni kundi la kijasiriamali, na inawezekana ndilo kundi lenye mwelekeo na fursa za kiushirika ambalo ni kubwa zaidi Wilayani Biharamulo na nchini kote kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani mahususi juu ya kundi hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha Ibara ya 57(b) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inatekelezwa kikamilifu kuhusu uwezeshaji, Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imeweza kuvitambua na kuvisajili jumla ya vikundi 1,940 vya wajasiriamali vikiwemo vikundi 34 vya vijana waendesha bodaboda. Aidha, waendesha bodaboda 2,000 wametambuliwa kwa jitihada kubwa za Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri na wakawekewa utaratibu wa utoaji huduma ya usafiri wa pikipiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilaya ya Biharamulo imewezesha jumla ya waendesha bodaboda 410 kupata mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki na kupata leseni za kuendesha na kufanya biashara hiyo.
Natoa wito kwa Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha waendesha bodaboda wajiunge kwenye vikundi na SACCOS ili watambulike kisheria na kupata fursa ya mikopo inayotolewa kupitia asilimia 10 ya vijana na wanawake pamoja na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Walimu Wilayani Biharamulo na kwingineko nchini wanalalamika kwamba jitihada zao kwenda masomoni kujiendeleza zinafuatiwa na kusitishwa kwa upandaji wa madaraja yao katika utumishi wa umma. Pale ambapo mwalimu kapanda daraja kunaenda sanjari na yeye kuwa masomoni.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kero hii na kukatishwa tamaa kwa walimu wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawapongeza walimu wote na wataalam mbalimbali wanaojiendeleza kwa lengo la kuongeza ufanisi wao wawapo kazini. Kwa utaratibu wa sasa kupanda daraja kunaendana na matokeo ya ufanisi kazini baada ya kupimwa jinsi mtumishi alivyotekeleza malengo yake. Kwa utaratibu uliopo, mwalimu aliyejiendeleza hadi ngazi ya stashahada au shahada anapaswa kubadilishiwa muundo baada ya kuwasilisha vyeti vyake kwa mwajiri wake. Hivyo, waajiri wote wanapaswa kuzingatia taratibu za utumishi kwa kutenga bajeti kwa watumishi walio katika maeneo yao.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Watanzania wenye ulemavu wanakabiliwa na kero mbalimbali za kimaisha ikiwemo ukosefu wa ajira kama ilivyo kwa Watanzania wengine, aidha, zipo changamoto za jumla kama vile kijana mwenye ulemavu wa ngozi asiye na ajira ana changamoto ya mahitaji ya kujikimu na pia ana changamoto za kipekee za mahitaji ya kiafya na kiusalama.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu umuhimu wa kuwatazama vijana wenye ulemavu mbalimbali kwa namna ya pekee na kama zipo sera na mikakati ya kiujumla kwa vijana wote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua vijana wenye ulemavu kuwa ni kundi mojawapo miongoni mwa Watanzania wenye ulemavu nchini ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma maendeleo yao. Mojawapo ya changamoto hizo ni ukosefu wa ajira, huduma za afya, uwezo mdogo wa kuyamudu mahitaji ya kujikimu, umaskini na changamoto ya kiusalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la watu wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu, Serikali iliunda Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu ambalo kazi yake kubwa ni kutoa ushauri kwa Serikali na wadau mbalimbali wanaohusika na masuala ya watu wenye ulemavu juu ya namna bora ya kushughulikia changamoto zao, kuzijumuisha zile za kundi la vijana wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuunda Kamati za Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Wilaya, Kata na Mtaa/Kijiji. Kazi kubwa ya Kamati hizi ni kuhakikisha kuwa masuala ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa katika mipango yote ili kuondoa kero mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu elimu, ajira, afya na mikopo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nichukue pia fursa hii kuwakumbusha na kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia ipasavyo utekelezaji wa suala hili ambalo liko kisheria na pia ikizingatiwa kuwa maagizo kadhaa yamekwishatolewa kwa maneno na kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha vyuo vya mafunzo ya ufundi vya watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kuajiriwa na kijiajiri na kupata ujuzi mbadala wa kumudu maisha yao.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Kijiji cha Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo kiko kwenye njia panda kwenda Kigoma, Kahama, Ngara na kina wakazi wapatao 15,000. Kulingana na hali hiyo, kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinaibuka na idadi ya watu inaongezeka kwa kasi; aidha, kijiji hicho pia kimebanwa na hifadhi inayopakana nacho.
Je, Serikali ipo tayari kujadiliana na Halmashauri ya Wilaya na wakazi wa Nyakanazi ili kuona uwezekano wa upanuzi wa eneo la kijiji kwa upande wa hifadhi inayopakana na kituo cha polisi kwa nia ya kufungua fursa za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa ya mwaka 2002 Sura Na. 282, shughuli za makazi, ufugaji, kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu huwa haziruhusiwi isipokuwa kama Wizara yenye dhamana ya Maliasili na Utalii itaruhusu kwa kibali maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, endapo ardhi ya Nyakanazi haitoshelezi mahitaji, kijiji kinapaswa kuwasilisha maombi ya ardhi ambayo yatajadiliwa katika vikao vya Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa ili kupata ufumbuzi. Maoni hayo yatawasilishwa Wizara ya Maliasili na Utalii na endapo Wizara hiyo yenye dhamana itaridhia upanuzi wa eneo hilo la kijiji, basi unaweza kufanyika.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Serikali inakusudia kuyaondolea hadhi ya uhifadhi baadhi ya maeneo ya hifadhi kwa kuwa yamepoteza sifa hiyo. Kwa mujibu wa kauli ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akihutubia huko Benaco Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera mnamo tarehe 22 Desemba, 2015.
(a) Je, Serikali imeshaanza kuandaa mpango kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha kuwa kuna matumizi yenye tija na usawa baina ya wakulima na wafugaji pindi maeneo hayo yatakapokuwa huru ili kukuza uchumi na kuondoa hatari ya uvunjifu wa amani unaotokana na mgawanyo usio sawia kama ilivyo sasa?
(b) Je, kama Serikali imeshaanza kuandaa mpango huo, ipo tayari kuzishirikisha mapema Halmashauri za Wilaya zitakazoguswa na jambo hili ili nazo zianze kufanya maandalizi ya suala hili kwa ngazi yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya hifadhi yameanzishwa na kutangazwa kisheria kwa kuzingatia umuhimu wake kiikolojia, kiuchumi, kiusalama na kijamii kwa maslahi ya Taifa. Aidha, baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uvamizi unaotokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii imesababisha baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa kupoteza sifa ya kuendelea kuhifadhiwa. Kutokana na hali hiyo, Wizara yangu ilifanya tathmini ya maeneo hayo na kubaini jumla ya mapori tengefu 12 yalipoteza sifa na hivyo kuanzisha mchakato wa kuyarudisha kwa wananchi ili yatumike kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu imepanga kufanya tathmini ya maeneo yaliyopoteza sifa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). Maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na vitalu vya uwindaji wa kitalii yatafanyiwa tathmini ili kubainisha yale yote yaliyopoteza sifa za kuendelea kuwa hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini kukamilika, Serikali itaandaa mpango ambao utahusisha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Halmashauri za Wilaya ili kuhakikisha kuwa maeneo yatakayoondolewa hadhi ya uhifadhi yanatumika ipasavyo.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Je, ni lini Jeshi la Kujenga Taifa litakuja na mkakati wa kuwa na miradi itakayounganishwa na jitihada za vijana wasiokuwa na ajira Wilayani Biharamulo na kwingineko kwa namna isiyohitaji uwekezaji mkubwa wa kujenga Kambi za Kijeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hitaji kubwa la kuanzishwa Kambi za JKT kwenye Mikoa na Wilaya ambazo hazina Kambi za JKT ikiwemo Biharamulo. Jeshi la Kujenga Taifa limeeleka nguvu kwenye vikosi vilivyoanzishwa awali na baadaye kusitisha shughuli za kuchukua vijana mwaka 1994. Aidha, JKT inaanzisha kambi mpya katika maeneo mbalimbali kwa awamu kwa kadri bajeti yake itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Jeshi la Kujenga Taifa limejikita katika kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana waliojiunga na JKT kwa kujitolea. Lengo ni kuwa endapo vijana hawa watakosa ajira katika vyombo vya Ulinzi na Usalama waweze kujiajiriwa na taasisi nyingine za Serikali, sekta binafsi au wajiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana wanaopata fursa hii ya kujiunga na JKT kwa kujitolea ni wachache kulingana na mahitaji; wazo la Mheshimiwa la kulitaka Jeshi la Kujenga Taifa kuanzisha miradi iliyohitaji uwekezaji mkubwa na kuwashirikisha vijana wasio na ajira katika maeneo mbalimbali yasiyokuwa na kambi za JKT ikiwemo Biharamulo ni wazo zuri ambalo tunalipokea na tunaahidi kulifanyia kazi ili kuona uwezekano wa kulitekeleza.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Wananchi wa Kijiji cha Luganzu na majirani zao wa Ntumagu wanakabiliwa na adha kubwa ya matukio ya ujambazi pamoja na ukosefu wa Kituo cha Polisi kijijini hapo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Luganzu na Ntumagu kama yalivyo maeneo mengine ya nchi kumekuwa na uhalifu mdogo na wa kawaida katika siku za hivi karibuni na hakuna tukio lolote kubwa la ujambazi ambalo limeripotiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiografia Vijiji vya Luganzu na Ntumagu vipo katika vituo vikubwa vya polisi vya operation vya Nyakanazi, Kalenge na Kakongo ambavyo hufanya doria za magari ya mara kwa mara katika kudhibiti uhalifu. Hali hii imepelekea wahalifu kukimbilia katika vijiji tajwa hivyo kuleta hofu na wasiwasi kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kudhibiti Jeshi la Polisi limefungua kituo kidogo cha polisi katika kijiji cha Ntumagu ili kudhibiti njia ya wahalifu waliokuwa wakiingia vijijini kutokea maeneo ya Nyakanazi, Kalenge na Kakongo walikodhibitiwa.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-

Ni matarajio ya wananchi wa Wilaya ya Biharamulo kwamba Serikali Kuu inao mpango mkakati ambao unazitambua fursa za viwanda, biashara na uwekezaji zilizopo Biharamulo.

Je, Serikali Kuu inasemaje kuhusu nafasi ya Wilaya ya Biharamulo kwenye ushiriki wa fursa za viwanda, biashara na uwekezaji ambazo zimeibuliwa na kutambuliwa na Serikali ili ziunganishwe na jitihada za Halmashauri ya Wilaya na wananchi wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa Mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali Kuu ina jukumu la kutunga Sera na miongozo ya kisekta ambayo utekelezaji wake hufanyika katika ngazi za Serikali za Mitaa. Katika sekta ya viwanda Wilaya ya Biharamulo ina fursa ya kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani za mazao ya kilimo. Tayari Kampuni ya GESAP imetoa eneo la kujenga kiwanda cha kusindika nafaka ili kuongeza thamani za mazao ya alizeti, muhogo na mpunga katika kata ya Nyarubungo.

Vilevile Wizara yangu kupitia SIDO inatekeleza mkakati wa Wilaya moja, bidhaa moja yaani ODOP ili kuchochea maendeleo ya viwanda vidogo. Mkakati huo unakusudia kuibua na kuendeleza bidhaa moja ambapo katika Wilaya ya Biharamulo zao la muhogo limepewa kipaumbele huku mazao ya ndizi, kahawa, mahindi, maharage na kadhalika wakitumia utaratibu wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya biashara mbali na soko la ndani, Serikali imekuwa ikijadiliana na nchi nyingine kupitia majadiliano ya nchi na nchi yaani by lateral, Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC na Soko Huru la Afrika kupitia majadiliano hayo, fursa za masoko zimepatikana katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki, SADC na Soko Huru la Afrika na soko la Marekani kupitia Mpango wa AGOA. Hivyo Wilaya ya Biharamulo, inaweza kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa zinazohitajika katika masoko hayo kulingana na mali ghafi zinazopatikana Wilayani humo.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-

Wananchi wa Kijiji cha Busiri, Wilayani Biharamulo ni miongoni mwa Watanzania ambao wanaendesha maisha kwa shughuli za uchimbaji mdogo kama ilivyo kwa wenzao wengi na kwingineko nchini. Uchimbaji mdogo wa Busiri unahitaji kuungwa mkono na Serikali kimkakati:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaunga mkono wachimbaji wadogo wa Busiri na ni upi?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuwatembelea wananchi wa Kijiji cha Busiri ili kuwaelewesha ni namna gani itaanza utekelezaji wa mpango huo wa kuwaunga mkono wachimbaji hao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye vipengele
(a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mikakati mingi ya kuwaunga mkono wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa Kijiji cha Busiri, Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mkakati wa kuwasadia wachimbaji wadogo nchini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limenunua mtambo mkubwa wa kusaidia kufanya utafiti wa kina kwa kuchoronga miamba kwa bei nafuu ili kubaini mashapo zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini inakamilisha uandaaji wa kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania, toleo la nne, ambacho kinaonesha uwepo wa madini katika mikoa, wilaya, vijiji, hivyo kusaidia wananchi na wachimbaji wadogo ikiwemo wa Kijiji cha Busiri kutambua madini yaliyopo katika maeneo yao na matumizi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP), inakamilisha kujenga vituo vya umahiri katika Wilaya za Bukoba, Bariadi, Songea, Handeni, Musoma, Mpanda na Chunya ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kujifunza kwa vitendo. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa wachimbaji wadogo ili wanufaike zaidi na kazi ya uchimbaji.
MHE. ALEX R. GASHAZA (k.n.y. MHE. OSCAR R. MUKASA) aliuliza:-

Mwanzoni mwa mwaka 2016 wananchi wa Kijiji cha Kabukome Kata ya Nyarubungo Wilaya ya Biharamulo walivamiwa na tembo na kupoteza asilimia kubwa ya mazao yao:-

Je, ni lini wananchi hao watapata fidia ya mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kufuatia kuongezeka kwa juhudi za uhifadhi nchini na kupungua kwa ujangili, wanyamapori hususan tembo wamekuwa wakitoka ndani ya hifadhi na kupita maeneo ambayo ni shoroba au maeneo ya vijiji yanayopakana na maeneo ya hifadhi, ikiwemo baadhi ya vijiji vinavyopakana na yaliyokuwa mapori ya akiba ya Biharamulo na Burigi, kwa sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato katika Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo, Wilaya imekuwa ikichukua hatua kadhaa ili kunusuru maisha na mali za wananchi ambazo ni pamoja na kushughulikia matukio ya uvamizi wa wanyama kama tembo kwa haraka ikiwezekana pindi yanapojitokeza na kutoa elimu ya uhifadhi kuhusu namna ya kujilinda, lakini pia wananchi kuepuka kulima kwenye shoroba na mapito ya wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikitoa fedha kama pole kwa wananchi wanaoathirika na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni pamoja na kifuta jasho na kifuta machozi, siyo fidia kwa mujibu wa Kanuni ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi ya Mwaka 2011. Aidha, Kanuni husika zinafanyiwa marekebisho ambapo kwa sasa maoni ya wadau ndani na nje yamekusanywa, hatua inayofuata ni kuwasilisha kanuni hizo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na baada ya hapo zitasainiwa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2019, Wizara yangu haijapokea maombi yoyote kutoka Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubongo, Wilaya ya Biharamulo. Hivyo ninashauri Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri ya Wilaya kuwasilisha maombi husika ili yafanyiwe kazi kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za Mwaka 2011. Wananchi watakaokidhi vigezo watalipwa kifuta jasho mara baada ya taratibu kumalikika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. OSCAR R. MUKASA) aliuliza:-

Kata ya Biharamulo Mjini imetangazwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo hivi karibuni; kwa sasa kuna mahitaji makubwa ya upangaji wa ardhi na makazi hasa katika hadhi ya kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo:-

Je, Serikali ipo tayari kuwaunga mkono wananchi wa Biharamulo Mjini wakati huu ambapo wao wenyewe wanaendelea na jitihada za ndani kuhakikisha wanakuwa na upangaji wa makazi unaoendana na hadhi mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kuwaunga mkono wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo Biharamulo katika upangaji wa makazi ya mji huo. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imekamilisha michoro elfu tisa ya mipango miji yenye jumla ya viwanja 6,356 vyenye ukubwa wa ekari 8,753.7 kati ya viwanja hivyo, viwanja 2,337 vimepimwa na upimaji unaendelea kulingana na upatikanaji wa fedha. Mpango wa baadaye ni kujenga barabara ya lami yenye urefu wa mita 700 ili kuboresha utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, upangaji na upimaji wa makazi unawawezesha wananchi kupata faida mbalimbali ikiwemo kuongeza thamani ya ardhi, kupunguza migogoro ya ardhi, wananchi kupatiwa hati miliki ambazo zinawawezesha kuzitumia kupata mikopo katika taasisi za fedha na kuwawezesha wananchi kuishi kwenye makazi yaliyopangwa hivyo kurahisisha uwekaji wa huduma kama barabara, umeme na maji. Nazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kuhamasisha wananchi na kuwashirikisha katika upangaji, upimaji na urasimishaji wa ardhi na makazi yao.