Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Khadija Shaaban Taya (5 total)

MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, ni upi mgawanyo wa vitabu 812 vya nukta nundu vilivyotolewa katika Mpango wa Fedha za Mapambano dhidi ya UVIKO 19?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nichukue fursa hii adhimu na adimu kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu alitupa kibali cha kukutana katika eneo hili kwa siku ya leo. Shukrani ya pili nimpelekee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Mama Samia Suluhu Hasan kwa kuendelea kuniamini na kutuamini sisi, mimi na Profesa Mkenda kuweza kumsaidia katika eneo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayasi na Teknolojia, kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vitabu vya Nukta Nundu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wasioona kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wasioona wapatao 514 wanaosoma katika shule za sekondari nchini, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ilitenga shilingi milioni 704 kwa ajili ya kuchapa jumla ya nakala 18,200 za vitabu kwa ajili ya wanafunzi wasioona vya masomo yote ya sekondari, ambapo nakala 9,100 ni vitabu vya nukta nundu na nakala 9,100 ni vitabu vya michoro.

Mheshimiwa Spika, uchapaji wa vitabu hivyo upo katika hatua za mwisho na utakapokamilika vitasambazwa katika mikoa yote kulingana na mahitaji. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika mikoa yote wakiwemo wanafunzi wasioona. Nakushukuru.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa waajiri ambao wanasuasua katika kuwaajiri watu wenye ulemavu wenye sifa stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya Wazir Mkuu naomba kujibu swali namba 135 lililoulizwa na Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2010, Serikali ilitunga Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 kwa lengo la kusimamia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu. Katika kifungu cha 31(1) kinaeleza kuwa kila mwajiri wa umma au binafsi, endapo kutatokea nafasi ya ajira na mtu mwenye ulemavu aliyekidhi viwango vya chini vya ajira hiyo akaomba atalazimika kumwajiri. Aidha, kifungu 31(2) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya 2010 kinaeleza kuwa kila mwajiri mwenye waajiriwa kuanzia 20 na kuendelea anatakiwa kuwa na watu wenye Ulemavu wasiopungua asilimia tatu ya waajiriwa wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia takwa hili la sheria naomba kuwakumbusha waajiri wote kuzingatia viwango hivyo vya ajira kama vilivyoelekezwa katika sheria na tutaendelea kufanya kaguzi na kuchukua hatua kwa wasiotekeleza takwa hilo la msingi la kisheria na kibinadamu.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi inajumuisha takwimu za watu wenye ulemavu na aina ya ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dodoso la sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchini mwezi Agosti, 2022 limejumuisha maswali 10 yanayohusu hali ya ulemavu. Maswali hayo yataulizwa kwa watu wote ikijumuisha umri, jinsi na ulemavu na hivyo kutoa takwimu za hali ya ulemavu nchini. Kupitia sensa hiyo, ni matarajio yetu kuwa Serikali itapata takwimu rasmi za hali ya ulemavu nchini kwa maeneo ya kiutawala, jinsi, hali ya ndoa, kiwango cha elimu, ajira na viashiria vingine muhimu vilivyoainishwa katika dodoso la sensa.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuungana na Serikali kuwahimiza wananchi kushiriki kikamlifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti, 2022 - Sensa kwa Maendeleo, jiandae kuhesabiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuinua ushiriki wa Watu wenye Ulemavu katika michezo ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa wavu na pete?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitoa haki sawa ya ushiriki katika michezo kwa makundi yote ikiwemo watu wenye ulemavu. Moja ya mikakati ya Serikali katika kuinua ushiriki wa watu wenye ulemavu hususani kwenye mpira wa miguu, wavu na pete ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kushirikisha watu wenye ulemavu katika michezo, kusajili vyama na vilabu vya michezo kwa watu wenye ulemavu, kushirikisha michezo ya watu wenye ulemavu katika matukio yote ya michezo hususani yanayoandaliwa na Serikali, hii ni pamoja na kuziwezesha timu za Taifa za watu wenye ulemavu zinaposhiriki katika mashirikisho mbalimbali ya Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo imeendelea kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya michezo yenye mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, Serikali kwa kushirikiana na Wahisani ina mpango gani mahsusi wa kutoa Bima za Afya bure kwa watu wenye Ulemavu wa kudumu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Afya imetoa utaratibu wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum wasio na uwezo. Hata hivyo Serikali inakamilisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambapo utawezesha watu wote wakiwemo watu wenye ulemavu kupata huduma katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za afya, ahsante.