Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khadija Shaaban Taya (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. HADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii. Ikiwa leo ni siku ya kwanza nazungumza katika Bunge lako hili tukufu naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu sana, mwingi wa rehema na mwenye kurehemu amenijalia mimi kuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais na chama chake, Chama Cha Mapinduzi, Wajumbe wa Baraza wa Dodoma hii Mkoa, Wajumbe wa Baraza wa Taifa, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Ndugu Heri James na Umoja wa Vijana na Wazazi wote ahsante sana, muda hautoshi kushukuru wote, lakini naomba niishukuru familia yangu sana kwa support kubwa ambayo wamenionesha mpaka sasa kufikia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa leo ni siku saratani duniani, mimi kama mtu mwenye ualbino nimeomba niongee leo ili niwaambie umma kwamba Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri sana kwa watu wenye ulemavu au watu wenye ualbino, amefanya kazi nzuri sana. Amenunua mashine ambazo zinasaidia kuondoa tatizo la saratani. Hizi mashine ziko saba katika mikoa ya Singida, Iringa, Mara, Lindi, Zanzibar na kwingineko, lakini naomba nimuombe Mheshimiwa Rais kwa huruma yake, kwa uwezo wake, kwa kupenda kwake wanyonge, aongeze hizi mashine zitapakae mikoa yote kwa sababu hizi mashine mimi ni shuhuda wa hizi mashine. Nilikuwa na alama hapa shingoni kwangu ambayo ingeweza kunisababishia kupata saratani, hii mashine imenisaidia mimi kupona leo hii ninavyozungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba Serikali yako tukufu, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, naomba kwa sababu ni sikivu sana, iongeze idadi ya lotions kwa watu wenye ualbino. Hizi lotions zinatusaidia sana kuondoa tatizo la kupata mionzi ya jua, hili tatizo ambalo linatufanya sisi tusiishi kwa amani tupate saratani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natamani kila Mbunge aliyekuwepo hapa aende Ocean Road aone jinsi gani saratani ya ngozi inavyotumaliza na namna gani saratani ya ngozi inavyotuua. Na hata life span yetu ni miaka 35. Hapa nipo nina miaka 33 naingia miaka 34 tarehe 7 Februari, keshokutwa nashukuru Mungu kwa sababu familia yangu imeweza kunitunza na labda pia wamekuwa na uwezo kwa muda mrefu kunipa haya mafuta, lakini si kila familia ina uwezo wa kupata haya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na yote haya naomba nimshukuru Rais mara ya mwisho kabisa. Nimwambie Mheshimiwa Rais ahsante sana kwa miaka mitano aliyoingia yeye ameondoa lile janga kubwa lililokuwa linaumiza Watanzania, lililokuwa linawaumiza na kuwaliza, lilimliza Waziri wetu Mkuu katika Bunge hili tukufu, janga la kuwauwa watu wenye ualbino. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imani ile potofu imeondoka na sasa hivi tunaishi kwa raha, tunaishi kwa amani, tunajidai.

Ahsante sana Mheshimiwa Rais, lakini naomba nikwambie tena umejali sana watu wenye ulemavu, sasa hivi kila shule inajengwa kwa kuzingatia mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu kupita, lakini Mheshimiwa Rais pia nakuomba uboreshe mazingira ya vyoo kwa ajili ya afya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. HADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niunge hoja, naungana na hoja, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Nimepata taabu kukatiza Mheshimiwa Keisha.

MHE. HADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, basi naomba niendelee.

SPIKA: Hapana, basi tena. Siku nyingine nitakufikiria leo muda umebana kidogo. (Kicheko)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. HADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuzungumza leo mara ya pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikupe pole wewe pamoja na Bunge lako Tukufu na Wabunge wote kwa kuondokewa na kipenzi chetu, rafiki yetu, Mheshimiwa Nditiye.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa mbele kuzungumza juu ya hii sheria ambayo imekuja kuhusu kutumia Kiswahili katika Mahakama zetu. Mimi naona umuhimu wa hili. Nitashangazwa sana kama kuna mtu ataona hakuna umuhimu katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa msanii kwa muda mrefu sana na katika tasnia ya sanaa, kikubwa sana kilichokuwa kinatufanya tupoteze haki zetu ni kwa sababu ya kutokujua lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo ilikuwa inaandikwa katika mikataba yetu mingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi sana wamepoteza haki zao, wengi sana wamepoteza uwezo, mpaka sasa ambapo tumeweza kuwa na uwezo wa kumiliki Wanasheria. Kwa muda huo tulikuwa hatuna uwezo wa kuwa na Mwanasheria, fedha hizo tulikuwa hatuna. Kwa hiyo, nafahamu umuhimu wa kutumia Kiswahili katika hizi Mahakama zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee jambo lingine kwamba tulipopata safari ya kwenda China kupata mafunzo ya Chama cha Mapinduzi, nilipendezwa sana na tabia za Wachina. Vile vikao vilikuwa vinaendeshwa kwa lugha ya Kichina japokuwa wanajua kuzungumza Kiingereza. Wanazungumza Kichina, anatokea mkalimani anazungumza Kiingereza, halafu sisi mwenzetu anazungumza Kiingereza halafu anatafsiri kwa Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa naibu Spika, kwa hiyo, tunatakiwa tutambue umuhimu wa hii lugha kwa sababu itatuletea heshima kama Watanzania. Watanzania wengi wanakwenda China wanafanya biashara na Wachina wengi wanakuja Tanzania wanafanya biashara pamoja na kutokujua lugha lakini wanafanya biashara. Kwa hiyo, naomba Bunge hili Tukufu liunge mkono hoja hii kwa kutambua umuhimu wa uzalendo wa nchi yetu na Mheshimiwa Rais ameonyesha uzalendo wa nchi yetu kwa kuzungumza Kiswahili katika vikao vyake vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hii hatua ambayo tunakwenda kutumia Kiswahili katika Mahakama zetu ni heshima kubwa sana kwa Tanzania. Kama kuna mtu ambaye hawezi kufahamu hili, namshangaa kwa nini amekuja kuwa Mbunge kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi wake ambao wanazungumza Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lugha ambayo tunatumia hapa Bungeni ni Kiswahili, nasi ndiyo watunzi wa hizi sheria. Kwa hiyo, nashangaa kwa nini mtu hawezi kuona umuhimu wa kutumia sheria ya Kiswahili au kutumia Kiswahili katika Mahakama zetu kwa ajili ya kutoa haki? Hatujakataza kutumia Kiingereza, endapo kutakuwa na uhitaji wa kutumia Kiingereza watatumia, lakini bado itatafsiriwa kwa Kiswahili ili iweze kutusaidia baadaye kwa ajili ya records. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja hii iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri, kama Mwanakamati wa Katiba na Sheria na Mwanasheria mpya sasa. Nashukuru sana kwa kuchangia leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)