Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haji Amour Haji (5 total)

MHE. HAJI AMOUR HAJI Aliuliza:-

Kwa kuwa Serikali imeruhusu uwepo wa Mawakala wa Ajira nchini:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya ajira za nje ya nchi kwa Vijana wetu?

(b) Je, ni upi mchango wa Mawakala wa ajira hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasadia vijana wetu kupata ajira za nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kubaini nchi za kimkakati zenye fursa za ajira za staha na kuingia makubaliano (bilateral agreement) na nchi husika; kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kuwa na ujuzi utakaowawezesha kushindania fursa za ajira ndani na nje ya nchi; na kujenga mfumo wa huduma za ajira ambao pamoja na mambo mengine utarahisisha utafutaji wa kazi nje ya nchi; kuweka mwongozo wa kuratibu shughuli za wakala binafsi wa huduma za ajira wanaopeleka watu nje ya nchi; na kufanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2014 ili kuweza kuendana na mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Juni, 2021 Mawakala wa ajira nchini wamechangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya vijana 39,273 wamepewa huduma ya ushauri nasaha (employment and career counseling). Aidha, vijana 19,509 wamepewa mafunzo ya watafutakazi, vijana 11,371 wameunganishwa na fursa za mafunzo ya utarajali na vijana 10,554 wameunganishwa na fursa za kazi ndani na nje ya nchi. Ahsante sana.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Chombo Maalum (Agency) kitakachosimamia shughuli zote za kampuni binafsi za ulinzi ili kuongeza wigo wa kiutendaji pamoja na kuwepo kwa sheria itakayosimamia kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni sababu ya kuanzisha chombo maalumu (Agency) cha kusimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Jeshi la Polisi linatosha kusimamia shughuli za makampuni hayo kama ilivyo sasa kwa sababu ndiyo taasisi iliyopewa mamlaka kisheria ya kutoa leseni na hati za umiliki wa silaha hapa nchini ambazo pia humilikiwa na makampuni hayo. Utaratibu huo hutoa urahisi wa kufuatilia mwenendo wa makampuni katika utunzaji na matumizi ya silaha hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa sheria itakayosimamia makampuni binafsi ya ulinzi. Tayari mapendekezo ya kutungwa kwa sheria hiyo yapo kwenye hatua zaa awali za mawasiliano baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Baada ya maridhiano kati ya Serikali zetu mbili kufikiwa, maandalizi ya sheria hiyo yataendelea kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutunga Sera na Sheria ya Kampuni Binafsi za Ulinzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Sheria na Sera inayosimamia kampuni binafsi za ulinzi. Kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kutunga Sheria ya Huduma za sekta binafsi za ulinzi umekamilika na utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya maamuzi baada ya kupata maoni ya kina ya wadau wa pande zote mbili za Muungano juu ya Rasimu ya Sheria hiyo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, muswada wa sheria utawasilishwa Bungeni.
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itashughulikia suala la mtambo wa kielektroniki ulioharibika kwa zaidi ya mwaka sasa na kusababisha mlundikano mkubwa wa hati za ukaazi katika Idara ya Uhamiaji Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwezi Januari, 2020 hadi Juni, 2020 mtambo wa kuchapisha kadi za vibali vya elektroniki vya hati za ukaazi (E-Permit) wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar ulisitishwa na kupelekea kadi za hati za ukaazi 139 kuchelewa kuchapishwa kwa sababu ya hitilafu ya mtambo wa kuchapia kadi za vibali vya hati za ukaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, huduma za utolewaji wa hati za ukaazi ziliendelea kutolewa kwa wageni kwa kugongewa muhuri katika pasipoti ili kuthibitisha kuwepo kwao kihalali hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Julai, 2020 huduma za utoaji wa hati za kielektroniki ziliendelea kutolewa ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2022 jumla ya vibali 799 vya hati za ukaazi vya kielektroniki vimetolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. HAJI AMOUR HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na matukio ya uhalifu ukiwemo wizi katika Jimbo la Pangawe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea na kazi ya kulinda maisha ya watu na mali zao kwa kufanya doria, kuendesha operesheni mbalimbali na misako ili kuwabaini na kuwakamata wahalifu. Jeshi la Polisi limewapanga Wakaguzi wa Polisi kila Shehia katika Jimbo la Pangawe ili kusimamia usalama na kuishirikisha jamii kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalifu ni zao la jamii, hivyo naomba kutumia nafasi hii kuwaomba wazazi, walezi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuwalea kwa maadili mema vijana wetu ili waepuke kujiingiza katika uhalifu. Aidha, watumie fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa wale watakaokaidi wajiandae kukabiliana na mkono wa sheria. Nashukuru.