Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Haji Amour Haji (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kushukuru kupata nafasi hii ya kuja kushiriki katika Bunge letu hili Tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza.

Napenda kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuweza kunichagua kwa kura nyingi sana katika Jimbo langu la Pangawe, Zanzibar. Pia napenda kuishukuru familia yangu kwa kunipa ushirikiano mzuri hadi kufikia hii leo na kushinda katika Uchaguzi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kisha napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, hasa katika hotuba yake hii aliyoitoa mwezi wa Novemba, tarehe 13 ambayo mimi naiita ni hotuba shirikishi, ni hotuba ambayo imetupa mtazamo ambao ni mkubwa sana katika nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kwamba hii ni hotuba ambayo inazungumzia masuala ya maono, yaani masuala ya programu ya miaka mitano kwa kipindi ambacho kimeanzia kipindi hiki, hasa ntazungumzia katika ushirikishi uliokuwa humo kwa upande wa nchi zetu mbili; Tanzania Zanzibar pamoja na Tanzania Bara, kazungumza mengi sana kiasi ambacho ametupa moyo sisi Wazanzibari ambao tumeshiriki katika Bunge letu hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hii pia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumza vizuri sana katika kumpa ushirikiano Rais wetu wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye pia nampongeza kwa jitihada zake kubwa ambazo anazifanya na kwa weledi ambao ameupata kutoka katika Bunge hili na kwa fikra ambazo amezipata kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nadhani kwamba huko kila mmoja anasikia kuwa kazi ambayo anaifanya Rais wetu wa Zanzibar, Dkt, Hussein Ali Mwinyi, ni nzuri sana na nampongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imezungumzia suala la kimuungano hasa katika masuala ya kiuchumi, ushirikiano wa uvuvi hasa katika Sekta ya Bahari Kuu ambayo ni sekta ya Muungano. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake na ushirikiano wake mzuri na kwa kuona ule umuhimu wetu wa kuunganisha nchi zetu wa kusema kwamba atanunua meli nane ambazo nne zitakuwa kwa upande wa Zanzibar na nne zitakuwa kwa upande wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona jitihada na tunaona umuhimu wa meli zile katika hotuba ile na kipengele kile kimezungumzia suala la ajira 30,000. Tunatumai katika ajira hizo Wazanzibari labda tutapata ajira 15,000 na upande wa Bara zitakuwa ajira 15,000, itakuwa si haba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi hasa kuzungumzia suala la ajira. Nitazungumzia suala mtambuka la upande wa Muungano; tuna tatizo kubwa la ajira hasa ajira ambazo wakati mwingine tunazizungumzia kwamba ni ajira rasmi na kuna ajira ambazo siyo rasmi. Nadhani kwamba Waziri wa Ajira upande wa Tanzania yupo hapa; kuna suala ambalo limekuwa ni tatizo hasa linalohusiana na suala la ajira hizi za nje, employment agencies, ambazo hizi kwa upande mmoja kama tutaweza kuziwekea mkazo hasa ni ajira ambazo wakati mwingine linaweza likaleta soko kubwa, hasa kwa vijana wetu waliomaliza na hawana kazi. Kwa sababu wakati mwingine tunazungumzia suala la ajira kwamba labda watu waende kwenye kilimo, waende wapi. Ukiangalia hasa kuna fursa kubwa kwa kwa upande wa Tanzania kwa fursa zinazotokea nje ya nchi ambazo wakati mwingine zinakuwa ni ajira ambazo nazo ni rasmi lakini zinahitaji kuangaliwa ule umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna ajira ambazo zipo katika Nchi za Kiarabu kule, wakati mwingine tunakuwa na ufahamu ambao ni hasi kuziona kwamba zile ajira wakati mwingine kama ni human trafficking, lakini zipo ambazo zinakuja katika hali ya urasmi na zinakuja kwa mpangilio maalum, hasa kwa mikataba maalum na kwa muda maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kinachosikitisha ni kwamba wakati mwingine zile ajira zinakuja. Zipo ajira karibu, kwa mfano kwa upande wa Zanzibar kipindi hiki niliona zimekuja ajira kwa Tanzania karibu 1,200. Kwa kampuni moja ambayo ni Transguard ambayo iko Dubai pale, lakini utakuta kwamba Watanzania fursa ile tunashindwa kuitumia na kushindwa kwetu maana yake ni kwamba inawezekana milango ime…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja tu nifafanue kidogo tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo linalokuja ni kwamba milango kwa upande wa Tanzania Bara ile milango imefungwa kwa kuwaruhusu wale vijana kwenda kufanya kazi kule nje, ile fursa ya kupewa vile vibali, lakini kwa upande wa Zanzibar ile fursa inatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Waziri mhusika kwamba hiyo fursa aitoe na tupange mipangilio mizuri itakayoweza kuwapatia ajira vijana wetu wa Tanzania kwa ujumla na zinapotokea zile fursa maana yake ziwe kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine zile fursa kwa upande wa Zanzibar tunazitumia vizuri, lakini upande wa Tanzania Bara inakuwa kidogo kama kuna milango ambayo imefungwa kwa zile fursa kwa upande wa vijana wetu kwa upande wa huku. Sasa nahisi kwamba tufanye mipango mizuri kupitia Balozi zetu kuunganisha suala hili ili kwamba nayo iwe ni fursa kwa vijana wetu kupata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kutokana na muda, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Pangawe, nipo hapa kwa ajili ya kuchangia Mpango wa Taifa wa mwaka 2020/2021 pamoja na Mipango yote miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nami sina budi kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasilisha Mpango huu ambao ulikuja na theme ya uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Sasa mpango huu kwa kweli nauunga mkono na kwa kweli nasema kwamba jitihada kubwa zimefanyika katika Serikali hii ya Muungano na mambo mengi ambayo nimeyaona katika Mpango uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wowote ule wa dunia kitu kikubwa ambacho unaangalia ni suala la amani. Amani yetu tuliyokuwa nayo katika nchi yetu ya Tanzania inatosheleza kuweza kufanya uchumi wa aina yoyote. Bahati nzuri katika nchi yetu ya Tanzania, kwa mujibu wa jinsi tulivyo katika maumbile yetu, maana yake tuna uwezo wa kufanya kitu chochote. Tukija katika suala la elimu, tuna uwezo wa kuwasomesha vijana wetu na kuweza kufikia katika hatua kubwa sana ya kimaendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu nilichokuja nacho kwa pamoja katika ushirikishwaji wa nchi mbili kwa pamoja ni suala la utalii. Bahati nzuri nchi yetu ya Tanzania ikiwemo Tanzania Bara pamoja na Visiwani ina kitu ambacho ni cha kimaumbile ambacho tukija katika suala la kiutalii, tuna uwezo wa kuziunganisha nchi hizi mbili zote tukasema kwamba tuwe na utalii wa pamoja ambao ni kwa maendeleo ya nchi zote mbili. Kwa sababu kwa maumbile ya nchi yetu, kwa upande wa Bara tuna mbuga ambazo tunaweza tukazitangaza kwa pamoja na zikaleta matunda kwa ajili ya maendeleo ya watu wote. Kwa upande wa visiwani kule, tuna utalii unaotokana na fukwe pamoja na bahari tuliyokua nayo, tukizishirikisha nchi hizi, maana yake kwa Tanzania tutaleta uchumi ambao ni endelevu na mkubwa sana. Vilevile kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeunga mkono ile azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ule uchumi wa bluu ambapo ndiyo theme ambayo kwa sasa hivi inazungumzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwamba kuna vitu vitakuwa vinaonekana kwamba siyo shirikishi, lakini kimaumbile yake na kwa mujibu wa nchi yetu ilivyo, hivi ni vitu ambavyo ni shirikishi. Kama tutaweza kuunganisha utalii wa Tanzania ukawa ni utalii tunaoutangaza kwa pamoja, nadhani tunaweza tukafanya kitu ambacho ni kikubwa sana kwa mujibu wa maumbile ya nchi yetu ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa rai katika Mpango huu, pamoja na kwamba yamezungumzwa mengi; kulizungumzwa suala la utalii hasa kwa upande wa vivutio vya mbuga, ila mimi napenda zaidi tukauzungumzia katika utalii wa fukwe, tukaipa nguvu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kuichanganya ili tuwe na utalii wa pamoja. Pato litakaloweza kupatikana maana yake litaweza kuleta tija kwa nchi zetu zote mbili. Hii itaweza kufanikisha ule umoja wetu ambao tumekuwa nao katika nchi zetu kuweza kuwa shirikishi hasa katika maendeleo ya pamoja. Tanzania ni moja, watu wa Tanzania ni wamoja. Hiki siyo kitu cha ubishi. Maendeleo yoyote yale ambayo yataweza kufanyika kwa upande wa Bara, ikiwa ni kilimo maana yake faida itakuwa ni ya kwetu sote (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono Mpango wa Maendeleo, ahsante sana. (Makofi)