Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (2 total)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa sababu amenihakikishia kwamba mradi unakamilika Machi mwaka huu, napenda sasa kupata kauli ya Serikali kwa sababu bado tuna vijiji takribani 25 pale Biharamulo ambavyo havina umeme, kwa hiyo, labda ningehakikishiwa na Serikali sasa kwamba wakazi wa Biharamulo wajipange kwa ajili ya kusambaziwa umeme kwa sababu jibu ilikuwa tuko low voltage ndio maana hatukusambaziwa umeme katika vijiji vingine. Kwa hiyo, labda nipate kauli ya Serikali kutuhakikishia kwamba vijiji vilivyobaki baada ya kukamilika mradi huu vitaweza kupata umeme pia? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, uniwie radhi sana ili niweze kusimama kwa ajili ya kuongeza majibu na nimesimama kwa sababu hivi karibuni nilitembelea Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, Biharamulo wana vijiji takribani 79 na bado vijiji 27. Hivi karibuni pamoja na Mheshimiwa Mbunge nilitembelea vijiji hivyo, tumeshakamilisha matayarisho yote na si kwa Biharamulo peke yake.

Napenda nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba vijiji vyote ambavyo havijapata umeme 2,159 kati ya vijiji 12,268 tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia tarehe 15 mwezi huu ndani ya miezi 18, nimeona nianze na taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Biharamulo umeme ambao tunajenga ambao kwenye jibu la msingi umeelezwa wa kutoka Geita-Nyakanazi, Nyakanazi-Rusumo na Nyakanazi- Kigoma ni mwarobani kwa kuwapatia umeme wananchi wa Biharamulo na Mkoa wa Kagera na mikoa ya Geita pamoja na Kigoma. Mradi wenyewe peke yake kabla ya kupeleka umeme kwenye mpango wa REA utapeleka vijiji 32 na katika vijiji 32 vijiji saba ni vya Biharamulo, ikiwemo Nyakafundwa, Kalenge, Kasonta pamoja na Nyanyantakala, Mavota mpaka Nakahanyia vyote vitapelekewa umeme.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nitoe shukrani kwa Serikali kwa majibu mazuri kabisa ya kuridhisha kwa ajili ya wananchi wa Biharamulo lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Miji ya Nyakanazi, Nyakahura na Nyanza ni miongoni mwa sehemu ambazo zinapanuka kwa kasi katika Wilaya ya Biharamulo lakini bado zina ukosefu wa maji. Naomba kujua au kusikia kauli ya Serikali jinsi gani hawa wananchi wataweza kupatiwa huduma ya maji katika mwaka huu wa fedha au mwaka ujao ili tuweze kuondoa kero hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kata ya Kaniha na Nyantakala zinabeba shule mbili kubwa za boarding pale Biharamulo na shule zile zina uhaba mkubwa wa maji. Naomba kupata kauli ya Serikali ni lini wataweza hata kuchimbiwa visima viwili virefu katika shule zile ili watoto hao waweze kuondokana na adha ya kupata maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua vema tatizo la maji lililopo pale Biharamulo. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alikuwa katika Kata ya Nyakahura kwenye ziara yake ya kikazi. Kwa sasa maji toka Bwawa la Nyakahura ambapo vijiji vinne vinapata maji, tunatambua utekelezaji wake unakwenda vizuri kwa vijiji vile vinne.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunafahamu kuna ushirikiano mzuri kati ya RUWASA pamoja na BWSSA. Tayari Serikali inafahamu chanzo kile bado hakitoshelezi kwa sababu ya ongezeko la watu. Tayari Serikali kupitia EWURA imeshatenga fedha za usanifu wa maji kutoka kwenye Mto Myovozi. Lengo ni kuona kwamba eneo lote la Nyakahura linakwenda kupata maji safi na salama ya kutosheleza hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye kwenye Kata ya Nyanza usanifu unaendelea. Pia tutahakikisha maji ya kutosha yanakwenda kupatikana. Tayari kuna chanzo chenye uwezo wa lita 50,000 kwa saa ambapo maji haya yatasaidia sana mpaka kwenye Kata ya Nyanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inatambua umuhimu wa maji mashuleni. Tayari kwenye Shule ya Mbaba kuna kisima kirefu pale kimechimbwa na maji yanapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Nyantakara, mradi umetekelezwa. Pale tuna mradi mkubwa tu ambapo fedha zaidi ya shilingi milioni 300 zimeelekezwa na maji yatafika mabombani muda sio mrefu, haitazidi wiki tatu.