MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza:-
Je, ni lini mradi wa kujenga Sub-station ya Nyakanazi (KV 220) toka Rusumo na Geita utakamilika ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme Biharamulo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovolti 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi. Mradi huu unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Geita - Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 144 ambapo Mkandarasi Kampuni ya M/S Kalpataru Power Transmission Ltd kutoka nchini India anaendelea na kazi za mradi. Hadi sasa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo cha kupoza umeme umefikia asilimia 60.
Mheshimiwa Spika, gharama ya mradi ni EURO milioni 45 sawa na takriban shilingi bilioni 117.79. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Machi, 2021. Ni mategemeo ya Serikali kuwa mradi utakapokamilika utaimarisha na kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya Wilaya ya Biharamuro na maeneo mengine ya jirani.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa mradi wa kutoa maji toka Ziwa Victoria kuyapeleka Biharamulo kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi hapo tarehe 16/09/2020 alipokuwa Biharamulo katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu, 2020?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Ezra John Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za upatikanaji huduma ya maji katika Wilaya ya Biharamulo. Hivyo, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali inatekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji wenye urefu wa km 10.9 katika maeneo ya Ng’ambo, Kalebezo, Nyakatuntu, Rubondo Chuoni na Rukaragata na kuchimba kisima katika eneo la Rukagarata. Thamani ya mradi huu ni shilingi milioni 178.9 na utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya uhaba wa maji katika Mji wa Biharamulo, Serikali iliamua chanzo cha uhakika cha maji kiwe Ziwa Victoria badala ya bwawa na chemichemi vinavyotumika kwa sasa. Hivyo mradi wa usambazaji maji katika Mji wa Biharamulo ambao utatoa maji katika Ziwa Victoria umefikia katika hatua ya kuandaa makabrasha ya zabuni (tender documents). Utekelezaji utaanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Aidha, kupitia Mradi wa Maziwa Makuu, Wilaya ya Biharamulo itanufaika kupitia chanzo cha Ziwa Victoria ambapo jumla ya vijiji 12 vya Rwekubo, Rusese, Kabindi, Runazi, Rukora, Kikomakoma, Kagoma, Songambele, Kasozibakaya, Nyamigogo, Chebitoke na Nyabusozi vitapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha.