Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, kwanza na mimi nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijaalia kuwa sehemu ya Bunge hili la Kumi na Mbili. Lakini pia nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi wa Biharamulo walioniamini na kunichagua kwa kura nyingi za kishindo niwe muwakilishi wao katika Bunge hili, lakini bila kumsahau mke wangu mpenzi Engineer Ebzenia kwa support kubwa ambayo amenipa na watoto wangu wawili Isack na Ebenezer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haraka haraka mimi ningependa kuchangia kwa sababu ya muda nimekuwa katika viwanda kwa muda mrefu kidogo takriban miaka 14 nimekuwa nafanyakazi katika viwanda kama engineer, kwa hiyo ningependa nijikite hapa zaidi. Nimejaribu kuangalia tumetengeneza ajira takribani 480,000 katika viwanda 8,447 ambavyo tumevizalisha katika muda huu wa miaka mitano. Sasa nikijaribu kuangalia average ni sawasawa na kila kiwanda kimetengeneza ajira 56, sasa najaribu kuangalia tuna-target ya kutengeneza ajira milioni nane na tukisikiliza au kupitia hotuba ya Rais aliyoitoa hapa focus kubwa tuna target kuangalia integration ya mazao ya kilimo yaweze ku- integrate na viwanda ili tuone sasa mambo ambayo tunayachakata hapa katika kilimo, mifugo na uvuvi ambao umeajiri Watanzania wengi ndiyo viweze kuwa vyanzo vikubwa vya ku-integrate ajira hizi katika viwanda.

Sasa nilikuwa najaribu kupiga hesabu let’s say tunataka ku-create ajira milioni mbili tu kutoka katika viwanda maana yake tunahitaji tutengeneze viwanda takribani 33,000 tukienda na mwendo huu viwanda vile vya kawaida. Sasa ninachojaribu kukichangia hapa ni nini au maoni yangu ambayo ninayo ni nini? Tujaribu kujikita zaidi katika kuwezesha watu wenye viwanda ambao wanaviwanda tayari.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Breweries wana-import ngano hapa na tumeangalia hotuba ya Rais inasema tunaingiza ngano takriban tani 800,000 kwa mwaka. Sasa tukiongea na Breweries tukajipanga tukawapa mashamba wao kwanza wawe ndiyo watu wa kwanza wa kulima kama wanavyofanya watu wa miwa na watu wengine yeye mwenyewe azalishe raw material kwa ajili ya ku-feed viwanda vyake huyo atatutengenezea ajira, ataajiri vijana wetu ambao wanasoma katika vyuo kwa mfano SUA na sehemu nyingine hiyo tu ni ajira tosha kwanza itazuia importation ya ngano, lakini vilevile itatengeneza ajira kwaajili ya vijana.

Mimi nimekuwa katika viwanda vya sukari nimekuwa naona kwa mfano kiwanda kimoja unakuta kimeajiri takribani Watanzania 10,000 wanaofanyakazi katika kiwanda cha Kagera au Mtibwa, ni watu wengi sana hawa ambao wamekuwa wameajiriwa huko. Kwa hiyo nikawa nasema same applies kwenye alizeti, niko katika Kamati ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Waziri uliongelea suala la Kiwanda cha Singida kwamba kina-operate katika 35% of installed capacity sasa kiwanda ambacho kinafanyakazi katika 35% of installed capacity, kama tungekiwezesha kwanza kiwanda chenyewe tukakipa eneo la kulima kama kiwanda, kikalima alizeti yake yenyewe maana yake kiwanda kile kingeajiri Watanzania katika mashamba yake ya alizeti watu wengine pia wangeweza kulima na kuuza katika kiwanda kile maana yake kiwanda tungeweza ku-boost production yake ikapanda zaidi kwa sababu raw material ipo na kiwanda hakifanyi kazi katika installed capacity kwa sababu malighafi ya ku-supply katika kiwanda kile huenda ina scarcity yake pia. Same applies kwenye sehemu kama za kwetu…

SPIKA: Engineer Ezra mbegu ya alizeti hakuna, mbegu ya alizeti iko wapi? Endelea tu.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, najua mbegu ya alizeti hakuna ndiyo tunapohitaji sasa Wizara ya Kilimo ijikite katika hili kwa sababu kama tunategemea ajira ya Watanzania wengi iko katika kilimo tukasema mbegu ya alizeti hamna, halikadhalika tutasema na mbegu ya michikichi Kigoma hamna na bado tunaagiza mafuta it’s a shame kwa nchi kama hii juzi meli ya mafuta inakuja hapa Waziri anashangilia anasema meli ya mafuta imekuja hapa wakati wale watu kule bado tunaweza tukaongea nao hata wao wenyewe wanachokifanya kule tukaweza kuki-copy hapa tulete wawekezaji kule wanaozalisha mafuta ya mchikichi tuwaleta Kigoma pale, tuwaambie na sisi tuna michikichi hapa hebu waweke kiwanda Kigoma halafu tuwahimize watu wao wenyewe wenye kiwanda kwanza watalima mashamba yao, wataajiri jirani zangu wa Kigoma, halikadhalika walio na mashamba ya michikichi pale wataweza kuuza kwenye kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata mimi nina maeneo makubwa, Biharamulo tuna mapori ambayo yamekuwa yanateka Watanzania wanaumia kwa muda mrefu tunaweza kulima alizeti pale au tukaweka mwekezaji akalima alizeti ndugu zangu wa Biharamulo pale wakaweza kuajiriwa. (Makofi)

Lakini ajira tunapoipata ile maana yake tunabeba wakulima watu wa chini kabisa ambao wanashida ni wakulima hata mimi mtu atalima heka moja, atalima heka mbili, kwa sababu anajua kiwanda kiko pale ataweza kuuza kwenye kiwanda.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, naona muda hautoshi naomba kuunga hoja 100% nadhani nitaongea kwenye mipango pia. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mimi nami pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kwa Presentation nzuri ya Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka mitano lakini pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa presentation nzuri pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na timu yake nzima kwa kuliona suala la Bandari ya Bagamoyo ambayo hata Mheshimiwa Spika ameliwekea msisitizo hapa. Labda kwa haraka, nadhani mpango unao maeneo matano makubwa ambayo Waziri ame - present hapa lakini kwasababu ya muda mimi nitaongelea mbili tu. Nitaongelea kwenye kuimarisha uwezo wa Viwanda na utoaji wa huduma, lakini pia kukuza uwekezaji na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mara ya kwanza kabisa niliposiamama wakati nachangia nilisema kwamba nimekuwa katika viwanda kwa takribani miaka 14 nikifanya kazi kama engineer, kwa hiyo nina uzoefu mkubwa kidogo katika suala la viwanda; na bahati nzuri nipo kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara kwa hiyo sana naongea kwa experience yangu ambayo ninajua nimeiishi kama kazi lakini pia yale ambayo nimekuwa ninayaona huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ila labda tu niweke angalizo. Tunapokuwa tunachangia hapa sio kusema tumetumwa labda na mabosi zetu wa zamani au tunakuja kumsemea mtu yeyote hapa. Tunachangia kwababu tunahakika na tunajua kila ambacho tunakifanya ni sehemu ya expertism yetu. Kwasababu ninakumbuka mara ya mwisho hapa kuna mtu aliniambia au hao wafanyabiashara wanawatuma mje kuwasemea, na hawapo humu by the way kwa hiyo tupo hapa kwa ajili ya kuwasemea kwababu tunajaribu kuangalia mianya ya kutengeneza kodi, mianya ya kukusanya fedha ili zile fedha ambazo Waziri hapa amewasilisha Trilioni 40 kwa miaka mitano tuweze kuzipata; tutazipata huko kwenye private sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mmemsikia mchangiaji aliyepita Abbas Tarimba. Jana nimeona we are proud kwamba kuona Mtanzania sasa anakuwa recognize na nchi kubwa ambayo imeendelea kiviwanda kama South Africa. Kwa hiyo lazima tujue tunazo hazina hapa, kwa hiyo sasa ni jukumu la Mheshimiwa Waziri kuwaangalia wafanyabiashara wakubwa walioko kwenye nchi hii aweze kuwatumia. Maana najua ameweka mpango wa trilioni 40 kutoka sekta binafsi, anataka atengeneze ajira milioni nane kwa muda wa miaka mitano, mpaka 2026. Hizi ajira milioni nane hataweza kuzipata kama hatatafuta hawa watu wenye viwanda huko nje. Watu kama akina Dewji hawa na wafanyabiashara wengine wakubwa. awatafute akae nao na tuje na hii mipango mikubwa ambayo tunayo hapa, maana tunataka tutengeneze ajira, tunataka tukuze uchumi lakini huu uchumi hatutaweza kukukuza kama wenzetu huko nje hawajui mipango yetu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha tafuta muda wa kukaa na wafanyabiashara wakubwa na ni sisitizo usikae nao kupitia kwenye taasisi zao zile, kaa nao mmoja mmoja, mtafute mmoja baada ya mwingine, mwite, mwambie tuna mpango huu, unaweza ukawekeza kwenye nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana niko huku kwetu kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara tunahangaika kutafuta wawekezaji kutoka nje tuwalete hapa, lakini bado wapo wawekezaji wa Kitanzania wakubwa ambao wanaweza wakafanya biashara kutokaea hapa kuliko hata kumtafuta mtu wa nje ukamtumia mfanyabiashara wa Kitanzania aliyekuwepo hapa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hili ambalo ameliona, hasa suala la Kodi maana mimi last time tumefanya ziara EPZA pale Ubungo niliumia sana, kwamba pale kuna Mtanzania ambaye anafunga kiwanda chake anakipeleka Uganda. Sasa nikawa nafikiria unapofunga kiwanda, leo sasa tunatafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza hapa ila Mtanzania ambaye alikuwa ameweka mle ndani, anaondoa anakipeleka kiwanda kwenye nchi Jirani. Maana yake ni nini, obvious unapoenda kule watakuuliza kuna nini huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haya mazingira ambayo Rais amesema mwende mkakae na wawekezaji. Ninaomba uyafanyie kazi haraka ili Watanzania ambao ndio watu wa kwanza kuwaleta watu wa nje kuja kuwekeza hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina experience kidogo, nilikuwa natoa mfano. Ukienda katika nchi ya Egypt, kuna sehemu ile ya ukanda wa Suez nimetembelea pale, mimi nikaona, yaani lile eneo utafikiri ni kama nchi ya China imehamia pale. Walichokifanya cha kwanza ni kwamba ili uweze kumvutia mwekezaji aje pale lazima uwe na Bandari. Ile Bandari ya Black Sea pale ndiyo inayotumika. Wachina wameletwa pale wakapewa eneo, bandari imejengwa wamejenga viwanda vingi sana maeneo yale. Kwa hiyo wanachokifanya wanaleta vitu vyao wanafanya process pale Bandari ipo wana-export kwenda Europe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo badala ya kuchukua mzigo kutoka China uusafirishe kwenda Europe kutoka Egypt kuushusha mzigo Ulaya inakuwa rahisi Zaidi, ndiyo kazi kubwa wanayoifanya hapa, sasa na sisi kama Kamati ya Bajeti ilivyo-suggest, tunayo nafasi kubwa zaidi ya kutumia Bandari ya Bagamoyo, kwasababu lile eneo la Bagamoyo ambayo tayari tulishalitenga na lilishalipiwa fidia takriban bilioni 27 zimewekwa pale. Hatuwezi kusema kwamba tuitelekeze.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiweka pale na umwambie mfanya biashara atoke Dar es salaam anatoa mzigo Bandari ya Dar es Salaam anausafirisha mpaka Bagamoyo, aanze kuzalisha pale akimaliza kuzalisha ausafirishe tena kuurudisha Bandari ya Dar es Salaam afanye export, huo muda haupo, maana ni cost ya transportation ya kuja na kurudi, lakini vile vile na logistic inakuwa ngumu. Kwa hiyo nishukuru na niomba Waziri wa Fedha pigana unavyoweza bandari ile inyanyuke pale ili sasa fidia zile ambazo tumezifanya na uwekezaji mkubwa tunaotaka kuufanya Bagamoyo uweze kufanyika pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo, kwababu tunaongelea viwanda vinavyoweza kuzalisha mazao haya ya kilimo mazao ya mifugo na pia uvuvi na madini. Labda upande wa kilimo Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Waziri wa Viwanda Waziri wa Killimo na hali kadhalika Waziri wa Fedha, mjaribu kutuangalizia njia sahihi ya kufanya. Wakulima wa nchi hii wanahangaika sana. Mimi ninaweza nikatolea wakulima wa upande huu wa Kagera; nilikuwa ninajaribu kufuatilia. Nchi ya Ecuador ndio nchi ambayo inaongoza kwa ku-export banana, ndizi hizi, 3.3 billion dollar per year, ina-export ndizi, hiyo ni hela nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika lakini sisi tupo pale, tulihamasishwa ndizi, watu wa Kagera mnaelewa, tumelima ndizi sasa hivi ndizi za mtwishe si zipo kule zimekaa hatuna hata watu wa kuwauzia tena? Maana unalima ndizi, Mkungu ambao hata hauwezi kuunyanyua shilingi 5,000 hatupati mteja tena. Sasa Mtusaidie. Maana nilikuwa ninaangalia hapa kwa Tanzania tume- export kwa mwaka tani 258. Tani 258 ukipiga kwa bei ya tani moja dola 300 katika World Market unaongelea dola elfu 75. Yaani mtu ana – export ndizi kwa dola 3.3 bilioni wewe hata dola laki moja haifiki, na bado tuna wakulima wanalima ndizi hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Unaongelea nchi kama Egypt, nimekuwa Egypt. Ukitoka Egypt, kama unatoka Cairo unaenda Alexander ile njia yote unapotembea imejaa zabibu, imejaa migomba na vitu vingine; nikawa najiuliza hawa watu wanafanyaje hawana maji hawana chochote kile. Wanachofanya zile ndizi wanatumia Irrigation.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unashangaa mtu hana mvua ana irrigate ndizi zile, ana export ndizi anapeleka Dubai ndilo soko lao kubwa. Sasa mimi hapa nina m vua ya Mungu ndizi zinaozea kule mtusaidie ili sasa tuweze kufanya biashara na tuweze ku-export ili ndizi hizi ambazo tunazilima katika kanda hizi ziweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua wako Mbeya wako Kilimanjaro Mzee Mheshimiwa Dkt. Kimei amekuwa anaongea sana suala la ndizi kwa hiyo, haya ni mambo ambayo Serikali ikiingia kati ikaangalia jinsi ya kutusaidia itatutoa hapa tulipo itusogeze mbele maana hatuwezi kuongelea pamba tu hatuwezi kuongelea vitu vingine nadhani mmesikia hapa bei inashuka na kuongezeka. Lakini bado tunazo fursa nyingine za kupeleka matunda huko nje na vitu vingine vikaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado dakika tano suala lingine niongelee suala la Liganga na Mchuchuma Mheshimiwa Waziri nimefika kule kwenye ziara yetu ya Kibunge lile eneo ni pori maana mwanzoni nilikuwa nawaza labda kuna hata majumba kuna hata nini ukifika kule mambo yale yanashangaza lakini umeiweka kwenye mpango humu vipaumbele sita ambavyo inabidi tuende navyo Liganga na Mchuchuma imo humu na mbaya zaidi Serikali tayari imeshaanza kuwekeza fedha nadhani mnajua tunajenga barabara ya zege tusingeweza kujenga barabara ya zege ya kilomita 50 sasa ya kuruhusu magari yaende kule kwenye ile migodi ile ni pesa nyingi sana ambayo tumeweka pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe nadhani kuna mambo ya kimkataba au mambo mengine ambayo yamekuwepo hapa biashara ni maelewano lazima ifikie stage ushuke ukae chini. Nimewahi kutoa mfano siku moja nimekuja kufuatilia biashara nimekuwa nafanyakazi kama Sales Manager kwa muda mrefu saa nyingine unaenda mpaka usiku hunywi pombe unakaa na mtu bar hapo unatafuta biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku nimeenda siku moja mchina mmoja anavuta sigara akipuliza moshi unaniingia puani lakini siwezi kumwambia usipulize maana nimekuja kutafuta biashara. Kwa hiyo, saa nyingine mkubali kushuka chini wafanyabiashara hawa tunapokuwa tunawatafuta kubalini kushuka chini twende tukae chini na hawa wachina, maana unashangaa hivi Mungu huyu aliwaza nini kipindi anakileta hiki kitu kwamba hapa kuna makaa ya mawe na hapa kuna mlima wa chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu ametuletea kitu cha kufanya sasa niombe hiki kitu tuondoke sasa hivi Mheshimiwa Waziri jaribu kupigana waiteni hawa watu tukae nao chini tuongee kama huu mradi kweli una faida kubwa kama hiyo ni lazima huyu mwekezaji hawezi kuja kushindwa kuwekeza hiki kitu hapa ili tuondoke sasa kwenye hii stori ya Liganga na Mchuchuma ambayo tumeisoma tangu Shule ya Msingi mpaka leo watu tunapata mvi na haijawahi kufanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri hili suala lichukulie serious ili sasa itutoe hapa maana matatizo mengine madogo madogo tunayoyasema yatakwisha na yatakwisha kabisa yatamalizika. Maana najua tunawekeza hela nyingi sana kwenye bwana la Mwalimu Nyerere lakini ile ni megawati 2115 hapo unaongelea megawati 650 almost 1/3 tu sasa 1/3 tunashindwa kukomboa pale maana ni vitu vingi tutapata chuma tutapata umeme, tutapata makaa ya mawe vitu vyote vitamalizika pale na bado Serikali itapata pesa ya kuweza kutusaidia kufanya miradi kwa hiyo niombe na hilo uweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia suala la kumalizia niombe viwanda nimekuwa naongea hilo jambo hata kwenye kamati Mheshimiwa Waziri ukijaribu kuangalia wenzetu ningeomba mfanye kitu kimoja kama Serikali na kama Wizara tunazungukwa na nchi tisa hapa ambazo zinatumia Bandari ya Dar es Salaam leo hatuna haja ya kuacha Toyota wana-assemble magari Japan halafu Toyota wana export magari ambayo yako assembled wanayaleta hapa? Why don’t we sit down na Toyota tujaribu kuangalia Serikali ni mteja mkubwa wa Toyota tuangalie tuongee na Toyota tunavyokuja kutengeneza sehemu hii ya Bagamoyo special economic zone, tumuombe Toyota aje aweke hapa akiweka plant yake yaku-assemble tu maana yake ni kwamba nchi zote Jirani ambazo zinatumia magari ya Toyota tutapata advantage magari yanakuwa assembled hapa kutoka kwenye bandari yetu wanakuja wanachukua hapa kiwanda kinakuwa cha kwake analeta watu wake lakini tunapata ajira pia na uzoefu wa kuweza kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana nimeona hiyo sehemu nyingi hata Nairobi leo tukiongelea pump za KSB Waziri wa Maji yuko hapa nimalizie hiyo dakika moja Waziri wa Maji yuko hapa pump za KSB the needing company ni Wajerumani wale lakini leo assembly inafanyika Nairobi ilikuwa inafanyika South Africa lakini leo assembly inafanyika Nairobi wenzetu wamefanya bidii ya kwenda ku-lob kule hatimae ikaja hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe brand kubwa ambazo wengi wana export kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri angalia Serikali muangalie kama tunaweza kuonana na hawa watu waje waweke viwanda vyao hapa wafanye assembly hapa vitu vitakuwa vinatoka vimekamilika vinaenda kwa wenzetu naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii. Kwanza kabisa, nimpongeze Rais kwa usimamizi mzuri wa miaka mitano hii kwa ambacho kimefanyika, ni very impressive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nataka nijikite kwenye suala la mchango wa sekta binafsi. Nimejaribu kupitia hapa Mpango, naona sekta binafsi tunategemea ichangie almost 40.6 trillion shillings na nikafanya average kwa mwaka ni 8.12 trillion, huo sio mchango mdogo sana kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu ambacho nimekuwa najiuliza, nimekaa sekta binafsi kwa muda mrefu, labda kwa upande mwingine ningeomba Serikali pia ihusike kwenye ku-support sekta binafsi. Kwa nini nasema hivi? Ni kwa sababu unapoiweka sekta binafsi kwenye Mpango halafu huishirikishi mipango kidogo inakuwa gumu maana tunawaacha wanakuwa separate halafu baadaye tunaenda kukamua maziwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nayasema haya? Sasa hivi nimetoka kwenye Kamati tulikuwa na semina nikajaribu kuuliza swali kwa watu wa TANTRADE kwamba nyie kazi yenu kwa sehemu kubwa ni kuhakikisha mnatafuta masoko na mnashauri. How many times mmechukua muda wa kwenda kushauri sekta binafsi, maana nitaenda nitamkuta Mheshimiwa Musukuma na biashara yake ya mabasi naanza kuchukua kodi pale, lakini Mheshimiwa Musukuma amekuwa anaongea humu anasema darasa la saba ndiyo matajiri au ndiyo mabilionea tunaweza kuona kama anafurahisha lakini reality ipo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kitu kimoja kifanyike, ni lazima Serikali ijikite kwenye kuhakikisha tunashirikisha sekta binafsi kwenye mipango yetu, maana wapo matajiri au wafanyabiashara ambao leo hawajui hata Ilani ya CCM inalenga nini lakini wapo kule. Wale watu wanakopesheka kwenye mabenki na wana uzoefu wa biashara, kwa hiyo, tukiwatumia vizuri wanaweza wakatusaidia kwenye kukuza uchumi. Maana hapa basically tunachojaribu kukiangalia ni nini? Tunajaribu kuangalia possibility ya ku-raise pesa kutoka sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ambacho nashauri ni kitu kimoja, tuangalie Serikali iweze kuwatafuta hawa watu, tusiwatafute kwenye makundi maana wafanyabiashara wa Tanzania kwa sehemu kubwa kila mmoja anaficha mambo yake, hakuna mtu ambaye yuko tayari kufunguka. Ukiita semina ya wafanyabiashara hapa hakuna ambaye yupo tayari kufunguka, lakini tukijaribu ku-identify labda wafanyabiashara kumi potential, tukaangalia huyu mtu uwezo wake ni mkubwa katika industry fulani na bado benki anaweza akakopesheka. Huku mfanyabiashara kupata bilioni 300, bilioni 400 benki unampelekea idea ya biashara maana tunahangaika na viwanda hapa, kuna mwingine yupo kwenye mabasi lakini anaweza akajenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafute kupitia TANTRADE, iende imshauri, tuwatembelee hawa watu tusikutane nao tu wakati tunatafuta kodi maana haya mambo hata kwenye halmashauri zetu huko yaani Afisa Biashara ni kama Polisi, yeye atatembelea duka lako, atatembelea sehemu yako ya biashara anakagua leseni au anakagua vitu vingine. Wapate muda wa kuwatembelea watu hawa, ujue huyu mtu ana shida gani, sometimes mtoe hata out maana private ukijaribu kuangalia wanaotu-train private aliongea mtu mmoja aliyekuwa anachangia asubuhi, kwamba investment hata kwenye Makampuni ya Simu na Serikalini huku ni tofauti, yaani unayemweka am-audit mtu wa private, mtu wa private anajua zaidi kwa sababu wale watu wame-invest hela nyingi Zaidi, sisi tumekuwa tunasafirishwa tufanye kazi private, tunasafirishwa sana na makampuni nje, sio kusema yule mtu hakusafirishi tu bila manufaa, anataka uelewe ili kurudi umfanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hali kadhalika hata watumishi wetu umma watafute muda wa kukaa na watu wa private, wawaulize matatizo yao ni nini. Wawatembelee hata ofisini, wawatoe hata out jioni wakae sehemu waongee hizi bajeti ziwepo, maana hawa watu washirika, mtu wa kukuchangia trilioni 40 kwa miaka mitano huwezi tu kuwa unakuta naye kwenye tax collection, hapana lazima tuwatafute tushirikiane nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limekuwepo, watu wengi sana wameongelea habari ya TRA, niombe Serikali. Nimekuwa kwenye biashara, tunafanya kazi na Serikali, una-supply mzigo au contractor anafanya kazi, baada ya hapo kuna raise certificate, ipelekwe wizarani, baadaye iombewe hela hazina ije ilipwe, inachukua almost miezi miwili au miezi mitatu ndio hela inakuja. Hela inafika kuna maelekezo sasa hivi kwamba kabla ya kumlipa mkandarasi au supplier yoyote yule, uanze kwanza kuwauliza TRA kwamba huyu mtu anadaiwa. Sasa hata yule niliyefanya naye biashara taasisi ya umma naye amegeuka tax collector, leo hanilipi hela yangu kwamba kama nadaiwa ile hela anaihamisha moja kwa moja inaenda TRA. Jamani nafanya kazi na wewe, ni mfanyabiashara unajua ofisi yangu, nilipe kwanza maana sisi tunakopa kwenye mabenki, hawa ndio partners, sasa leo ukichukua bilioni yote na mtu wa TRA anakwambia unadaiwa, sometimes anakwambia ile ilipe kwanza, ikishalipwa kwanza tutakuja tuta-negotiate, hela haiwezi kuingia kule ikarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachoomba, TRA wasiwe Polisi, hawa ni partners, ni watu wa kufanya nao biashara, tuwashirikishe lakini tushirikiane nao maana wako registered, kila mfanyabiashara tunajua alipo na hizi trilioni 40 ndio hao wanaotakiwa wazichangie lakini tusiwa- discourage kwenye biashara. Nasema hili kwa sababu haya mambo yanatokea sana hawa watu wanakata tamaa kuendelea kuwekeza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nije nalo, kwa sababu ya muda nilikuwa najaribu kupitia, nikaangalia historia ya Northern Ireland, wale watu wakati wanataka kuanzisha viwanda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda umekwisha Mheshimiwa, lakini unaruhusiwa kupeleka mchango wa maandishi, kwa hiyo usiwe na wasiwasi.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami niungane na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Spika wa Bunge na wewe mwenyewe kwa sababu Rais aliyetangulia alikuwa sehemu ya Bunge. Pia nitoe pole kwa wakazi wa Chato na Biharamulo kwa ujumla sababu sisi ndiyo wenyeji zaidi pale kwa hiyo, msiba ule ulikuwa nyumbani na nawashukuru wote walioungana nasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kuchangia ninayo mambo mawili ya kumuelezea Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Cha kwanza kila binadamu anapozaliwa ana mambo mawili makubwa katika dunia hii. Incident mbili kubwa katika dunia kwa mwanadamu, kwanza ni kuzaliwa na pili kugundua kwa nini umezaliwa. Watu wengi tunaishi hatujui kwa nini tumezaliwa au kwa nini tupo hapa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kesi ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aligundua purpose ya Mungu kumleta duniani. Nakumbuka mwaka 1990 nikiwa mdogo akiwa anagombea Ubunge kwa mara ya kwanza Biharamulo kila alichokuwa anakifanya au statement yake kila mmoja alikuwa anamuelezea. Tukiwa wadogo tunaambiwa kuna mtu anaitwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli that time yuko Chato mimi niko Biharamulo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa Mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995 nyote ni mashahidi, Naibu Waziri wa Ujenzi kila alichokigusa aliacha alama. Hakuna sehemu Raisi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amepita hakuacha alama. Mmemsikia Rais Jakaya Kikwete juzi kwenye suala la ujenzi, ardhi, uvuvi na hata alipomrudisha ujenzi. Hatimaye Watanzania na Chama cha Mapinduzi kikaona na kumuweka kuwa Rais. Alipokuwa Rais alama ile aliyoiweka katika maisha yake kwamba kila anachokabidhiwa kufanya lazima akifanye kwa hundred percent haikukoma. Watanzania wote ni mashahidi ujasiri wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuamua mambo, ujasiri wa katika kuipigania nchi hii haukuanza akiwa Rais umeanza back-and-forth na alipokuwa Rais mambo aliyoyafanya ni makubwa mmeyasikia hatuna haja ya kuyarudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo moja kubwa ambalo nilimuuliza Mungu wakati ule napokea taarifa hizi, nikasema why God, kwa sababu niliumia sana nikajiuliza kwa nini uruhusu hili jambo katika wakati kama huu? Ila nikarudi katika Maandiko Matakatifu nikamkumbuka Musa alivyopigana na wana wa Israel, najua safari ilikuwa ngumu hata safari ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuwa ngumu kwa sababu kipindi anaenda hivi kuna wengine walitaka kurudi nyuma na wengi wamekuwa wanapigana kurudi nyuma lakini hakukata tamaa. Nikakumbuka Musa alipopandishwa katika mlima ule na akaoneshwa nchi ya ahadi kule lakini akaambiwa kazi yako imeishia hapa na hautarudi huko na wala hutaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwaambia ni nini? Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliletwa na Mungu kwa ajili ya kazi maalum katika nchi hii, amemaliza kazi ile ambayo Mungu alimleta aifanye, tuendelee kumuombea na kuyaishi yale aliyofanya. Ninachotaka kuwasihi Watanzania na Wabunge wenzangu baba huyu aliletwa kwa purpose, akagundua purpose iliyomleta hapa, kafanya sehemu yake na amemaliza. Hata sisi sasa tunachotakiwa tumuenzi nacho kila mmoja ajitafakari ajue purpose yangu mimi kuwa duniani ni nini na purpose ya wananchi walioniamini kunileta Bungeni ni nini. Tukiyajua hayo basi tukaisimamie Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili maendeleo haya ambayo Rais wetu alitamani kuyaona aweze kuyaona yakifanyika na Watanzania waweze kuyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuwasihi Watanzania na Waheshimiwa wabunge wenzangu, baba huyu aliletwa kwa purpose akagundua purpose iliyomleta hapa kafanya sehemu yake amemaliza. Hata sisi, tunachotakiwa tumuenzi nacho, kila mmoja ajitafakari ajue purpose yangu mimi kuwa duniani ni nini? Purpose ya wananchi walioniamini kunileta Bungeni ni nini? Ili tukiyajua hayo tukaisimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ili maendeleo haya ambayo Rais wetu alitamani kuyaona aweze kuyaona yakifanyika na Watanzania waweze kuyapokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo labda, nirudi kwenye suala mama pia, kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme neno moja tu; watu wote wameongea katika habari ya wanawake, lakini mimi niseme hakupewa nafasi ya Makamu wa Rais kwa sababu ni mwanamke, alipewa nafasi ya Makamu wa Rais kwasababu ame-demonstrate na ameonesha uwezo wa kupata nafasi ile. Kwa hiyo tunaposimama hapa, tusimame hapa tukijua tunaye Rais mwenye uwezo ambaye aliaminiwa na Chama mwaka 2015 kipindi Magufuli anaingia, akiwa hajulikani kama atayafanya haya halikadhalika Mama Samia aliingia akiwa hajulikani kama atayafanya haya. Lakini chini ya uongozi imara, chini ya Ilani ya CCM wakayasimamia wakatufikisha hapa walipotufikisha. (Makofi)

Labda neno moja tu la biblia ambalo nataka niliseme kwa ajili ya Mheshimiwa Rais, nikikaribia kukaa, maana najua wote tumeshaongea mengi. Tuki-refer katika Kitabu cha Ezra 10:4 inasema “Inuka maana kazi hii inakuhusu wewe. Na sisi tu pamoja nawe, uwe na moyo mkuu ukaifanye”.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Wabunge tuko na Rais wetu, Watanzania wako na Rais wetu, ameambiwa ainuke na maandiko hayo tuko pamoja naye, awe na moyo mkuu akaifanye. Tunachotakiwa ni kumuombea ule moyo mkuu ambao umesemwa, uwe juu yake akaifanye. Nina uhakika itafanyika vizuri na tunashukuru Mungu kwa sababu ya Dkt. Philip Mpango ambaye ameteuliwa leo, Mungu awasaidie watufikishe katika nchi ya maziwa na asali ambayo ilikuwa tamanio la Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na niseme ninaunga mkono hoja hizi ambazo zimetolewa hapa. Ahsante sana. (Makofi)