Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima (10 total)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango maalum wa kurasimisha makazi ya wananchi wa Mabwepande, Nakasangwe, Chasimba, Chatembo, Chachui, Ndumbwi na Jogoo ili kumaliza migogoro ya ardhi na kuiongezea mapato Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Urasimishaji wa Makazi ya Wananchi Nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Nyakasangwe, Mabwepande na upangaji na upimaji wa maeneo ya Chasimba, Chatembo na Chachui, kadri ya matakwa ya kisheria. Pia, Halmashauri kwa kushirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Afro Map Limited, imeandaa michoro nane ya urasimishaji katika eneo la Nyakasangwe yenye jumla ya viwanja 9,472 ambapo viwanja 7,790 upimaji umekamilika na taratibu za umilikishaji zinaendelea kwa wananchi waliokamilisha malipo.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Mabwepande, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Mosaic Company Limited imeandaa michoro saba ya urasimishaji yenye jumla ya viwanja 1,431. Viwanja hivyo viko katika hatua mbalimbali za upimaji na umilikishaji.

Aidha, katika maeneo ya Chasimba na Chachui (Mtaa wa Basihaya) na Chatembo (Mtaa wa Wazo), Serikali imepanga na kupima jumla ya viwanja 4,098 ili kutatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi na wamiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maeneo ya Mtaa wa Ndumbwi, Serikali inashirikiana na Kampuni ya Upangaji ya Urban Vision pamoja na Kampuni ya Upimaji ya AG Sun Land Consult kufanya urasimishaji katika maeneo ya Ndumbwi ambapo kazi ya kuandaa michoro saba ya mipangomiji yenye jumla ya viwanja 956 imekamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni itaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Urasimishaji wa maeneo ya Mtaa wa Jogoo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Umilikishwaji wa viwanja vipatavyo 15,957 katika maeneo yote yaliyotajwa kutawezesha wananchi kuwa na milki salama, kupunguza migogoro na kupanua wigo wa makusanyo ya Serikali yatokanayo na sekta ya ardhi.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakuja na Mpango Madhubuti wa kuitumia Bahari kwa Programu za Uvuvi wa Bahari Kuu na michezo ya bahari ili kutengeneza ajira kwa Vijana wa Jimbo la Kawe, hasa ikizingatiwa nusu ya Jimbo hilo lipo Mwambao wa Bahari ya Hindi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha uvuvi wa bahari kuu kwa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania, TAFICO ili kuiwezesha nchi kunufaika na rasilimali za uvuvi. Hususani zile zilizopo katika ukanda wa uchumi wa bahari kuu na bahari ya ndani. Hadi sasa Serikali ina mpango wa kununua meli tano za uvuvi, ambazo zitavua katika maji ya Kitaifa, Bahari kuu pamoja na kutoa leseni kwa meli kubwa zinazomilikiwa na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga bandari ya uvuvi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi. Ambapo uwepo wa bandari hiyo, utawezesha meli za uvuvi zinazovua katika ukanda wa uchumi wa bahari ya Tanzania na bahari kuu kutia nanga, kushusha mazao ya uvuvi na kupata huduma mbalimbali, zikiwemo mafuta na chakula ambapo meli hizo zitachangia kutoa ajira kwa wananchi wakiwemo wa Jimbo la Kawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha mazingira na usalama katika fukwe na visiwa vya Bahari ya Hindi, ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika shughuli mbalimbali za michezo katika fukwe na visiwa hivyo.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuzipandisha hadhi barabara za ndani za Jimbo la Kawe ili zihudumiwe na TANROADS kwa kuwa uwezo wa TARURA kuhudumia ni kilometa 120 wakati Jimbo lina barabara zenye jumla ya kilometa 1,463?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria na huzingatia vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Barabara ambayo inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi inatakiwa ijadiliwe kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo vyote Bodi ya Barabara ya Mkoa husika itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo vya kuwa na hadhi ya barabara ya Mkoa na hivyo ipandishwe daraja na kuwa barabara ya Mkoa chini ya Wakala wa Barabara Tanzania kwa maana TANROADS. Hivyo, ni vema taratibu hizo zikafuatwa ili kupandisha hadhi barabara zilizopo katika Jimbo la Kawe.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuiongezea bajeti TARURA ili kuiwezesha kuzihudumia barabara zake ikiwemo kuongeza tozo kwenye mafuta katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 itakayowezesha TARURA kupata fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara.
MHE. KASALALI E. MAGENI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti kwa wakulima ili kuzalisha mafuta ya kula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbuge wa Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa, nchi yetu inazalisha alizeti itakayo changia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha mafuta ya kula na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula, Serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 1,500 zilizokuwepo awali hadi tani 5,000 kwa lengo la kuongeza eneo kubwa zaidi la uzalishaji wa alizeti ili kuweza kufikia malengo; Kuendelea kutekeleza mkakati wa uandaaji wa mashamba makubwa zikiwemo block farms ambayo kwa asilimia kubwa yatatumiwa na wakulima kwa kilimo cha alizeti; na Wakala wa Mbegu (ASA) tayari ameanza usambazaji wa mbegu bora ya alizeti aina ya record ambayo imethibitishwa ubora na inauzwa kwa bei ya ruzuku ili kuhakikisha kwamba inamletea tija mkulima.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha mifumo ya Kitambulisho cha Mpiga Kura na Kitambulisho cha Taifa ili kuepusha usumbufu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha mifumo ya Kitambulisho cha Mpiga Kura na Kitambulisho cha Taifa ili kutumia Kitambulisho cha Taifa katika uchaguzi wa kawaida na ule wa kieletroniki (e- voting).

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi haya yatapunguza gharama kwa Serikali katika kuandikisha na kutengeneza daftari pamoja na kurahisisha usimamizi wa wapiga kura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano kati ya Taasisi hizi mbili yenye dhumuni la kuwezesha kanzidata ya NIDA kutumika katika katika zoezi la uboreshaji wa daftari la Wapiga Kura yameanza mwezi Machi, 2022. Mazungumzo ya awali kati ya wataalam wa taasisi zote mbili yenye nia ya kuunganisha mifumo hiyo miwili yamepangwa kufanyika kabla ya mwezi Mei, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio ya Serikali ni kuona mifumo hiyo inaunganishwa ili kuwarahisishia wananchi kushiriki katika shughuli za uchaguzi na kuipunguzia Serikali gharama katika uandikishaji na uchapishaji wa vitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.(Makofi)
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapanua barabara ya Tegeta kuelekea kiwanda cha Saruji Wazo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kipande cha barabara ya Tegeta – Wazo Hill kilikarabatiwa Mwaka 2014 kwa kiwango cha lami kwa njia mbili (Single Carriage Way) ya upana wa mita 7 na njia za waenda kwa miguu zenye upana wa mita 1.5 kila upande. Upana huo unakidhi viwango vinavyohitajika kwa matumizi ya barabara ya njia mbili. Hata hivyo, kutokana na kuongezeka kwa wingi wa magari katika sehemu hii ya Tegeta – Wazo Hill, Serikali ina mpango wa kupanua barabara hii kuwa njia nne na utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha.Ahsante.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kuitumia Bahari kwa michezo mbalimbali ya majini ili kuongeza kipato cha wananchi wa Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995, Ibara ya 7(i) hadi (vi), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi. Hata hivyo, Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wako katika mkakati wa kuziendeleza fukwe za Kunduchi na Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kukuza mchezo wa Soka la Ufukweni ambao tayari TFF wameshaanzisha Ligi yake ambayo ilianza tangu Tarehe 19/08/2023 na inafanyika kwa siku za Jumamosi na Jumapili katika fukwe za Koko, na jumla ya Timu 16 zinashiriki Ligi hiyo. Aidha, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa mwezi Julai, 2023, Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ilishiriki mashindano ya mchezo huo Barani Afrika yaliyofanyika Nchini Tunisia na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Morocco na Senegal.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa rai kwa wadau wa michezo mingine kama Mitumbwi na Ngalawa, Kuogelea, Mpira wa Kikapu na Wavu kuwekeza katika michezo hii ya ufukweni na kuziendeleza fukwe tulizonazo ili kukidhi matakwa ya michezo yao, kwani pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi, michezo hii pia inasaidia kuimarisha afya na kutoa burudani kwa wananchi.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza migogoro ya ardhi maeneo ya Chasimba, Chatembo, Chachui, Nkasangwe na Mabwepande – Kawe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi katika Jimbo la Kawe kwa ujumla inahusu wananchi wa Chasimba, Chatembo na Chachui kuvamia eneo la Kiwanda cha Wazo, wananchi kuvamia mashamba ya wananchi wengine katika eneo la Nkasangwe na wananchi kufanya maendelezo katika mashamba yenye miliki likiwemo Shamba la Shirika la DDC katika eneo la Mabwepande.

Mheshimiwa Spika, kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikishughulikia migogoro hii kwa kuwashawishi wamiliki wa maeneo yaliyovamiwa kuyaachia maeneo hayo ambapo wananchi tayari wameshavamia na kufanya maendelezo na wanapaswa kulipa fidia kwa wamiliki. Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo za Serikali kutatua migogoro hiyo kiutawala, kumekuwa na mwitikio mdogo kwa wananchi kulipa fidia kwa maeneo waliyovamia na hivyo kuchelewesha upatikanaji wa suluhisho la kudumu la migogoro hii.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wenye viwanda vilivyokufa au havifanyi kazi kwa sababu mbalimbali ikiwemo kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kupikia cha Famili kilichopo Salasala katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali kupitia utekelezaji wa blue print ni kuhakikisha changamoto zote zilizokuwa zinavikabili viwanda visivyofanyakazi zinatatuliwa ili kuwezesha viwanda hivyo kufanya kazi ikiwemo kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Famili. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni nini Mpango wa Serikali kudhibiti Mto Nakasangwe na Mto Tegeta na kadhalika inayopanuka kwa kasi na kutishia maisha ya watu na mali katika Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za kupanuka kwa Mto Nakasangwe na Mto Tegeta kama ifuatavyo:

i. Kuandaa Mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

ii. Kutoa elimu kupitia vipindi vya redio, televisheni, maonesho na mikutano kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika ngazi zote ili kuongeza kasi ya uhifadhi vya vyanzo vya maji na kingo za mito.

iii. Kuhamasisha Umma kuhusu upandaji wa miti rafiki kwa vyanzo vya maji ambavyo itasaidia katika kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito na kuimarisha mtiririko wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kusisitiza utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 kuhusu uhifadhi ya eneo la mita 60 katika kingo za mito, fukwe za bahari na maziwa yanayozuia matumizi yeyote ya kibinadamu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kutambua kupanuka kwa kingo za mto Tegeta na Nakasangwe, Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya tathmini katika maeneo hayo kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu kama ilivyofanyika katika maeneo mengine ambapo Serikali ilibuni na kutekeleza miradi ya ujenzi wa kuta, kama vile ujenzi wa ukuta wa Pangani na fukwe katika Barabara ya Barak Obama katika jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.