Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa dakika chache hizi za kuchangia na mimi katika hotuba ya Rais ya kufunga Bunge na hotuba ya kufungua Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, kila mara ninapomkumbuka Dkt. John Pombe Magufuli na hotuba zake na uongozi wake inanikumbusha kitabu kimoja kilichoandikwa na Dkt. John C. Maxwell. Kwenye kitabu chake anasema; ikitokea vita kati ya kundi hili na kundi lile au kati ya nchi hii na nchi ile na ikatokea kwamba jeshi moja wanajeshi wake wote ni simba na kiongozi wake ni simba na jeshi lingine wanajeshi wake wote ni kondoo na kiongozi wake ni simba, basi hizi timu mbili zikipigana kwa maana ya timu ambayo kiongozi ni simba na askari ni simba na timu ambayo kiongozi ni kondoo na askari ni simba, definitely timu ambayo kiongozi ni kondoo itapoteza vibaya sana. (Makofi)

Lakini pia Maxwell akasema kwamba; pamoja na kwamba jeshi linaweza kuwa na masimba wote ilimradi tu kiongozi ni kondoo, lazima jeshi hilo litapoteza; alikuwa anaongea kwa habari ya dhana ya uongozi, kwamba maendeleo au ushindi ni kiongozi. Kwa bahati nzuri Tanzania tumepata kiongozi Simba na majeshi nayo ni simba na kwa hakika ushindi wetu upo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninapokumbuka dhana ya uongozi wa kidiplomasia, ninakumbuka mambo mawili; kwenye diplomasia, uchumi wa kidiplomasia tuna mambo mawili; tuna uchumi pamoja na biashara, lakini kwenye diplomasia ya uongozi tuna mambo matatu; cha kwanza tunasema strong power, cha pili soft power na cha tatu smart power.

Mheshimiwa Spika, sasa strong power ni nini; strong power ni mahali ambapo kiongozi anashawishika kwamba watu wangu nikiwapeleka mpaka pale wantanufaika na maisha yao na maisha yao yatakuwa salama. Lakini watu wale ama kwa kujua au kwa kutokujua hawajui kwamba wakifika pale watakuwa salama. Sasa strong power maana yake ni kiongozi huyu anawakokota hawa watu wapende wasipende wakifika pale wakagundua faida zake wanamshukuru yule kiongozi wanasema ahsante kwa kutufikisha hapa, hiyo inaitwa strong power.

Mheshimiwa Spika, soft power ni kwamba unaanza kuwabembelezabembeleza, unawaeleza faida za wanakokwenda, watakakofika na mambo ambayo watayapata, unawabembelezabembeleza mpaka unawafikisha pale baadaye wanakushukuru wanasema ahsante kwa kutufikisha hapa, hiyo inaitwa soft power.

Mheshimiwa Spika, lakini smart power unaunganisha strong power pamoja na soft power; kuna wakati mwingine unawaburuza wanakwenda, kuna wakati mwingine unawabembeleza na hiyo ndiyo aina ya uongozi ambayo Dkt. John Pombe Magufuli anayo. Dkt. John Pombe Magufuli ni smart power na Mawaziri wetu na Waziri Mkuu pia ni smart power, watatufikisha tunakotakiwa kwenda kwa uhakika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TARURA; hai-make sense ukiona kwamba mtandao wa barabara za TARURA ni takribani kilometa 130,000 na mtandao wa barabara za TANROADS ni takribani kilometa 40,000, hai-make sense kwa nini mpaka leo TARURA anapewa asilimia 30 na TANROADS anapewa asilimia 70; hai-make sense. (Makofi)

Nikisema hivyo sina maana kwamba nadharau ukweli wa kwamba ubora wa barabara za TANROADS unatakiwa kuwa imara zaidi kwa sababu una-cut accross mikoa kwa mikoa, lakini hai-make sense kwa nini huyu ambaye ana mtandao wa kilometa 130,000 apewe asilimia 30 na huyu mwenye mtandao wa kilometa 40,000 apewe mgao wa asilimia 70; hakuna mateso tuliyonayo Wabunge kama TARURA kukosa fedha kule mikoani, ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano kwenye Jimbo langu la Kawe. Kwenye Jimbo la Kawe Wilaya nzima ya Kinondoni tuna kilometa za barabara za ndani 1,663. Kilometa 200 ziko Jimbo la Kinondoni kwa pacha wangu Mheshimiwa Tarimba, lakini kilometa 1,463 ziko Jimbo la Kawe; kilometa I,463, ni sawasawa na kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma lakini zote ziko ndani ya Jimbo la Kawe. Nilipowatembelea TARURA wana fedha za kutengeneza kilometa 120. Ina maana kuna kilometa 1,300 ambazo haziwezi kutengenezwa, this is not acceptable kwa wakati wowote katika nchi yetu; haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kama kweli tuna ndoto ya kuwaletea watu maendeleo, siyo Jimbo la Kawe tu, lakini kwenye kila jimbo barabara zinazotakiwa kujengwa kwa kutumia fund ya TARURA hazitajengwa kabisa kama TARURA hataongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Road Fund kama unavyojua ni mawazo yaliyoanza mwaka 1999 mpaka 2000 nyakati zile Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi. Kuanza kuchukua shilingi 200 kwenye kila lita moja ya mafuta na kuchukua asilimia 70 kwenda TANROADS na asilimia 30 kwenda TARURA.

Ninawaomba watendaji wawaze mawazo mengine tena ya kuongezea fedha. wasitegemee mawazo yaleyale ya Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa Waziri wa Ujenzi, wawaze mawazo mengine ya kuongezea fedha. There is nobody here who is a copy of the other, everybody is an original from the Almighty God; lazima watendaji kazi wetu mjiongezee zaidi, muwaze zaidi, muwe creative zaidi kwa namna ya kumuongezea TARURA fedha, vinginevyo it is a nightmare kuwapa watu maendeleo kwa kupitia TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna huyu mdudu anaitwa Corona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, dakika tano zimekwisha. (Makofi/Kicheko)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pasipo kifani kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umewakilishwa na Waziri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa mama Kilango Malecela leo alikuwa anachangia nikamwomba aniazime dakika zake tano na akakubali. Sasa kama wewe itakupendeza basi niunganishe dakika tano za Mheshimiwa mama Malecela na za kwangu nipate dakika kumi ili niweze kutoa nilichonacho. Nimezungumza naye akasema anachangia na akaniruhusu lakini nikasema nikipata ruhusa yako na hekima yako itapendeza sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima, hiyo hairusiwi, Wabunge huwa hawapeani muda lakini muda wako sasa unazidi kwenda kwa hayo maombi ambayo yamechukua muda kidogo, tafadhali anza kuchangia. (Makofi/Kicheko)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno machache sana kwa sababu ya muda wangu, kuna hoja zinazungumzwa hapa kuonyesha kana kwamba awamu ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijafanya jambo lolote. Mtu yeyote ambaye haoni kwamba miaka mitano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijafanya chochote basi anaweza kuwa na ugonjwa hatari sana ambao hauwezi kutibika hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua fika kwamba kuanzia mwaka 1976 mpaka 1981, Tanzania ilikuwa na ndege almost 11 na mpaka tunafika kwenye ubinafsishaji tulikuwa na ndege 9 na mpaka Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anaingia madarakani tukawa hatuna ndege. Hata hivyo, tangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameingia madarakani tuna ndege zinaelekea 12 sasa. Asiyeona hayo ana ugonjwa special unahitaji daktari special. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unakumbuka vizuri Shirika la TANESCO, kabla ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajaingia madarakani lilikuwa linaendeshwa kwa kupewa ruzuku shilingi bilioni 438 kila mwaka, lakini tangu 2015 Shirika la TANESCO linajiendesha kwa fedha yake lenyewe na linafanya vizuri sana. Asiyeona ana ugonjwa maalum unahitaji daktari maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, mwaka 2015 Tanzania yote ilikuwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa na umeme lakini leo ndani ya miaka mitano vijiji 10,263 vina umeme katika nchi ya Tanzania. Kwa taarifa ya asiyeona ni kwamba vimebaki vijiji 2,005 tu Tanzania yote iwe na umeme. Pamoja na mambo mengine yote lakini mwenye macho ni muhimu aone kitu gani kimefanyika na wapi tunaelekea kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanasema msiongelee sana Stigler’s Gorge ni ileile, sikiliza nikwambie tangu Tanzania ianze ina megawatt za umeme 1,602, hii ni tangu Mwalimu Nyerere, Mheshimiwa Mwinyi, Mheshimiwa Mkapa na Mheshimiwa JK Kikwete, utaachaje kuongelea Stigler’s Gorge ambao ni mradi mmoja wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambao umetupa megawatt 2,115. Lazima akili iwe likizo au ina matatizo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu tuseme ukweli, mimi nimekuwa Japan, wao wana treni inakwenda kwa speed 250 na wana nyingine ambayo watazindua mwaka ujao inayotembea chini ya ardhi inayokwenda kilomita 500 kwa saa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania kwa Afrika Mashariki tumekuwa nchi ya kwanza kutekeleza mradi wa treni yenye uwezo wa kwenda kilomita 160 kwa saa. Utasemaje Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajafanya vitu vyake? Unahitaji dawa maalum na daktari maalum kusema hivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi, hebu tuangalie ukweli, wakati Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli anaingia madarakani tunaambiwa tembo wa Tanzania walikuwa wamebaki 15,000, leo kwa taarifa ya Wizara ya Maliasili tuna tembo 60,000. Kwa utawala wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mpaka tembo wanaanza kuzaana bila utaratibu. Huwezi kusema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano afya, nagusia kila mahali kwa sababu muda wangu haunitoshi, tangu Uhuru tumekuwa na Hospitali za Wilaya 77 lakini miaka mitano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumejenga Hospitali zingine za Wilaya 102. Utabezaje hizo juhudi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haraka haraka tulikuwa na Hospitali za Rufaa za Mikoa 18 tu tangu Uhuru ndani ya miaka tano zimejengwa mpya 10. Asiyeona ana ugonjwa unaitwa Schizophrenia.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsubiri. (Kicheko)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda tu nimpe taarifa anayenisubiri, kwanza hapa tunachangia Mpango kushauri Serikali, tunavyosema Mpango haujatekelezeka hatumaanishi kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli wa Awamu ya Tano hajafanya kitu. Mfano kwenye umeme alipotaja target tuliyojiwekea mpaka 2021 ilikuwa tufikie megawatt 4,915 lakini mpaka sasa hivi tuna megawatt 1,601 wakati mwaka 2014/2015 ilikuwa ni megawatt 1,501. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema kwamba wanaweka target na hazifikiwi siyo kwamba tunasema hakijafanyika kitu lakini wanavyoweka viashiria basi viweze kufikiwa angalua kwa asilimia 80. Asipambe bali ashauri ili Serikali ifanyie kazi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Esther Matiko. Mheshimiwa kabla sijakuuliza kama unapokea taarifa, nadhani tuwe tunaelewana vizuri, mtu anayegoma kutambua kilichofanyika na mtu anayetambua kilichofanyika lakini anatoa ushauri wa nini kifanyike zaidi kuna tofauti kati ya hayo mambo mawili. Mheshimiwa Gwajima unapokea taarifa hiyo? (Makofi)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimwambie msomi yeyote kabla hajaenda mbele ana-refer kwanza kule alipotoka. Mimi nime- refer kwanza alipotoka Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Mpango uliowekwa na Waziri wa Magufuli Mheshimiwa Dkt. Mpango wa kule tunapoelekea. Kwa hiyo, taarifa yake haina maana yoyote kwangu, naomba niendele Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vituo vya afya tangu Uhuru tulikuwa na vituo vya afya 535 lakini ndani ya miaka mitano tumejenga vituo vya afya 487. Kama hiyo haitoshi tangu uhuru tulikuwa na zahanati 4,554 lakini ndani ya miaka mitano tumejenga zahanati mpya 1,998.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja kwamba haya yote niliyoyasema hayamaanishi kwamba tusitekeleze Mpango mpya uliowekwa mbele yetu. Nataka kila mtu afahamu kuna ugonjwa wa COVID-19 ambao ni ugonjwa umetikisa dunia na nchi yetu imechukuwa msimamo tofauti na nchi nyingine zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge nataka kutumia nafasi hii kuwatia moyo; msiogope. Msiogope mnapoambiwa kwamba kuna phase ya pili ya COVID-19. Kilicho na nguvu nyuma ya COVID-19 ni woga uliotengenezwa juu ya COVID-19; the fear over COVID-19 is even more powerful than COVID-19 itself.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote na watu wote tushinde woga, tusiogope, tumeshinda, tusonge mbele. Msimamo wetu wa kutokuchanjwa na msimamo wetu wa kutokufanya social distancing ni msimamo sahihi na utatufikisha mahali sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho, watu wengi wanazungumza kusahau tulikotoka wakifikiri historia when you don’t remember where you are coming from, you are bound to make mistakes where you are going thinking you are doing development, but you may do the same because you don’t know where you are coming from.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kule nyuma ilikuwa na miradi ya wachimba madini. Tulikuwa tunapewa royalties peke yake, nchi yetu ilikuwa inapata royalties peke yake ya makampuni ya madini. Sasa hivi Mheshimiwa Rais amesukuma tunapata almost asilimia 50 na Tanzania ni wamiliki wenza wa madini yanayochimbwa na kampuni za madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)