Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa hitimisho la hoja ya Mpango na Makadirio ya Matumizi ya fedha ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka huu wa 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru sana Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mhandisi Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho kwa ushirikiano mkubwa anaonipa ambao umeniwezesha kutekeleza majukumu yangu ya Unaibu kwa urahisi. Pia namshukuru Naibu mwenzangu hapa kwa jinsi tunavyoweza kushirikiana katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi niweze kujibu hoja mbalimbali ambazo zimejitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo la barabara wameongea kwa hisia kali sana. Ni kweli mahitaji ya barabara na hasa kwa kiwango cha lami, ni makubwa sana. Tukirudi nyuma miaka michache tu, miaka sita, tutakumbuka miundombinu ya barabara ilivyokuwa. Hivyo, tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa awamu zote kwa jinsi ambavyo imekuwa ikifanya vizuri katika sekta ya miundombinu. Kikubwa tu ni kwamba barabara hizi ni nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba moja ya kigezo kikubwa sana ambacho kimeiingiza Serikali ya Awamu ya Tano na Wabunge wengi kupata kura nyingi sana za kishindo kilichangiwa sana na eneo hili la jinsi Serikali ilivyofanya vizuri katika sekta ya miundombinu ikiwa ni barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niende kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, imesema nini? Ni kweli kwamba tuna ilani ambayo tunatekeleza, lakini ilani hii inatekelezwa kwa miaka mitano. Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025, kilometa ambazo zimeainishwa zitajengwa kwa kiwango cha lami, kwanza zinakamilishwa 1,716, zinazojengwa ni 6,006 kwa kipindi hiki cha miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha inayohitajika kukamilisha barabara hizi ni takribani shilingi trilioni 11. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge isingekuwa rahisi barabara zote hizi ambazo zimeainishwa zikapata nafasi kwa kipindi hiki, lakini tukubali kwamba tunatekeleza barabara hizi kwa miaka mitano. Barabara ambazo zitafanyiwa upembuzi yakinifu zina kilometa 7,500; zinahitaji karibu shilingi trilioni 11.5. Kwa hiyo, ukiangalia unaweza ukaona hiyo bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu hoja ya mchangiaji mmoja na hasa Mkoa wa Kigoma. Mkoa wa Kigoma sasa hivi wana barabara tatu zinazoingia makao makuu. Barabara ya Kigoma – Nyakanazi wakandarasi wote wako site. Barabara inayounga Tabora na Kigoma imebaki kipande cha Malagarasi – Uvinza ambacho muda wowote kinaanza kutengenezwa. Pia Mpanda kwenda Kigoma, wakandarasi wapo wanapunguza barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nadhani ni Mkoa wa Katavi tu na Kigoma ambao wanafika Makao Makuu bila kupita kwenye lami, lakini wakandarasi wako site. Angalau mikoa yote mtu ana uwezo wa kufika Makao Makuu kupitia kwenye lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lilijitokeza la muda wa barabara. Nitolee mfano barabara ya Dodoma – Iringa; tatizo kubwa ilikuwa, barabara hii ni traffic projection ambayo hatukutegemea kama barabara itakuwa na mzigo mkubwa na wingi wa magari kama hayo ambayo yamejitokeza hapo katikati, lakini ndiyo maana umepunguziwa muda ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la matuta lilijitokeza. Iko sheria ambayo imetoka, miongozo ambayo pia tunayo ya SADC ambao tunashirikiana nao, niwahakikishie Wabunge kwamba tumeendelea kutoa matuta yale ambayo hayakindi vigezo ama hayaendani na huo mwongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwape comfort Waheshimiwa Wabunge kwamba barabara zote ambazo zimeathirika kutokana na mafuriko, tumejipanga; yako madaraja ya muda ambayo tumeyaagiza, tutahakikisha kwamba tunafanya tathmini na kurudishia maeneo yote ambayo yamekatika ikiwa ni pamoja na kuinua matuta sehemu ambazo zimeathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la vigezo vinavyotumika kutengeneza barabara za lami, barabara ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami lazima iwe ni barabara ya ukanda, yaani barabara ambazo zinaunga kwenye ushoroba, ziwe zinaunga mikoa, barabara iwe ni ahadi ya viongozi wa kitaifa kwa maana ya Mheshimiwa Rais, Makamu ama Waziri Mkuu, iwe ipo kwenye Ilani ya Chama Tawala, iwe ni kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano. Pia barabara zinazoenda kwenye eneo la kuchochea uchumi ambalo ni kama utalii, uzalishaji mali na vitu kama hivyo na vile vile liwe ni eneo la ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge watupitishie bajeti ili twende tukatekeleze hiyo mipango ambayo wananchi wanahitaji sana barabara zao zikatengenezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge sasa nimwite Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Engineer Dkt. Leonard Madaraka Chamuriho aje ahitimishe hoja yake.