Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Tarimba Gulam Abbas (2 total)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba na mimi nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu mazuri ya swali lililopita lakini naomba nimuulize juu ya changamoto ambazo zipo katika matumizi ya Sheria ya Road Traffic (Road Traffic Act), ile Cap 168 pamoja na Kanuni zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na matatizo ya matumizi ya barabara hasa kwa waendesha pikipiki/ bodaboda ambao wanakiuka sheria zilizopo katika mahitaji ya jinsi gani ya kuendesha vyombo vyao. Na sasa imezidi pale Dar es salaam hasa watumiaji wa barabara za mwendokasi, madereva wa mwendokasi wanapita kwenye taa nyekundu; hadi jana usiku saa moja na nusu wameua vijana wawili.

Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha watumiaji wote wa vyombo vya moto barabarani wanafuata sheria na kwamba polisi/trafiki wanasimamia sheria zile ipasavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hizi ambazo tumeziweka sisi hapa Bungeni tunatarajia kwamba kila Mtanzania atakuwa anatekeleza wajibu wake bila ya kushurutishwa. Matumizi ya barabara yameainishwa kikamilifu kupitia sheria zetu na usimamizi unaendelea pia kwa vyombo ambavyo tumevipa jukumu la kusimamia kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini usimamizi wa sheria hautakiwi usimamiwe na Jeshi la Polisi peke yake tu, kila Mtanzania anatakiwa kufuata sheria pale ambapo sheria imeshatungwa na inataka itekelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba watumiaji wa pikipiki walio wengi hawajali matumizi haya ya sheria zetu na kujali kwamba sheria hizi ni lazima zitekelezwe. Lakini pia Jeshi letu la Polisi linacho kitengo kinatoa elimu kila siku, na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mnajua kwenye televisheni zetu za TBC, ITV, Star TV lakini pia Azam tumetengewa muda na Jeshi la Polisi linafanya kazi hiyo vizuri sana, kuelimisha Watanzania kuhusu matumizi sahihi ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunasimamia sheria hizi nitoe wito kwa watumiaji wa barabara hasa watumiaji wa vyombo vya moto wote kwamba ni muhimu sana kuzingatia Sheria za Barabarani. Hii ni muhimu sana kwa sababu inalinda uhai wa Watanzania wote, kuanzia yeye mtumiaji wa chombo chenyewe cha moto, watumiaji wa njia hizo wanaotumia kwenda kwa miguu lakini pia pamoja na wale wanaotumia barabara hizi za mwendokasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu njia hii ya mwendokasi tumeshaieleza wazi, kwamba njia hii tumeitenga maalum kwa ajili ya magari ya mwendokasi, lakini pia tumetenga njia nyingine kwa ajili ya magari yetu ya kawaida. Tumejenga na njia ya pembezoni ya watembeaji wa miguu pamoja na vyombo vingine vya moto. Kwa hiyo, ni wajibu wetu Watanzania kutekeleza sheria, ikiwemo na kujali matumizi ya barabara zetu hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali hapa ni kuendelea kutoa elimu na kusimamia sheria. Pale ambapo tunaona kuna mtu anavunja sheria, hatua za kisheria zinachukuliwa hapohapo; huo ndio mkakati ambao tunao kwa sasa. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Swali langu linahusu huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, natambua, nathamini na vilevile naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa sana za kuhakikisha kwamba Taifa hili linakuwa na umeme wa uhakika. Nafahamu vilevile kwamba kumekuwa na initiatives nyingi za Serikali ikiwemo hii ambayo imetolewa tarehe 30 Juni, 2014 ambayo ni ya Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap. Katika utafiti huo inaonekana kuna matatizo makubwa ya generation, transmission pamoja na distribution.

Mheshimiwa Spika, sasa TANESCO inaonekana kuhemewa na kazi hii hasa kwa kuwa tunakwenda kuwa na umeme mkubwa kutoka Mwalimu Nyerere Hydropower Supply. Kwa hali hiyo, Serikali haioni kwamba muda muafaka sasa wa kwenda kuifumua TANESCO ili tuwe na makampuni matatu ya generation peke yake, transmission peke yake pamoja na distribution kama ilivyo katika nchi nyingine na hata majirani zetu wa Kenya, Uganda, South Africa na kwingineko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba ridhaa yako angalau hili eneo la mwisho naweza kulitolea ufafanuzi kama ambavyo Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, mwanamichezo alivyouliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shirika letu la umeme nchini linafanya kazi kubwa sana. Kazi hiyo kubwa ambayo inafanywa kwa sasa, lenyewe ndiyo linazalisha, lakini TANESCO pia inasafirisha umeme na inafanya kazi ya kugawa. Unapofanya jukumu hili, pia tunaangalia na maslahi ya Taifa, kwamba maeneo haya unaweza ukawa umeyakatakata ukawapa watu tofauti tofauti ikakuletea athari kwenye usalama wa nchi. Pale ambako nchi inahitaji umeme wakati wote, halafu mmoja miongoni mwao anafanya mambo anayoyataka tu, halafu ukashindwa kufikia malengo ya kupeleka umeme kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wake. Hali tuliyonayo sasa nchini, maeneo yote yanayozalisha umeme tunaendelea kuzalisha umeme. Tuna maeneo ya maji; tunapopata mvua za kutosha kama sasa maji yamejaa, mfano Kidatu na Mtera, tunayo maji ya kutosha na uzalishaji unaendelea. Kwa hiyo, eneo hili halina matatizo. Kwenye eneo la gesi pale Kinyerezi uzalishaji unaendelea. Pia maeneo mengine tunayotumia mafuta yanaendelea pia na uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, TANESCO kwa sasa maeneo yote ya uzalishaji, uzalishaji upo. Changamoto tuliyonayo sasa ni miundombinu iliyopo kwenye maeneo hayo ya uzalishaji. Hii inasababisha pia hata sasa naona kuna baadhi ya maeneo umeme unakatika, lakini ni kwa sababu ya kukosekana miundombinu. Sasa nini mkakati wa Serikali?

Mheshimiwa Spika, moja, tumewapa kazi TANESCO kufanya tafiti. Wanaweza kuja kwenye hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameipendekeza. Pale ambapo tutakuwa tumejipanga na tunaona nani tunampa jukumu la kuzalisha, nani anasafirisha lakini pia msambazaji ni nani? Zinaweza kuwa ni taasisi za Serikali ambazo pia lengo lake ni moja. Kwa hiyo, tukifikia hapo kupitia utafiti unaoendelea sasa na Shirika letu la Nmeme Nchini, tutaweza kufikia hatua nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, suala la usambazaji, kama ambavyo mmeona Serikali leo ina mkakati wa kupeleka umeme mpaka vijijini, hii hatua tutaifikia kwa sababu tumefanya kazi nzuri sana na leo umeme unapatikana mpaka vijijini. Bado kazi hiyo inaendelea na malengo yetu kufikia Desemba mwaka huu tuwe tumefikia vijiji vyote nchini kupata umeme. Kwa nini? Tuna uhakika wa uzalishaji na bado tunaendelea kutafuta maeneo mengine ya uzalishaji, bado pia shirika letu limetoa nafasi kwa taasisi kuja kuwekeza kwenye uzalishaji. Kwa hiyo, nchi yetu itakuwa na umeme wa kutosha na kwa maana hiyo, eneo la uzalishaji halina matatizo kabisa. Tutajiimarisha pia kwenye eneo la miundombinu ya kwenye eneo la uzalishaji, usafirishaji na ugawaji kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachukua ushauri wake, tutaufanyia kazi na hivi TANESCO wanafanya kazi hiyo. Tukishakamilisha haya, tutatoa taarifa kwenu Waheshimiwa Wabunge na hasa Mheshimiwa Mbunge ambaye ametoa pendekezo hili, tutakupa mrejesho wa hatua ambayo tutaifikia. Ahsante sana. (Makofi)