Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salim Alaudin Hasham (1 total)

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Waziri yupo tayari kutembelea baadhi ya zahanati, vituo vya afya pamoja hospitali ya wilaya ili kujionea changamoto hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa upungufu wa watumishi katika jimbo langu umefikia asilimia 67, je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi wa afya katika Jimbo la Ulanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Salim Alaudin Hasham, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kama ombi, je, tupo tayari kutembelea jimbo lake na kujionea changamoto hizo zinazolikabili. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge tupo tayari mimi na mwenzangu Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya Mheshimiwa Dkt. Dugange na tutafika katika eneo lake na kushuhudia haya ambayo ameyazungumza na tutachukua hatua za kimsingi kuwasaidia wananchi wa jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, ameuliza kama tupo tayari kuongeza watumishi. Niseme tu kwa kadri tutakapokuwa tunaendelea kupata kibali cha kuajiri kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi tutaendelea kuajiri na kuongeza watumishi. Kwa hiyo, katika nafasi chache tunazozipata kama ambazo tunakwenda kuziajiri nafikiri kabla ya mwisho wa mwezi huu tutakuwa na watumishi kwenye kada ya afya karibu 2,700. Kwa hiyo, miongoni mwa watumishi hao wengine tutawaleta katika jimbo lako ili waweze kusaidia kuongeza ile ikama ya watumishi wa kada ya afya. Ahsante.