Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salim Alaudin Hasham (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu japo ametumia jina langu Salimu Almas jina la biashara jina langu kamili naitwa Salimu Alaudin Hasham Mbunge wa Jimbo la Ulanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niniiponge Wizara kwa kazi kubwa waliofanya kwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya madini mpaka hii leo kuonekana sisi pia wachimbaji wadogo ni watu ambao tunachangia katika pato la Taifa. Lakini kuna vitu vichache ambavyo napenda kuvichangia kwenye Wizara ya Madini ili kuviweka sawa inawezekana ikachangia pato zaidi kwenye upande wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natokea kwenye upande wa madini ya vito na nimekulia kwenye madini ya vito cha kwanza kabisa naomba nichangie katika upande wa value addition. Kwenye upande wa value addition, Tanzania tuna madini ya aina nyingi sana na Tanzania inaachangia duniani kwa asilimia karibu 30 kwenye madini ambayo yanaingia kwenye soko la dunia.

Lakini niseme ukweli kabisa kwamba Serikali bado hatujajipanga vizuri kwenye upande wa value addition na hii nitatoa mifano michache kutokana na ufinyu wa muda mfano mkubwa kabisa tuna madini aina ya safaya ambazo zinachimbwa Tanga na ambayo yanachimbwa Tunduru kwenye Jimbo la ndugu yangu Hassani. (Makofi)

Mheshimimiwa Naibu Spika, madini yale yamewekwa kwenye utaratibu kwamba mwongozo unasema madini yale yasafirishwe kuanzia gramu mbili kushuka chini ndio yasafirishwe yakiwa ghafi. Kwa maana hiyo kwamba madini ya juu hayawezi kusafishwa lakini kinachotokea ni kwamba kwenye upande wa safaya madini ya safaya ili yaweze kuongeza thamani lazima yafanyiwe treatment kwa maana yachomwe na utaalamu ule bado haujaingia kwenye nchi yetu kabisa huko Thailand peke yake na hawajawahi kuugawa utaalamu ule kwenye nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo Serikali itakuwa imeamua kuuwa biashara ya madini aina ya safaya, vinginevyo wangeruhusu yale madini mengine yaweze kusafirishwa madini ya vito yasafirishwe yakiwa ghafi ina maana labda kuna uwezekano ingesaidia utoroshaji wa madini katika sekta ya madini. Ninayo mifano mingi lakini kutokana na ufinyu wa muda kwa sababu nina vitu vingi vya kuchangia naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upande wa ma-valuer kiukweli Serikali ina ma-valuer wachache sana kwa upande wa Tanzania katika idadi ambayo tulionayo katika takwimu inaonyesha tuna ma-valuer 18 peke yake ambao hawatoshi lakini naamini kabisa Serikali inapambana kuongeza ma-valuer lakini pia ma-valuer wetu wengi awana uzoefu mkubwa wa kufanya valuation ya madini tuliyo nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naamini kipindi ambacho wanaendelea kufanya kazi watapata uzoefu ili kujihakikishia kazi ambayo wanaifanya. Lakini pia kuna maneno yanasemekana kwamba ma-valuer wetu ndiko mapato yanakopotelea jibu nasema sio kweli kabisa na inawezekana ma-valuer hawa wanawapatia faida zaidi Serikali kuliko wafanyabiashara kwasababu mara nyingi Serikali kuliko wafanya biashara kwasababu mara nyingi wakikosea wanakosea kwenye kuongeza thamani ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kodi utakayolipa itakuwa ni kubwa zaidi naomba Serikali ijikite zaidi kuangalia madini yanapotelea wapi lakini sio mapato yanakopotelea naamini kabisa madini yakifika kwa ma-valuer Serikali haina kinachopoteza. Kwa hiyo, ijikite kwenye kuangalia madini yanatoroshwa vipi lakini si yanapotea kutokana na wanaofanya valuation.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa lingine naomba nichangie na hii itakuwa ni special case Mheshimiwa Waziri unisaidie kidogo kwenye upande wa Jimbo langu kuna kampuni mbili ambazo zinataka kuja kufanya miradi mikubwa ya madini ya kinyo yaani graphite. Kampuni zile ni Tanzagraphite na ingine inaitwa Mahenge - resource. Mwaka 2017 walifanya uthamini juu ya kuwalipa fidia wana Kijiji wa Ipango, lakini mpaka mwaka 2019 uthamini ule ulikuwa ume-expire kwa maana hiyo kampuni ya Tanzagraphite ilipaswa kuwalipa posho ya usumbufu wananchi wa Ipango kulingana na kucheleweshwa na kusitishwa shughuli zao za maendeleo na waliandikiwa barua walihimizwa kwamba wafungue akaunti ili waweze kulipwa posho hizo lakini mpaka leo hawakuweza kufanya kitu kama hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, na bado watu wale wamesitishwa kabisa kufanya shughuli za maendeleo kwa hiyo nilikuwa naomba kupata muhafaka wa kampuni ile nini kinaendelea na nipate muafaka mzuri nione jinsi gani ya kuwajibu na katika sehemu ambayo nilipata changamoto kipindi nafanya kampeni zangu Mheshimiwa Waziri, nilifika niliwakuta wananchi wale wamekaa chini badala ya kunishangilia. Matokeo yake ikabidi nibadilishe mkutano kwa kikao kama cha familia ili waweze kunielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuna kampuni nyingine ya Mahenge resource ambayo pia imeshafanya uthamini, tunaomba pia uhalali wa kampuni ile na uhakiki wa kampuni ile kwamba ipo tayari kuja kufanya kazi katika vijiji vyetu kwasababu isije na wenyewe wakatokea ikawa kama yenyewe ni Tanzagraphite ambako wananchi wale pia wamesitishwa zaidi ya vijiji vinne havifanyi shughuli za maendeleo.

Mheshimia Naibu Spika, naomba nizungumzie kwenye value of chain kwenye upande wa madini kuna mchimbaji, kuna broker na kuna dealer, ukiweka hawa watu ukiwakusanya pamoja lazima mmoja wapo… broker ni mtu ambaye ana mtaji mdogo mwezangu na mimi au la hana mtaji kabisa. Obvious mchimbaji yule hawezi kufanya kazi na broker akachagua kufanya kazi na dealer, kwasababu wana-cash, maana yake utakuwa umemuuwa yule broker hawezi kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wale tunawalazimisha wakate leseni watu wanakadiliwa kodi ya mapato mwisho wa mwaka wanapaswa kulipwa na ndio wengi zaidi ambao wanaunganisha biashara kati ya mchimbaji na dealer. Kwa hiyo, naomba pia Serikali iliangalie hili kwa kina zaidi ione ni jinsi gani inaweza kufanya mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nirudi kwenye upande wa GST bado haijafanya vizuri sana kwenye upande wake, ningeomba Serikali iwawezeshe sana GST waende kufanya utafiti katika madini yenye thamani kubwa kama vile kama ya aluminum, copper lithium maganize nickel graphite, silver na mengine mengi lakini pia kuna layer- ath-stone kama ruby spinel na madini mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, GST iende ikafanye utafiti mkubwa ili kuongeza wawekezaji waje kwa wingi kufanya, lakini pia Serikali iwaangalie sana wawekezaji wa ndani kwa sababu wawekezaji wa ndani sasa hivi wana uwezo mkubwa wa kufanya, na iwaangalie kwa jicho la tatu ili waweze kuwasaidia na hasa kwenye upande wa mikopo ya wachimbaji wadogo. Wachimbaji wadogo hatuamini kabisa mabenki pamoja wanashauriwa kwa ajili ya kutukopesha lakini mabenki bado hayatuamini kwa hiyo tungeifanya biashara yetu iwe biashara ambayo inatambulika duniani na watu waaamini kile ambacho tunakifanya naamini Serikali yetu ingeweza kuongeza pato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Naibu Spika, sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika Wizara hii japo nimeona malalamiko mengi sana ya Wabunge kuhusu suala la barabara na kuna uwezekano mkubwa sana Serikali ikawa haina bajeti kubwa kwa ajili ya barabara lakini inawezekana pia ikawa hawajajipanga vizuri kwenye mgawanyo kwa ajili ya barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara za upande wa jimbo langu; kuna barabara ya kutoka Ifakara - Ulanga kujengwa kwa kiwango cha lami, imekuwa bingwa kuongoza kutajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu lakini mpaka leo hii sijaona hata kilometa moja ambayo imetengewa barabara ile ili wananchi wangu wa Ulanga waweze kupata barabara ya lami. Hata kama ni kwa kilometa chache basi mgawanyo ule ungezingatia kidogo kuona kwamba watu wengi wana uhitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mbunge mwenzangu jana alitaka kuruka sarakasi hapa kuona kwamba kuna mtu ana lami anaomba bajeti ya kurekebishiwa lami yake wakati sisi wengine hatuna lami na hatujawahi hata kuiona. Sijui huwa wanatumia vigezo gani, kiukweli inaumiza sana.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja na special case kabisa, kwenye jimbo langu kuna daraja liko kwenye Kijiji cha Ikangao ambayo inaunganisha Kata mbili za Ilonga na Ketakeli. Daraja lile limekatika na linahudumia zaidi ya watu 28,000 na wanafanya shughuli za maendeleo ikiwemo ni pamoja na kilimo. Watu wale mwaka jana walilima ufuta walikuwa wanauza Sh.3,000 kwa kilo, baada ya daraja lile kukatika wakawa wanauza ufuta kwa shilingi 1,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia suala la kilimo ni lazima tujue kwamba bila barabara hakuna kilimo ambacho kitaenda kwa sababu mazao yale hayawezi kufika sokoni kabisa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri mara Bunge litakapoisha nifanye naye ziara kwenye jimbo langu kwa sababu jimbo lile limesahaulika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri yupo hapa, naomba daraja hili liende likajengwe, mimi sitaki kujua fedha zitatoka TARURA au TANROADS.

Naomba wananchi wangu wakajengewe daraja hili kwa sababu lisipojengwa tena mwaka huu ina maana biashara zitakuwa zimekufa na wale wananchi mwaka ujao inawezekana wasilime kabisa kwa sababu hawana wanakoweza kupeleka bidhaa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tutaendeleza sana kudumaza uchumi wa nchi hii kama hatutazingatia suala la barabara. Barabara ni muhimu sana, huwezi kuzungumzia viwanda kama hujazungumiza barabara, huwezi kuzungumzia kilimo kama hujazungumzia barabara. Kwa hiyo, mimi niwaombe sana, inawezekana kweli Wabunge wengi wamelalamikia suala la barabara, kuna uwezekano kwamba mkatakiwa kwenda kujipanga vizuri lakini pia hata kama mkienda kujipanga naomba sana daraja hili lipewe kipaumbele ili wananchi hawa waweze kuendelea shughuli zao za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madaraja mengine ambapo wananchi tumejipanga kwenda kufanya kazi wenyewe kujenga daraja lile kwa sababu watu wanakufa kwa ajili ya kuliwa na mamba. Tumesema tutaenda kufanya kazi na wananchi wangu kwa kuweka hata daraja la mbao ili waweze kuendelea na shughuli zao lakini hili ni daraja kubwa sana ambalo linaunganisha watu wengi sana. Hawa nimezungumzia wananchi wachache 28,000 kutoka kwenye hizi kata mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye mpango huu wa bajeti. Pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika hapa siku ya leo. Pia nisiwe mchoyo wa fadhila, bila kumshukuru Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuhakikisha anaiendesha nchi hii katika usawa na utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kama matatu ya kuchangia kwenye Bajeti. La kwanza nitagusa kwenye mambo ya barabara. Kwanza niwapongeze Wizara zote kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pia nawapongeza Wizara ya Ujenzi inavyopambana, tumeona miradi mingi ambayo inatekelezwa, miradi ambayo imekamilika, lakini hatuwezi kurudi nyuma maana miundombinu ya barabara ndiyo chachu ya maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana niliuliza swali hapa Bungeni kuhusu barabara zetu hasa kwenye Jimbo langu la Ulanga. Majibu ya Mheshimiwa Waziri yalikuwa ni mepesi, lakini sijui ni kwa sababu gani? Kikubwa, ninapozungumzia barabara ya kutoka Kilombero kwenda Ulanga ya kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 67 ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015, lakini iliingia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Bajeti zote; mwaka 2020/2021, 2021/2022 na 2022/2023 tumekosekana. Tuna imani labda bajeti ijayo tunaweza tukaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu ya msingi kuombea barabara ile. Jimbo la Ulanga sasa hivi ni kitovu cha madini na pia ndiyo Mkoa wa Madini ambao Mheshimiwa Dotto alikuja kuufungua juzi. Tuna miradi mikubwa sana ambayo inakwenda kufanyika kwenye jimbo lile. Wawekezaji wanaenda kuweka zaidi ya Dola milioni 200. Sasa hivi wako kwenye mchakato wa kulipa fidia kwa wanakijiji ili kuweza kupisha miradi ile. Barabara zetu sasa hivi tunapitisha Noah tu; na gari kubwa inayopita ni Fuso, lakini ikinyesha mvua network inakatika kwa maana hiyo barabara haipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshajiuliza hivi hawa wawekezaji tusipowawekea mazingira mazuri, kesho wakianza kukafanya mobilization: Je, watawezaje kufanya kazi yao na biashara yao inafanyika masika na kiangazi? Inamaanisha adha kubwa itaenda kuwakuta wananchi wa Jimbo la Ulanga, na pia wawekezaji wale watakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kufanya kazi yao. Hiyo ni kampuni moja nimezungumzia, Jimbo la Ulanga tunaenda kufanya makubaliano na kampuni nyingine mbili ambazo zinaenda kuchimba madini ya Kinywe. Madini haya yanaenda kubebwa kwenye magari makubwa. Barabara ile haitaweza kukidhi na kuwasaidia wawekezaji hawa kuweza kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninapozungumza, nipo hapa na ndugu yangu Mheshimiwa Taletale anakuja, ametoka kunilalamikia suala la barabara. Nikamwambia mimi sio Waziri, Mheshimiwa Taletale, ongea na Mheshimiwa Waziri, mimi mwenyewe nina majanga yangu kibao jimboni kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu Mawaziri hawa wanatakiwa watupe kipaumbele sana. Sijui kama kuna mawasiliano katika hizi Wizara. Mheshimiwa Dotto ameshamaliza kazi yake kwenye upande wa madini, kwamba watu wanaenda kufanya kazi zao. Kungekuwa na mawasiliano basi, kwamba jamani, tumeshamalizana na hawa watu wanakuja kuwekeza, waende kwa Waziri wa Ujenzi, jamani, barabara zetu zikoje? Zinaweza kukidhi mahitaji ya wawekezaji? Au hospitali, kwamba watu wanakuja kuajiriwa zaidi ya 1,000, je, hospitali zetu zinakidhi mahitaji ya watu na kuwekeza? Siyo mradi mdogo, watu wanakwenda kuwekeza zaidi ya Dola milioni 200 halafu hamna barabara, hakuna hospitali za maana, tutaenda kuchekesha, na hata hao wawekezaji watatuona hatuko serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nirudi kwenye Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia. Ndugu yangu Mheshimiwa Francis hapa amesema, nami ilikuwa katika mpango wangu wa kuchangia leo; unamwambiaje mwananchi huyu? Kwanza unamwambia akinunua kifurushi cha siku, kwa wiki atatumia shilingi 10,000; akinunua cha wiki atatumia shilingi 5,000. Maana yake huyu mtu umemhamasisha kwamba anunue kifurushi cha wiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu coverage network yake ni mbaya, vijiji vingi havina network na maeneo mengi hayana network. Mkulima amejiunga kifurushi chake cha shilingi 5,000, ameenda zake shambani, baada ya siku nne anakuja mjini anaambiwa kifurushi chake kimeisha. Kifurushi chake kimeenda wapi? Hela yangu nani amekula? Tusijibizane majibu rahisi rahisi, ni lazima watu tujue kwamba hii ni dalili ya wizi watu wanaibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumlazimisha mtu anunue kifurushi cha shilingi 35,000 anatumia wiki mbili, wiki mbili nyingine unamwambia kifurushi chako kimeisha, mimi sioni kama ni sahihi na Waziri yuko hapa anatusikiliza. Tuna jambo la kufanya kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia sekunde thelathini.

MWENYEKITI: Hizo ni za mwenzio. Haya, malizia.

MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye mawasiliano na teknolojia, tuone sababu za msingi za kufunga kamera kwenye miji yetu mikubwa kwa ajili ya Security. Wenzetu Kenya wameshafunga kamera miaka saba iliyopita, sisi population inaongezeka, uhalifu unaongezeka, tunawatuma askari wanaenda porini hawajui hata mhalifu yuko wapi? Hili ni jambo la msingi sana, miji yetu mikubwa ikafungwe kamera kwa ajili ya security. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)