Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Issa Jumanne Mtemvu (4 total)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Mradi wa Maji Chunya unafanana na ule mradi wa 2F2B pale Tegeta A, ujazo wa lita milioni sita. Je, Wizara inaweza ikatuambia ni lini mradi ule utakamilika ili uweze kusaidia wananchi wote wa Goba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ule mradi wa tanki Mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mpiji Magohe, Makabe yote na Msakuzi.

Je, ni lini pia mradi huo utakamilika ili wananchi wapate maji salama?

SPIKA: Swali sio lako, kwa hiyo unapaswa kuuliza swali moja tu, sasa chagua mojawapo katika hayo ya kwako.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Niweze kufahamu mradi unaotaka kujengwa mshikamano kwa ajili ya wananchi wa Mbezi, Makabe na Mpiji Magohe utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Mtemvu kutoka Kibamba kama ifuatavyo:-.

Mheshimiwa Spika, Wizara sasa hivi inapitia miradi hii yote ambayo usanifu wake ulikamilika. Kwa hiyo nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge huo mradi upo katika miradi ambayo inakwenda kutekelezwa awamu hii kabla mwaka huu wa fedha haujaisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa Busanda unafanana sana na ule mradi uliopo Wilaya ya Ubungo, hasa mradi wa 2f2b, unaoanzia Changanyikeni, Chuo Kikuu mpaka Bagamoyo na hasa ujenzi wa tanki kubwa la lita milioni sita pale Tegeta A, Kata ya Goba. Je, mradi huu utakamilika lini ili wananchi wote wa Kata ya Goba wapate maji safi, salama na yenye kutosheleza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu kutoka Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote hii ambayo tayari utekelezaji wake unaendelea Wizara tunasimamia mikataba na namna ambavyo mkataba unamtaka yule mkandarasi kukamilisha mradi ule. Mheshimiwa Mbunge ninakupa uhakika kwamba tutasimamia kwa karibu na mradi ule utakamilika ndani ya muda ambao tumeupanga.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo la Kibamba ipo ahadi ambayo ndani ya Ilani ya miaka mitano mfululizo 2015/2020 na 2020/2025 ujenzi wa barabara ya Makabe – Msakuzi – Mpiji Majohe ikiungana na barabara ya Kibamba Njiapanda – Mpiji Majohe kwenda Bunju kupita Mabwepande. Lakini pia ikumbukwe barabara hii pia ni ahadi ya mwisho kabisa ya Mheshimiwa Hayati Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba ni kati ya ahadi za mwisho kabisa za Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Nadhani aliitoa wakati yuko kwenye ile stand na bahati nzuri nilikuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ikishakuwa na Mheshimiwa Rais ni utekelezaji. Lakini atakubaliana nami kwamba ahadi aliyotoa isingekuwa rahisi kwamba tumeanza kuitekeleza, lakini ahadi ambayo tunaizingatia na tayari shughuli zimeshaanza kuona namna ya kuanza kutekeleza ile ahadi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi kama zile zikishatolewa, kinachofuata ni utekelezaji na mimi nimhakikishie kwamba Serikali kupitia Wizara yangu hiyo ahadi tutaitekeleza. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ya kuridhisha kwa kiasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamekuwa na watumishi wengi ambao wamekaa muda mrefu, zaidi ya miaka kumi hadi ishirini wakiwa wanalilia suala la muundo huu ambapo umetoka Waraka Na.3 wa Mwaka 2015 bila kutekelezwa kwa wakati. Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyeo vyao kwa mserereko ili kuzingatia muda waliotumia kazini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la hadhi ya Kitengo cha Uhasibu, ni kweli Serikali inajibu juu ya vigezo ambavyo vinafanyiwa tathmini mara kwa mara na Ofisi ya Rais, Utumishi. Natambua vigezo vyenyewe vinazingatia job analysis na job design. Kwa msingi huo, ni ukweli kada hii imeacha kutumia local standards kwa muda mrefu sana na sasa wanatumia international standards katika kutengeneza mizania mbalimbali ya taasisi. Vilevile hata ripoti za CAG tunaziona jinsi gani zinavyotoka tayari kila mmoja anahamaki juu ya kuiona hadhi ya taasisi inabebwa na sehemu au kitengo hiki. Tunao mfano, juzi tu taarifa ya CAG baada ya kuitoa tayari viongozi wa Serikali wametoa maelekezo magumu kwa section hii, yaani Wakuu wa Idara au Vitengo hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho hadhi hii inategemea kazi kubwa wanayoifanya. Tayari uchumi na mipango wana hadhi ya Kurugenzi…

SPIKA: Mimi nilifikiri swali huwa linakuwa ni swali.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni swali, natengeneza hoja ya kuuliza swali la mwisho hili.

SPIKA: Hapana, unahutubia Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi kwa misingi hiyo miwili sasa Serikali haioni ni muda mwafaka wakifanya analysis yao wa kukipa hadhi Kitengo hiki cha Uhasibu na Idara ya Ukaguzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu kwa kuwatetea watumishi hawa, lakini nimjulishe kwamba ni dhamira ya Serkali na Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka kuhakikisha kwamba inapandisha vyeo na hadhi za wafanyakazi na watumishi wake ambao wanafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hao Wakaguzi wa Hesabu, Wahasibu pamoja na Wasaidizi wao watapandishwa vyeo pale ambapo hali ya bajeti itaruhusu lakini kwa kuzingatia vigezo ambavyo vimewekwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na vigezo hivyo, kama ambavyo nimejibu katika swali lake la msingi ni kwamba utaratibu huu ambao umewekwa upo kwa mujibu wa Sheria ile ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi ambayo ndiyo imesababisha kutayarishwa Waraka huu Na.3. Kwa kuzingatia sheria hiyo na Waraka ule, ndiyo utaratibu huohuo ambao utaendelea kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi.