Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana (5 total)

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, kaka yangu Dkt. Dugange kutoka Wanging’ombe, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi tumesema kwamba inatokana na mapato ya kipindi husika asilimia 10, napigia mstari neno kipindi husika. Naomba kupendekeza maboresho kwamba halmashauri zinapokusanya pesa, let say, ya 2020; baada ya yale marejesho, inapokwenda 2021, ichukuliwe ile ya 2020 ichanganywe na 2021, ule Mfuko uwe Cumulative Revolving Fund na fedha ziwe nyingi. Halafu tunapokwenda 2022 tunachanganya ile miaka miwili, yaani Mfuko unakuwa mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, hatuoni sasa wakati umefika wa kukusanya ule Mfuko wa kukopesha ukawa ni Revolving Fund?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hatuoni kama wakati umefika, maafisa wanaosimamia mikopo hii wakapata elimu kama Maafisa Mikopo katika benki zetu ambao mara nyingi ni Maafisa Maendeleo ya Jamii kama Loan Officer?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mikopo ya asilimia 10 kutolewa kwa kipindi husika, kama ambavyo jibu la msingi limesema, ni kweli kipindi husika cha makusanyo ndicho ambacho tumesisitiza kama Serikali kuhakikisha halmashauri zinatenga asilimia 10 kwa ajili ya mikopo kwa makundi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo hiyo ni ile ambayo inahusisha wajasiriamali ambao fedha zile ambazo zinakopeshwa zinatakiwa kurejeshwa ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kuweza kukopa fedha hizo. Kwa hiyo, napokea ushauri mzuri wa Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana kwamba tutaendelea kusimamia, kuhakikisha kwamba mapato yanayokusanywa kwa kipindi husika, asilimia 10 inatengwa na kupelekwa kwenye vikundi hivyo ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao za ujasiriamali kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana naMfuko huu kuwa Revolving Fund, kimsingi Mfuko huu ni Revolving Fund mpaka sasa, kwa sababu baada ya kukopeshwa, vikundi vinarejesha kiasi cha fedha kilichokopwa bila riba kwa ajili ya kuwawezesha wakopaji wengine waweze kunufaika na mfuko huo. Kwa hiyo, tutaendelea kuelimisha jamii yetu na vikundi vya wajasiriamali kuweza kurejesha mikopo hiyo ili na wengine wapate fursa hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mchango na ushauri wa kuwa na maofisa ambao wanapata mafunzo mbalimbali ya mifumo hii katika benki na maeneo mengine, tunauchukua ushauri huo.
MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la masoko nje ya nchi limeendelea kuwa changamoto hususan baadhi ya bidhaa zetu, kwa mfano parachichi na hivi karibuni tumeona parachichi letu la Tanzania limefika nchi fulani na ikaharibiwa nje ya nchi.

Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masoko haya ya nje ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pindi Chana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jitihada zinazofanywa na wenzetu hasa katika nchi zinazotuzunguka hasa nchi kama za SADC ku-sabotage wafanyabiashara wa Kitanzania kuuza mazao katika nchi zao wakati sisi kama nchi tunaruhusu kwa mujibu wa sheria na mikataba tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukio alilolitaja Mheshimiwa Mbunge ni tukio ambalo limetokea katika nchi moja iliyoko Kusini mwa Afrika. Tumeanza mazungumzo na wenzetu wa Foreign Affairs na mimi nataka niwahakikishie Wabunge, Tanzania imeshiriki katika ukombozi wa nchi nyingi katika Afrika, hatutaruhusu wafanyabiashara wetu kudhalilishwa kwa njia yoyote ile. Tutachukua hatua dhidi ya nchi hii na sisi tutazuia bidhaa zao pale ambapo itabidi kufanya namna hiyo. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na mikakati yote hii ya Serikali ambayo ni mizuri kuhusiana na soko la mazao ya mahindi bado mahindi ni mengi sana kwa wakulima. Hivi sasa debe la mahindi limefikia Sh.3,000, mahindi yam waka jana wakulima bado wanayo na mwezi Juni tunavuna tena yataungana. Serikali inaweza kuiagiza NFRA waende msimu huu wakaokoe adha hii kwa wakulima kwa kununua mahindi haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la moja la Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba wakulima ama wanunuzi bado wana mazao mengi ya nafaka na wakati huo huo yanakutana na msimu wa mavuno hivi karibuni, huu ni ukweli ambao hauwezi kufichika.

Hata hivyo, sasa hivi hatuwezi kutoa commitment kwamba NFRA waende wakanunue nafaka hizo lakni hatua za awali ambazo tunazichukua na naamini baada ya muda mfupi tutalitatua tatizo la biashara kati ya sisi na nchi ya Kenya ambayo imekuwa ikinunua mazao yetu ya mahindi kwa muda mrefu. Naamini kwamba soko hilo likifunguka litaongeza idadi ya mahindi yanayokwenda nje. Vilevile sasa hivi tuna mazungumzo na wenzetu wa WFP ambao nao wameonesha demand ya kununua mahindi zaidi ya tani kama laki moja na nusu.

Mheshimiwa Spika, lakini hatua nyingine ya msingi ambayo tunachukua kama Wizara ni kwamba tunaongea na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuruhusu taasisi zetu NFRA na CPB kuruhusiwa kupata vibali ziweze kuchukua fedha katika taasisi za fedha na kununua mazao mengi ya wakulima kwa sababu uwezo wetu wa hifadhi sasa hivi umefika zaidi ya metric tons laki tano na kiwango tunachokihifadhi hakizidi laki moja na nusu.

Kwa hiyo, wakipewa kibali kutoka Wizara ya Fedha wataweza kukopa na kununua mahindi mengi pale ambapo tunakumbana na situation kama hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na niwaombe Watanzania wenzangu na wakulima wa nchi hii tunafanyia kazi jambo hili la kuijengea uwezo NFRA na CPB. Wakati huohuo tunaruhusu wafanyabiashara wa Kitanzania, yeyote anayepata soko popote duniani aje Wizara ya Kilimo tutampa kibali bure aweze kwenda kuuza mazao yake bila kuzuiliwa popote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuziomba halmashauri zisizuie mahindi, mpunga au mchele unaouzwa popote nje ya mipaka yetu kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni kutomtendea haki mkulima na wala hatuhitaji ukiritimba wowote kwenye trade ya mazao. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, asante. Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Njombe, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Serikali imesema kwamba, wanatafuta hizi fedha shilingi milioni 322. Ningependa kujua mkakati mzima wa upatikanaji wa hizi fedha na zitakuwepo kwenye bajeti ipi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; eneo ambalo wamepanga kujenga Ofisi ya Mkoa wa Njombe (Central Police), ni eneo hilohilo Ofisi ya Mkoa imepangwa kujengwa na Mahakama ya Mkoa; Ofisi ya Mkoa na Mahakama zimeshajengwa, sasa hii bado.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Njombe wangependa kujua ni lini hasa ofisi hii itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe, maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa anauliza; je, katika bajeti hii tumepanga kuweza kupata hizo fedha?

Mheshimiwa Spika, kubwa tu nimwambie kwamba katika bajeti hii hakuna fungu hili, lakini tutajitahidi katika bajeti ijayo pesa hizi ziwepo na tumuahidi Mheshimiwa kwamba, tutampa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba, eneo hili linapata kituo hicho cha polisi ambacho kitatoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini je, ni lini sasa Serikali italipa hiyo fidia? Nimwambie tu kwamba, tutajitahidi na tumuahidi mwaka ujao wa fedha tutajitahidi tulipe hiyo fidia, ili sasa ujenzi huu uweze kuanza haraka na wananchi waweze kupata huduma hizo za ulinzi na usalama. Nakushukuru.
MHE. BALOZI DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali hususan kuhusu zao la parachichi, bado mikoa ya Kusini hususan Njombe, zao la mahindi limeendelea kuwa ni changamoto. Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuondokana na hii changamoto ya zao la mahindi? Ikiwa ni bei ya mahindi pamoja na changamoto ya mbolea kwa Mkoa wa Njombe na Mikoa ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja; Serikali kupitia Wizara ya Kilimo tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara tumeamua sasa hivi kubadili mfumo wa uuzaji wa mazao ya kilimo badala ya kusubiri wanunuzi kuja ndani ya mipaka ya Tanzania sasa tunawafuata katika maeneo yao. Serikali sasa hivi imeanza mchakato wa kufungua maghala katika baadhi ya nchi ikiwemo nchi ya South Sudan, tunafungua ghala letu la kwanza kwa ajili ya kuuza mazao, ghala hilo litatumika vilevile na private sector pale ambapo private sector wanataka kuuza. Vilevile tunafungua ghala la kuuza mazao ya chakula katika Jiji la Nairobi kwa ajili ya kuuza processed products kwa maana ya unga wa mahindi, mchele na mafuta ya kula ya alizeti, pia tunafungua ghala katika Jiji la Mombasa kwa ajili ya kuhudumia processors walioko katika nchi ya Kenya.

Mheshimiwa Spika, pia tumeanza juhudi ya kuangalia uwezekano wa kufungua maghala katika nchi ya Kongo, especially Kongo Mashariki ili badala ya sisi kusubiri wanunuzi kuja katika nchi yetu tunahakikisha kwamba bidhaa zinakuwepo katika masoko yao na inakuwa rahisi kuwahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine la muda mrefu ni uwekezaji katika tija ili kupunguza gharama za uzalishaji na cost per unit na kufanya mazao yetu kuwa competitive katika masoko yanayotuzunguka. Moja ya soko kubwa ni nchi kama Kenya ambayo ina deficit ya zaidi ya tani laki sita kwa mwaka ya mahindi ambayo tunaichukulia kama ni fursa kubwa na kipato cha mwananchi wa Kenya asilimia 50 anatumia katika chakula.

Mheshimiwa Spika, hivyo, kwetu hili ni eneo la fursa na ndiyo maana tunaamua kuwekeza katika miundombinu ambayo itatumika na Serikali lakini vilevile na sekta binafsi wanaweza kutumia kuuzia hizo outlets tunazofungua katika nchi hizo. (Makofi)