Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana (2 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Hili suala la wastaafu kwa kweli ni kero kubwa katika nchi yetu. Nashukuru majibu ya Serikali, lakini niseme tu Serikali inatakiwa kujitahidi kwenye jambo hili, kwa sababu wastaafu waliomaliza ku-document document zao ambao wapo kwenye maeneo, wanaolia, wanaokwenda kwenye maofisi, wana miezi sita, miaka tano, miaka minne, ni wengi kuliko ilivyo kawaida.

Kwa hiyo, Serikali itafute mfuko thabiti wa kuzingatia mambo haya ili watu waweze kupata fedha zao. Watu wanakufa wanadai fedha, kwa nini mtu ameitumikia nchi, halafu anakufa anadai fedha.

Mheshimiwa Spika, naiomba tu Serikali itengeneze jambo hili liwe nzuri zaidi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu, Serikali ya Awamu ya Sita na hasa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma baada ya kuingia na kugundua kwamba wakati mwingine ucheleweshaji wa mafao hayo ya wastaafu yanatokana na haya malimbikizo ya michango. Michango mingi ambayo inatakiwa ipelekwe na waajiri, imekuwa ikicheleweshwa kupelekwa kwa mazingira ya aina moja ama nyingine. Serikali imekuja na suluhu hiyo ya kutengeneza mfumo ambao utawasaidia wafanyakazi wote kutambua ni lini wanastaafu na haki zao zikoje?

Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha sasa na upande wa pili wa mifuko, tumewaagiza na wameshatekeleza. Kwa mfano, Mfuko wa PSSSF wameshatengeneza mfumo ambao unaitwa PSSSF Kiganjani. Mfumo huo sasa umeshasambazwa na unaendelea kusambazwa kwa wanachama wote. Wanachama ambao wanakaribia kustaafu, wamekuwa sasa wakiwezeshwa kuzitambua haki zao kupitia kwenye mfumo na kuanza kuwasiliana na ofisi zote kabla ya muda kustaafu ili kupunguza hiyo kadhia ambayo imekuwa ikiendelea.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo tumewahagiza Mfuko wa PSSSF na mifuko mingine, kabla ya muda wa kustaafu, wastaafu wote watarajiwa tumeanzisha sasa vikao maalumu mfuko kukutana na wastaafu watarajiwa kuwatambua na kuandaa mafao yao mapema na hivyo kadiri tunavyokwenda kadhia hii itakuja kuondoka na tunapenda wastaafu waweze kupata mafao yao kwa muda unaotakiwa. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anajibu, amesema moja ya changamoto ya kuchelewa kulipwa kwa wastaafu ni pamoja na waajiri kuchelewa kupeleka michango. Wakati jana nimeomba mwongozo, nimepokea message 165, wengine hawajalipwa kuanzia mwaka 2012; lakini kwenye Bunge la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliji-commit kwamba atafanya ziara kwenye vyombo vyote vya habari kuhakikisha wanapeleka michango ili Waandishi wa Habari na watu wengine binafsi walipwe kwa wakati. Sasa nataka niulize, ni lini ataanza hiyo ziara ili Waandishi wa Habari michango yao ipelekwe ili na wenyewe wawe na uhakika, baada ya kumaliza kazi zao wapate stahiki zao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, masuala haya ya haki ya wafanyakazi ni masuala yanayotakiwa kuangaliwa kwa utaratibu mzuri sana. Masuala haya hayafanani tu labda na maamuzi ya mtu, kuamua kukaa hapa, ukae na nani na ufanye nini? Hapana, ni lazima kuyatengenezea utaratibu madhubuti.

Mheshimiwa Spika, naomba kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tumeshaanza hiyo kazi. Kazi ya kwanza tuliyoifanya ni kupata ushirikiano kutoka kwa Waandishi wa Habari, kutambua vyombo ambavyo vimekithiri kwa kutokulipa mishahara na mafao ya Waandishi wa Habari. Kazi hiyo, tumeshaitekeleza na baada ya hapo sasa ndipo tutakwenda kuanza ziara ya kukutana na vyombo hivyo. Huwezi kuanza tu kukutana nao kabla hujapata taarifa.

Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge Serikali inafanya kwa utaratibu, inatengeneza mikakati kusudi utaratibu huo ukianza kuchukuliwa hatua, hatua hizo ziwe zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu. (Makofi)