Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato (8 total)

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza Chuo cha MUHAS kimedahili wanafunzi wengi sana kiasi kwamba wanafundishwa somo hilo hilo kwa session mbili kwa siku. Je, Serikali inaonaje sasa ikachukua hatua ya haraka sana kuhakikisha kwamba haya majengo ambayo yanamilikiwa na Serikali yakatumika haraka ili wanafunzi wakayatumia ili kuweza kupunguza hiyo changamoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nahato, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba ndiyo maana nikamwambia Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali la msingi uwepo wa majengo yale kule Bagamoyo ni fursa kwake; na sababu mojawapo ni hilo analolisema Mheshimiwa Mbunge kwamba wanafunzi sasa wamerundikana pale Muhimbili na somo lilelile linaingia darasa hilo hilo mara mbili na wanafunzi wa session tofauti, lakini darasa lilelile.

Kwa hiyo, kimsingi tutakwenda kufanya haraka na tutakwenda kushauriana kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023, fedha ziweze kuwekwa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ili kuweza kukarabati majengo yaliyopo Bagamoyo na haya Mlonganzila iweze kutumika ili wanafunzi wa MUHAS waweze kufundishwa kwa wakati mmoja.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba kumuuliza maswali mawili.

Tunafahamu Serikali inaenda kutekeleza Mradi wa High Education for Economic Transformation (HEET); sasa namuuliza swali; je, mradi huo unatarajia kusomesha wahadhiri wangapi?

Je, Serikali inatuhakikisha kuwa Mradi huu wa HEET utapunguza uhaba wa Wahadhiri katika vyuo vikuu kwa kiasi gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Nahato kwa pamoja kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, tumepata mkopo wa jumla ya dola za Kimarekani milioni 425, sawa na shilingi bilioni 972.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi huu, pamoja na mambo mengine utakwenda kuimarisha miundombinu kwenye vyuo vyetu vya Umma karibu 14, vilevile utashughulikia masuala ya Wahadhiri pamoja na watafiti katika nchi yetu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, katika mradi huu tunatarajia kufanya maendelezo ya Wahadhiri wetu katika Vyuo Vikuu wapatao 831, ambapo katika kada ile ya PhD., ambayo tunaita Uzamivu, ni wahadhiri 444 na wale wa Masters yaani Uzamili ni 387.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi, jambo hili tutakwenda kulifanya na kuhakikisha tunataondoa changamoto hii ya wahadhiri katika vyuo vyetu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DKT. PAULINE D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Je, ni lini kutakuwa na usawa wa jinsia katika uongozi wa juu katika Vyuo vyetu Vikuu kwa sababu kwa sasa hivi katika Vyuo Vikuu hakuna usawa wa jinsia kwa uongozi, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Dkt. Nahato kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto sana kwenye usawa wa jinsia kwenye level hiyo ya Vyuo Vikuu na hii ni kutokana tu kwamba wakati tunaendelea na masuala haya ya kusoma, wenzetu hawa wa jinsia ya kike huwa wana drop sana. Lakini nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge jambo hili sasa tunaenda kulizingatia katika taratibu za sasa hivi utumishi maeneo haya ya jinsia yanazingatiwa sana hasa katika mradi wetu ule wa HEET ambao nilizungumza katika kipindi kilichopita, zaidi ya Wahadhiri zaidi ya 600 tunaenda kuwasomesha na miongoni mwao tutaweka ajenda maalum kabisa katika kuhakikisha kwamba jinsia inaweza kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana.(Makofi)
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuhakikisha malimbikizo hayaendelei tena kutokea katika kipindi kijacho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kulipa riba katika malimbikizo ya malipo yaliyochelewa kulipwa kwa Wahadhiri kama inavyofanya kwa wakandarasi wanaochelewa kulipwa malipo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Paulina Nahato, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi, kwamba Serikali hulipa malimbikizo pamoja na stahiki nyingine za watumishi kulingana na bajeti. Kwa hiyo, mkakati wetu kama Serikali jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunaweka bajeti stahiki na toshelezi ili malimbikizo kwanza yasitokee na pili watumishi wanapokuwa na madai yao yaweze kulipwa kwa wakati. Huo ndiyo mkakati wetu kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la pili la riba, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba malipo haya hulipwa kwa mujibu wa kanuni, sheria taratibu na miongozo na kwa kanuni tulizonazo hivi sasa, hazina eneo ambalo linaonesha kwamba malipo yatakapochelewa yalipwe na riba. Kwa hiyo, halipo na badala yake tunasimamia utaratibu wa kawaida ambao ni bila riba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mahabusu kuna wanawake ambao wanakuwa wamewekwa mle wakiwa na matatizo mbalimbali na ni wajawazito, sasa wanajifungua wakiwa bado kesi zao hazijasilikizwa.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha wale watoto wanaozaliwa mama zao wakiwa mahabusu hawapati changamoto za kisaikolojia mama zao wanapokuwa pale ndani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna wakati baadhi ya wafungwa wanakuwa na changamoto, wanakuwa na hali ya ujauzito na kujifungua watoto wakiwa magerezani. Upo utaratibu unaowawezesha wafungwa wa namna hii kupata huduma stahiki ikiwa ni pamoja na hao watoto wanatengwa na kupewa nafasi ya kunyonyeshwa na mama zao kama miongozo ya sekta ya afya inavyoelekeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi juu ya watu hawa kwa sababu taratibu za kuwalinda zipo. Nakushukuru.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Ni nini mkakati wa Serikali wa kujenga mabweni ya wasichana katika shule za sekondari za kata nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, katika shule hizo kumi ambazo mnajenga, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha shule hizo zinafunguliwa ifikapo Julai, mwaka 2023? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI
ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kujenga shule maalum hizi za bweni za wasichana katika kila mkoa katika nchi yetu hii. Hii itaenda kusaidia kupunguza dropout na mimba za utotoni, kwa sababu watoto wote katika mkoa ule wataenda kwenye shule hizi maalum.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, baadhi ya shule hizi ambazo zimejengwa, shilingi bilioni 30 imekwenda katika mikoa kumi kwa maana ya shilingi bilioni tatu kila Mkoa. Tayari baadhi ya shule hizi zimesajiliwa na ifikapo Julai mwaka huu 2023 shule hizi zote kumi zitaanza kupokea wanafunzi wa kike ili kuanza masomo yao ya sayansi katika maeneo hayo ambayo fedha imeshaenda.
MHE. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwapatia mikopo wanafunzi wote wenye ulemavu wa aina yoyote katika vyuo vyetu vikuu kwa 100%?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Nahato kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi sasa kigezo kimoja wapo cha wanafunzi kupata mikopo ni wale wenye ulemavu naomba nimuondoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge watoto wetu vijana wetu wenye ulemavu wanapata mikopo kwa 100% na huo ndiyo mpango wa Serikali.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na jitihada za Serikali kuongeza miundombinu zinazoendelea, bado kuna baadhi ya kozi hazitolewi hapa nchini.

Je, Serikali haioni haja ya kushirikiana na vyuo vingine nchi za nje ili kutoa kozi hizo hasa katika sekta ya afya.

Swali la pili, pamoja na mkakati huu wa miundombinu, Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Wahadhiri katika Vyuo Vikuu hapa nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Pauline Nahato kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza, kwanza tukiri kwamba kuna baadhi ya kozi katika Sekta ya Afya ni kweli hazitolewi hapa nchini. Lakini nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi kifupi tumeweza kupata uzoefu kutokana na janga hili la UVIKO-19 kuna wanafunzi wengi sana walirejeshwa hapa nchini, vilevile kama mnavyofahamu mwezi Februari, Machi mwaka huu kutokana na vita vya Ukraine pamoja na Urusi wanafunzi wengi wameweza kurejeshwa miongoni mwao ni wale ambao walikuwa wanachukua kozi ya ambazo hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza mjadala wa kuangalia namna gani tunaweza kuangalia mashirikiano ya karibu ya kuangalia tunaweza kushirikiana vipi na vyuo vingine vya nje ya nchi ili kozi hizo zinaweza zikatolewa kule kwa ushirikiano vilevile na hapa nchini. Naomba tulibebe wazo hili lakini tubebe ushauri huu wa Mheshimiwa Paulina tuendelee kuufanyia kazi kuweza kuangalia kozi hizi ambazo hazitolewi namna gani tunaweza tukazifanya kwa mashirikiano na vyuo vingine vya nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa eneo la pili la uongezaji wa Wahadhiri, nadhani swali hili nimeshawahi kulijibu hapa Bungeni. Kwanza kupitia mradi wa HEET tunakwenda kusomesha Wahadhiri wapya zaidi ya 1,000. Kwa hiyo, pamoja na uongezaji huu wa miundombinu lakini utakwenda sambamba na kusomesha Wahadhiri katika awamu ya kwanza karibu Wahadhiri 625 tunakwenda kuwasomesha wa kozi ndefu lakini wale kozi fupi zaidi ya Wahadhiri 400. Kwa hiyo, tunaamini tunaweza kupunguza uhitaji huo wa Wahadhiri kwenye vyuo vyetu.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili Serikali mara nyingi sana huwa inatoa vibali vya kuajiri walimu wapya, wahadhiri wapya nao vilevile mfumo huo tutautumia. Lakini vyuoni kule kuna mpango vilevile vyuo vyenyewe huwa vinakuwa na mpango wa kusomesha Wahadhiri na kuajiri wale Wahadhiri wa mikataba ya muda mfupi. Kwa hiyo, mipango hii yote tukiijumuisha tunakwenda kuondoa tatizo hili la Wahadhiri.

Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu Serikali yetu imeweza kuongeza mikopo ile ya elimu ya juu kwa wanafunzi wale ambao wanaoingia katika elimu ya juu, eneo hili kwa vile tutakuwa na udahili mkubwa wa wanafunzi wa elimu ya juu, ni dhahiri kabisa tutaweza kupata wahadhiri wa kutosha kwenye vyuo vyetu hivi ambavyo tunatarajia kuvijenga. Nakushukuru sana.