Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia. Napenda kumshukuru Mungu sana kwasababu ni mara yngu ya kwanza kuwa katika Bunge hili na kuchangia hotuba ya Rais. Hotuba ya Rais hii nimeipitia yote na ni hotuba yenye maono mazuri sana, yenye mwelekeo mzuri, iliyosheheni kila aina ya maendeleo ambao wananchi wowote wangehitaji kuwa nayo katika nchi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amejipambanua katika Afrika kuwa Rais ambaye ni wa peke sana, vyombo vya habari vimekuwa vikimsema sana kwa muda mfupi na haijawahi kutokea kwa Rais kama yeye kusemwa na nchi mbalimbali. Hiyo ni dalili tosha kwamba ameleta mabadiliko ya kutosha na tumeona katika miaka hii mitano akiwa anashughulikia nyanja mbalimbali japokuwa yeye kama alivyokwisha kusema mtu mmoja ni msomi katika eneo moja. Lakini amekuwa mtaalam katika maeneo yote karibu ya nchi yetu hii. Kwa hiyo, pongezi nyingi sana nazitoa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa safari hii pia napenda kumshukuru sana kwa sababu ukiangalia hata baraza lake la Mawaziri wengi tulitegemea, wakati bahasha inaletwa Waziri Mkuu nilijua atarudi yuleyule. Kwa sababu kwa kazi aliyoifanya Mheshimiwa Kassim Majaliwa nilitegemea tu angerudi, na wengine nilijua watarudi na wamerudi kweli. Kwa hiyo, ninamuona kabisa kwamba Rais amewaamini na hata wale ambao wengine wamefanya kazi pamoja naye amewaamini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nichangie suala la elimu. Elimu imetolewa sasa ni bure kuanzia darasa la kwanza mpaka form four na hii imesaidia sana katika kupunguza mambo mengi. Kwa mfano tulikuwa na wasichana wengi waliokuwa wanamaliza darasa la saba, uwezo wa wazazi wao ulikuwa ni wa chini ndio walikuwa wanategemewa kuwa ma-house girl katika sehemu mbalimbali na kwa kweli hawa walikuwa wananyanyasika sana, ma-house girl wengine walikuwa wanapata mishahara midogo na mwisho walikuwa wanaishia tu katika kuhangaika, lakini sasa hivi katika umri huo wa utoto wengi watakuwa shule, kwa hiyo, hayo ni mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile hata upatikanaji wa mimba kwa watoto wa kike utashuka sana kwa sababu umri huo wa watoto wa chini ya miaka 18 watakuwa mashuleni, kwa hiyo, hii elimu bure itakuwa na faida kubwa sana. Lakini vilevile hata vijana wa kiume ambao wengi walikuwa wanajiingiza katika makundi makundi ya kuwa wezi na wadokozi, sasa nao watakuwa shule, kwa hiyo, baadae watakuwa wakubwa na watakuwa ni wa kuwajielewa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni katika upande wa afya, afya pia imeamirika sana kulikuwa kuna changamoto sana ya wananchi hasa ya kinamama kuogopa kwenda hospitali na kwenda kwa waganga wa kienyeji kwenda kupata tiba huko kwa sababu walikuwa wakifika hospitalini walikuwa wanapata changamoto. Lakini kutokana na Chama cha Mapinduzi ambacho kimeongeza hospitali nyingi hadi kufikia katika vijiji sasa imebaki kazi moja kuwahamasisha wananchi wote kuzitumia hizi huduma afya na kubadilisha mtizamo ule wa kuamini maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo pia ninaweza labda nikaiona je, Serikali sasa iweze kujikita katika kuwasaidia wananchi katika kubadilisha mtazamo, kubadilisha mtazamo ni jambo ambalo ni gumu kitu mtu anachokiamini tangu amezaliwa ni ngumu hospitali inaweza ikawepo, dawa zikawepo, wahudumu wakawepo lakini bado mtu asiende kule kwa sababu zake binafsi labda alihaminishwa kwamba hospitali sio sehemu sahihi ya kwenda ukienda kwa mtu fulani ndiyo atakayekuhudumia au hasa katika wazazi unakuta mama mjamzito haendi kwenda kujifungua hospitalini au anakwenda hospitalini baada ya hatua imeshafikia mbaya na mwisho wake ndio vile vifo vichache ambavyo tunavisema wakati ambapo huyu mama kama angeweza kwenda mapema angeweza kupata huduma ambayo ni sahihi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa ni kazi yetu sisi kuweza kuhamasisha wananchi wetu kuanzia chini kabisa kubadili tabia zao ili kuweza kuepuka magonjwa yale ambayo yanaweza kuzuilika na kuzitumia huduma zetu za afya ili waweze kupata afya njema na kuweza kupona magonjwa ambayo yanazuilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitizama katika Dira ya Maendeleo ya 2025 pamoja na masuala mengi ambayo yameongelewa tunazungumzia juu ya elimu bora kwa wasomi wetu wa vyuo vikuu ili tuweze kupata Taifa bora lakini sasa katika elimu hiyo ya vyuo vikuu tunaona kwamba kuna maeneo ambayo tunatakiwa kuyazingatia. Eneo la kwanza ambalo tunatakiwa kuzingatia zaidi ni teknolojia ya ufundishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kabisa kwamba kulingana na idadi ya wanafunzi ambao tunao katika vyuo vikuu vyetu mbalimbali, ili kuweza kuwafikia wanafunzi wote ni lazima teknolojia ya mawasiiliano iboreshwe kwa sababu sio rahisi wanafunzi wote kukaa darasani kwa wakati mmoja. Bado eneo hili la elimu ya masafa marefu halijatiliwa mkazo na mfumo huu kimsingi ungeweza kupunguza gharama hata za ada kwa wanafunzi kwa kuwa wanafunzi hao wanaweza wakasoma hata wanapokuwa sehemu mbalimbali katika mikoa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia upo umuhimu wa kuboresha ufundishaji kwa vitendo. Ukiangalia sasa hivi tumeboresha zaidi kujenga majengo kama mabweni lakini katika ufundishaji wa vitendo, hususan katika fani ya sayansi na teknolojia, Serikali iweke kipaumbele katika kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana katika university zetu zote. Pia ipo haja ya kuhakikisha vyuo vinapanua uwezo wake wa kufundisha wanafunzi kwa kutumia teknolojia na uwezo ambao utaongeza wanafunzi kuwa wengi katika vyuo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna tatizo la motisha kwa wafanyakazi. Wafanyakazi wengi ambao wapo pale hawana motisha. Walimu wengi au wahadhiri hupandishwa madaraja lakini hawalipwi stahiki zao kwa wakati. Unakuta kwamba mtu anajitahidi kufanya utafiti lakini akishapandishwa daraja hapati pesa kwa wakati na hiyo huwafanya kukata tamaa sana hasa katika eneo la utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili linaenda sambamba na kuhakikisha kuwa wale waliopandishwa madaraja wanapata motisha ili uweze kuwasaidia. Mtu anakuwa labda ni Assistant Lecturer amekuwa Lecturer au amepanda cheo amekuwa Profesa unakuta anaitwa Profesa lakini mshahara haujapanda. Kwa hiyo, mimi naishauri Serikali kwamba iweze kuangalia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala ya motisha kwa wafanyakazi, hasa Wahadhiri, ni pamoja na kuangalia masuala ya maeneo wanayoishi kwa mfano hata kupewa allowance za nyumba, allowance za kufanya kazi kwa muda ule wa ziada ili waweze kufanya kazi kwa motisha na madarasa pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloweza kulishauri ni kwamba, sasa hivi Serikali imeongeza wanafunzi wengi sana katika vyuo vyetu na unakuta Mwalimu huyo anafundisha muda mrefu na anaweza akafundisha hata mara tatu kwa sababu wanafunzi wanaingia session tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nafikiri pia liangaliwe zaidi ni katika suala la hili GPA, unakuta kwamba mwanafunzi amemaliza degree yake ya kwanza ana GPA nzuri lakini sasa hapati yale masomo ya kuendelea, anapofika Masters (Shahada ya Uzamili) anatakiwa apate GPA ya 4. Kwa hiyo haya masuala yote yaweze kuangaliwa ili katika elimu ya juu tuweze kutoa wanafunzi ambao ni bora na Walimu nao waweze kuwa katika mazingira mazuri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Ahsante sana.