Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Festo John Dugange (36 total)

MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa Barabara za lami na kufunga taa za barabarani katika Mji wa Mafinga chini ya Mpango wa Uendelezaji Miji nchini?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia mimi na Waheshimiwa Wabunge wote afya njema na kutuwezesha kuwa wawakilishi wa wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa imani kubwa aliyonipa kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe kwa kunichagua na kuchagua mafiga matatu ya Chama cha Mapinduzi na niwahakishie utumishi uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nijibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi,Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (Tanzania Strategic Cities Projects -TSCP) umetekelezwa katika Halmashauri za Majiji ya Tanga, Dodoma, Mbeya, Arusha na Mwanza na Halmashauri za Manispaa za Mtwara- Mikindani, Ilemela na Kigoma-Ujiji kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 355.5 sawa na shilingi bilioni 799.52.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (Urban Local Government Strengthening Programme - ULGSP) umetekelezwa katika Halmashauri za Manispaa za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Iringa, Mpanda, Lindi, Singida, Musoma na Bukoba na Halmashauri za Miji Kibaha, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi na Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Miji ya Kimkakati (TSCP) pamoja na Mradi wa Kuendeleza Miundombinu katika Miji 18 (ULGSP) ilimalizika muda wake Mwezi Desemba, 2020. Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuanza kutekeleza Programu nyingine ya kuendeleza miundombinu itakayohusisha Halmashauri26 zilizokuwepo kwenye Programu zilizomalizika pamoja na Halmashauri nyingine 19 za Miji ikiwemo Mafinga.
MHE.DKT. PINDI H. CHANA Aliuliza:-

Serikali imekuwa ikisaidia sana vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nchini kupitia Halmashauri za Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mifuko hiyo ili kutoa viwango vikubwa zaidi vya mikopo?
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pindi Hazara Chana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato kutokana na vyanzo vya ndani vya halmashauri inatolewa na halmashauri zote nchini kutokana na fedha zilizokusanywa na halmashauri kwa kipindi husika baada ya kutoa vyanzo lindwa kama vile fedha za uchangiaji wa Huduma za Afya, ada za taka na ada za Shule za Sekondari Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha kiwango cha mikopo inayotolewa na halmashauri Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzisimamia halmashauri kutekeleza Sheria ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, kuzijengea uwezo Kamati za Huduma za Mikopo za Kata na Halmashauri ili ziwe na ujuzi wa kutosha wa kuanzisha na kuendeleza vikundi vya wajasiriamali pamoja na ujuzi wa kusimamia utoaji na urejeshwaji wa mikopo, kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanufaika wa mikopo kabla ya utoaji wa mikopo kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na kuzielekeza halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato.
MHE. ANNA R. LUPEMBE Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara za Kata ya Katumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 420.97 ambazo tayari zimeingizwa katika mfumo wa barabara za Wilaya (DROMAS). Aidha, Kata ya Katumba ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 185.88 ambazo ni sawa na asilimia 44 ya mtandao wote.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018 hadi 2019/2020 Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Nsimbo umetumia kiasi cha shilingi milioni
246.08 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na Ikondamoyo – Kalungu. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 81.2 imetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na barabara ya Kituo cha Afya Katumba – Mto Kalungu.

MheshimiwaSpika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara kote nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: -

Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: -

Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Hivyo, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuchangia nguvu hizo za wananchi katika kukamilishaji vituo hivyo ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo kukamilisha maboma ya majengo ya kutolea huduma za afya yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo ujenzi wake ulisimama kwa kukosa fedha. Hadi kufikia Septemba 2020 jumla ya shilingi bilioni 315.31 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mheshmiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya kukamilisha maboma 555 ya zahanati nchini yakiwemo maboma manne (04) katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ili kuunga mkono jitihada za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini michango na nguvu za wananchi na itaendelea kuchangia nguvu za wananchi katika kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI) aliuliza: -

Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba ni Halmashauri mpya iliyotoka Wilaya ya Kilombero: -

(a) Je, ni lini Serikali itaipa Mlimba hadhi ya kuwa Wilaya hasa ikizingatiwa umbali mrefu wa takriban Km 200 ambao Wananchi wanatembea kufuata huduma Makao Makuu ya Wilaya?

(b) Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Halmashauri na kuboresha miundombinu ya barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa miongozo na taratibu, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala unahusisha uhitaji wa wananchi, Viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao huwasilisha maombi ya mapendekezo yao kwenye vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa hatua zaidi. Ofisi ya Rais-TAMISEMI, haijapokea maombi rasmi ya Mkoa wa Morogoro kuomba Mlimba kuwa Wilaya. Serikali inashauri utaratibu huu uliowekwa ufuatwe.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Mwezi Januari mwaka huu, Serikali imekwisha peleka kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi wa jengo hilo la utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa miundombinu ya barabara, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020, Serikali imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 54, imejenga kalvati 22 na madaraja manne (4) kwa gharama ya shilingi milioni 545.87. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia TARURA imetenga kiasi cha shilingi milioni 517.56 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA) Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatengeneza eneo la Katokoro linalounganisha Kata za Katoro na Kyamulaile katika Jimbo la Bukoba Vijijini ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

MheshimiwaSpika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo korofi la Katokoro ambalo limejaa maji lina urefu wa kilomita 5 ambayo ni sehemu ya barabara ya Katoro – Kyamulaile – Kashaba yenye jumla yakilomita 15.7 inayounganisha Kata za Katoro, Kyamulaile na Ruhunga. Aidha, barabara hiyo pia inaunganisha maeneo mbalimbali ya Halmashauriya Wilaya ya Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanya usanifu kwa ajili ya kuboresha eneo hilo korofi ambapo kiasi cha fedha shilingi milioni 572 kinahitajika kunyanyua tuta la barabara na kujenga makalvati.

Mheshimiwa Spika, ili kupata ufumbuzi kwa sasa katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 87 kwa ajili ya kurekebisha eneo korofi katika barabara hiyo. Hata hivyo, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkandarasi aliyekuwa anafanya kazi hiyo alisimamishwa kutokana na eneo hilo kujaa maji.

Mheshimiwa Spika, wakati jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa barabara hiyo zikiendelea, mara maji yatakapopungua, mara moja Serikali itamrejesha kazini mkandarasi huyo ili kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.
MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020, Serikali imejenga Hospitali 101 za Halmashauri na kuongeza idadi ya Hospitali za Halmashauri kutoka Hospitali 77 zilizokuwepo mwaka 2015 hadi Hospitali 178 Septemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kigezo muhimu kwa Halmashauri kupata fedha za ujenzi ilikuwa ni kuandaa eneo la ujenzi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ilikosa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri kwa kuwa hadi wakati wa tathimini ya Halmashauri zilizotenga maeneo ya ujenzi, Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga ilikuwa haijapata eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 27 mpya nchini. Aidha, kwa kuwa sasa tayari Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga imebainisha eneo la ujenzi, Serikali itaipa kipaumbele sambamba na Halmashauri nyingine ambazo hazina Hospitali za Halmashauri kwenye awamu zinazofuata kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA Aliuliza:-

Je ni lini Serikali itajenga chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2019/2020, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya halmashauri. Majengo yaliyohusika katika awamu ya kwanza ni jengo la wagonjwa wa nje na maabara. Ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 60.5 ambapo kiasi cha shilingi 33.5 ni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali za halmashauri 67 nchini na kiasi cha shilingi bilioni 27 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 mpya ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe inaelekezwa pamoja na majengo mengine, kujenga jengo la kuhifadhia maiti pindi itakapopokea fedha za ujenzi kwa kuwa tayari ina majengo mawili kati ya majengo saba yanayotakiwa kujengwa na hivyo fedha iliyotengwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 itakuwa sehemu ya fedha ya kujenga jengo la kuhifadhia maiti.
MHE. JAFARI W. CHEGE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Mto Mori kwani mto huo umekuwa ukisomba watu na kusababisha vifo kwa wananchi wanaofuata huduma upande wa pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Mori unakatisha katika barabara ya Kirogo-Nyamaguku yenye urefu wa kilomita 15, ikiunganisha Tarafa za Luo-imbo, Suba na Nyancha katika Wilaya ya Rorya. Barabara hii ilifunguliwa mwaka 2008 kwa nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto huu umegawanyika katika matawi mawili ambayo ni Mto Mori Mkuu wenye upana wa mita 43 na Wamala wenye upana wa mita 16 ambapo madaraja mawili (2) yanahitajika kujengwa. Hivyo, kwa sasa, barabara hii haipitiki kutokana na kutokuwepo kwa madaraja hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imewasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, maombi maalum ya Shilingi bilioni 1.54 ambayo ni makisio kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika Mto Mori na matengenezo ya kawaida katika Barabara ya Nyamaguku- Kirogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itatenga fedha kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya usanifu wa madaraja mawili ya Mto Mori ili kufahamu mahitaji na gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo na kisha kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Aidha, ujenzi wa madaraja na miundombinu ya barabara hizi utatekelezwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ASIA A. HALAMGA Aliuliza:-

Ni Halmashauri ngapi nchi zimetekeleza kwa asilimia 100 sheria ya utoaji mikopo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani kwa makundi ya vijana, akinamama na watu wenye mahitaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu zilizopo hali ya utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri nchini imeimarika hasa baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 yaliyofanyika Julai, 2018 kwa kuongeza Kifungu cha 37A kuhusu Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Mheshimwa Naibu Spika, tangu kuanza kutumika kwa Sheria hii mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020 Halmashauri 79 zimetoa mikopo kwa asilimia 100 na Halmashauri 54 zimetekeleza kwa asilimia zaidi ya 85.

Mheshimwa Naibu Spika, utekelezaji wa shughuli hizi za mikopo umewezesha kuongezeka kwa mikopo inayotolewa na halmashauri nchini ikilinganishwa na kipindi kabla ya kufanya marekebisho ya sheria. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 (kabla ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 26.1 zilitolewa; mwaka wa fedha 2018/2019 (baada ya marekebisho ya sheria) shilingi bilioni 42.06 zilitolewa; na mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya mikopo iliyotolewa ilikuwa ni shilingi bilioni 40.7 zilitolewa.

Mheshimwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kifungu namba cha 24(2) cha Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu za mwaka 2019, Mkurugenzi yeyote ambaye atashindwa kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu inaweza, kwa kadri itakavyoona inafaa, kumchukulia hatua za kinidhamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba kutoa rai kwa Wakurugenzi wote nchini kote kuhakikisha kwamba wanazingatia takwa hilo la kisheria.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. SILVESTRY F. KOKA) Aliuliza:-

Miundombinu ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha ilijengwa miaka 50 iliyopita kwa kutumia mabomba ya Asbestos ambayo siyo rafiki kwa afya za binadamu, lakini pia ni chakavu sana:-

(a) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji katika shirika hilo?

(b) Je, ni lini Serikali itakarabati majengo ya Chuo cha FDC katika Shirika hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya maji katika Shirika la Elimu Kibaha inayotokana na miundombinu mibovu na ya muda mrefu ambayo ni kutokana na uwepo wa mabomba ya maji ya kipenyo cha milimita 200 yenye urefu wa kilomita nne na kipenyo cha milimita 150 yenye urefu wa kilomita mbili yaliyojengwa kwa asbestos tangu kuanzishwa kwa Shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali ilikwishabadilisha bomba la asbestos lenye urefu wa kilomita 0.75 la kipenyo cha milimita 200 na bomba lenye urefu wa kilomita moja na kipenyo cha milimita 150 kuwa PVC. Serikali itaendelea kubadilisha mabomba hayo kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Shirika linaendelea kufanya matengenezo madogo madogo kwa kutumia mapato ya ndani pindi uharibifu unapotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa shirika hili, imekamilisha ukarabati wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.6. Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Shirika la Elimu Kibaha ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.48 kinahitajika ili kufanya matengenezo. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati. Hata hivyo, Shirika la Elimu Kibaha lilifanya ukarabati mdogo wa madarasa na jengo la utawala kwa kutumia mapato ya ndani ambao uligharimu shilingi milioni 25.73.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Pangani umekatisha kwenye kipande cha barabara ya Same – Ruvu – Mferejini chenye urefu wa kilomita 34.2. Barabara hiyo inaunganisha Kata za Same na Ruvu katika Wilaya ya Same na sehemu ya mto inayopendekezwa kujengwa daraja ina upana wa mita 70. Sehemu hii haipitiki kwa sasa kutokana na kukosekana kwa daraja la kuunganisha Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekuwa ikikihudumia kipande cha barabara hiyo kwa kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni 48 kilitumika. Aidha, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 63 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ambapo kwa sasa mkandarasi anaendelea na matengenezo ya kipande cha kilomita 7.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya usanifu wa daraja ikiwa ni pamoja na kipande cha barabara yenye urefu wa kilomita 34.2 kwa upande wa Same hadi kufikia eneo la Mto Pangani panapohitajika kujengwa daraja ili kuunganisha Wilaya za Same na Simanjiro. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa daraja na miundombinu ya barabara hiyo muhimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA Aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Newala ina Kata 22 na Vijiji 107, lakini ina Vituo vya Afya vitatu tu, kati ya 22 vinavyohitajika.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga Vituo vipya vya Afya katika Halmashauri ya Newala ili kuboresha huduma za Afya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Kuanzia mwaka 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imejenga Zahanati 1,198; imejenga na kukarabati Vituo vya Afya 487 na imejenga Hospitali za Halmashauri102.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 na 2019/2020, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kiasi cha Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 400 kwa ajili kufanya ukarabati wa Kituo cha Afya Kitangari. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni moja (1) kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri na Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. GRACE V. TENDEGA Aliuliza:-

Akina mama wajawazito wamekuwa wakitozwa fedha kuanzia shilingi 50,000/= hadi 70,000/= wasipojifungulia katika Vituo vya Afya hasa katika Jimbo la Kalenga; huku vituo hivyo vikiwa mbali na maeneo wanayoishi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga maeneo ya kusubiri kujifungua katika Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, majengo ya wajawazito kujisubiria yanalenga kupunguza umbali kwa wajawazito kufika kwenye vituo vya huduma za afya pindi wanapokaribia kujifungua. Lengo likiwa ni kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyosababishwa na umbali kutoka katika vituo vya kutolea huduma.

Meshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hii, Serikali imeendelea kujenga vituo vya huduma za afya kote nchini na kujenga Hospitali za Halmashauri 102, Vituo vya Afya 487 na Zahanati 1,198 katika kipindi cha Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 67; shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali 67 za Halmashauri na shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya za Halmashauri. Kiasi cha shilingi bilioni 27.5 pia kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati 555.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya nchini kote, umepunguza umbali kwa wananchi kuvifikia vituo vya huduma za afya na hivyo viashiria vya huduma na vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 11,000 mwaka 2015 hadi 3,000 mwaka 2020. Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya huduma za afya kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU K.n.y. MHE. SIMON S. LUSENGEKILE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa katika Hospitali ya Wilaya ya Busega ili huduma bora za afya ziendelee kutolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ni miongoni mwa hospitali 67 za Halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka 2018/2019 kwa kupewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ambayo ni jengo la utawala, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la wazazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhia dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.

Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.
MHE. ZAYTUN S. SWAI Aliuliza:-

Kutokana na changamoto za vyanzo vya mapato hususan katika Halmashauri zilizo nje ya miji kumekuwa na uwiano usio sawa wa utoaji wa mikopo.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta njia ya kuweka uwiano sawa wa mikopo hiyo bila kujali mapato ya Halmashauri husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kwa kuzingatia kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019. Halmashauri inatakiwa kutenga na kutoa asilimia 10 ya fedha za makusanyo ya ndani katika kipindi husika kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya kuondoa vyanzo lindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa sheria hii ni asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kwenye Halmashauri husika ambayo yanatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine kutokana na fursa zilizopo. Hivyo, kiwango cha mikopo inayotolewa kinategemea uwezo wa makusanyo wa Halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka hususan baada ya kuwepo kwa sheria ambapo mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 42.06 mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo Serikali inatambua changamoto zinazotokana na utaratibu huu na itaendelea kuuboresha ili kuongeza tija na kufikia malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hii.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY) Aliuliza:-

Mwaka 2015 Serikali ilitangaza kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Mbulu Wilaya na Mbulu Mji walipitisha rasmi mgawanyo wa rasilimali na madeni.

Je, ni lini Serikali itarejesha tamko la mapendekezo hayo ili kufanikisha maendeleo ya mambo yaliyopendekezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji Mbulu waliridhia na kupitisha mgawanyo wa rasilimali na madeni na kuwasilisha mgawanyo huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Tarehe 9 Novemba, 2018 mgawanyo wa mali na madeni ya Halmashauri hizo ulitolewa na Waziri mwenye dhamana na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Toleo Namba 45 la mwaka 2018 pamoja na mgawanyo wa mali na madeni wa Halmashauri nyingine 42 kupitia Tangazo la Serikali Namba 696 la mwaka 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa rasilimali watu, magari, pikipiki, rasilimali na madeni umefanyika kwa asilimia 100 kwa kuzingatia Mwongozo wa Ugawaji wa Mali na Madeni ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wa mwaka 2014. Katika mgawanyo huo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu (Halmashauri mama) ilipata asilimia 60 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipata asilimia 40.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Magu kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imeendelea na ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri 100 ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambazo kwa ujumla zimegharimu kiasi cha shilingi bilioni 147.33.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Magu ambalo litagharimu shilingi bilioni tano hadi kukamilika. Hadi mwezi Februari 2021, Serikali ilikuwa imekwishatoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo ambalo tayari limeezekwa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 750 kwa ajili ya kuendelea na hatua ya ukamilishaji wa jengo hilo.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya kisasa Mkoani Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Hospitali za kisasa za Halmashauri na za Rufaa za Mikoa ili kuboresha huduma za afya za rufaa katika ngazi hizo. Kupitia mpango huo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro itakarabatiwa na kupanuliwa. Mpango huo utahusika ujenzi wa jengo la kisasa la wagonjwa wa nje, jengo la kutolea huduma za dharura, jengo la huduma za uchunguzi wa mionzi na maabara, matibabu ya viungo, huduma za famasia, utawala pamoja na Wodi Maalum (Private Wards).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa eneo ilipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa sasa ni dogo, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro inakamilisha taratibu za umiliki wa eneo lenye ukubwa wa ekari 100 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi katika Mkoa wa Morogoro, Serikali imejenga Hospitali tano za Halmashauri ya Malinyi, Gairo, Morogoro, Mvomero na Kilombero kwa gharama ya shilingi bilioni 7.5 katika kipindi cha Juni, 2016 hadi Juni, 2020. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ya Mlimba na Mvomero. Aidha, shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa wodi tatu katika Halmashauri za Wilaya za Malinyi, Gairo na Morogoro.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali ya Wilaya ya Olturumet katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwa kuipatia jengo la OPD, Wodi ya kulaza Wagonjwa, Jengo la X-Ray na mashine ya X-Ray ili Hospitali hiyo iweze kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemberis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Olturumet Arusha, ambazo zinahitaji ukarabati na upanuzi wa miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Ukarabati wa Hospitali kongwe 43 nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa Hospitali 21 za Halmashauri nchini. Mpango huo utaendelea kutekelezwa kwa awamu hadi ukarabati na upanuzi wa hospitali kongwe zote nchini utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge Noah kuwa Hospitali ya Wilaya ya Olturumet Arusha ni miongoni mwa hospitali ambazo zitafanyiwa ukarabati na upanuzi.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA Aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi na vifaa muhimu kwenye hospitali inayojengwa katika Mji wa Tunduma ili ianze kufanya kazi mapema?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza madaktari na wakunga pamoja na kuongeza bajeti katika Kituo cha Afya cha Tunduma ili kukidhi mahitaji ya kituo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa tangu Mheshimiwa Rais aliponipa dhamana ya kumsaidia kama Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini nimuahidi kwamba nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Tunduma ambayo ilianza kujengwa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Ujenzi wa awamu ya kwanza unahusisha jengo la ghorofa moja lenye sehemu tisa za huduma mbalimbali za OPD ambalo limetumia shilingi bilioni nne ambalo hadi Machi, 2021 ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kuidhinishiwa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Baada ya kukamilisha ujenzi huo Serikali itapeleka watumishi na huduma za OPD zitaanza kutolewa. Serikali imeshawapanga madaktari wawili katika hospitali hii ambao kwa sasa wanaendelea kutoa huduma kwenye Kituo cha Afya Tunduma wakisubiri kukamilika kwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Tunduma kina jumla ya watumishi 74 kati ya watumishi 52 wanaohitajika katika ngazi ya kituo cha afya na hivyo kuwa na ziada ya watumishi 22. Idadi ya watumishi waliozidi inatokana na kituo hiki kutumika kama Hospitali ya Mji wa Tunduma. Hivyo, watumishi hawa watahamishiwa katika hospitali mpya ya mji mara itakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itaomba kuindhinishiwa shilingi milioni 409 kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika Kituo cha Afya cha Tunduma ambalo ni ongezeko la shilingi milioni 84 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi milioni 325 iliyoidhinishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa kimkakakti wa machinjio Iringa Ngelewala ili kuwekezaji huo uanze kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilianza ujenzi wa machinjio ya Ngelewala katika mwaka wa fedha 2008/2009. Hadi Juni, 2018 kiasi cha shilingi milioni 928.99 kilikuwa kimetumika ikiwemo shilingi milioni 550 kutoka Serikali Kuu, shilingi milioni 108 mapato ya ndani ya Halmashauri, shilingi milioni 101 kupitia programu ya kuendeleza kilimo nchini ASDP na shilingi milioni 169 kutoka UNIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 mradi huu ulijumuishwa kwenye miradi ya kimkakati ya Halmashauri inayotekelezwa ili kuziongezea Halmashauri uwezo wa kutoa huduma na kukusanya mapato. Miundombinu ambayo tayari imejengwa ni pamoja na mabwawa ya maji machafu (oxidation ponds), zizi la kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa, shimo la kutupa nyama isiyofaa kuliwa na binadamu, jengo la utawala, uzio eneo la shughuli za dobi, kichomea taka, maabara na jengo la kubadilishia mavazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mradi kukamilika kwa kujenga miundombinu yote, utagharimu shilingi bilioni 1.147. Mkandarasi anaendelea na ujenzi na anatarajiwa kukamilisha mradi ifikapo tarehe 1 Agosti, 2021.
MHE. KENNETH E. NOLLO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa GoTHOMIS kwenye zahanati kama ilivyo kwenye vituo vya afya ili kuondoa mwanya wa upotevu wa mapato?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfumo wa Kieletroniki wa Uendeshaji wa Huduma za Afya (Government of Tanzania Health Operations Management Information System - (GoTHOMIS) ni mfumo wa usimamizi wa uendeshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kukusanya taarifa za wagonjwa na magonjwa, taarifa za malipo ya matibabu, taarifa za madawa na vifaa tiba na taarifa za huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu ulianzishwa mwaka 2016 na kuanza kusimikwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote. Mfumo umeboreshwa na kuunganishwa na mifumo mingine kama Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG), mfumo wa NHIF kwa ajili ya usimamizi wa madai na mfumo wa Kuomba Madawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (ELMIS).

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Februari 2021, Mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika vituo vya kutolea huduma 921, ikiwa ni hospitali 21 za mikoa, hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za wilaya 22, vituo vya afya 385 na zahanati 411. Kazi ya kusimika mfumo huu katika vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote nchini inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri zimekuwa zikitumia vyanzo vyake vya ndani kusimika mtandao kiwambo na kununua vifaa vingine zikiwemo kompyuta na wataalam wa halmashauri kushirikiana na wataalam wa mikoa katika kusimika mifumo hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya vituo vilivyofungiwa Mfumo wa GoTHOMIS na ambavyo vina miundombinu wezeshi kama mawasiliano ya internet vinatumia moja kwa moja Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) na hivyo kuwezesha wapewa huduma kulipa moja kwa moja benki au kupitia mitandao ya simu na hivyo kuwezesha makusanyo ya vituo kuongezeka na kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufungaji wa mifumo huu utaendelea kutekelezwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati au kujenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa kwa kuwa Hospitali iliyopo ni ya muda mrefu na miundombinu yake ni chakavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa hospitali kongwe na chakavu katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 102 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kuwa, bado kuna Halmashauri 28 zisizo na Hospitali ya Halmashauri, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 14 ili kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka kipaumbele kwa kuanza ujenzi katika Halmashauri hizo na baada ya hapo ukarabati wa Hospitali chakavu ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa utafanyika. Ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha uanzishwaji wa hati fungani za Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/22 Waziri wa Fedha na Mipango aliwasilisha kuhusu kuanzisha hati fungani za Halmashauri. Kifungu cha 92 ya hotuba yake ilieleza, katika jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya mapato rasilimali fedha Serikali itaangalia uwezekano wa kutumia hati fungani zitakazotolewa na Halmashauri za Manispaa na Majiji kama njia mbadala ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, hatua hii itapunguza mzigo kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali hasa kwa Halmashauri zenye miradi ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa na uhakika wa uwezo wa miradi hii kurejesha kwa faida kwa maana ya bankable projects.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund – UNCDF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (Capital Markets and Securities Authority- CMSA) imeanza mchakato wa kupitia miradi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji yatakayokidhi vigezo na masharti ya matumizi ya hati fungani yanaanza kutumia utaratibu huu katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapima maeneo yote ya umma ikiwemo Shule, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kutumia Sheria Na. 4 na Na. 5 ili kuondokana na matatizo ya migogoro ya mipaka kwa Wananchi, lakini pia kuondokana na hoja za ukaguzi ambazo zaidi ya asilimia 90 ya Halmashauri wanazipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa baadhi ya maeneo ya umma yaliyoainishwa na kutengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali za umma zinazotolewa na Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa hayajapimwa na kuwekewa alama zinazoonekana kwa urahisi. Hali hii husababisha migogoro ya mara kwa mara ya ardhi na uvamizi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kupima maeneo yote ya taasisi za umma zilizo chini ya mamlaka hizo; ikiwa ni pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuepusha migogoro ya ardhi na kuzuia uvamizi unaofanywa na baadhi ya wananchi. Serikali ilishatoa maelekezo haya kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; hivyo nitumie fursa hii kuzisisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga fedha na kutekeleza maelekezo hayo. Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kutatua migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi wa Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba kumekuwa na migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji katika kilimo na wananchi katika Kata za Kapele, Ndalamo, Ikama, Nzoka, Msanyani na Kamsamba. Migogoro hii imetokana na uuzaji holela wa ardhi uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji katika kata hizo.

Mheshimiwa Spika, ili kutatua migogoro hiyo, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Momba imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 38. Kati ya migogoro hiyo, migogoro 34 tayari imetatuliwa na migogoro minne ipo katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu rasmi wa kisheria katika uuzaji na ukodishaji ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wawekezaji na wananchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU Aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi na Vitendea kazi vya kutosha katika Zahanati mpya 24 zilizojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita?

(b) Je, ni lini Serikali itadhibiti upotevu wa mapato katika Zahanati, Vituo vya Afya hadi Hospitali za Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu Mbunge wa Geita Mjini lenye sehemu (a) and (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Geita ina jumla ya watumishi 162 wa kada mbalimbali ya afya na upungufu wa watumishi 469. Mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali iliajiri watumishi 2,726 na kupanga katika vituo vilivyokuwa na upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 halmashauri imeomba jumla ya watumishi 126. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya katika kuendelea kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi, ikiwemo watumishi kwenye Halmashauri ya Mji Geita.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhibiti upotevu wa mapato kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambapo hadi Februari 2021, mfumo wa GoTHOMIS umesimikwa katika hospitali 21 za Mikoa, Hospitali 82 za halmashauri, hospitali teule za Wilaya 22, Vituo vya Afya 385 na zahanati 411. Aidha hatua za kinidhamu na kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa watumishi wanaothibitika kuhusika na upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji Geita inaendelea kufunga mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Afya na fedha ili kuboresha ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea huduma za afya, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi milioni 28.2 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa Mfumo wa ukusanyaji wa mapato (GoTHoMIS) katika Zahanati 11 kati ya Zahanati 13 zilizopo ambazo hazina Mfumo wa GOT- HOMIS. Hospitali ya Geita pamoja na Vituo viwili vya Afya vilivyopo tayari vimefungwa mfumo wa GoTHOMIS. Ahsante sana.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Hayati Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais wa sasa na Waziri Mkuu ya kujenga Kituo cha Afya Kata ya Murungu katika Wilaya ya Kibondo ili kusogeza huduma na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Jimbo la Muhambwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati Vituo vya Kutolea huduma za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa Huduma za Afya ya Msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati wa huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza mkakati huu, Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 25.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Tarafa 90 zisizo na Vituo vya Afya ikiwemo Tarafa ya Kibondo Mjini inayoundwa na Kata tisa za Murungu, Bunyambo, Kibondo Mjini, Biturana, Kumwambu, Kitahana, Rusohoko, Misezero na Bitare ambapo kiasi cha shilingi milioni 250 kimepelekwa kwa jili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Bunyambo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mkakati huu, Serikali, itaendelea kutoa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi zote za Viongozi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa Jengo la Manispaa ya Tabora ambao umesimama kwa muda mrefu sasa huku shughuli za Manispaa zikiendelea kufanyika kwenye majengo ya zamani yaliyochakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mhesimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa baadhi ya halmashauri nchini ambazo hazina majengo ya utawala na uwepo wa majengo chakavu. Serikali kwa kutambua hilo, inaendelea na ujenzi wa majengo ya utawala ya Halmashauri 100 nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa Tabora kwa kutumia mapato ya ndani, mwaka 2015 ilianza kujenga jengo la utawala la ghorofa nne ambalo lilikadiriwa kugharimu kiasi cha shilling bilioni 5.7 mpaka litakapokamilika. Ujenzi wa awamu ya kwanza unaohusisha boma la jengo hilo umekamilika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja ili kuendeleza ujenzi wa jengo hilo ambapo ujenzi wa awamu ya pili utatumia utaratibu wa force account ili kupunguza gharama za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, imeelekezwa kukamilisha taratibu za kuwasilisha maombi ya fedha za ujenzi huo Wizara ya fedha na Mipango ili ujenzi uanze mara moja.

Mheshimiwa Spika, aidha, halmasahuri imeelekezwa kuanza ukamilishaji wa baadhi ya maeneo ya jengo hilo ili watumishi waweze kupata ofisi wakati ukamilishaji ukiendelea.
MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. MOHAMED L. MONNI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga stendi katika Mji wa Chemba ambao unakuwa kwa kasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Wilaya ya Chemba kuwa na kituo cha kisasa cha mabasi. Kwa umuhimu huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga eneo la ekari 22 kwa ajili ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi katika Mji wa Chemba ambayo imekadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 643.8 mpaka kukamilika kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi milioni 37 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo ambapo ujenzi wa vyoo na ofisi za muda umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni saba ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma za stendi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 16 ili kuendeleza ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati unahusisha andiko maalum la mradi linaloandaliwa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kufuata utaratibu huo ili Serikali itafute fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Ahsante sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI Aliuliza: -

Serikali ilichukua eneo la Mlima Nkongore ambao ndani yake kulikuwa na makazi ya wananchi na kuliwekea beacon na kusababisha kaya zaidi ya 10 zilizochukuliwa maeneo hayo kuishi kwa hofu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzilipa fidia Kaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mlima Nkongore uliopo katika Halmashauri ya Mji Tarime una eneo lenye ukubwa wa ekari 266.65. Wananchi wanaozunguka eneo hilo walikuwa wakiutumia Mlima Nkongore kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukataji kuni, uchomaji mkaa na kilimo kinyume na taratibu za Mamlaka ya Upangaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Mlima Nkongore ni moja ya eneo lililokuwa limekithiri kwa shughuli haramu ikiwemo kilimo cha bangi. Hivyo, mwezi Novemba, 2017 Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime ilikabidhi eneo hilo kwa Jeshi la Magereza ili kuhakikisha kuwa eneo hilo linalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004 kifungu cha 58(1) na (2) ambacho kinazuia kufanya shughuli zozote zinazoweza kusababisha hifadhi ya mlima kuharibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira inakamilisha taratibu za kulifanya eneo la Mlima Nkongore kuwa hifadhi. Hivyo, eneo la Mlima Nkongore litaendelea kuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Magereza hadi taratibu zitakapokamilika na kulitangaza kuwa eneo la hifadhi, ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya shilingi milioni 400 aliyoahidi Waziri Mkuu kuchangia katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasekese kinachojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Serikali kuchangia shilingi milioni 400 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasekese imetekelezwa, ambapo fedha hizo zimepelekwa kwenye Kata ya Kasekese tarehe 25/8/2021 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, majengo manne yanatarajiwa kujengwa, ambayo ni jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo na nyumba ya mtumishi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje la Kituo cha Afya Kasekese umekamilika kwa gharama ya shilingi 164.9 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wenye Viwanja eneo la Miganga West na East, Kata ya Mkonze katika Manispaa ya Jiji la Dodoma kwa kuwa uthamini ulishafanywa na baadhi ya Wananchi bado hawajalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifauatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Miganga West na East katika Kata ya Mkonze ni miongoni mwa maeneo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo yamepangwa, kupimwa viwanja na kumilikishwa kwa wananchi ili waviendeleze kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Mji Mkuu (Master Plan).

Mheshimiwa Spika, kufuatia uwepo wa miradi ya kimkakati wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV kutoka Chalinze hadi Zuzu inayotekelezwa na Serikali kupita katika eneo hili na kuathiri viwanja vilivyomilikishwa, imelazimu eneo hilo kutwaliwa chini ya Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya Mwaka 1967, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, Kanuni za Ardhi za Mwaka 2001, Miongozo ya Uthamini na Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Na. 7 ya Mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya uthamini kwenye jumla ya viwanja 309 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.77 vilivyoathiriwa na mradi wa reli ya kisasa ambapo kiasi cha shilingi milioni 576.5 imeshalipwa kwa wananchi ikiwa ni fidia ya viwanja 231. Viwaja 78 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 vinaendelea kuhakikiwa na Ofisi ya Mthamini Mkuu ili kukamilisha taratibu za fidia zao kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeshafanya uthamini kwenye viwanja 123 na makaburi manne vyenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1.1 vilivyoathiriwa na mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao viwanja vyao vimeathirika na mradi huo, watalipwa fidia mara baada ya Mthamini Mkuu kukamilisha taratibu za kisheria. Ahsante sana.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Makete katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2014/ 2015 Halmashauri ilianza ujenzi kwa gharama ya shilingi milioni 40; na katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Halmashauri imepanga kutenga fedha kwenye mapato ya ndani ili kuendelea na ujenzi wa kituo hicho

Mheshimiwa Spika, Serikali inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Makete kufanya tathimini ya ujenzi wa kituo cha mabasi na kuandaa andiko ili kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya ujenzi. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatafuta mkakati wa kudumu wa kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Lindi kumekuwa na ongezeko la migogoro ya wakulima na wafugaji, hususan katika Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale. Migogoro hii imetokana na ongezeko la mifugo ambapo kumeongeza uhitaji wa nyanda za malisho na maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 19, ambapo jumla ya migogoro 12 imetatuliwa na migogoro saba iko katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretariati ya Mkoa wa Lindi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 81, na kuunda kamati ya utatuzi wa migogoro kwa kila halmashauri ili kuwahamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwa kuendeleza ranch ndogondogo, na kila halmashauri kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vitano kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Halmashuri za Mkoa wa Lindi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 279.22 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 15, ikiwa ni hatua za utatuzi wa migogoro hiyo. Ahsante.