Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Festo John Dugange (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango mingi na muhimu sana ambayo wameitoa katika mjadala wa bajeti hii na kwa muktadha huu katika eneo la TARURA na afya.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa muhtasari niweze kupita kwenye hoja mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa. Kwanza kwa takriban asilimia 99 ya wachangiaji wamegusa TARURA, wametoa ushauri na michango mingi sana muhimu ya kuhakikisha kwamba tunaiwezesha TARURA kutenda kazi kwa ufanisi mkubwa unaotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua sana kwamba tuna changamoto kubwa ya barabara zetu zinazohudumiwa na TARURA, lakini uhitaji mkubwa wa madaraja na makalvati, lakini inatambua kwamba pia tuna tatizo la changamoto ya bajeti ya TARURA. Serikali imeendelea kuweka jitihada za kuhakikisha kwamba tunaboresha sana bajeti ya TARURA kuiwezesha kuhudumia mtandao wa barabara ambao inahudumia. Kwa mwaka wa fedha uliopita shilingi bilioni 275 zilitengwa ikilinganishwa na shilingi bilioni 578 za mwaka wa fedha ambao tunaelekea, ongezeko la bajeti ya TARURA kwa zaidi ya mara mbili na nusu. Kwa hiyo hii ni dalili kwamba Serikali inatambua sana umuhimu wa kuiwezesha TARURA.

Mheshimiwa Spika, tunapokea mawazo na michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wametoa kuhusiana na kuboresha vyanzo vya mapato kwa maana ya simu, mafuta, lakini na maeneo mengine. Serikali itaendelea kuyafanyia tathmini na kuona njia bora zaidi ya kuongeza bajeti ya TARURA ili kuiwezesha kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana suala la kuona namna ambavyo vyanzo vya ndani vya halmashauri vitachangia ujenzi wa barabara kupitia TARURA na Serikali itatoa mwongozo kwa Majiji na Manispaa kuanza kutenga fedha kwa ajili ya kuchangia nguvu za TARURA kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa nguvu ni kuhusiana na vigezo vinavyotumika katika mgao wa fedha za TARURA katika halmashauri. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali inatambua kwamba halmashauri zetu zinatofautiana kwenye ukubwa wa maeneo na hivyo mtandao wa barabara, lakini hali za kijiografia, milima, tambarare na mvua. Hivyo, katika kuweka vigezo hivi, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itapitia vigezo hivi, kwa sababu vigezo na mgao uliowekwa awali ulizingatia zile barabara za kilomita elfu 56 na sasa tunakwenda 108,000 na hadi 144,000. Kwa hiyo niwahakikishie kwamba hii itapitiwa vizuri na itakwenda vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna hoja ya kuthibitisha Mameneja wa TARURA na ni kweli kama tunavyofahamu TARURA haina muda mrefu tangu imeanza na taratibu hizi za uteuzi wa viongozi wa Serikali kuna hatua mbalimbali zikiwemo za upekuzi kwa maana ya vetting. Niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imeendelea kufanya kazi hiyo na sasa imeshawafanyia vetting kwa maana ya upekuzi watendaji 111 kati ya 126, sawa na 88% na hawa hatua za kiutumishi za kuwathibitisha zitaendelea na zoezi hili ni endelevu.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni suala la miradi hii kuchelewa kuanza na barabara mara nyingine kujengwa wakati wa msimu wa mvua. Serikali imeboresha sana utaratibu wa kupata zabuni kwa njia ya kielektroniki kwa maana TANePS. Katika mwaka wa fedha ujao tunatarajia miradi hii yote itatangazwa mapema, wazabuni watapatikana kwa wakati na barabara zitaanza kujengwa na kukarabatiwa kwa wakati na si wakati wa mvua.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili, maeneo ya madaraja na makalvati yamesisitizwa sana na Serikali imekwishatambua jumla ya madaraja 3,182 nchini kote, lakini pia makalvati 62,817 na imeweka mkakati ambao tutahakikisha labda kila baada ya mwaka wa fedha tunakwenda kutengeneza madaraja robo na makalvati pamoja na barabara za udongo kwenda changarawe.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la TARURA kwa ujumla wake Serikali itaendelea kuimarisha sana uwezo wa TARURA lakini pia kuuboresha sana mfumo wa utendaji wa TARURA ili kuhakikisha kwamba barabara zetu zinaboreshwa.

Mheshimiwa Spika, niende eneo la afya katika eneo hili Waheshimiwa Wabunge wamepongeza sana kazi kubwa ya Serikali ya kujenga na kukarabati miundombinu, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Sisi kama Serikali tunaendelea na tunatambua kweli pamoja na kazi kubwa bado tuna mahitaji makubwa ya vituo vya afya na ndiyo maana katika mwaka wa fedha ujao, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Afya ametangulia kusema hospitali mpya 28 zimetengewa shilingi bilioni 14 zitaanza ujenzi, lakini hospitali za awamu ya kwanza 68 zitaendelea na ujenzi kwa bilioni 55.7, lakini pia hospitali 27 za awamu ya pili nazo zimetengewa bilioni 11.4.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la hospitali tunafahamu hospitali chakavu na kongwe tunakwenda kufanya tathmini na kuona njia bora zaidi kama ni kuzikarabati ama kuanza ujenzi ili ziweze kuwa na viwango bora. Vituo vya afya katika mwaka ujao tunatarajia kuendelea na ujenzi na ukamilishaji wa vituo vile vya afya 52, zimetengwa bilioni 15.6. Pia ujenzi wa vituo vipya 121, kuna shilingi bilioni 60.51. Jumla vituo vya afya 173 nchini kote kwa gharama ya shilingi bilioni 76.1, utaona ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, eneo la zahanati, tumetambua kwanza maboma Waheshimiwa Wabunge wameongelea suala la maboma ya zahanati ambayo wananchi wamechangia, tumekwisha yatambua maboma yote, mpaka Februari tulikuwa na maboma 2,350 na tayari katika mwaka huu wa fedha maboma 555 yametengewa shilingi bilioni 27.75 na tayari bilioni 20 zimekwishapelekwa, kazi za ujenzi zinaendelea, bilioni 7.75 zinaendelea na hatua za upelekaji kukamilisha maboma hayo.

Mheshimiwa Spika, mwaka ujao wa fedha maboma 758 yametengewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 38.15 na hivyo tutakuwa tuna jumla ya maboma 1,313 ambayo tayari yatakuwa yanaendelea na ujenzi na ukamilishaji, tutabaki na maboma 1,037 ambayo tutaendelea kuyakamilisha kwenye mwaka mwingine wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la vifaa tiba dawa na vitendanishi, Mheshimiwa Waziri wa Afya ameeleza vizuri, lakini Serikali imeendelea kutenga fedha kwenye hospitali za Halmashauri. Hospitali 67 tayari zimeshapata bilioni 32.5, vituo vya afya tayari bilioni 26 mwaka huu, bilioni 15 tayari vifaa vimeshanunuliwa vinapelekwa, bilioni 11 hatua za manunuzi zinaendelea. Kwa mwaka ujao wa fedha bilioni 12.3 tunatarajia pia zitakwenda kununua vifaa tiba. Kwa hivyo tutahakikisha tunaendelea kuboresha vifaa tiba katika maeneo hayo. Dawa imeongelewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, tayari hatua za manunuzi ya dawa hizo zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kuongelea eneo la CHF, Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa na eneo hilo ni kipaumbele cha Serikali, tumepanga kuwa na ajenda ya kudumu kwenye vikao vyote vya kisheria kuanzia ngazi za mitaa, vijiji, kata hadi ngazi za mkoa. Tumekwishahamasisha wananchi na utaratibu huu unaendelea wananchi 3,300,000 wameshajiunga na shilingi bilioni 19 tayari zimekwishakusanywa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Niwashukuru sana Wajumbe wote wa Kamati ya LAAC na Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni, mapendekezo na michango muhimu sana. Serikali imeichukua michango yote na tumeipokea kwa mikono miwili tutakwenda kuitekeleza moja baada ya nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nikianza na hoja ya matumizi ya fedha mbichi. Serikali ilishaweka utaratibu na miongozo kwamba ni marufuku taasisi yoyote ya Serikali kutumia fedha kabla ya kupeleka benki na tumeendelea kuboresha mifumo ya kielektroniki kuhakikisha mapato yote yanapelekwa benki na kutumika baada ya kupelekwa benki.

Mheshimiwa Spika, ni kweli baadhi ya watumishi bado wamekuwa na utaratibu wa kutumia fedha kabla ya kupelekwa benki na tutaendelea kuchukua hatua kuhakikisha tunadhibiti matumizi ya fedha mbichi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kufutwa kwa baadhi ya miamala. Serikali hivi sasa tumewekeza sana kuboresha mifumo ya kielektroniki, lakini tunakwenda kuiboresha kuweka system ambazo zitadhibiti wale operators wasiwe na access ya kufuta miamala kwa manufaa yao binafsi. Kwa hiyo, hili Serikali tumelichukua, tunakwenda kuweka mifumo hiyo kudhibiti wale ambao wana nia mbaya ya kutumia vifaa hivyo kufuta miamala.

Mheshimiwa Spika, pia tutaweka bureaucracy ili Maafisa Masuhuli wawajibike kufuta miamala na siyo kila operator awe na access ya kufuta hiyo miamala.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Force Account kuweka kiwango, ni kweli tuliweka utaratibu majengo ya ghorofa yanakwenda kwa Makandarasi, yale ya chini tunatumia Force Account. Hata hivyo, wazo ni zuri, tumelipokea, tutakwenda kuweka kiwango ambacho kitakuwa cha Force Account na kiwango ambacho kitakuwa lazima kitumie contractors. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Wahandisi, Rais wetu ameajiri kwa dharura Wahandisi 246 mwezi Oktoba, 2021 kwa ajili ya Halmashauri zote 184 na mikoa yetu yote na zoezi hili ni endelevu, tutaendelea kuboresha ikama ya Wahandisi ili wasimamie vizuri miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na udhahifu wa makusanyo ya mapato ya ndani, ni wajibu wa Halmashauri zote kuhakikisha wanakusanya mapato ya ndani kwa 100% na kuhakikisha fedha zile zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi yenye tija na kukamilisha miradi ile kabla ya kuanza miradi mingine. Kwa hiyo, tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati na Serikali tumeanza kutoa maelekezo hayo kuhakikisha hili linatekelezwa na fedha hizo zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo 40%, 60%, na 10%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Wakuu wa Idara kukaa kwa muda mrefu katika Halmashauri zetu; tayari Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeanza kufanya tathmini nchi nzima kwa Wakuu wa Idara wote waliokaa kwa muda mrefu na tumeanza na Waweka Hazina, Maafisa Utumishi, Wakaguzi wa Ndani pamoja na Maafisa Mipango. Utaratibu huo ni endelevu. Tunataka tuhakikishe Wakuu wa Idara hawa overstay kwenye vituo vyao ili kuepusha kuwa na mazoea kufanya kazi na baadaye kuwa na mianya ya upotevu wa fedha za Serikali. Kwa hiyo, suala hili tunakwenda kulifanyia kazi na tutahakikisha tunafanya hili zoezi kuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake niseme Serikali tumepokea maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge na tutakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha mamlaka ya Serikali za Mitaa zinatoa huduma na kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi kwa kadri ya malengo ya Serikali kwa manufaa ya wananchi wenzetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, namshukuru sana na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia afya na uhai, pili nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ambayo ameendelea kuifanya katika ujenzi wa Taifa letu kila kona na tunampongeza sana kwa miongozo yake nasi Wasaidizi wake Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza juhudi katika utekelezaji wa shughuli za TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii na wale ambao hawakuchangia. Kwanza tuwashukuru sana kwa maoni yao, ushauri wao tumepokea na tutakwenda kuonyesha kwamba tunatekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea maeneo mawili. Eneo la kwanza litakuwa la Afya ya Msingi na eneo la pili la miradi ya maendeleo hususan miradi ya kimkakati na ujenzi wa majengo ya utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya afya Waheshimiwa Wabunge wengi zaidi ya asilimia 90 wamechangia kuhusiana na changamoto ya upungufu wa vifaatiba, watumishi hali ambayo imepelekea baadhi ya vituo vilivyokamilika kutoanza kutoa huduma za afya kama ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mwaka mmoja wa Serikali hii ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kazi kubwa sana imefanyika ya ujenzi wa vituo vya huduma za afya. Katika mwaka huu jumla ya shilingi bilioni 437 zimetolewa katika ujenzi wa hospitali mpya za Halmashauri 28, vituo vya afya 304 na zahanati 614.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia IMF Serikali imejenga majengo ya wagonjwa wa dharura EMD 80 pamoja na vifaa vyake, ICU 28 pamoja na vifaa nyumba za watumishi 150 za three in one, ununuzi wa magari ya wagonjwa ambulance 195 ambazo zitakwenda kwenye Halmashauri zote 184 pamoja na magari ya usimamizi wa huduma za afya 212.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo kutokana na ujenzi huu tumekuwa na upungufu wa vifaatiba lakini pia na watumishi katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge Rais wetu na Serikali yetu imesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge na katika mwaka wa fedha ujao Serikali imetenga Shilingi Bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika hospitali zetu zote za Halmashauri zilizokamilika, zahanati na vituo vya afya. Pia Serikali imeweka mpango wa kuajiri watumishi wa sekta ya afya wa kada mbalimbali, watumishi 7,612 ambao watapelekwa kwenye vituo vyetu vyote vilivyokamilika ili vianze kutoa huduma za afya mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ya Waheshimiwa Wabunge wengi ilikuwa ni changamoto ya ujenzi wa vituo vya afya ambavyo tayari vimeanza ujenzi na kama tutaendelea na ujenzi ama tutaishia hapa katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa vituo vya afya kwa maana ya ukamilishaji wa majengo ambayo tayari yameanza, ukamilishaji wa maboma pia ukamilishaji wa hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 40.15 kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali za Halmashauri 59 ambazo ujenzi wake unaendelea na kufanya jumla ya hospitali ambazo zitaendelea na ukamilishaji wake kufikia 102 katika mwaka ujao wa fedha. Pia ukarabati wa hospitali chakavu za Halmashauri 19 utaendelea kufanyika ambapo jumla ya shilingi bilioni 16.55 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini ukamilishaji wa majengo ya maboma ambayo wananchi wetu wametumia nguvu zao na kujenga maboma ambayo yanahitaji ukamilishaji Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kukamilisha maboma 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu na ukamilishaji wa majengo haya utazingatia ubora, thamani ya fedha lakini na kuhakikisha kwamba yanakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja ya uchakavu wa vituo vya afya na zahanati zilizojengwa muda mrefu, zipo zilizojengwa kabla ya uhuru na nyingine baada ya uhuru ambazo zimechakaa sana. Serikali imechukua hoja hii tutafanya tathimini nchini kote kutambua vituo vya afya chakavu na zahanati chakavu na kuviwekea mpango mkakati wa kwenda kuvikarabati ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upungufu wa baadhi ya dawa katika vituo vyetu. Serikali imeweka mwongozo kwamba lazima dawa muhimu katika vituo vyetu zifike angalau asilimia 95 hadi asilimia 100. Ni kweli kumekuwa na upungufu wa baadhi ya dawa katika vituo vyetu lakini Serikali yetu Mheshimiwa Rais katika kipindi cha mwaka mmoja mpaka Februari 2022, tayari amepeleka fedha Shilingi Bilioni 333.8 katika Bohari Kuu ya Madawa (MSD) na taratibu za manunuzi ya dawa hizo zinaendelea. Hali hii itatuwezesha sana kupunguza upungufu wa baadhi ya dawa katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja kwamba baadhi ya watumishi siyo waaminifu wanapelekea dawa kupotea katika vituo vyetu. Ni kweli Serikali imeendelea kuchukua hatua, mpaka Februari mwaka huu jumla ya Watumishi Wakuu wa Idara na Waganga Wakuu wa Mikoa takribani 14 na watumishi wengine wameshushwa vyeo lakini pia tumeendelea kuchukua hatua za kinidhamu kwa Wakuu wa Idara wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kusimamia mapato ya Halmashauri, mapato ya vituo na matumizi bora ya dawa. Utaratibu huu ni endelevu, tutaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha tunadhibiti upotevu wa fedha lakini pia dawa katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mfumo wa GoT-HoMIS ni mfumo ambao umeonesha tukiufunga katika vituo vyetu unaongeza sana mapato katika vituo vyetu kwa zaidi ya mara tatu hadi mara nne lakini pia unadhibiti upotevu na matumizi mabaya ya dawa tumeelekeza halmashauri zetu zote kutenga bajeti ya kuweka na kuhakikisha mifumo ya Got- HoMIS inafanyakazi ili dawa zote zinazokwenda kwenye vituo ziweze kuwa-tract kutoka kuingia mpaka kwenda kutumika kwa wagonjwa wetu lakini pia mapato ya vituo vyetu yaweze kudhibitiwa upotevu wake. Kwa hiyo suala hili tumelizingatia kwa dhati kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la miradi ya maendeleo kuna ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri zetu lengo ni kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma kwa wananchi lakini na mazingira ya kutoa huduma. Serikali imetenga fedha Bilioni 83 kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo ya utawala lakini miradi ya mikakati itakwenda pia kuhakikisha kwamba tunafanya tathmini na kutoa kipaumbele kwenye maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya ninakushuku sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Innocent Bashungwa Waziri wetu kwa ushirikiano na umahiri wake lakini na timu nzima ya TAMISEMI kwa kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya afya na uzima, pili, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kunipa imani ya kuhudumu katika dhamana hii muhimu sana ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ninamhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba nitaendelea kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na weledi wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, tatu ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki kwa uchapakazi wake na umahiri mkubwa, pia ninakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako mahiri sana wa kuliongoza Bunge letu Tukufu na kwa kweli unalitendea haki nafasi hiyo ambayo Bunge hili limekupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe kwa imani waliyonipa na ushirikiano wanaoendelea kunipa na niwahakikishie kwamba tutaendelea kuchapa kazi kuhakikisha tunaendelea kutatua changamoto mbalimbali katika Jimbo la Wanging’ombe.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingi zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, nianze kwa kusema kwamba hoja zote ambazo zimetolewa mapendekezo, ushauri na maoni, Ofisi ya Rais - TAMISEMI tumeyapokea na tutakwenda kuyafanyia kazi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya hoja kwa sababu ya muda nitaomba nizipitie. Hoja ya kwanza ilikuwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa kukaa mara kwa mara Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya kuhusu upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaatiba kupitia Bohari ya Dawa - MSD. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ilikwishaweka utaratibu wa Wizara hizi mbili kukaa kila robo mwaka na kufanya tathmini ya upatikanaji wa dawa lakini pia mfumo wa usambazaji na tutahakikisha tunaendelea kufanya hivyo ili kuondoa changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vyetu pia kuongeza ufanisi wa kupeleka dawa na vitendanishi katika vituo vyetu.

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao unatumika kwa sasa ni wa electronic ambao unasaidia kituo cha afya na wahudumu kuweza kuomba dawa kutoka kwenye kituo chao moja kwa moja kwenda kwenye Bohari ya Dawa na Bohari ya Dawa kuleta dawa katika kituo husika bila kulazimika mtumishi kusafiri kwenda kwenye kituo husika. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha mfumo huu wa ki-electronic katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni suala la kuweka michoro inayofanana katika majengo yetu ya Serikali, majengo ya Ofisi za Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya lakini wa Halmashauri na nyumba za Wakuu wa Idara. Serikali ilikwishafanya mapitio ya michoro yote ya majengo rasmi ya Serikali kuanzia ngazi ya Mikoa mpaka ngazi za Halmashauri lakini tunaenda hadi ngazi za Kata Ofisi za Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji tutakuwa na ramani moja ambayo itakuwa standard kwa nchi nzima ili kuleta uniformity lakini pia kuwa na msawazo sawa wa gharama za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la hospitali zetu na vituo vya huduma za Afya. Ni kweli Waheshimiwa Wabunge tulio wengi tumechangia juu ya umuhimu wa kuwa na vituo vya afya katika Kata zetu za kimkakati lakini pia katika Tarafa za kimkakati vilevile kuwa na zahanati katika vijiji. Serikali imefanya kazi kubwa sana katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan sote ni mashuhuda katika Majimbo yetu kila sehemu, zimejengwa zahanati kwa wingi, Vituo vya Afya, Hospitali za Halmashauri, majengo ya dharula EMD, ICU na Vifaatiba kwa wingi sana.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha yale majengo ambayo tayari yamejengwa lakini hayajakamilika, yanakamilika kwanza ili yaanze kutoa huduma za kutosha kwa maana ya uwezo wao katika vituo hivyo na baadae tuweze kwenda kwenye ujenzi wa vituo vingine. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunatambua uwepo wa Kata za Kimkakati na Tarafa za Kimkakati ambazo bado hazijapata vituo vya afya na zahanati lakini baada ya kumaliza kipaumbele cha ukamilishaji basi tutakwenda kwenye ujenzi wa vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Deus Sangu la hospitali ya Halmashauri. Kwa mujibu wa sera ya Wizara ya Afya hospitali ya Halmashauri inakuwa moja katika Halmashauri. Kwa kuwa, Halmashauri ya Sumbawanga tayari ina hospitali ya Halmashauri na kwa kuwa Serikali inatambua na kuthamini afya za wananchi wa Laela tunapeleka pale fedha Shilingi 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Laela ili wananchi wasifuate umbali mkubwa kilometa 180 kwenda kupata huduma katika kile Kijiji cha Mto Wisa.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii, imechangiwa na Waheshimiwa wengi ya vifaatiba. Serikali katika kipindi cha miaka hii miwili imepeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika vituo vyetu vyote vilivyo kamilika na kazi ya usambazaji wa vifaa unaendelea na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge zoezi la kupeleka vifaatiba ni endelevu ili kuwezesha vituo vyetu hivi kutoa huduma bora za Afya kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, suala hili linaendelea na kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha, fedha zimetengwa kwa ajili ya kuendelea kununua vifaatiba.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la mpango wa ukamilishaji wa vituo lakini na vifaatiba na hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisemea, ile ni moja ya hospitali kongwe 19 ambazo zimetengewa fedha lakini mwaka ujao wa fedha zimetengewa Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya kuifanyia ukarabati na upanuzi, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge Serikali ilikwisha ainisha hospitali zote kongwe na chakavu pia vituo vya afya vyote vikongwe na chakavu kwa ajili ya kuendelea kutenga fedha kwa awamu ili viweze kuboreshwa na viendelee kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda ambayo changamoto yake ni kwamba majengo yale hayajakamilika, hii inafanana na hospitali nyingi za Halmashauri na ambazo zilipewa fedha kipindi cha mwaka 2018/2019, 2019/2020 lakini Serikali imeshafanya tathmini iko hatua za mwisho za ukamilishaji wa mahitaji halisi ya gharama za ukamilishaji wa vile vituo na hospitali na fedha itatafutwa kwenda kukamilisha majengo yote ambayo hayajakamilika likiwemo hili la hospitali ya Halmashauri ya Bunda Vijijini, Halmashauri ya Mlele na maeneo mengine ambayo hospitali zina sura ya aina hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wananchi kukosa huduma kutokana na miradi kutokamilika pamoja na Serikali kupeleka fedha, Serikali imeshaweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwanza wale wanaohusika na upotevu wa fedha za Serikali hatua stahiki za kinidhamu na kisheria zinachukuliwa kwao pia hatua za kisheria zinafuatwa na kuhakikisha kwamba hakuna watumishi ambao watakuwa wanatumia vibaya pesa za Serikali, lakini pili yale majengo ambayo hayajakamilika sasa ndio hayo ambayo yanatafutiwa fedha kwa ajili ya kwenda kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la wazabuni kuwa na madeni, Serikali ilishatoa maelekezo kwamba Halmashauri au taasisi yoyote ya Serikali kabla ya kutangaza zabuni lazima ijiridhishe kwamba kwanza kuna bajeti ya shughuli hiyo lakini pili fedha zipo ili zabuni ikitolewa fedha zile ziweze kuwa zinapatikana na kulipwa kwa wakati ili kuepusha usumbufu kwa wazabuni lakini pia kuepuka kutengeneza madeni ya Serikali yasiyo ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la utawala bora ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamechangia lakini Mheshimiwa Mrisho Gambo aliongea kuhusu suala la ubadhirifu mkubwa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Mheshimiwa Spika, hatua zimeshaanza kuchukuliwa na ndiyo maana Wakuu wa Idara kadhaa tayari wameshachukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu lakini aliyekuwa Mkurugenzi alishachukuliwa hatua za Kisheria na taratibu zinaendelea, pia tutaendelea kuchukua hatua kwa wote ambao watathibitika kuhusika kwa namna moja ama nyingine katika matumizi ambayo siyo sahihi ya fedha za Serikali. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge Serikali iko macho katika eneo hili na kazi inaendelea kufanyika na kuhakikisha kwamba tunatenda haki katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu. Kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa umeendelea kuimarika lakini tunatambua bado kuna changamoto ya upungufu wa baadhi ya dawa muhimu na hususan dawa za matibabu kwa wazee lakini pia watoto chini ya miaka mitano na wakina mama wajawazito. Mpango wa Serikali, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tumeshaweka mkakakti wa kuainisha dawa muhimu ambazo zinatoka kwa wingi zaidi ili tuhakikishe kwamba dawa hizo zinapatikana kwa wingi kwenye vituo vyetu lakini tumeongeza orodha ya dawa zote muhimu kutoka 33 hadi 241, hii itasaidia kuhakikisha kwamba wananchi sasa wana wigo mpana wa kupata dawa katika maeneo hayo kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Spika, nihitimishe kwa kukushukuru sana na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na kuhakikishia kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakwenda kutekeleza haya yote kuhakikisha tunaboresha huduma kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)