Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Condester Michael Sichalwe (50 total)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa ya kunipa kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ubovu mkubwa wa miundombinu ndani ya Jimbo la Momba. Je, ni lini Serikali itatusaidia kutujengea kilometa 15 za kiwango cha lami kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba katika Kata ya Chitete ikiwa ni sambamba na ahadi ya mama yangu mpendwa Mheshimiwa Makamu wa Rais alipotembelea Jimbo la Momba tarehe 13 Oktoba, 2020 alituahidi angeweza kutusaidia barabara hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naombakujibuswali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-

MheshimiwaNaibu Spika, ni kweli ahadi ya Makamu wa Rais wakati wa kampeni ilitolewa mwaka huu wa kampeni 2020; kwa hiyo, kama Serikali ahadi hii tumeichukua na tunaifanyiakazi. Kwa hiyo, katika awamu inayokuja ya bajeti tunategemea kwamba zitakuwa ni kati ya barabara ambazo zitatengewa fedha na once zikitengewa fedha barabara hiyo itajengwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuongeza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nini tamko la Serikali kutokana na wawekezaji hawa wakati mwingine kujichukulia sheria mkononi na kuwafungulia watu kesi na kuwaweka ndani ikiwa hata wao hawafuati Sheria ya Ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwa na hati sahihi, kuendeleza maeneo yale pamoja na kulipa kodi ya ardhi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati usimamizi bora wa matumizi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo inaendelea kushika kasi ndani ya Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester.

Mheshimiwa Spika, napenda tu nimhakikishie; kwenye swali lake la kwanza anataka kujua nini tamko la Serikali kwa hawa wawekezaji ambao wanajichukulia sheria mkononi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe rai tu kwa wananchi kuhusu namna ya uuzaji wa ardhi kwa wawekezaji. Tuwaombe sana, kwa sababu mara nyingi wawekezaji wanaenda moja kwa moja kwenye maeneo, wanaonana na watu bila kufuata taratibu na wanauziana bila kuzingatia sheria; na hatima yake anapokuwa amepewa hati yake wewe ulimuuzia hekari 100, anakuja na hati yenye hekari zaidi ya 100, ni kutokana na nyaraka ambazo zinatakiwa kuwepo kwa kuzingatia sheria yenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi niwaombe, kwanza nitoe rai, kwamba, ili kuondoa hii migogoro uuzwaji wowote wa ardhi lazima uhusishe halmashauri husika ambao ndio wanaotambua mipaka yako na namna ambavyo mnaweza kuuziana ardhi kwa wawekezaji. Na wakati mwingine unaweza ukamuuzia mtu ambaye hata si raia wa Tanzania ilhali hairuhusiwi kwa raia wa kigeni kuweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la kodi ambazo hawalipi, tayari tulishaanza mkakati wa kuwafuatilia. Tunachohitaji tu ni halmashauri husika kuona ni namna gani pia ya kuanza ule mchakato wa kufuata sheria, taratibu zile za kutoa maonyo kuanzia kwenye Kifungu cha 45 mpaka 48 ambavyo vinaelekeza njia nzuri ya kuweza kumnyang’anya mtu hati yake hata kama amepewaa kisheria.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema ni lini Wizara itaingilia kati ili kumaliza migogoro hii ya wakulima na wafugaji. Tatizo hilo linaweza likaisha pale tu ambapo kijiji kitakuwa na mpango wa matumizi ya ardhi; na matumizi ya ardhi hayapangwi na Wizara, yanapangwa na maeneo husika. Kwa hiyo sisi kama Wizara intervention yetu inakuja pale ambapo tunakuja sasa kuridhia kile ambacho mnakubaliana katika kutenga maeneo. Kwamba wafugaji wanatengewa maeneo yao, wakulima maeneo yao, maeneo ya makazi nayo yanakuwepo. Kwa hiyo tunapokwenda sisi ni kuweka ile mipaka kwa ajili ya kuheshimu taratibu hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama vijiji hivi havijawa na mpango wa matumizi basi tunaielekeza pia Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ikashirikiane na Wilaya ya Momba waweze kuweka matumizi ya ardhi katika maeneo yenye mgogoro. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Miaka 20 iliyopita ndani ya Jimbo la Momba Ivuna, kuna kimondo kidogo kilidondoka (Ivuna Meteorite) na kikachukuliwa na watu wa NASA. Je, Serikali ina mpango gani wa kufuatilia kimondo hiki kwa ajili ya kukirudisha na kuendelea kuongeza idadi ya watalii nchini? (Makofi)
WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza kwanza Mheshimiwa Condester kwa kazi nzuri anayowafanyia wananchi wa Momba na ndiyo maana walikuchagua kwa kura nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeshaanza kufanya mawasiliano na Balozi wetu aliyeko nchini Marekani kuanza kufuatilia jambo hili. Tutakapopata majibu, tutamjulisha Mheshimiwa Condester na Bunge lako Tukufu. Ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nilikuwa nasema kwa kuwa barabara nyingi za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA zimeonekana kutokuwa na uteshelevu wa bajeti na angalau TANROADS kuonekana wana bajeti ya kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha barabara nyingi ambazo zipo vijijini zinazochelewa kupandishwa hadhi kwenda TANROADS ili angalau ziweze kusaidiwa kwa sababu barabara za vijijini tunapata shida sana na bajeti ya TARURA ni ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Vijijini na Mijini imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi katika mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 bajeti ilikuwa bilioni 275.034 lakini mwaka ujao wa fedha ni shilingi bilioni 400, ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 125. Jitihada hizi zote ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha uwezo wa TARURA kuhudumia barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Spika, na naomba nichukue hoja yako, tutaendelea kufanya tathmini kwenye barabara hizo ambazo zinahitaji kusajiliwa wa TARURA lakini zile ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda TANROADS kuna utaratibu ambao Serikali imeelekeza naomba tuufuate huo ili tuweze kupata barabara zenye hadhi hiyo na kufanyiwa matengenezo kwa wakati, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nilikuwa nasema kwa kuwa barabara nyingi za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA zimeonekana kutokuwa na uteshelevu wa bajeti na angalau TANROADS kuonekana wana bajeti ya kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha barabara nyingi ambazo zipo vijijini zinazochelewa kupandishwa hadhi kwenda TANROADS ili angalau ziweze kusaidiwa kwa sababu barabara za vijijini tunapata shida sana na bajeti ya TARURA ni ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bajeti ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Wakala wa Vijijini na Mijini imeendelea kuboreshwa mwaka hadi mwaka. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi katika mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 bajeti ilikuwa bilioni 275.034 lakini mwaka ujao wa fedha ni shilingi bilioni 400, ongezeko la zaidi ya shilingi bilioni 125. Jitihada hizi zote ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha uwezo wa TARURA kuhudumia barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Spika, na naomba nichukue hoja yako, tutaendelea kufanya tathmini kwenye barabara hizo ambazo zinahitaji kusajiliwa wa TARURA lakini zile ambazo zinahitaji kupandishwa hadhi kwenda TANROADS kuna utaratibu ambao Serikali imeelekeza naomba tuufuate huo ili tuweze kupata barabara zenye hadhi hiyo na kufanyiwa matengenezo kwa wakati, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa Wilaya ya Momba makao yake makuu yako ndani ya Halmashauri ya Momba, je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha polisi ambacho kina hadhi ya wilaya ili kiweze kusaidia kuepusha changamoto na uovu wote ambao unaoendelea ndani ya Jimbo la Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali kupitia Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapatiwa huduma za ulinzi na usalama kupitia kila chombo ambacho wananchi watakuwa wanahitaji. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba awe na Subira, tutajitahidi sana tuhakikishe kwamba ndani ya jimbo hilo au ndani ya eneo hilo ambalo limekosa hicho kituo cha polisi basi tuone namna ya kuweza kupata fedha ili tukawatengenezee wananchi kituo cha polisi waweze kupata huduma za ulinzi. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhalisia kwamba halmashauri zetu nyingi nchini zina changamoto sana ya miundombinu. Serikali haioni kuna haja ya kubadilisha usafiri kutoka kwenye pikipiki na kuwapatia magari maafisa maendeleo ya jamii hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na kwa uwanda mkubwa? Kwa mfano, kipindi cha mvua mtu huyo atatumiaje pikipiki maana yake atakuwa analowa, hawezi kutekeleza majukumu yake. Serikali haioni umuhimu wa kuwanunulia magari maafisa maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMIS): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyogeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, maafisa hawa wanatembea kwa pikipiki kwa ajili ya kufuatilia wafanyakazi hawa au vitendo mbalimbali vinavyotokea katika jamii. Serikali kama nilivyoeleza imejipanga kuzungumza na wadau ambao wanaendeleza maendeleo haya ya jamii ili kuhakikisha kwamba maafisa hawa hawatopata tabu katika kazi zao katika mazingira yao ya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo, ahsante nashukuru. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto ambayo inawapata wananchi wa Busega inafanana kabisa na changamoto ambayo inawapata wananchi wa Jimbo la Momba.

Je, ni lini Serikali itaona kuna haja ya kutupa upendeleo ili tuweze kupata Mahakama yenye hadhi ya wilaya ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya mwendo mrefu kufuata huduma za Mahakama kutoka Jimbo la Momba mpaka Mji wa Tunduma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe kutoka Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi katika Mpango Kazi wa kuendeleza ujenzi wa hizi Mahakama zetu za wilaya, 2022/ 2023 tunakwenda kuanza ujenzi wa Mahakama yake ya Momba ili kumpunguzia hiyo adha ambayo wananchi wanaikabili kwa sasa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Jimbo la Momba lina vijiji 72 na vitongoji 302. Katika vijiji hivyo, vijiji ambavyo vinapata majisafi na salama ambayo yanafaa kwa matumizi ya binadamu haviwezi kuzidi 20; isipokuwa tunatumia mbadala wa maji ambayo yametuama kwenye madimbwi na kwenye mito midogo midogo ambapo tunakunywa pamoja na ng’ombe, punda, mbuzi na wanyama wote: -

Je, ni lini Serikali itaona katika vijiji vilivyobaki, watusaidie kutuchimbia visima vya dharura wakati tunaendelea kusubiri miradi mikubwa ya maji ili tuendelee kupata maji safi na salama kama ambavyo binadamu wengine wanapata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jimbo la Momba bado lina changamoto ya maji na ni moja ya maeneo ambayo yapo kimkakati katika Wizara na tumetupia jicho la kipekee kabisa pale. Visima ni moja ya miradi ambayo tunakuja kuitekeleza ndani ya Jimbo la Momba. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, tutakuja kutekeleza wajibu wetu, kwa sababu wananchi wale pia wapo Tanzania. Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan, amesema wanawake wote lazima tuwatue ndoo kichwani. Mantahofu, tunakuja kufanya kazi Momba. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado, changamoto ya maji kwenye Jimbo la Momba ni kubwa sana. Naomba kuiuliza Serikali niongeze maswali mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji ambavyo umevieleza tunavyo vijiji 72 na vitongoji 302 inaonyesha kwamba hata nusu ya vijiji hivyo vitakuwa bado havijapata maji safi na salama. Ombi langu kwa Serikali, viko baadhi ya visima ambavyo vilishawahi kuchimbwa nyuma na wakoloni, vilishawahi kuchimbwa nyuma na wamishionari lakini pia na baadhi ya wakandarasi ambao walikuja kujenga barabara kwenye Jimbo la Momba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, nini kauli ya Serikali kwenda kuvitembelea visima vile ambavyo vimeshawahi kufanya kazi vizuri huko nyuma kutokana bado kuna changamoto ya maji vinaweza vikatusaidia vikawa kama njia nyingine ya mbadala kutatua changamoto ya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa, baadhi ya vijiji ambavyo vimeonyesha vinao miradi hiyo ya maji lakini zipo Taasisi kama Vituo vya Afya, Zahanati pamoja na Sekondari havipati utoshelevu wa maji. Watoto wetu especially wa kike wameendelea kuteseka sana kufuata maji wakati mwingine zaidi ya kilomita 10. Mfano, Shule ya Sekondari Chikanamlilo, Shule ya Sekondari Momba, Shule ya Sekondari Uwanda, Shule ya Sekondari Ivuna, Shule ya Sekondari Nzoka na shule zingine 13 ambazo ziko ndani ya Jimbo la Momba pamoja na Zahanati na Vituo vya Afya kama Kamsamba na Kapele. Je, ni nini kauli ya Serikali kutuchimbia visima virefu ili Taasisi hizi ziweze kujipatia maji yake bila kutegemea kwenye vile vituo ambavyo tunang’ang’ania na wananchi na havitoshelezi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kutembelea visima ambavyo ni chakavu hii ni moja ya jukumu letu na tayari, Mheshimiwa Waziri amewaagiza watendaji wote kwenye mikoa yote, kwa maana ya Regional Managers (RMs) na Managing Directors (MDs) wasimamie visima vyote ambavyo ni chakavu. Vile ambavyo uwezekano wa kuvirejesha katika hali njema ya kutoa maji safi na salama vyote viweze kurejeshwa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Jimbo la Momba sisi kama Wizara tumeshaleta Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuchimba visima virefu. Hivyo, visima hivi ambavyo vya kukarabati lakini uchimbaji wa visima virefu kwenye swali lako la pili la nyongeza, navyo tayari vimeshaanza kufanyiwa kazi katika baadhi ya maeneo. Tayari visima vitano vimeshachimbwa kati ya visima 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, napenda tu kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba sisi kama Wizara tutakwenda kuhakikisha katika sehemu zote ambako Taasisi za Serikali zipo kama zile Shule alizozitaja pamoja na Vituo vya Afya na Hospitali maji ni lazima yafike na huo ndio Motto wa Wizara. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kutokana na ongezeko kubwa la wananchi ndani ya Jimbo la Momba kwa baadhi ya vitongoji na vijiji: -

Je, ni lini Serikali kwa kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili watakaa kwa pamoja ili kugawa baadhi ya maeneo ambayo ni ya hifadhi ili kuwapatia wananchi wa vitongoji vya Mbao, Ntungwa, Twentela pamoja na Kaonga ili wapate sehemu ya kulima kwa sababu wamekuwa kama wakimbizi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama mnavyojua kwamba nchi yetu inaongozwa na utaratibu wa sheria, ugawaji wa maeneo yote ni jambo linalofuata kisheria. Nami nimwagize tu au nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huu uanze kwao ili watuletee tuweze kupeleka kwa mtu aliyekabidhiwa mamlaka kugawa vipande vya ardhi katika nchi hii, yaani Mheshimiwa Rais, ili sasa utaratibu mwingine uweze kufanyika. Nashukuru. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukurru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mloo - Kamsamba - Utambalila kupitia Chitete yenye kilometa 145.14 iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/ 2025 kwenye ukurasa wa 75: -

Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilishafanya maandali ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Tayari usanifu wa kina umeshafanyika. Changamoto iliyokuwepo ya Daraja la Momba, imejengwa kwa ajili ya kupokea barabara hiyo. Kwa hiyo, itategemea na fedha zitakapopatikana, kwa sababu taratibu zote za awali zimeshakamilika ili barabara hii ambayo inaunganisha Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Rukwa hadi Katavi iweze kujengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mlowo – Kamsamba kupitia Utambalila na Chitete ikiwa iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2025? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara Kamsamba – Utambalila – Chitete ni barabara ambayo ni sehemu ya barabara ya Mlowo – Utambalila – Kamsamba; barabara hizi ziko kwenye package moja. Kwa sababu tulishakamilisha usanifu, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Je, ni upi mpango wa Serikali kupitia Wizara hii ya Uwekezaji kuangalia yale makundi ya asilimia 10 ambayo hayana vigezo vya kukopeshwa. Kwa mfano wanaume ambao wamepita umri wa vijana kwa ajili ya kuwawezesha, lakini pia kwenye asilimia 10 zipo baadhi ya halmashauri hazina uwezo kukidhi makundi yote asilimia 10. Ipi kauli ya Wizara hii kuwawezesha makundi hayo ambayo yanabaguliwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mbunge kwa kufatilia kuhusiana na asilimia 10 za fedha zinazotengwa kwenye halmashauri zetu ili kuwasaidia akina mama, vijana na wenyeulemavu katika kufanya biashara zao ndogo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati ya Serikali sasa ni kuona makundi haya kwanza yanapata elimu ya ujasiriamali kupitia wataalamu wetu wa Maafisa Biashara katika halmashauri pia kwa kushirikiana na Shirika letu la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) ili waweze kutimiza malengo ambayo wamekusidia katika mikopo hiyo. Lakini zaidi tutaangalia namna ya kuwezesha zile halmashauri ambazo kidogo zina mapato machache ili nao waweze kutosheleza mahitaji katika kuwakopesha vijana na akina mama ambao wanahitaji mikopo kwa ajili ya kufanya biashara zao katika halmashauri zetu na majimbo yetu. Nakushukuru sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ndani ya Jimbo la Momba wapo baadhi ya wananchi wengi kadhaa ambao wamekosa kunufaika na Mfuko wa TASAF na zoezi la kuandikishwa kwenye mbolea kwa sababu wamekosa vitambulisha vya Taifa.

Je, ni lini Serikali itachukuwa jambo hili kwa haraka na kwa dharula ili wananchi hawa waweze kupata haki yao ya msingi kwenye mahitaji hayo? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wananchi kukosa huduma mbalimbali, nilieleza katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Fakharia kwamba namba za utambulisho zinaweza kutumika katika kupata huduma mbalimbali. Lakini kama kuna changamoto katika maeneo mahususi ambayo ameyagusia Mheshimiwa Mbunge, kwa mfano eneo hili la TASAF na sensa kama nilivyosikia sawa sawa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, na mbolea.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, na mbolea! Basi nilichukuwe pamoja na kukaa na Mawaziri wa sekta husika hili tuweze kulifanyia kazi kama Serikali. Lakini suluhisho la kudumu ni kuhakikisha kwamba watanzania wote wanapata vitambulisho vyao, na ndicho kipaumbele cha Serikali na tunachukuwa jitihada ili kuhakikisha hili linatekelezeka. Na kwa bahati njema katika bajeti hii ya mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 42.5 kwa ajili ya ununuzi wa kadi ghafi milioni nane laki tano.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa kadi ghafi hizo utasaidia sana kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge amezungumza.
MHE. CONDESTER MICHAEL SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nimesikiliza majibu ya Serikali siyo mbaya, ni hivyo hivyo. naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba na kwamba wanatambua uzalishaji ambao upo vijijini Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna haja ya kubadilisha Sheria ya Vilevi na Vileo (The intoxication Liquors Act) ambayo ni ya mwaka 1968 na marekebisho yake ya mwaka 1978. Hauni kuna haja; kwamba, sheria hii ikibadilishwa inaweza ikaendana na mazingira tuliyonayo sasa kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia wananchi waliopo kule vijijini? Kwasababu Sheria iliyopo sasa hivi inaongelea sana mambo ya leseni.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kulingana na Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kusisitiza uchumi wa viwanda Je, Wizara hii haioni sasa ipo haja kabisa ya kuwapa SIDO jukumu la kuwasaidia wananchi hawa wanawake wa vijijini na sehemu zote, kuwapa elimu, kupata takwimu halisi ili waweze kuwasaidia kuboresha hizo pombe zao za kienyeji na ziweze kuwa kwenye viwango na ziweze kuuzwa nje ya nchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester Sichalwe Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, na ninadhani ni mawazo mazuri, kwamba tuangalie namna ya kupitia sheria zetu za vileo na vilevi ili iweze kuendana na uhalisia wa sasa. Nadhani hii kama Serikali tuichukue. Na kwasababu ni wajibu wetu kama Wabunge kutunga sheria hizi basi na sisi tutalifanyia mchakato ili tuweze kuona uhalisia kama kuna uhitaji wa kubadilisha sheria hizo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kupitia SIDO Serikali inaboresha baadhi ya mitambo lakini pia na kuboresha mikopo kwa ajili ya wajasiliamali mbalimbali ikiwemo wanawake. Na sasa labda tutaangalia mahsusi kwa ajili ya hawa wazalishaji wa pombe za kienyeji ambao huenda watataka teknolojia mahsusi au mfuko maalum ili waweze kuwezeshwa kuzalisha pombe ambazo zina viwando badala ya kuendelea kuzalisha hizi pombe ambazo tunaita ni za kienyeji. Nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Je, ni lini Serikali itaboresha kituo cha afya cha Ndalambo ikiwa ni sambamba na kuongeza majengo? Kituo hiki kinahudumia kata zaidi ya tano zilizopo kwenye Tarafa ya Ndalambo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya vituo vya afya ambavyo ujenzi wake ulianza, lakini haujakamilika na inaweka mpango wa kukamilisha vituo vya afya vile havijakamilika ili viweze kutoa huduma za afya kwa wananchi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuwa kituo kile kilishaanza ujenzi na hakijakamilika, tutakwenda kukamilisha kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kutoa taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba mpango na dhamira ya Serikali ni kukamilisha kwanza vituo vya afya ambavyo vilianza ujenzi na havijakamilika ili vipate vifaa tiba na kuanza kutoa huduma za afya kabla ya kuendelea kujenga vituo vingine vipya. Vile vile tutaendelea kujenga zahanati za kimkakati isipokuwa vituo vya afya vipya mpaka pale tutakapokuwa tumekamilisha ujenzi wa vituo vya vya afya ambavyo tayari vimeshaanza. Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na barabara hiyo, ombi langu ni kwamba, Serikali haioni haja katika kipindi ambacho tunasubiri matengenezo ya hiyo barabara tupate daraja la dharura ambalo limefanya kusiwe na mawasiliano kabisa ya wananchi hawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, ni kwamba, katika jibu letu tumeshaweka commitment ya kutenga fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Bahati nzuri mwaka wa fedha huu unaoanza, ambacho naweza nikamhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Momba ni kwamba, daraja hilo litajengwa katika mwaka wa fedha unaokuja, kabla ya msimu wa mvua kuanza. Kwa hiyo, hiyo ndio commitment ya Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nimepokea majibu ya Serikali na ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi. Swali langu la kwanza lipo katika mfumo wa ombi, je, Naibu Waziri anaonaje kama atatafuta siku ya weekend katikati ya Bunge hili la Bajeti aongozane nami kwenda Jimboni Momba, kunisaidia kutoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kijiji cha Namchinga ili waweze kuelewa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali inaonaje kama itatoa mwongozo kwa makampuni haya ya simu ili kuhakikisha wanapolipa pango la ardhi kwa Mmiliki lakini watoe na percent kwenye Serikali ya Mamlaka husika, aidha, Serikali ya Mtaa au Kijiji ili kutoa mgongano wa maslahi kwenye jamii.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Siku mbili tatu hizi tumekuwa tukiongea na Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Mtaa na Mwenyekiti wa Kata katika Kijiji hiki cha Namchinga. Kwa kweli anafanya kazi kubwa sana na hakika Jimbo la Momba wamepata Mbunge kwelikweli.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusu suala la kwenda kutoa elimu, naomba nilipokee na tutakaa tutajadili kadri nafasi itakavyoweza kupatikana tutaweza kufanya hivyo. Nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutafanya kulinganana na nafasi itakayopatikana.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine kuhusu suala la kutoa percent kwa wananchi wetu na dhana kubwa ambayo inasababisha kwamba wananchi wanahitaji kupewa percent kuna dhana imejengeka kwamba minara hii iliyopo katika maeneo ya wananchi ina mionzi ambayo inawaathiri sana wananchi kiasi kwamba wanataka hii percent kama fidia.

Mheshimiwa Spika, Wabunge na wananchi wote, nikuhakikishie kwamba minara hii kiwango ambacho kimewekwa katika minara yetu, kiwango cha chini ni Volt Saba per meter, lakini minara yetu nchi nzima iko chini ya Volt Saba maana yake ipo kati ya Tatu mpaka Nne. Kwa hiyo, suala la mionzi naomba huu mtazamo tuutolee elimu ya kutosha ili wananchi wafahamu.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa Sheria ya Mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2020 inasema kabisa kwamba makampuni ya simu yatatoa asilimia 0.3 kwenye Halmashauri kulingana na minara inayotumika katika Halmashauri husika. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nimesikia majibu ya msingi ya swali hili. Kwanza naomba kabisa kabla sijauliza swali; Mheshimiwa Waziri tunaomba ufanye ziara kwenye vijiji vyetu ili hayo matamko ambayo wewe unayatoa hapa uweze kuwaambia wananchi wenyewe wasikie kama sehemu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu: Je, ni lini Serikali itavimegea nafasi za kulima wananchi wa Itumbula, Ivuna, Mlomba, Itelefya pamoja na maeneo mengine yote ambayo yapo ndani ya Jimbo la Momba ambayo yanahitaji kumegwa kupata maeneo ya kulima kwa sababu maeneo yao yote yamezungukwa na hifadhi na maeneo hayo wananchi wenyewe walitoa kwa Serikali kwa ajili ya kulinda misitu; na sasa hivi wamezaliana? Wataenda wapi ili waweze kulima na kuendeleza shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kulinda meneo yaliyohifadhiwa. Kama kuna ombi la wananchi kumegewa, basi walete maombi hayo yataangaliwa, lakini pia na sisi tutaangalia kama maeneo hayo yana vyanzo vya maji, yana shughuli ambazo zinapaswa kuhifadhiwa vizuri, basi tutawataarifu wananchi namna iliyo bora.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Kwa kuwa Wizara ya Kilimo iliongezea fungu Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa lengo la kuwasaidia wakulima wadogo wadogo, inaonaje kama itatenga percent ya fedha hizo kwa ajili ya kutumia ruzuku ili bei ya mbolea kwenye msimu unaokuja iwe sawa na vile wananchi wamezoea ili kuwaondoa kwenye changamoto na majonzi ambayo wameyapitia katika msimu uliopita kwa mfumko mkubwa wa mbolea ambao wameupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatumia instrument gani kwa ajili ya kutoa ruzuku. Niwaomba Waheshimiwa Wabunge wasubiri kwamba tumalizane kazi tunayoifanya kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo kama tutatuma through TADB, tutatumia mfumo mwingine wowote ule tutalitaarifu Bunge lako Tukufu, uhakika tu ni kwamba kuanzia Julai tutatoa ruzuku kwa ajili ya kushusha bei ya mbolea. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ikiwa Jumuiya hizi zinapoanzishwa kila Jumuiya inakuwa na lengo lake. Mfano, SADC ukisoma malengo yake ilianzishwa kwa ajili ya siasa na usalama zaidi wa nchi zetu. Ikiwa kama COMESA ilianzishwa kwa ajili ya kuwepo kwa soko la pamoja na katika majibu ya msingi kwenye swali inasema kwamba kuwepo kwa tripartite arrangement kunachangia kuondoa changamoto hizi.

Je, mbona bado wafanyabiashara wetu wanapotaka kuyaendea masoko ya hizo nchi ambao ni wanachama na ambao sisi siyo wanachama, wanaendelea kupitia changamoto. Mfano, wafanyabiashara wa Tanzania wanapotaka kuliendea soko la Congo wanakutana na changamoto nyingi lakini hata mazao yanapokuwa yanauzwa kwenye nchi mfano Misri, tunapata tozo kubwa ya ushuru wa bidhaa zaidi ya 30%.

Swali la pili, je, Serikali haioni sasa ipo haja kwa umuhimu kabisa kwamba toka tujitoe kwenye COMESA mwaka 2000 na sasa hivi ni miaka 13, Serikali inaonaje iende kufanya utafiti kukaa na wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kwenye nchi hizi wanachama, zituletee zipi faida ambazo sisi tulipata kutoka kwenye COMESA na zipi hasara ambazo nchi imepata katika kipindi cha miaka 13 kujitoa kwenye COMESA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwani amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana katika masuala ya biashara hasa baina ya sehemu anakotoka huko Momba na soko la DRC. Nianze kwanza na swali la pili alilosema kuhusu utafiti, tuangalie utafiti au tufanye utafiti na tuone kama tumeathirika au hatujaathirika na Tanzania kujitoa katika COMESA.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla ya Tanzania kujitoa COMESA, ilifanya utafiti mkubwa sana na kujiridhisha kwamba hakuna hasara yoyote na hakuna athari yoyote ya Tanzania kujitoa COMESA.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na changamoto ambazo zipo hasa katika soko la Congo. Changamoto hizi hazitokani kabisa na Tanzania kujitoa COMESA. Changamoto na vikwazo vya kibiashara ambavyo siyo vya kiforodha zimekuwepo katika nchi mbalimbali na kila zinapojitokeza basi hushughulikiwa kwa kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana specific na suala la Congo -DRC ni kwamba, Tanzania imechukua hatua nyingi sana za kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu hawapati vikwazo wanapofanya biashara nchini Congo. Hatua hizo ni kwanza kuhakikisha JPC ambayo ni uhusiano wa kibiashara kati ya DRC na Tanzania na ni mwezi Septemba tu last year JPC ilikutana na ilizungumzia masuala mbalimbali ya kukuza biashara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ikiwa wananchi wanapoharibu miundombinu ya maji wanachukuliwa hatua, je, ni ipi kauli ya Serikali pale ambapo miradi au miundombinu inapokuwa imekamilika watu wa mwenge wanapokuja kuzindua mradi, maji yanatoka lakini baada ya wiki mbili, hakuna maji tena, mnachukua hatua gani kwa udanganyifu wa wakandarasi wao ambao wanaidanganya jamii na hakuna maji na limekuwa ni jambo ambalo limezoeleka kwenye miradi mingi ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, udanganyifu wa aina hii Mheshimiwa Waziri alishaukomesha kwa kutuma vikosi kazi kuhakikisha mradi kama umezinduliwa unabaki kuwa endelevu. Nitafuatilia mradi huo anaouongelea Mheshimiwa Mbunge kujua tatizo ni nini ili kuhakikisha huduma iliyokusudiwa inapatikana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa vijiji vya Twentela, Mbalwa, Ntungwa, Mbawo, Moraviani na Itumbula wamezungukwa na hifadhi, hapo nyuma wananchi hao wenyewe kwa ridhaa yao walitoa maeneo hayo ya hifadhi ambayo yalikuwa ni ya kwao.

Je, Serikali haioni ipo haja ya kumega kipande kidogo tu cha hifadhi kuwasaidia wananchi hawa wapate eneo la kulima kwa sababu wamezaliana na hawana sehemu nyingine ya kwenda kwa ajili kuendesha shughuli zao, lakini kwa kufuata utaratibu na kutoa elimu bila kuathiri sheria zetu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili pia aliwahi kuuliza Mheshimiwa Mbunge na taratibu nilimwelekeza kwamba, maombi yanatakiwa yaletwe na sisi tutaangalia tathmini, kama kuna umuhimu wa kumega eneo hilo basi tutapeleka mapendekezo kwa Mheshimiwa Rais, lakini pale ambapo tutaona kuna haja ya kutunza vyanzo vya maji basi wananchi wataelimishwa na maeneo haya tutayahifadhi kwa ajili ya kizazi hiki na kinachokuja.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba mfano x-ray machine na ultrasound kwenye Vituo vya Afya vya Kamsamba, Mkulwe, Msangano, Ndalambo pamoja na Kapere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taratibu na sera za afya, vituo vya afya vinapelekewa mashine za ultrasound lakini vituo vya afya ambavyo vinapata mashine za x-ray ni baada ya tathmini ya kuona idadi ya wananchi wanaotibiwa katika maeneo hyo.

Kwa hiyo, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge, tufanye tathmni ya kuona idadi ya wananchi wanaotibiwa kaita Kituo cha Kamsamba na vingine ambavyo amevitaja kama vinakidhi sifa za kuwa na mashine za x-ray, lakini nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Momba kwamba mashine za ultrasound ziko ndani ya uwezo wa halmashauri kununua wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha kuongeza nguvu katika maeneo hayo, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Spika, uchafuzi wa mazingira kwenye nchi yetu ni jambo ambalo linaendelea kushamiri sana, kwa mfano unaweza wakati unatoka Dar es Salaam labda kuelekea Momba, ukapita sehemu kabisa hakuna makazi ya watu, lakini utakuta takataka nyingi sana zimejaa barabarani.

Je, Serikali haioni kuchukua ushauri huu kutumia vijana wetu ambao wako mtaani hawajapata ajira waliomaliza ngazi za certificate, diploma na hususan wale ambao wamepitia na jeshini hawajapata ajira. Je, hamuoni muanzishe programu maalum kwa ajili vijana hawa kutunza mazingira yetu ikiwa ni pamoja na kuweka faini kwa mtu yeyote ambaye atabainika anatupa takataka hovyo ili kipato pia cha kuwalipa vijana hawa kitokane na faini ambazo tutakuwa tunatozwa sisi wenyewe Watanzania kwa kutokutunza mazingira yetu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza siyo utaratibu kwa mtu unaposafiri na kutupa takataka nje. Naomba suala hili niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba siyo outaratibu na ndiyo maana magari mengi ya usafiri sasa hivi kuna utaratibu ambao kunakuwa na dustbin ambayo mtu yeyote msafiri anatakiwa aweke uchafu na mahali tukifika gari basi watakwenda kutupa takataka.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa vijana nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumeuchukua kusaidiana na wenzetu wanaotunza miji ambao ni TAMISEMI kuona namna wanavyoweza kufanya kunapotokea uchafu mbalimbali kando kando ya barabara zetu.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Je, ni lini Serikali itatumia chanzo cha Ziwa Rukwa kulisambazia Jimbo la Momba maji ili kuondoa kadhia na changamoto ya maji ambayo tunaipata?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Kwa kweli vyanzo toshelevu ndiyo suluhu ya matatizo ya changamoto katika Majimbo mbalimbali. Kwa hiyo, mkakati wa Wizara na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba tunatumia rasilimali toshelevu katika kuhakikisha kwamba tunatatua matatizo ya maji.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutafuta fedha katika kuhakikisha kwamba tunatumia rasilimali toshelevu na wananchi wako wa Momba hatutowasahau katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru tena kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza maswali mengine mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo Serikali imetoa, majibu haya hayaendani na uhalisia wa sasa kwa namna ambavyo kiwanda kinaendelea. Haya ni majibu ya zamani kabisa. Pamoja na hivyo ninaomba niongeze maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi huu ni mradi wa kimkakati, tunauliza ni lini Serikali itaanza kutupatia fedha kuendeleza mradi huu kuliko kuanza kutafuta wawekezaji wa kuanza kuwekeza maana yake tulikuwa tumesha ahidiwa kupewa fedha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kupitia Wizara ya Madini, Waziri mwenye dhamana husika alipotembelea Momba alisema angetuma wataalamu wake waje kutuandikia andiko na kufanya utafiti ni kwa namna gani tuweze kuzalisha kiwango kingi cha chumvi na tuweze kuongezea fedha. Je, Serikali mmeshapata andiko hili la wataalam ili tuweze kuombea fedha ya ziada kutoka kile kiwango ambacho tulikuwa tumepewa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshsimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunajua changamoto ya kiwanda hiki na tathmini inaonyesha tunahitaji takribani shilingi milioni 535 ili kukamilisha ujenzi au uendelezaji wa kiwanda hicho lakini Waheshimiwa Wabunge tunajua kwamba Serikali haifanyi biashara tunachokifanya ni kuwawezesha kama hii mradi maalum wa wale wananchi ili waweze kuendeleza mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema tunahamasisha pia wawekezaji wengine ambao wanaweza kuingia na kushirikiana nao wananchi ambao wameanzisha mradi huu wa chumvi ili uweze kuwa na faida kwa wananchi. Kwa hiyo, Serikali kimsingi haiwezi kufanya biashara lakini inawawezesha wananchi ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kupitia mradi huu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la andiko ambalo linaweza kuonesha umuhimu wa kupata fedha kupitia Wizara ya Madini. Hili tutalifanyia kazi na tutawasiliana na Wizara ya Madini ili tuone tumefikia wapi na kumpa jibu kamili Mheshimiwa Mbunge.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuwa muwazi na kukiri kwamba tunayo changamoto ya maji kwenye Jimbo la Momba. Nitauliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inawasilisha mpango wa bajeti hapa walisema upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 78, na Mheshimiwa Waziri amekiri hapa kwamba tunayo adha ya maji; je, kwa kuwa anaenda kuanzisha Mradi wa Mto Momba, ipi commitment yake kwamba, mwaka wa bajeti unaokuja nasi tutafikia asilimia 78 kama wenzetu wa vijijini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Tarehe 11 Novemba, 2022 Mheshimiwa Rais wakati anazindua vifaa vipya vya kisasa vya uchimbaji, yapo maneno kadhaa ambayo alimweleza Mheshimiwa Waziri, nami sitaki kuyarejea, kwani anakumbuka, kwamba hatavumilia kuona wataalam wanaendelea kusema wamefanya utafiti na hawajaona maji. Momba hayo mambo yanaendelea, kila wakienda kufanya utafiti hawaoni maji: Ipi kauli ya Mheshimiwa Waziri kudhibitisha yale maneno ya Mheshimiwa Rais siku ya tarehe 11 Novemba, 2022?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wananchi wake wa Momba. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba tunakwenda kutumia rasilimali toshelevu kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji. Vivyo hivyo sasa tunakwenda kutumia Mto Momba kwa ajili ya kutatua tatizo la maji Momba, na maji yale yatakwenda mpaka Tunduma ili wananchi wale waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni juu ya suala zima la utafiti. Nikiri miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto juu ya vitendea kazi. Mheshimiwa Rais ametupatia fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa ambavyo vitaweza kufanya tafiti na kuhakikisha rasilimali za maji zilizokuwa chini ya ardhi zinatumika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata yale magari ya Mheshimiwa Rais ambayo tumeyapata katika kila mkoa, hivi ninavyozungumza lipo katika Jimbo lake la Momba katika kuhakikisha tunachimba visima na wananchi wake wanapata huduma ya majisafi na salama. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Katika Jimbo la Momba kuna vijiji zaidi ya 20 ambavyo wananchi wamejenga maboma na wanahitaji kuungwa mkono na Serikali. Mfano, Kijiji cha Mwenehemba, Mamsinde one, Namsinde two, Kakozi, Chilangu na vinginevyo.

Je, ni lini, Serikali itatusaidia ili kumalizia maboma haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itasaidia umalizaji wa maboma haya 20 aliyotaja Mheshimiwa Condester Sichalwe kadri ya upatikanaji wa fedha. Nitumie nafasi hii kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanatenga fedha katika mapato yao ya ndani kuunga mkono juhudi za wananchi katika maeneo yao ya kiutawala ili kuweza kumalizia iwe ni katika zahanati iwe ni katika shule.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Je, Wizara ya Kilimo inaonaje ikitumia muda huu kufungua dirisha la kuwakopesha wakulima mbegu, mbolea, viuatilifu na vitendea kazi vingine ili kujiandaa na msimu wa kilimo ambao unakuja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Mbegu tupo katika utaratibu wa kuanza kusambaza mbegu kwa msimu unaokuja, kwa kufungua madirisha kupitia hayo maeneo tofauti tofauti. Vilevile tunao Mfuko wetu wa pembejeo ambao nao ni mahsusi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kuweza kupata pembejeo hizi kwa wakati na kwa bei nafuu. Hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wakulima wote nchini Tanzania kutumia madirisha haya mawili kwa ajili ya kuweza kupata pembejeo hizi kwa wakati ili wakati wa msimu wawe tayari wanazo na kuanza kutumia kwa ajili ya kilimo.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimeyasikia majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nataka tu kumwambia kwamba, migogoro ipo kwa sababu wananchi wanachukuliwa wanawekwa ndani. Sisi hii tunai-term kama mgogoro. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameshawahi kutuambia tulete maombi Wizarani. Tumeshaleta maombi: Ni lini maombi yetu yatajibiwa ili kuwapa wananchi kipande cha ardhi ili waendelee kuendesha shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, kama maombi haya yakitoka yatakuwa hapana, Serikali inachukua hatua gani kuendelea kuwasaidia wakulima hawa wapate maeneo ya kulima kwa sababu, ni Watanzania na hawana mahali pa kwenda ili kuendelea kulea watoto wao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa aliwahi kuleta maombi yake na haya maombi mchakato wake unaendelea. Ila kwenye upande wa matokeo ya haya maombi kwamba, yatakuwaje, inategemea sasa na maeneo ambayo sisi tunayaona kama ni ya muhimu, hususan kwenye maeneo ambayo tunatunza vyanzo vya maji na maeneo ambayo ni muhimu kwa kuhifadhiwa. Kwa hiyo, Serikali itafanya tathmini na itaangalia umuhimu wa maeneo haya kwa ajili ya kutunzwa na Serikali na yale ambayo tutaona tunaweza tukayaachia, basi wananchi wataweza kufaidika na maeneo ambayo tutaweza kuyaachia.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa, barabara ya Mlowo – Kamsamba iliingizwa kwenye bajeti kwa mwaka huu wa bajeti tulionao. Ningependa kujua ni lini Serikali itaanza kufanya kazi kwa vitendo, kuwaona wakandarasi site? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara zote ambazo tumezitengea kuanza utekelezaji kwa mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 ndiyo kwanza taratibu zinaandaliwa ikiwa ni pamoja na kuaanda tender documents ili ziweze kutangazwa, wakandarasi waombe na waweze kufanyiwa taratibu zote za manunuzi. Kwa hiyo, tupo kwenye taratibu za awali kwa sababu ndiyo tunaanza utekelezaji wa bajeti wa mwaka huu wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Momba hatuna stendi hata moja na kuna uhitaji mkubwa; je, ni lini Serikali itatupatia fedha tuweze kujenga kituo cha mabasi ili kitumike kama chanzo cha mapato kwenye Halmashauri yetu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wa Wakurugenzi wa Halmashauri kutambua maeneo kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwemo stendi, pia, ni wajibu wao kuanza kutenga fedha kupitia mapato ya ndani na kuwasilisha maandiko Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tunatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Momba kufanya tathmini ili tujue gharama zinazohitajika ili waanze kutenga mapato ya ndani lakini pia ofisi ya Rais TAMISEMI tuone uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya shughuli hiyo, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni lini Wizara ya Ardhi itaingilia kati kutusaidia kutatua migogoro iliyopo ndani Kata ya Kapele kwa kuwafuatilia watu wote ambao wamehodhi na kupora maeneo ya wananchi kinyume na utaratibu bila kuwa hati na wengine kuwa na hati za uwongo kwa kigezo na kusingizia wametumwa na wakubwa huko juu? Ni lini Wizara ya Ardhi mtatusaidia kutatua jambo hili?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Nina nyongeza ndogo kwenye majibu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa kuzungumza, naomba dakika moja kutoa shukrani. Kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambae amenipa kibali kuhudumu kwenye Wizara hii ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuhudumu na kumsaidia kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ninachoweza kumuahidi ni utumishi uliotukuka wa uadilifu. Nitatumikia kwa nguvu zangu na akili zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliomba Bunge lako tukufu ushirikiano na wakati wote nitakuwa tayari kwa ajili ya kufanya kazi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa nyongeza ndogo ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Serikali imejipanga na lipo suala la migogoro ya ardhi. Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri Nane ilishafanya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa 26 yote ya nchi nzima, kuendelea na utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge ambao wengi tumekutana na wameelezea kero zao akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Momba, Mheshimiwa Condester. Baada tu ya Bunge hili kuna mkutano wa Kimataifa Arusha na unaisha Alhamisi, tutajipanga kuanza ziara nchi nzima kutekeleza maagizo ya Baraza la Mawaziri kwenye vijiji 975. Vilevile, kutatua migogoro yote ambayo inajitokeza kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushirikiano. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa kata ya Ikuna ni miongoni mwa kata za kimkakati na ni kata ambayo ina wakazi wengi, na wananchi wameshaanza kujenga kituo cha afya kwa nguvu zao zaidi ya miaka miwili.

Je, ni lini Serikali itatupatia kiwango cha fedha ili tumalizie kituo hicho cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nawapongeza wananchi wa Kata hii ya Ikuna kwa kuanza kujenga kituo cha afya kwa nguvu zao. Tutakwenda kuchangia nguvu za wananchi kumalizia kituo hichi cha afya baada ya kufanya tathmini ya kuona hatua waliyofika na kiasi gani cha fedha kinahitajika. Lakini pia nimuombe Mkurugenzi wa Halmashauri atenge fedha pia za mapato ya ndani wakati tunatafuta fedha za Serikali Kuu. Ahsante.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Momba ni miongoni mwa halmashauri 56 ambazo zimewekwa kwenye kundi ambalo tutapangiwa hela za maendeleo asilimia 20. Je ni upi mkakati wa TAMISEMI kutujengea stendi kwenye Kata ya Kamsamba ukanda wa chini, Kata ya Ikana ukanda wa juu kwa sababu sehemu zote hizi zinaunganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Rukwa na kuna uhitaji kubwa sana wa stendi ili zitumike kaka chanzo cha mapato kwenye halmashauri.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sichalwe amekuwa akilifuatilia sana hili na amekuja mara kadhaa Ofisi ya rais TAMISEMI kulifuatilia hili jambo na tutaendelea kutenga fedha kadri ya upatikanaji wake ili tuweze kuwajengea wananchi wa Momba stendi hizi na kuiwezesha Halmashauri ya Momba kuwa na uwezo wa kupata fedha ya mapato kutokana na miradi hii.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, uhamisho pia ni sehemu ya maslahi ya walimu, je upi utaratibu ambao Serikali inautumia kwa ajili ya kuhamisha walimu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ili waache kutufuata Wabunge tuwasaidie uhamisho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, suala hili la uhamisho kuwa ni sehemu ya maslahi ya walimu, utaratibu uko wazi na Mwalimu anapokuwa ameajiriwa kwanza atakaa mwaka mmoja wa probation katika eneo lake ambalo amepelekwa kufanya kazi. Baada ya hapo pia atatumikia nafasi hiyo kwa miaka mingine miwili kabla ya kuomba uhamisho.

Mheshimiwa Spika, kwenye hili kumekuwa kuna influx kubwa sana ya watumishi kutaka kuhamia Mijini na kuhama maeneo ya pembezoni. Wakumbuke wakati wanaajiriwa waliajiriwa kwa sababu ya upungufu uliopo maeneo ya pembezoni ikiwemo maeneo mengine ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba kule. Hivyo ni wajibu wao kubaki katika maeneo yale na kuhudumia Watanzania waliokuwepo kwenye maeneo yale.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nataka kumweleza Mheshimiwa Waziri kwamba suala la pombe za kienyeji ni kwa lengo la kulinda viwanda vyetu vya ndani pia kulinda ubunifu wa watu wetu, kuongeza ajira na kuongeza uchumi kwa ajili ya kulinda mawazo ambayo yamezalishwa na wananchi wetu. Naomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka nimechangia hoja yangu ni mwezi umepita sasa. Je, ni upi mkakati wa Serikali kwa mwezi huu mmoja mmeshaanza kuzipatia leseni zile pombe ambazo mmezikataza kutumika kwenye jamii, mfano gongo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Je, kwa nini Serikali isiongeze kodi kwenye pombe zote ambazo zinaingizwa kutoka nje mithili hiyo ya spirit na pombe zingine ili kuzipa thamani pombe zetu za ndani na kuwavutia wawekezaji wote waje wawekeze kwenye pombe zetu za ndani ili tulinde soko letu la ndani na mawazo ambayo yametokana na watu wetu wa ndani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli tunajua mchango mkubwa sana wa sekta hii ya pombe na hasa pombe za kienyeji ambazo akina mama wengi ndiyo wanashiriki huku kama wajasiriamali kutengeneza pombe hizi za kienyeji na ndiyo zimekuwa nguzo na msingi mkubwa kulea familia katika kaya nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mkakati madhubuti na ndiyo maana nimesema tumeshaweka mikakati mojawapo ni kuona namna gani tunawasaidia kuwafundisha na kuwawekea teknolojia sahihi ili waweze kuzalisha pombe za kienyeji zinazokidhi viwango na ambavyo vitakuwa havina madhara kwa wanywaji. Kupitia TBS kwa maana ya shirika la viwango na SIDO tumeshaweka fedha katika bajeti ambayo itatumika kama ruzuku kuwafundisha, kuwafuata kwanza wazalishaji wa pombe hizi za kienyeji kule waliko vijijini lakini kuwafundisha namna ya kuzalisha pombe ambazo zinakidhi viwango ili ziweze kuendelea kutumika katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zile pombe ambazo zilikuwa na madhara ambazo ndiyo wanasema zimepigwa marufuku tunataka tuwasaidie ili athari ile isijitokeze na baada ya hapo zitaruhusiwa kuendelea na kupewa ithibati ya ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Serikali inafanya juhudi mbalimbali na hili ni dhahiri kwamba katika kuhakikisha tunafungua uchumi wa nchi yetu ni pmoja na kuruhusu biashara huru kulingana na taratibu na kanuni zilizopo, kwa maana ya kurusu pia bidhaa kutoka nje ya nchi kama vile ambavyo sisi tunauza nje ya nchi bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vyetu. Kwa hiyo, tunaendelea kuweka mkakati madhubuti kulinda viwanda vya ndani pale ambapo tutaona kwamba vinatakiwa kufanya hivyo na tumeshaanza kufanya na katika sekta hii ya pombe pia tutafanya hivyo ili kuwasaidia wananchi kunyanyua kipato lakini kuinua uchumi wa nchi yetu. Nakushukuru.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nilitaka tu nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba tumelipokea wazo lake la kuongeza kodi kwenye pombe na tutakamilisha kufanyia kazi na tutatoa majibu tutakapokuwa tunatoa kauli ya Serikali kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka huu. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Ni kweli tulitengewa fedha, Shilingi bilioni moja kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amejibu kwenye maswali yangu ya msingi. Barabara hii ya Ikana – Chitete ni barabara ambayo inaunganisha Tarafa ya Ndalambo pamoja na Tarafa ya Msangano ambapo Tarafa ya Ndalambo ndiyo kuna soko la kimataifa. Shilingi milioni 400 ambazo tumetenga kwa sasa haziwezi kushusha ule mlima; je, Serikali haioni kupitia Wizara ya TAMISEMI angalau mtuongezee shilingi milioni 600 nyingine ili tuweze kushusha ule mlima kikamilifu kama ambavyo Mlima wa Jimbo la Kwela unapitika? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge, jiografia ya kule na kuna mito mingi kwa ajili ya kueleka katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya hii ya Momba kule Chitete na inaunganisha pia tarafa hizi mbili ya Ndalambo na Msangano. Kama nilivyokuwa nimeshasema kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali ilikuwa imeanza ukarabati wa njia hii katika yale maeneo ambayo yalikuwa ni korofi sana. Tutakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona ni namna gani tunaweza tukaongeza nguvu kwa ajili ya kuongeza ukarabati wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kuna maeneo ambayo mto unapita ukitoka juu kwa sababu tunapozungumzia ni chini na unatakiwa upite kwenda kupanda mlima mrefu sana na kukutana na barabara ya Zambia. Tayari Serikali ilikuwa imeshaanza ukarabati wa vivuko vile katika maeneo ambayo maji pia yanapita. Kwa hiyo, tutakaa na Mheshimiwa Condester kuweza kuona ni namna gani tunaendelea na ukarabati huu. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kumekuwa na changamoto ya wanafunzi kwenye Jimbo la Momba kupoteza maisha kwa ajili ya kwenda kufata maji mtoni. Siku za usoni tulipoteza mwanafunzi wa Momba Secondary na tukapoteza mwanafunzi wa Sekondari ya Kamsamba kwa sababu wanaenda kufata maji mtoni kwa mwendo mrefu. Je, ni ipi kauli ya Wizara ya Maji kwa udharula wake kwenda kutuchimbia visima kwenye hizi Sekondari ili tusiendelee kupoteza maisha ya watoto wetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupe pole sana kwa wananchi kupata kadhia hizi lakini sisi kama Wizara ni sehemu ya kuona kwamba tunafikisha maji safi na salama maeneo yote yanayotoa huduma, na kwa eneo hili la shule naomba nikuahidi kwamba tutakuja kuwachimbia kisima na kama kuna kisima jirani basi tutafanya extension ili kuhakikisha wanafunzi hawaendi mtoni na kupata madhara.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba yako Chitete na kwa bahati mbaya eneo hili halijapitiwa na Mkongo wa Taifa hivyo kusababisha changamoto ya mawasiliano kwenye tarafa ya Kamsamba na tarafa yote ya Msangano. Je, ni lini tutachepushiwa Mkongo wa Taifa kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna njia tatu za kufikisha mawasiliano pale ambapo hatujafikisha Mkongo wa Taifa. Tunatumia microwave na pale ambapo microwave haiwezi kufikisha tunatumia Virtual Satellite lakini kwa sababu ni nia na dhamira ya Serikali kuhakikisha nchi yetu yote inafikiwa na Mkongo wa Taifa. Mpaka sasa tumeshafikia Mikoa 25 lakini baada ya kufika Mikoa 25 tutaenda sasa Wilaya kwa Wilaya na mpaka sasa tumeshajenga kilometa 8319 lakini vilevile katika bajeti ya miaka miwili iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu. Mheshimiwa Rais aliridhia fedha takribani bilioni 345 kwa ajili ya kufikisha Mkongo wa Taifa katika maeneo mbalimbali ambapo ni kilometa 4442 zinaenda kujengwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini kwamba zikisha kamilika tutakuwa tumefikisha kilometa 12314 ambapo ni sawasawa na asilimia 85 ya utekelezaji na lengo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi kufikia mwaka 2025, nakushukuru.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka 2021 Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alifanya ziara kwenye Jimbo la Momba kumwonesha mahali ambapo tunapendekeza kujenga kituo cha forodha. Mwaka huu mwezi wa pili Mheshimiwa Waziri Mkuu pia tulimshirikisha wazo hilo na akaona ni jema;

Je, Serikali imefikia hatua gani kujenga kituo kipya cha forodha ndani ya Jimbo la Momba ili kunusuru kituo cha forodha kilichopo Tunduma kwa sababu kimezidiwa ili kiweze kutoa huduma kwa ufasaha?
NAIBU WAZIRII WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hicho ni kweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha alienda lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alienda. Tuna mpango wa kujenga kituo hicho. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subra mara tu fedha zitakapopatikana tutajenga kituo hicho.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza kilimo cha michikichi kwenye Mkoa wa Songwe kwa sababu uoto wa eneo hilo unakubali zao hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba zao la mchikichi linaendelea kulimwa katika maeneo yote ambako tumepima afya ya udongo na inakubali na kwa Mkoa wa Songwe kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema sasa hivi tuko katika uzalishaji wa miche na wenyewe pia tutauweka katika mpango wa kuhakikisha kwamba wakulima wa Songwe wanapata miche ya michikichi na wanafanya uzalishaji kama katika haya maeneo mengine.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nimesikia majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika vijiji ambavyo vimesalia nguzo zimepelekwa maeneo hayo na zimeachwa kwa muda mrefu na wananchi wamechukulia kwamba nguzo hizi zimetelekezwa; je, ni lini shughuli itaendelea kwa ukamilifu kuona nguzo zinasimikwa na vijiji hivi vinawashwa umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika vijiji ambavyo vimepatiwa umeme, umeme umekuwa sio toshelevu hivyo wawekezaji kuvunjika moyo kushindwa kufanya shughuli zao zinazohitaji umeme mkubwa; je, ni lini Serikali itatuwekea capacitor au booster kwenye vijiji hivyo ikiwa ni sambamba na kujenga kituo cha umeme mkubwa kwenye Kata ya Nkangamo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, kwenye hivi vijiji 20 ambavyo vimebaki kazi katika hatua mbalimbali zinaendelea. Mkandarasi anayefanya kazi katika Mkoa wa Songwe kwa ujumla anaitwa DEM, ni mkandarasi ambaye anaendelea kutekeleza kazi yake na katika mkoa yuko zaidi ya asilimia 80.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Condester kwamba kabla ya Disemba mwaka huu maeneo yote yatakuwa yamepatiwa umeme kwa sababu hatua ni moja moja kwenye maeneo tofauti tofauti, lakini nimhakikishe kwamba vifaa hivi ambavyo vimewekwa katika maeneo hayo ni vile ambavyo vitakuja kutumika katika maeneo hayo, havijatelekezwa na vitatumika kufanya kazi ambazo zinastahili kufanyika.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, ni kweli kwamba kumekuwa kuna upungufu wa umeme katika maeneo mbalimbali na ni kwa sababu ya mahitaji kuwa makubwa na sisi kama Wizara ya Nishati tunaendelea kufanya assessment, na katika awamu hiiya kwanza ya Mradi wetu wa Gridi Imara tumetenga vituo vya kupoza umeme 15 katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji makubwa yalivyo. Namhakikishia Mheshimiwa Condester pia kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo angalau mwaka 2030 kila Wilaya iwe imepata kituo cha kupoza umeme kulingana na uwezekano wa upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini, ili kuhakikisha kwamba tunafikisha umeme wa kutosheleza katika maeneo yote, lakini nimuombe baada ya hapa tutawasiliana ili tuone hilo eeo ambalo ni mahususi analolisema lina upungufu sana wa umeme saa hizi tulichukulie hatua mahususi na za haraka zaidi, ili kuwavutia wawekezaji zaidi.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ziko baadhi ya Halmashauri hapa nchini ambazo mapato yake sio toshelevu hivyo hawawezi kutosheleza kutoa mikopo ya asilimia 10.

Je, ni upi mkakati wa Wizara hii kuwawezesha wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya kitongoji na vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inawaagiza Maafisa Tawala wa Mikoa na Maafisa Ustawi wa Jamii waendelee kutoa elimu kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu, ili kuweza kujiinua kiuchumi na kuhakikisha wanakuwa vizuri katika maisha yao na maendeleo yao. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na majimbo ambayo hayana ofisi kabisa mpaka sasa ikiwa ni sambamba na kuona kama wanaweza wakaziboresha ofisi ambazo zilijengwa na Bunge na zimechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe, Mbunge wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wabunge wengi bado hawajafikiwa kupata ofisi kamili katika maeneo yao na Serikali tumekuwa tukitenga bajeti kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha kuhakikisha tunajenga. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwa muda ambao Serikali imejipangia, ninaamini Wabunge wote watapata ofisi kulingana na hadhi yao. Ahsante sana.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, katika majibu ya msingi ya wizara inaonesha wanazungumzia zaidi biashara kati ya nchi ya Zambia na Tanzania, lakini geti la Tunduma ninaongelea ni biashara kati ya nchi ya Zambia na nchi ambazo ziko SADC ambazo ni zaidi ya saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza kama yafuatavyo; kabla ya maboresho ya bandari zetu lile ilikuwa asilimia 70 ya mizigo inapitia geti lile, kwa hiyo tafsiri yake kama tumeboresha bandari zetu na Kongo wameingia kwenye East Africa ina maana kwamba nchi zingine zitapitisha mizigo pale.

Je, Serikali haioni kuna ulazima na uharaka sana kuhakikisha wanaongeza geti lingine ili kuboresha huduma na ufanisi unaotakiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kama ambavyo ziko nchi nyingine ambazo tunapakana nazo, mfano Kenya, kuna mageti ya forodha zaidi ya mawili au matatu, mfano Holili, Namanga, Tarakea na lile geti la Mombasa na Mheshimiwa Waziri alifanya ziara kwenye Jimbo la Momba mwaka jana.

Je, hamuoni sasa kuna haja kabisa ya kuhakikisha nchi ya Zambia ambayo inahudumia nchi zaidi ya saba ya SADC kupata geti lingine ndani ya Jimbo la Momba ili kuhakikisha tunaongeza mapato?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yanafanana maswali yake yote mawili kwa hiyo ni suala moja na nimesema katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali inafanya uchambuzi na tathmini kupitia katika sehemu hiyo pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tukiona Serikali ipo haja ya kuongeza geti basi Serikali yetu ni sikivu, na iko tayari kufanya hivyo, ahsante.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa. Skimu ya Umwagiliaji ya Naming’ong’o iliyoko kwenye makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Chitete ndio skimu ambayo tunaitegemea sana katika kuhakikisha wakulima wetu wanaweza kulima kwa ufasaha.

Je, ni lini Serikali itafanya maboresho ya skimu hii ya Naming’ong’o ili iweze kuleta tija ukizingatia mwaka huu hakukuwa na mvua na wakulima wengi wamekausha sana mpunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Condester, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya kazi kubwa ambayo tumeipa Tume ya Taifa Umwagiliaji ni kuhakikisha inazipitia skimu zote nchini Tanzania ili kufahamu status yake, kujau ipi inahitaji marekebisho na ipi ifanyike nini iweze kuboreshwa. Nimwahidi Mheshimiwa Mbunge na skimu aliyoitamka tumeweka katika mipango yetu kwa ajili ya utekelezaji ndani ya Serikali.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri nakuja kwako tena leo kwa mara ya saba, naomba commitment yako. Je, ni lini utatuboreshea mawasiliano kwenye Kata ya Mkomba, Kata ya Kapele na Ming’ong’o Chitete na maeneo mengine yote ambaypo kuna changamoto ya mawasiliano ndani ya Jimbo la Momba?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe kwa niaba ya wananchi wake wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba anawatetea wananchi wake wa Jimbo la Momba; lakini kwa bahati mbaya katika Mradi wetu wa Tanzania Kidijitali haikuweza kuchukua kata zote kwa sababu tunaelewa kwamba changamoto ya mawasiliano bado ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini habari njema sasa ni kwamba Mheshimiwa Rais ameshapata fedha na tayari Wizara yetu iko katika mchakato wa kukamilisha mambo ya mikataba ili tupate fedha kwa ajili ya kwenda kujenga minara mingine Zaidi. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kata ambazo amezitaja tutahakikisha kwamba zinakuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ahsante sana.