Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Condester Michael Sichalwe (14 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijalia kibali kusimama mahali hapa. Vilevile nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa heshima na imani ambayo walinipa. Pia nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Momba kwa kuniamini na kunituma mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuwashukuru sana wazazi wangu kwa kunilea na ushirikiano mkubwa ambao walinipa kipindi cha uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa asilimia 101. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Rais huyu na kusema kwamba ni miongoni mwa viumbe ambao wamemkopesha Mungu kwa kiasi kikubwa sana. Maandiko matakatifu yanasema kwamba anayemsaidia mnyonge na maskini anakuwa amemkopesha Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitano amefanya mambo mengi ambayo amewagusa wanyonge na maskini wengi sana na watu ambao walikuwa hawana watu wa kuwasemea, yeye amekuwa ni msemaji wao. Kwa hiyo, ninaamini hata katika vipindi vyake vigumu ambavyo atapitia, Mungu atazikumbuka na kuzitakabali hizo sadaka zake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ni kwa sababu ya muda, nilitamani kuchangia kwa kirefu kuhusiana na eneo la biashara. Kwenye eneo la biashara nitaenda kuongelea zaidi kwenye masuala ya mipaka. Sehemu nyingi ambazo ni za border kumeonekana kuwa na mwamko mzuri sana wa biashara. Nikitolea mfano kwa border ya Namanga na Tunduma, ni sehemu ambazo zina wafanyakazi ambao wamesoma na kuajiriwa wachache sana kuliko wafanyabiashara wanaokuwepo pale. Hivyo, inapelekea kuwepo kwa maendeleo mbalimbali ya kijamii, pia hata vijana na watu mbalimbali kuendelea kupata riziki na watu wengi kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa 26 nataka ku- quote kipengele kidogo tu kwa sehemu, Mheshimiwa Rais anasema hivi; “…na kwa bahati nzuri tangu mwaka jana tumeanza kutekeleza mpango wetu wa kuboresha mazingira ya biashara nchini, yaani blueprint for regulatory reforms to improve the business environment in Tanzania.”

Mheshimiwa Spika, nataka kusema hivi, nitolee mfano wa mpaka wa Zambia na Tanzania ambapo kidogo angalau nimekuwepo kwa hizi nchi za Kusini mwa Afrika na Afrika ya Kati. Naomba kuishauri Serikali na kuiomba, kama mawazo haya yanaweza yakawa chanya na yakasikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iweze ku-expand mipaka yake. Pamoja na kuipongeza kwamba imepiga hatua sana katika kujenga hizi One Stop Border, mfano border ya Namanga na Tunduma, zimejengwa katika kipindi cha miaka mitano, lakini ipo hasara kubwa sana ambayo Serikali inapata kwenye hii mipaka. Bado biashara nyingi ambazo ni haramu, biashara za magendo, kutoroshwa kwa mazao vinaendelea kufanyika kwenye hii mipaka kiasi kwamba kama Serikali ingeamua ku-expand ile mipaka tungeweza kuzuia biashara haramu nyingi na biashara nyingi za magendo ambazo zinafanyika kwenye hii mipaka, ikasababisha Taifa likaendelea kukusanya fedha ya kutosha ambayo itaendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nikitolea mfano mpaka wa Zambia na Tanzania, ndiyo mpaka ambao unabeba karibu nchi zote ambazo ziko Kusini mwa Afrika. Mfano, tunapoongelea mji mmoja wa Livingstone pale Zambia, ndiyo mji ambao unapokea mpaka wa Botswana, Namibia na Zimbabwe. Kwa hiyo, nitolee mfano labda bidhaa za magendo zinapotaka kupitia lile jengo la SADC zinapitaje?

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano wa kwenye Jimbo langu na hapa ninaiomba Serikali ikiwapendeza tupewe geti. Kwenye mfano huu naeleza, unapotoka pale Livingstone, kwenye zile nchi tatu, tuchukulie amekuja na biashara za magendo, anataka kukwepa kodi ya Serikali… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa, niendelee kukupongeza wewe kwamba katika kipindi chote ambacho mimi nimekuwa nikikufuatilia kuanzia ukiwa Naibu Spika na mpaka sasa hivi umekuwa Spika, kiukweli nafurahishwa na namna ambavyo unaendesha Bunge hili. Mimi niseme kwamba ni miongoni mwa Maspika bora kabisa Afrika ambao wanapaswa kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais na niendelee kusema kwamba hata yeye amekuwa ni record breaker. Ni miongoni mwa Marais ambao wameingia kwenye historia, hakuna Taifa lolote kwa sasa ambalo unapotaja jina la Dkt. John Pombe Magufuli hawamjui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuchangia Mpango wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja kwenye eneo la biashara na niendelee kuongelea kwenye eneo la mipaka. Mimi natamani kuishauri Serikali, kama ambavyo ulisema hapo kwamba sisi Wabunge wawakilishi wa wananchi ndiyo watu wa kwanza kabisa na sahihi wa kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado haijautendea haki mpaka wa lango la SADC. Napoiongelea nchi ya Kenya ina mipaka zaidi ya minne, kuna mpaka wa Sirari, Namanga, Holili, Tarakea na ule ambapo ukipita Tanga unaenda Mombasa, bado yote ile ni Kenya. Nchi moja tu ina mipaka karibu mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali kwa kusema kwamba, there is no way Zambia itakuja kupata bahari. Dunia imeumbwa na itaondoka Tanzania ndiyo yenye bahari. Kwa vyovyote vile nchi zote ambazo ziko Kusini mwa Afrika zinategemea bandari ya Tanzania kutoa vitu vyao kutoka kwenye nchi za Ulaya na bado wanatarajia kupita Zambia kwa ajili ya kupeleka kwenye nchi nyingine. Kwa hiyo, naweza nikasema kwenye lile geti moja tu la pale Tunduma ni mpaka ndani ya mpaka. Unaonekana tunapakana na Zambia, lakini nyuma tumebeba nchi nyingi. Je, Serikali haioni sababu ya kupanua mpaka ule ili tuendelee kunufaika nao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natokea sehemu zile za Tunduma. Kumekuwa na wimbi kubwa sana la ndugu zetu kutoka vijijini, hata kwenye Kijiji changu ambacho mimi natoka, wapo wafanyabisahara pale wanasukuma baiskeli tu kwa ajili ya kupokea mizigo, lakini unapokuwa Tunduma hakuna biashara yoyote kubwa ya nyumba za kupanga kwa sababu hata Mtanzania wa kawaida ambaye hajui kusoma na kuandika kwa biashara ndogo ambayo anaifanya pale kwenye mpaka ana uwezo wa kujenga na kuishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaendelea kulalamika kwamba hakuna ajira. Je, hatuoni sababu ya kuboresha mipaka na sehemu nyingine hata wale wa darasa la saba mipaka itakapotanuliwa watakuja kupokea mizigo ya wageni, watajipatia riziki kwa sababu Mungu hakutuumba watu wote tukafanana ndiyo maana kuna Rais, Waziri, mwalimu wa shule ya msingi na kuna msukuma mkokoteni. Kwa hiyo, tutumie fursa tulizonazo kwa ajili ya kutatua matatizo. Bora kidogo cha halali kuliko kikubwa cha haramu, hata Maandiko Matakatifu yanasema, aliyenacho huongezewa asiyekuwanacho hunyang’anywa hata kile alichokuwanacho, lakini sisi tunavyo hatuvitumii sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano ule ambao nilitaka kutoa nilipoishia, ni kwa namna gani biashara za magendo zinavyotoka zile nchi za Kusini mwa Afrika na hata nchi za Afrika ya Kati mfano Kongo. Kwa mfano, nikiongelea vipodozi, vipodozi vya kutoka Kongo vimekatazwa kuingia hapa nchini Tanzania inachukuliwa ni magendo, lakini ukipita huko Dar-Es-Salaam na sehemu nyingine, bado unakuta carolite zinauzwa, zinapitaje kama pale patrol inafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Jimbo la Momba. Unapokuwa pale Livingstone, Zambia, mtu anapotoka na bidhaa Namibia, Zimbabwe au Botswana, anapoingia Lusaka unafika mji mmoja unaitwa Mpika, pale kuna njia mbili njiapanda. Whether uamue kwenda Ndola ambapo uende border ya Kasumbalesa kule mtu achukue vile vipodozi. Anapokuwa pale Mpika ana uwezo wa kuamua kupita barabara ya Tunduma atokee pale lilipo lango la SADC au aamue kupita mahali kunaitwa Kasama kutokea Mbara Road anaingia upande wa Jimbo la Momba ambapo kutokea inapoanzia Tanzania kuingia tarmac ya Zambia ni kilometa moja tu na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliyesimama hapa ni living testimony, natoka kwenye kata ya mpakani, kipindi chote nikiwa nasoma Mbeya Day, inapofika kuanzia mwezi wa kumi na mbili, wa kwanza, barabara hazipitiki tunapaswa kwenda kupita Zambia ili tuweze kufika Tunduma, mazao na mifugo mingi inatoroshwa kwa kutumia njia hiyo kwa sababu iko wazi, hakuna utaratibu wowote pale. Serikali kama mnasikiliza ushauri tunaona ipo sababu, iko nia na manufaa ambayo tutayapata pale ambapo tutaongeza geti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea kuongezea, kuna soko kubwa la kimataifa ambalo limejengwa ndani ya Jimbo la Momba kwenye Kata moja inaitwa Ndalambo, Kakozi. Ni soko la kimataifa zaidi ya shilingi bilioni 8 Serikali imeweka pale. Kwanza, Serikali yenyewe iliona kwamba ni soko la kimataifa la mazao na mifugo lijengwe kwenye mpaka. Sasa kama limejengwa kwenye mpaka soko hili litachochewa na nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutataka tena kutoa mazao ambayo yanatoka Rukwa, Jimbo la Momba yaende yakapite Tunduma? Hizi halmashauri nyingine zinakuwaje? Zinawezaje kujitegemea kama haziwezi kusimama, mazao yote yanatoka yanaenda Tunduma na hili soko? Pia lilipo soko ndipo ilipo barabara ambayo inapita kwenda kwa baba yangu Mheshimiwa Kandege kwenda kwenye bandari ya Kalemii. Kwa nini kusiwe kuna sababu ya kupata geti? Tunaiomba na kuishauri Serikali tupate geti mahali hapo ili tuweze kuzuia biashara zote haramu na za magendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, kumetokea migogoro mingi sana ya ardhi, kutokana na kwamba tuko mpakani Congolese na Zambians wengi wanawatumia Watanzania hawa kwa ajili ya kuja kumiliki ardhi kwa sababu ni kwenye mpaka. Tunaiomba sana Wizara yenye dhamana husika jambo hili muliangalie kwa karibu sana. Tunaomba Wizara ya Ardhi ifuatilie hati zote ambapo watu wanaonekana wanapata hati ndani ya Halmashauri ya Momba na muda mwingine ni wafanyabiashara hawa wanavaa uhusika wa Tanzania lakini wanawalinda hawa watu ni wahamiaji. Sheria ya Ardhi ya Tanzania inamkataza mtu yeyote asiyekuwa Mtanzania kumiliki ardhi. Kama anataka kumiliki kama mwekezaji ziko sheria ambazo zina mwongozo mtu huyo ni kwa namna gani anaweza kumiliki ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea hapohapo kwenye suala la ardhi. Sisi watu wa Halmashauri ya Momba na halmashauri nyingine ambao wanapitia changamoto kama hii, hatutamani kuona tunafika kwenye matatizo ambayo ndugu zetu wa Kiteto na Morogoro wanayo. Limetokea wimbi kubwa la wawekezaji ndani ya Jimbo la Momba kutokana na ule mwamko wa lile soko kuwepo na ule mpaka, kuja kumiliki ardhi kinyume na taratibu. Kaka yangu Mheshimiwa Kunambi alisema pale, tunaomba ardhi ambayo inaonekana iko sehemu ambayo ni muhimu, kwa mfano sehemu kama hizi za mipaka, kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wengi wao wanakuwa ni watu wa kipato kidogo, Serikali iingilie kati iyapime yale maeneo. Itusaidie kuyapima siku zijazo yatatusaidia kwa sababu tunajua tu lazima mpaka utafunguka, biashara nyingi zitafanyika na ardhi itapanda thamani mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji hawa cha kwanza wanamiliki ardhi kinyume na taratibu. Mtu anamiliki ardhi eka 800, lakini amepata hati ambayo amepewa na Kijiji au mtu anamiliki ardhi zaidi ya eka 100, kutoka eka 50 mpaka eka 100 alipaswa angalau apewe na halmashauri, lakini anasema ana hati ya Kijiji. Wanamiliki ardhi kinyume na taratibu lakini hawaziendelezi ardhi hizi pia hawalipi kodi ya ardhi. Wao ndiyo watu wa kwanza kuchukua sheria mkononi na kuanza kuwaweka watu ndani. Wao wameshavunja sheria tatu, lakini wanawaweka watu ndani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: AHsante sana Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kuishukuru na kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa mambo ambayo waliweza kutufanyia katika Jimbo la Momba katika Awamu ya Tano, na mambo ambayo wanaendelea kutufanyia katika Awamu hii ya Sita; tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwamba tuna imani sana na wewe kwenye Wizara husika ambayo umepewa kuisimamia, lakini pia kuendelea kuwapongeza kaka zangu, Manaibu hodari sana ambao wanamsaidia dada yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba niwasilishe baadhi ya changamoto za wananchi wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo. Nitaongelea kwenye miundombinu ya barabara pamoja na madaraja; miundombinu ya elimu; miundombinu ya vituo vya afya pamoja na zahanati na muda ukiwa Rafiki nitamalizia na namna gani kuendelea kuwawezesha akinamama wa vijijini katika ubunifu wao mbalimbali walionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Momba ndilo jimbo ambalo tuseme kwa Mkoa wetu wa Songwe linaongoza kwa kiasi kikubwa sana kulima mpunga, maharage pamoja na mahindi. Na tunaweza kusema ndilo jimbo ambalo linalisha Mkoa mzima wa Songwe kwa mbegu, au tuseme kwa zao la mchele. Lakini pamoja na nchi ambazo ni Jirani kama Kongo na Zambia, wanategemea sana mchele pamoja na maharage kutoka kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, kutokana na mambo ambayo Waheshimiwa wenzangu ambao wametangulia kueleza hapa. Ufinyu mkubwa uliopo kwenye bajeti ya TARURA ni wazi kwamba hata nitakapoeleza changamoto nyingi ambazo zinalipata Jimbo la Momba sitaweza kumaliza. Kiukweli Jimbo la Momba ni miongoni mwa majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa ambavyo ninaongea hapa ni kweli ziko kata ambazo ziko pia visiwani, zimebaki kwasababu hakuna madaraja, barabara siyo rafiki, hawawezi wakatoka kwenda kijiji kingine, hawaweze wakatoka kwenda kata nyingine, wanaendelea kusubiri mpaka mvua zitakapokauka ndipo waendelee kupitia kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hali hiyo imeendelea kusababisha kudorora sana kwa mapato ya halmashauri yetu, pamoja na kwamba jimbo linaendelea kuhudumia na nchi nyingine ambazo zipo mpakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali; kwa kuwa network ya barabara ambazo ziko ndani ya Jimbo la Momba ni barabara 57 zenye urefu wa kilometa 647.21, ninajua kwa ufinyu wa TARURA barabara hizi haziwezi kutekelezeka. Niende kwenye uhalisia; tunaomba tuombe barabara chache za kimkakati ambazo kuwepo kwa barabara hizi Serikali itakapotuwezesha, kunaweza kukachangia kwamba halmashauri ikaongeza mapato yake, lakini pia ikavutia maana zitakuwa ni barabara za kimkakati. Lakini pia inaweza ikafanya hata wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika maeneo hayo, yakawavutia kuendelea kubaki hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kwanza ambayo nianze kuiombea ni barabara ya Makamba – Ikana. Na barabara hii sababu ya kuiombea barabara hii ni kwamba ndiyo barabara ambayo inaunganisha Jimbo la Momba kwa ukanda wa juu na wa chini na soko la kimataifa la mifugo na mazao limejengwa katika Tarafa ya Ndalambo ambalo tunalitegemea sana katika kupandisha mapato ya halmashauri na kuliongezea Taifa mapato yake kwa kuwa tutaendelea kusambaza kwa wingi na kwa ubora kwenye nchi zetu ambazo ziko Jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii tutakapokuwa tumeipata barabara hii, itakuwa imerahisisha Tarafa za Msangana na Kamsamba ambazo zina jumla ya kata nane, kwa hiyo watapandisha mazao yao kwa urahisi kwa ajili ya kwenda kufika kwenye soko la mifugo na mazao ambalo lipo Kakozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayoiomba ni barabara ya Chindi – Msangano ambapo kuwepo hapo kuna daraja kubwa ambalo limetenganisha Halmashauri ya Wilaya ya Momba pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Kwa hiyo kama barabara hii itafunguka, na tutakapopata daraja katika eneo hilo, itatusaidia sana wananchi kuendelea kuwa na options mbalimbali kwa ajili ya kupeleka mazao mengine au na shughuli nyingine za kiuchumi kwenye Mji wa Tunduma ambao tunautegemea kama mji ambao uko mjini kwa ajili ya kuendelea kupata mahitaji mbalimbali, ikiwa na hospitali ya wilaya iko kwenye Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayoiombea ni barabara ya Ivuna – Chole. Barabara hii inaunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Momba pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe. Na wananchi ambao wapo katika Kata ya Mkomba wanatenganishwa na daraja kubwa. Mwenyewe kipindi cha mvua nikienda kufanya ziara ni lazima nibebwe mgongoni kwasababu baiskeli haiwezi kupita, pikipiki haiwezi kupita, gari haliwezi kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara nyingine ambayo naomba ushughulikiwe ni barabara ya Kakozi – Ilonga. Barabara hii ndiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Songwe pamoja na Mkoa wa Rukwa. Barabara hii pia Mheshimiwa baba yangu Mheshimiwa Kandege naye ninajua itamsaidia sana kuja kutumia lile soko la mifugo na mazao kwa sababu ataleta mazao yake pale. Vilevile barabara hiyo ndiyo ambayo inapita mpaka kufika kwenye Bandari ya Kalemii.

Kwa hiyo, itasaidia wananchi wa Jimbo la Momba na Majimbo mengine ambayo yapo kwenye Mkoa wa Songwe na kwenye Halmashauri zingine wanaweza wakaitumia kwa ajili ya kufikisha mazao yao au vitu vyovyote kwenye bandari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri kidogo kwa Serikali namna gani inaweza ikatusaidia kuongeza pato kidogo kwa TARURA. Nitolee mfano wa wananchi wangu wa Jimbo la Momba. Wananchi wa Jimbo la Momba kwa asilimia ni wachache sana ambao wana simu za smartphone, kwa hiyo, mtu anaponunua kifurushi anapewa dakika za maongezi, SMS za ku-chat pamoja na MB lakini kwa sababu ni watu wa kupiga tu hata ku-chat kwa SMS za kawaida hawa-chat, inapofikia kile kifurushi kina-expire anakuwa ametumia dakika lakini MB pamoja na SMS zinakuwa zimebaki lakini mtu yule anakuwa ameshalipia na kodi ya Serikali amekatwa kwenye ule muda wa maongezi. Mnaonaje kama TAMISEMI wataamua kwamba kile ambacho kinakuwa kimebaki kwa sababu ni cha mwananchi na alikilipia kwa pesa yake halali akatolea na kodi kwa nini isirudi ili ije kwa ajili ya kusaidia vitu kama hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwa Waheshimiwa Wabunge tuna experience kitu hiki, umenunua dakika, SMS na MB unatumia kidogo vinabaki vinaenda wapi? Kwa hiyo, tunayafaidisha makampuni ya simu ambayo yameshatuchaji na tunawaachia bure, hivi viki-expire tuwekeane mwongozo vinarudi kwa Serikali kwa sababu itakuwa ni changizo halali la mwananchi huyu. Kwa hiyo, mimi naona inaweza kutusaidia kukusanya na kuboresha barabara na katika hilo dada yangu Mheshimiwa Ummy mtukumbuke huko Momba, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kwenye miundombinu ya elimu, kutokana na Jimbo la Momba kuwa na changamoto nyingi za barabara imepelekea mazingira ya walimu wengi ambao wanafanya kazi ndani ya Jimbo la Momba yanakuwa si Rafiki. Walimu hawa kuna wakati wanakuwa wananung’unika, hawana motisha ya kufanya kazi vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa. Kwanza kabisa nianze kwa kusema kwa kuwa muda ni mfupi namwomba baba yangu Mheshimiwa Waziri Simbachawene pamoja na Naibu Waziri, wapate nafasi ya kutembelea Jimbo la Momba ili kwa haya ambayo nitayaainisha kutokana na muda mfupi, sitaweza kupata nafasi ya kuelezea kwa kina, watakuja kujionea kwa uhalisia wenyewe nitakachokiongea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kwanza ambayo nataka kueleza hapa ambayo inawapata Jeshi la Polisi na wanashindwa kutekeleza majukumu yao vizuri kwa wananchi wa Jimbo la Momba, jambo la kwanza ni usafiri. Jimbo la Momba ni Jimbo ambalo ni pana sana, lina square meter za mraba 5,856; vijiji 72 na vitongoji 302. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani Askari hawa wanawezaje kufanya kazi; kutoka kijiji kimoja kwenda kingine wakati mwingine ni zaidi ya kilomita 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uhalifu unapotokea mfano labda Kijiji cha Itumba, Kata ya Nzoka mpaka Askari huyu afike eneo la tukio kwenda kuwasaidia wananchi hawa, nasi tuko kwenye Jimbo la mpakani, unakuta wahalifu hawa wameshakimbia, wameondoka, wametokomea Zambia. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali na Wizara hii itutazame, tupatiwe gari ili Askari hawa waweze kufanya kazi yao vizuri. Wakati mwingine hata lambalamba tu wanatusumbua sana. Hatuwezi hata ku-deal na lambalamba.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Taarifa Mheshimiwa.

SPIKA: Endelea wa taarifa. Mheshimiwa Condester, kuna taarifa unapewa. Upande gani?

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hali iliyoko kule Momba ni sawa sawa na Nyang’hwale, tuna magari mawili Landcruiser lakini hayana matairi. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo, lakini sisi hatuna kabisa hiyo gari.

SPIKA: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, hatuna kabisa hilo gari, hata pikipiki hakuna; hata baiskeli hakuna.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Jimbo la Momba, yaani Halmashauri ya Wilaya ya Momba ndiyo Jimbo ambalo linabeba Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Majimbo mawili ya uchaguzi…

SPIKA: Kwa hiyo, Mheshimiwa Amar Hussein afadhali wewe una magari hayana matairi, mwenzako hata baiskeli hana. Sijui yupi zaidi sasa hapo. Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni kuhusiana na kwamba Jimbo la Momba yaani Halmashauri ya Momba ndio jimbo ambalo Makao yake Makuu inabeba Wilaya ya Momba, lakini hatuna kituo cha polisi ambacho kinafanana na hadhi ya wilaya. Tuna outpost mbili tu ambayo ni kituo kidogo cha Kamsamba ambacho kina askari nane, kituo kidogo ambacho kipo Chitete ambako ndio makao makuu, kina askari wanne, yaani hata ukipata ya Uchaguzi jamani askari huyu hana baiskeli, hana pikipiki anakwenda kumkamata nani.

Mimi kuna wakati nimefanya kampeni na lambalamba, maana yake nimekuta lambalamba anafanya mkutano wake na hawezi kuja kunisikiliza, wananchi wanafanya pale, kwa hiyo ikabidi tuwaombe kwa sababu hatuwezi kuwapigia Jeshi la Polisi watakuja na nini, watembee kilomita 50.

SPIKA: Mheshimiwa Condester, lambalamba ndio nini?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, lambalamba ni mkusanyiko. Ulinde dakika zangu Mheshimiwa Spika tafadhali, nitakapotoa ufafanuzi wa lambalamba.

Mheshimiwa Spika, lambalamba ni hawa wanajiita, sijui tusemeje! Sijui waganga wa kienyeji, kwa hiyo wakifika kwenye Kijiji wanahamasisha kwamba tumtafute mchawi na kitu kama hicho. Sasa vile vinaleta mgongano kwenye jamii, kwa hiyo utakuta wakati mwingine wananchi wanataka hata wakaague shule. Nimefika mahali nimewaambia Serikali haitambui uchawi, wananchi wanasema hapana si tunataka Mbunge ambaye anayetutetea, tunaumwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba sana, naamini kungekuwa na gari na kungekuwa na Kituo cha Polisi kizuri, kina Afisa mwenye nyota tatu, akapewa askari wa kutosha wangeweza kufanya patrol na kuzunguka, wananchi katika hali ya kawaida tunaogopa sana askari. Kwa hiyo kuona askari wanapitapita, wanalinda wanaona kwamba kuna usalama wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hatuna askari wa kike, nafikiri kwa sababu hatuna kituo ambacho kina hadhi ya wilaya ili Afisa mwenye nyota tatu akikaa pale kuna mwongozo wa Jeshi la Polisi ambao wanabidi awe na askari wa idadi fulani. Sasa tunajiuliuza sisi wananchi wa Jimbo la Momba sisi wote ni wanaume? Hapana, sasa tunakaguliwa na nani kama askari wote hawa ni wanaume? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hakuna nyumba za maaskari na wakati mwingine hata Kituo cha Polisi chenyewe huwezi ku-identify kama ni Kituo cha Polisi. Askari hawa wanalala wapi, wanajichanganya huko, wanapanga huko mitaani. Sasa kama ilivyo kuna imani za kishirikina, wakati mwingine wanaweza kuamini hata askari mwenyewe ni mchawi. Kwa hiyo akachomewa nyumba, kwa sababu kule watu wanakatana mapanga kwa hizi imani za kishirikina.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba baba yangu Mheshimiwa Simbachawene afike kule tu, kwa sababu muda hautoshi nisije nikasitishwa hapa, ili akajionee, tukatembee nimfikishe kule Katumba, nimpeleke kule Chole, Siliwiti na kule Kichangani Kamsamba. Akishaenda kuona tu, baada ya mwezi mmoja ataniletea askari hata 40 na atanipa gari.

Mheshimiwa Spika, ahsante san ana naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa rehema na huruma zake kuendelea kunipa kibali na nafasi kusimama tena kwenye Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nami niwasilishe maombi yangu kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali. Kupitia Jimbo langu natoa mchango huu kwa kuwa najua utakuwa unabeba taswira na azma nzima ya Taifa, natokea kwenye eneo la mpakani, tumekulia eneo hilo na kuona kwamba zipo fursa nyingi za ajira, biashara, maendeleo na vitu mbalimbali kutokana na watu ambao wanatoka mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni nini naomba kuishauri Serikali kupitia Wizara hii ambapo wao ndiyo wanatoa fedha na kusimamia rasilimali nyingi za Watanzania. Kuna haja kubwa ya kutazama na kurudia kupitia tena kuona vile ambavyo tunaweza tukaendelea kuimarisha na kuwekeza kwa kiwango kikubwa mpakani.

Mheshimiwa Spika, nataka kutolea mfano wa baadhi ya maeneo ambapo kuna border post (mipaka) za Holili, Namanga na Tunduma yenyewe nitolee mfano, wakazi ambao wanatoka Tunduma hawalimi, hawavui, hawafugi, hawafanyi chochote, kikubwa ambacho wanakifanya pale ni biashara. Sababu ambayo imechochea kuwepo na msukumo mzuri wa biashara Tunduma ni uwepo wa lile gate ambapo kuna mpaka kati ya nchi ya Zambia na Tanzania ambayo nyuma yake inazibeba nchi zote za SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ipo kwa bandari ya Dar es Salaam kuna ma-gate zaidi ya moja, Serikali inaonaje kuongeza ma-gate kwenye sehemu nyingi za mpakani ambazo zinapelekea kuwepo na mrundikano wa watu, lakini wakati mwingine huduma hizi za forodha kushindwa kutolewa kama inavyostahiki na wakati mwingine Serikali kupoteza mapato? Kama ilivyo Tunduma na sehemu zingine kama Namanga kumetokea uwepo wa wimbi kubwa la watu, watu wengi kupata ajira bila kujali elimu, umri au itikadi ya kitu chochote, imeonekana watu wengi wanapata sana ajira.

Mheshimiwa Spika, mfano watu ambao wanatoka Tuduma ajira zipo kwa wingi kwa watu ambao hawajasoma, kwa watu ambao wamesoma, wafanyabiashara kutoka kila pembe ya nchi hii wameenda kujikita pale wanafanya biashara. Waliofungua hoteli, vituo vya mafuta na huduma za kubadilisha fedha za kigeni, wote hawa wanajipatia riziki.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kwenda kutuwekea gate kwenye Jimbo la Momba ambalo pia litaenda kusabababisha Watanzania wengine na watu wengine ambao watataka kuwekeza ndani ya nchi yetu kuendelea kupata huduma kama ambazo wanapata katika sehemu zingine za mipaka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini naomba kuwepo na gate kwenye Jimbo la Momba. Naishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi imetujengea Soko la Kimataifa la Mifugo na Mazao mahali pale. Eneo ambalo limejengwa soko kutoka linapoanzia Jimbo la Tunduma mpaka unapolimaliza Jimbo la Momba ni zaidi ya kilometa 80 lote ni eneo la mpaka. Ina maana kwamba cha kwanza hata ardhi ambayo inayopatikana maeneo yale itakapopimwa itaonekana ni ardhi ambayo ina fursa kwa kuwekeza kwa sababu kila Mtanzania na watu mbalimbali watatamani kwenda kuwekeza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye eneo lile kuna njia za kutumia gari zaidi ya kumi ambazo zinatoka kutoka nchi ya Tanzaia kuingia nchi Zambia. Je, Serikali haioni watakapoweka gate pale itasababisha Wizara ya Ulinzi kuongeza usalama wa eneo lile? Pale Tunduma au sehemu zingine zinapotoa bidhaa kutoka Bandari ya Dar es Salaam wakati mwingine wanapitisha kinyume na taratibu kwa sababu njia zile zipo nyingi. Je, Serikali haioni kwamba tutakapopata gate itatuongezea fursa nyingi, watu watapata ajira lakini pia wawekezaji ambao watataka kufungua hoteli na vituo vya mafuta, shughuli za kibenki zitaongezeka mahali pale na mimi naamini hata ajira ambazo tunaendela kuzi-promote na kuzisema kwa Watanzania hawa zitapatikana. Kwa sababu mama lishe watatokea pale, kwa sababu pale kuna mnada wa mifugo watu mbalimbali wataendelea kujipatia riziki mahali pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaendelea kuona kwamba ipo namna, tuma watu wa SADC na COMESA waende kuutembelea mpaka ule, wakague na wajiridhishe uwezekano wa kuongeza geti pale. Kama ambavyo tunaendelea ku-promote kuongeza bandari nyingine hata kule Bagamoyo ili kuendelea kutoa huduma nzuri kwa ajili ya bandari yetu ya Dar es Salaam ipo haja pia kwenye mpaka kati ya nchi yetu na Zambia kuongeza geti kwa sababu lipo moja tu pale Tunduma. Wakati mwingine wafanyabiashara wanakaa muda mrefu pale zaidi ya wiki mbili kwa sababu kumeonekana kuwa na mrundikano na huduma hazifiki inavyotakikana hivyo inapelekea hata kupoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba hata Wizara ya Mama yangu Mheshimiwa Jenista kwamba…

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Condester.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa Mbunge wa Jimbo mdogo kuliko wote humu ndani kwa akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anachokizungumza Mbunge hapa ni jambo kubwa na la maana. Kwa mfano, sisi kule Mara yaani mtu atoke Serengeti mpakani wa Masai arudi apite Kirumi aende Tarime border ndiyo aende kutoa mzigo wake. Hivi nani anaweza kusafiri umbali mrefu hivi ili kupeleka hela Serikalini? Kwa nini Serikali sasa isifanye kama anavyozungumza ikague mipaka ya nchi yetu nchi yote ione wapi pa kwenda kuweka wafanyakazi ili watu tuendelee kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi amezungumza hapa Mheshimiwa Tarimba kwamba kwa mwezi mmoja wenye siku 30 na siku nne, yaani siku 34 wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wametumia shilingi bilioni 39. Sasa kwa nini wasidhibiti mipaka hiyo wakaweza kutafuta fedha nyingi ili waweze kupata mapato ya kutumia? (Makofi)

SPIKA: Taarifa inatosha.

Waheshimiwa Wabunge, kabla sijampa nafasi Mheshimiwa Condester, kuhusu hili suala la Wizara ya Fedha na matumizi yaliyofanyika kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyowatembelea naomba kwa sasa tusiwahukumu kwa sababu bado ni jambo linalofanyiwa kazi halafu taarifa itapelekwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu labda baadaye tutakuja kupata taarifa halisi. Sasa kwa kuwa linafanyiwa kazi tukipitisha hukumu kabisa nadhani tutakuwa a little bit unfair. Kwa hiyo, naomba hilo tuliache kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Condester, unapokea taarifa?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba Serikali kwamba kama vile Serikali ambavyo inatupia jicho la umakini pale Tunduma kwa sababu inajua inavyonufaika na zile nchi ambazo zipo SADC sasa watashindwaje kulichukua ombi hili na kulitekeleza? Kama mpaka wa Zambia na Tanzania nyuma umebeba mipaka mingine kwa nini tuwe na gate moja? Kwa nini tusingekuwa hata na mageti matatu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumeshapewa hela nyingi pale lilipo Soko la Mazao la Kimataifa basi kuna haja kubwa Serikali kutuwekea gate pale. Naamini Watanzania kutoka sehemu mbalimbali watanufaika, vijana wetu wa Kitanzania watapata ajira, mama zetu ambao wanatafuta riziki ndogo ndogo watajipatia pale kama ambavyo ipo Tunduma kwamba hata watu ambao siyo wasomi lakini ni matajiri wa kutosha kuliko hata wasomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mahali ambapo naendelea kuliombea liwepo gate ndiyo sehemu ambapo kuna barabara ambayo inaenda mpaka kwenye ile Bandari ya Karemii. Nchi ya Tanzania ilikuwa inapata changamoto kubwa sana…

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nimekuona.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa ridhaa yako, naomba nimpe taarifa mchangiaji, Mbunge anayeongea ujengaji wa hoja wa kwake ni wa viwango vya Wabunge wazoefu sana. Kwa kweli ndiyo maana Jimbo la Momba walimpitisha kwa kishindo na waendelee kumchagua. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi alivyojenga hoja, naomba nitoe taarifa kwamba Wizara pamoja na Mamlaka ya Mapato tutatembelea lile gate analolisema na tupate mfano ule aliousema ili tuweze kuzungukia na mageti mengine ili tuweze kutengeneza utaratibu wa kukusanya fedha na kuwawezesha wananachi wetu waweze kufanya shughuli zao kwa uangalifu. (Makofi/Vigelegele)

SPIKA: Mheshimiwa Condester ziara hiyo itafanyika, lakini kwa ruhusa ya Spika. Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nashindwa hata cha kusema, natamani hata kutoendelea kuchangia kwa sababu pale tukapojengewa gate ndani ya Jimbo la Momba hata siku nikifa nitahisi kwamba Mwenyezi Mungu kile alichonituma kuwatendea ndugu zangu wa Jimbo la Momba kitakuwa kimetia kwa sababu nitakuwa Mbunge wa kwanza kabisa kuwafanya ndugu zangu wa Jimbo la Momba kuishi kwenye mazingira ya biashara. Katika vijiji vyetu vyote 72 tulivyonavyo hatuna mji hata mmoja vyote ni kijijini hata mahali ambapo natokea, kwa hiyo, mtakuwa mmetusaidia sana kupata mjini ndani ya Jimbo la Momba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naendelea kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi na nisema kwa kauli hiyo nawashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Momba ambao kwa mara ya kwanza walimsimamisha Mbunge mwanamke na mdogo kwa umri na wakanipa heshima na wakaniamini. Kwa kauli yao walikuwa wakisema tunamtaka mtoto mdogo na mama ambaye tukimtuma anatumika. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 205. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, nianze kutoa mchango wangu kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo ameendelea kujitoa na kwa namna ambavyo ameendelea kuhakikisha anawafikishia Watanzania huduma mahali popote pale walipo. Lakini pia niendelee kuendelea kuwaomba wale ambao Mheshimiwa Rais amewaamini kama wasaidizi wake, Baraza la Mawaziri Wasaidizi mikoani na wilaya wahakikishe angalau wanakwenda na speed ya mama ili wasiendelee kumwangusha ili Watanzania wapate kile ambacho mama amekusudia kiweze kuwafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu katika maeneo matatu kama muda utakuwa rafiki, nichangie kwenye eneo la Kilimo, Nishati lakini kwenye eneo la Teknolojia namna ambavyo tukitumia teknolojia vizuri inaweza kutusaidia ku-speed up maendeleo lakini pia ambavyo inaweza kusaidia kutoa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwenye eneo la kilimo, nitachangia katika maeneo mawili. Suala la kwanza ni kwenye pembejeo kama ambavyo waliotangulia wamesema. Kwa kuwa sisi Tanzania siyo kisiwa, tulipopata janga la Corona Nchi nyingine zilipokuwa zimeathirika automatically na sisi Tanzania tuliathirika hata kama sisi hatukujifungia ndani tuliendelea kufanya kazi. Nchi nyingi ambazo zinazalisha mbolea pamoja na pembejeo zingine zilipata changamoto hizo, kwa ambazo zimepata changamoto hizo imesababisha hata vitendea kazi vya kilimo huko especially mbolea imekuwa ni changamoto. Kwa hiyo, tuiombe sana Serikali ambayo ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali Sikivu sana. Kwa sababu tuna wiki mbili tu tayari tumeshafika kwenye msimu wa kilimo, tunaomba Serikali itoe fedha ya dharula kwa ajili ya ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili tunaomba kwenye Mpango ambao utakuja baada ya kutoa mawazo yetu 2022/2023, tunaomba viwanda vyetu vya ndani ambavyo vinazalisha mbolea viwezeshwe. Viwanda hivi vikiwezeshwa vitakuja kutusaidia kwenye nyakati kama hivi, hakuna mahali panapoonesha kwenye mpango kwamba baadhi ya viwanda vyetu vitaweza kuwezeshwa ili mbolea ambayo itatoka na kuzalishwa ndani Nchi yetu iweze kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jambo la pili kwenye kilimo nichangie kuhusiana na masoko na hapa naomba niende kabisa soko la DRC Congo. Kwa kuwa mama ameonekana kuwa ni Mwanadiplomasia mzuri na katika kipindi kifupi hiki ameonesha namna ambayo ameionesha dunia kwamba tunaweza tukashirikiana na mataifa mengine. Tumuombe sana Mheshimiwa Rais, atusaidie kukaa na Nchi ya Zambia waweze kutuondolea vile vikwazo ambavyo wafanyabiashara ambao wanategemea soko la Congo wanavipitia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka kutoa takwimu ya namna ambavyo soko la Congo linaitegemea Nchi ya Tanzania kwa ajili ya kuwasambazia chakula, unaweza kuona hata zile bilioni 50 ambazo tulipoiomba Serikali tulipoleta hoja hapa waliweza kutusaidia, tusingeweza kwenda kuitumia kwa ajili ya kununua mahindi kwa Watanzania, soko la Congo peke yake lilikuwa linatosha wafanyabiashara kununua mahindi ya kutosha na kupeleka Congo au kusindika unga wa mahindi na kusambaza kule. Soko la Congo linatamani Watanzania sisi tuwa-supply tani za unga kuanzia laki moja na hamsini mpaka laki nne. Na inaweze hapo tunaongelea Congo Lubumbashi peke yake labda Katanga na Kolowezi lakini hapo hatuongelei Congo Kinshasa, hatuongelei Goma ni hiyo Congo Lubumbashi peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa vikwazo hivi vitaendelea, vinaendela kuwanyima nguvu wananchi ambao wanazalisha mazao ya nafaka especially wale ambao wanatokea Nyanda za Juu Kusini mikoa yote saba. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itafuta namna nzuri ambayo itakaa na Nchi ya Zambia waelewane vile vikwazo ambavyo wafanyabiashara wanapata na kwenye biashara nyingine viweze kuondoka ili tuweze kutumia kwa sababu mizigo mingi ambayo inatoka Tanzania inakwenda kama transit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kumalizia niongelee suala la teknolojia. Suala la teknolojia, teknolojia ni kama muda hauwezi kushindana na muda, wewe unapotaka kushindana na muda wewe utapitwa na wakati. Unaweza ukaona, sasa hivi hata Bunge letu vitu vingi tunaendesha kwa kutumia kishkwambi, lakini unaweza ukaona Nchi ambazo zimeendelea teknolojia hii ilipaswa itumike kwenye Bunge la Nane, Bunge la Tisa au Bunge la Kumi. Lakini tupo Bunge la Kumi na Mbili mwaka 2021 ndiyo tunatumia teknolojia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kwenye teknolojia nataka niongelee kuna kitu kinaitwa Block Chain Technology na kwenye Block Chain Technology nataka nitoe takwimu ndogo tu ikiwa kama Nchi zetu zitatamani kuendana na kasi ya teknolojia iliyopo duniani, tusiwe tunachelewa kupokea teknolojia, mambo ambayo tunapaswa kuyafanya sasa hivi tunakuja kuyafanya baada ya miaka kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu turudi miaka kumi iliyopita nyuma mwaka 2010. Mwaka 2010 wakati teknolojia ya Block Chain Technology inakuja, ndani ya Block Chain Technology kuna vitu vingi, watu wa kada mbalimbali wanaweze wakatumia Block Chain Technology lakini hapa niongelee suala la fedha ambalo naamini kila mtanzania tunafanya kazi ili tuweze kupata fedha. Ndani ya Block Chain Technology kuna kitu kinaitwa Digital Currency, Crypto Currency yaani BitCoin. Mwaka 2010 bitcoin ilikuwa inauzwa chini ya dola 5, ilikuwa inauzwa 0.5 USD ambapo mwaka 2010 dola ya Kimarekani ukilinganisha na fedha yetu ya Tanzania ilikuwa inakwenda kwenye 1,490 – 1500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa tafsiri yake kama Serikali ingesema sisi tumeilewa hii idea hebu tujaribu tu tuchukue bilioni 1 tuwekeze hapa kama vile ambavyo wananunua hisa na nimegundua inawezekana hata IMF hizi Benki za Dunia wanavyotukopesha wao wanawekeza kwenye vitu kama hivi halafu sisi ndiyo wanakuja kutukopesha tunabaki tunalipa madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ingeamua kuchukua bilioni moja ikanunua bitcoin ambayo ilikuwa ni Dola 0.5 ya Kimarekani ukizidisha na thamani ya dola kipindi kile unapata kama 750 maana yake bilioni 1 ukigawanya kwa hiyo fedha unakuja kupata bitcoin laki moja ama elfu thelathini na tano hivi. Ukizidisha na bei ya sasa ya bitcoin, bei ya bitcoin ya sasa ni dola za Kimarekani 66,000 ambapo almost na fedha ya Kitanzania kama Milioni mia moja na hamsini na.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tafsiri yake kama Serikali sasa hivi ingeamua kuziuza hizo bitcoin laki moja na thelathini na tano n.k. tungekuwa na uwezo wa kulipa hilo deni la Taifa ambalo tunadaiwa sasa hivi hizo trilioni 70 na. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bei ya bitcoin sasa hivi ukizidisha na kama Serikali ingenunua bitcoin kipindi hicho inakuja karibu trilion 90. Kwa hiyo, unaweza kuona namna gani hatuwekezi kwenye teknolojia tunapitwa, 2010 na sasa tulipo siyo muda mrefu. Unaopomuongelea Mwekezaji kama Mark Zuckerberg’s ambaye ndiyo mwanzilishi wa Facebook na sasa hivi hi WhatsApp kama kuna Watanzania 10 tu wangekwenda kununua hiza kwenye kampuni yake hata wakawa na share mojamoja sasa hivi ndiyo trillionaire.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie namna gani tunaweza tukawekeza kwenye teknolojia na ni maombi yangu na mapendekezo yangu, vijana wengi wa Kitanzania waliopo huko na nilipata nafasi kufanya research kwenye nchi za West Africa mwaka 2016/2017. Kipindi kile Nchi za Nigeria zilikuwa zina burn sana mambo haya ya cryptocurrency lakini sasa hivi tunavyoongea muda huu hata ukiongea na Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria. Nigeria wamepitisha cryptocurrency bitcoin ni miongoni mwa fedha ambayo inatumika na wameweka katika mfumo mzuri hata kwa kutumia local network za Nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata Mnigeria asiyejua kusoma ambaye hana uwezo hawezi kutumia internet anaweza akafanya, kwa hiyo ni kitu ambacho katika mpango huu tunaomba kuona Tanzania waisome teknolojia ya Block Chain Technology ili waweze kuiwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kwenye nishati. Kwa kweli sisi Wabunge ambao tunatokea vijijini kwenye umeme, kwa kweli kauli hii ambayo Serikali inasema sana umeme mpaka kwenye vitongoji inatutesa huko vijijini. Sera ya Serikali inasema kwenye kila Kijiji kilometa moja ya nguzo ambazo ziweze kupita. Lakini unagundua...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Dakika moja tu.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unagundua kwamba umeme haupiti kwenye nyumba kama inavyotakikana kwa hiyo wananchi wanajiulia hiyo umeme kwa kila Kitongoji imekuwaje? Na vijiji vingine ni vikubwa ina vitongoji vikubwa kwa hiyo, bado hii kauli inatupa mkanganyiko wananchi wakisikia umeme kwa kila Kitongoji lakini ukienda uhalisia kule umeme kwa kila Kitongoji hakuna.

Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali iliangalie jambo hili ikiwezekana umeme kwenye kila Kijiji angalau nguzo kilometa tatu. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kwanza kabisa nianze kukupongeza wewe kwa namna ambavyo umeliendesha Bunge hili na kuendelea kuwapa Wabunge nguvu zaidi na kuendelea kuliheshima Bunge, kwa dhati ya moyo wangu ninakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu kwanza kabisa niseme naunga hoja taarifa zote za Kamati ambazo ziko hapa mezani ambazo ni Kamati ya PAC, LAAC pamoja na PIC ambayo Mimi ni Mjumbe huko. Nitachangia katika maeneo mawili, nitachangia kwenye asilimia Kumi za Halmashauri pamoja na Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nikianza na asilimia Kumi ya mapato ya Halmashauri naona kabisa nia ya dhati kabisa ya Serikali kwanini waliweka kuwepo na asilimia Kumi hii ya Halmashauri. Lengo kubwa ilikuwa ni kuhakikisha wanampa mwananchi huyu nguvu kumuwezesha katika uchumi wake ikiwa ni sambamba ya kuendelea kumpa madaraka ya yeye kuendelea kujisimamia kama ambavyo Serikali yoyote inapaswa kufanya duniani kote.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na mchango wangu nataka kum-quote kidogo ambaye alishakuwa Rais wa Marekani Thomas Jefferson, anasema hivi, ‘‘The purpose of the Government is to enable the people of a Nation to live in safety and happiness. Government exists for the interests of the governed, not for the Governors’’. Akiwa na maana kwamba Serikali yoyote duniani maslahi yake kwanza ni kuwaridhisha wale ambao wanawatawala na siyo wale ambao watawaliwa. Tafsiri yake, viongozi wote wa Serikali na wasimamizi wote ambao wamepata dhamana cha kwanza kabisa jukumu lao ni kuhakikisha wanalinda maslahi ya wananchi ambayo sisi wao tunawatumikia au kwa lugha nyingine kama ni Serikali ambao tuseme wanawatawala.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo nataka nirejee kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, nitasoma mambo kadhaa. Kwenye sura ya Sita ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ukurasa wa 161 ukienda kwenye ukurasa wa 174 unasema hivi, kwa kutambua umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika hali iliyoshirikishi, Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka ijayo imetarajia kufanya yafuatayo: -

(i) Kuimarisha mifumo ya taasisi na uwezo wa Viongozi na Watendaji wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenda Vijijini kusikiliza na kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi kwa wakati na haki na uadilifu. Aidha, kupokea na kusikiliza na kuwahudumia wananchi wanaotembelea ofisi hizo kwa weledi hekima na busara;

(ii) Kufanya mapitio ya Sheria za Tawala za Mikoa na Sheria za Serikali za Mitaa ili kuendana na uboreshaji wa mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi;

(iii) Kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo ya mapato katika vyanzo vilivyopo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi;

(iv) Kuimarisha Serikali za Mitaa ili ziendelee kuwa chombo cha kuwapa wananchi uwezo na sauti ya kuamua kushiriki kwa karibu katika shughuli za maendeleo, mwisho na mengine yanaendelea;

(v) Kusimamia kikamilifu suala la utawala bora ndiyo hapa ambapo watu wamekula hela hapa, narudia, kusimamia kikamilifu suala la utawala bora, uadilifu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasimali za umma pamoja na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mamlaka hizo, itekelezwe kwa kiwango kinachokusudiwa kuhakikisha kuwa ubora wa miradi unalingana na thamani ya fedha iliyotumika.

Mheshimiwa spika, kwenye ripoti ya CAG inaonesha kwamba kwenye asilimia kumi zipo halmashauri kwamba kwenye asilimia kumi zipo asilimia 155 nchini hazikuweza kurudisha yale marejesho, bilioni 47.5. Bilioni 47.5 zote hizi cha kwanza, zimepora mamlaka ya wananchi ambazo ilani ya Chama cha Mapinduzi inasema; ‘kwamba mtawala yeyote anapokuwepo kwenye madaraka lazima ahakikishe anawapa nguvu wale ambao wao wamemuweka madarakani’. Hizi bilioni 47.5 zimepotea ziko kwenye mifuko ya watu, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa sio najiuliza na ni wazo langu katika maazimio ambayo wenyeviti wa Kamati wanaweza wakachukua. Nikaona tu; kwa mfano TAMISEMI wangeamua kwamba waweke dirisha maalum linaloshughulikia mikop tu, labda tuchukulie kwamba afisa maendeleo wao wamekuwa na shughuli nyingi na hawana huo utaalam wa kusimamia hizi fedha. Hizi fedha ambazo zimepotea bilioni 47.5 ni katika kipindi cha mwaka mmoja tu 2021/2022, bilioni 47.5.

Mheshimiwa Spika, nikachukulia mfano, wako vijana wengi mtaani ambao hawajaariwa ambao ni bankers, accountant, pamoja na wachumi. Tufanye kama TAMISEMI, ingeamua kuajiri kwa kutumia fedha hizi hizi ambazo ni za Serikali, zimeliwa toka kwenye mifuko ya watu au zimepotea kwa uzembe ambao unasababisha na wataalam wetu kutokuvaa, kuzimiliki zile fedha kwamba ni fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi nikawa najiuliza, kwenye mabenki yetu, CRDB, NMB na benki zingine zilizopo hapa hapa nchini, hao ambao ni wataalam wa kusasanya mikopo wametoka nje wapi? Si wamesoma hapa hapa ni ma-banker wamesoma hapa hapa nchini kwetu mbona wana huo utaalam wa kukusanya mikopo? Kuna mwananchi yeyote amekopa hela benki anaweza akala fedha? Sasa kwanini sisi Serikali isitenge dirisha kuwaajiri wataalam, wahasibu, wachumi, ma-banker wakasaidia kutoa elimu, kukusanya fedha hizi na fedha hizi zirudi?

Mheshimiwa Spika, nikaweka hesabu ya kawaida tu kwa mfano TAMISEMI, waamua kumuajiri graduate ambaye amemaliza degree yake ya uchumi, uhasibu whatever ambaye anaweza kusimamia vizuri mikopo, waanze kwa kumlipa mshahara wa Shilingi laki saba, wakaajiri watu watatu kwenye halmashauri 84, nikapata kwamba wakiwaajiri watoto watatu kwa mwezi watakuwa wanawalipa milioni 2,100,000, ukichukua milioni 2,100,000 katika halmashauri 184 tutapata milioni 386,400,000. Nikaweka kwamba tufanya kwa miaka mitano ya majaribio, hii ambayo tunatekeleza ilani utakuta hawa vijana umewalipa bilioni 1.932; lakini unaona kwa mwaka mmoja hela zimepotea bilioni 47.5. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tafsiri yake tungeweze kuajiri vijana watatu tu, ambao ni uhasibu, banker na mchumi wanakaa yaani wao kitengo chao ni special kusimamia mikopo tu ya asilimia 10, katika kipindi cha miaka hiyo mitano ambayo tumeweka tungeweza kuwalipa bilioni mbili. Tafsiri yake ni kwamba tungeweza kuokoa hela.

Mheshimiwa Spika, lakini bado nikapiga hesabu, ukiwaajiri vijana hao kwenye halmashauri 184 utaajiri vijana wakitanzania wasiopungua 520. Kwa hiyo pia tungekuwa tume-solve changamoto ya ajiri. Hata hivyo, kama wangesimamia kwa ufanisi, zile hela zingekuwa zinazunguka; maana yake kama mwaka huu watu walikopeshwa bilioni moja, mwaka huu halmashauri ikakusanya tena bilioni moja vikundi vitapata, nikatolea tu mfano, mfano nikachukulia halmashauri yangu. Labda halmashauri yangu sisi labda mwaka huu wa fedha tulipata bilioni 1.7, kwa hiyo ni milioni 170; tukivigawia vikundi vitano wangeweze kupata milioni 34 kwenye kila kikundi. Tafsiri yake milioni 34 hii ingekuja na mwaka mwingine siwangekusanya? Milioni 34 ingekuja na vikundi vingine na wakati huo mapato yaongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ni mapendekezo yangu kwa wenyeviti wa kamati, kwamba ipo haja ya kuona hili. Lakini wakati tunaendelea kuona ipo hoja ya kuona hivi hawa waliohusika na jambo washughulikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana na benki ya kilimo. Benki ya kilimo, pamoja kwamba mwaka wa nyuma kuna kiwango cha pesa ambazo walipewa kama bilioni 208, lakini walikuwa wanaomba waongezewe mtaji angalau bilioni 760. Ni kweli, mimi ninatamani waongezewe hicho kiwango cha fedha ili kuleta tija kwa wananchi wetu ambao ni wakulima; na tukiangalia nchi hii kwa kiwango kikubwa wazalishaji wakubwa ni wakulima.

Mheshimiwa Spika, pia nataka niseme, watu hawa wa Benki ya Kilimo pamoja na kwamba mnataka kuongezewa fedha na Waziri wa Kilimo upo hapa, pamoja hatukushauri tunakusimamia muda huu, tunaomba kuona mnapotaka kuwaongezea fedha hizi tuwape, zikalete tija kweli kwa wananchi, zifike kule kwa wananchi ambao tunawakusudia. Ni kweli tunaona kuna benki ya kilimo, lakini kuna wakati jamani kule vijijini hatuona sana tija hii ya benki ya kilimo mwananchi wa kawaida hakopesheki, mwananchi wa kawaida kule kijijini hapati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano mzuri tu pamoja naongelea Benki ya Kilimo. Miezi miwili iliyopita tulipata ruzuku ya mbolea, tukaambiwa Wabunge tukatoe taarifa kwamba Serikali inatuletea mbolea, ni kweli mbolea imekuja. Cha kushanga sasa hivi tunavyoongea tumebakiwa na wiki mbili tu msimu wa mvua urudi wananchi vijijini waanze kulima mpaka sasa mbolea hazijafika vijijini, mpaka muda huu mbolea bado na sehemu zingine mbolea imeenda ya aina moja tu.

Mheshimiwa Spika, sasa tunajiuliza wakati mwingine mnapotuomba Wabunge tuwasaidie kuwapikishia hiki tuona na tija ili wakati mwingine tunapokuja hapa; kwamba kama tuliwasaidia kuwapitishia hizi fedha au ndio mnaomba tuwapendekezee kama sisi Bunge maazimio yetu, tuone na mambo ambayo yanafanana na mambo hayo. Kama ni Benki ya Kilimo imewezeshwa imfikie kweli mkulima, lisionekane tu lipo kundi la mapapa hawa ambao wao tu ndio wana-grub na kuchukua wao tu lakini mwananchi wa kawaida yule ambaye ndiye mzalishaji halisi, yule ambaye mpaka sasa hivi analima kwa jembe la mkono, yeye ambaye sasa hivi kununua mfuko mmoja tu wa DAP ni changamoto, amekopeshwa, mwananchi huyu ambaye bado hata mbegu yenyewe kununua ni shughuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunategemea Benki ya Kilimo ndiye huyu tumkusudie apate. Wakati mwingine ukiwauliza watu wa Wizara wanasema Benki ya Kilimo kazi yake si kufungua matawi huko vijijini na sehemu zingine zingine kwenye wilaya kwa sababu hawafanyi transaction.

Mheshimiwa Spika, mimi ninajiuliza, kwani Mheshimiwa Rais, Mama Samia anaishi kwenye halmashauri zote 184? Si anaishi Ikulu hapa Chamwino na Dar es Salaam? Lakini mbona miradi yote akitoa inafikia halmashauri zote 184? Kote anapeleka. Kwa hiyo, kaeni na benki Dar es Salaam, whatever, wekeni kwenye kanda lakini tunachotaka huduma zifike. Whether mtatafuta mawakala wakufikisha hizi huduma kwa wananchi or mtaunda vikundi, lakini tunataka mkulima wa kawaida, yaani tunaongelea mkulima wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, na katika hili nimuombe Mheshimiwa Waziri Bashe, twende nikakukutanishe na wakulima wa kawaida huko vijijini ili tunapoongea muwasilize wenyewe kwa masikio yao, hawapati mikopo.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja zote za kamati ambazo ziko mezani, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii naomba kupitia Bunge lako Tukufu kwa heshima na taadhima niombe sana Serikali yangu Sikivu ya Chama Cha Mapinduzi ninaomba kwenu sana sana tunaiomba Serikali yetu tuwatazame wakulima walioko vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo simaanishi kwamba labda wakulima ambao wako mjini hawastahili kuombwa lakini Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi wakulima hawa ambao wako vijijini ndiyo ambao wamekuwa ni waaminifu kwetu mno katika kutupa kura na sehemu zingine hawaamini hata vyama vya upinzani wanaelewa ni CCM tu. Kwa hiyo, fadhila ya kuwalipa wakulima hawa ni sisi kuwatazama wakulima hawa jamani Benki ya Kilimo haiwafikii huko vijijini Benki ya Kilimo haiwafikii ndiyo maana wamegubikwa na wimbi la hawa watu ambao wanaitwa AMCOS. AMCOS mmewapa watu wa vijijini wawasaidie spidi ya watu wa vijijini hawafanani kabisa na spidi ya watu wa AMCOS, AMCOS ni waongo samahani Waheshimiwa wengine wametumia lugha na kusema ni matapeli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenyewe nimehusika katika kusimamia kuendelea kuwaombea mkopo wapiga kura wangu wa Jimbo la Momba ambao walikuwa wameomba AMCOS nimepiga simu kwa mameneja kadhaa wa Branchi husika za wilaya mpaka kwa mameneja wa kanda kwa ajili ya kuendelea kuomba mkopo wananchi wameahidiwa kupewa mkopo kuanzia mwezi wa 12 mpaka sasa wanaendelea kuomba kilimo kinaanza kulimwa kuanzia mwezi wa 11 mpaka wa 12 watalima nini? Hivyo Serikali yangu naomba kwa kuwa iko Benki ya Kilimo ambayo riba yake ni nafuu kwa wapiga kura hawa waaminifu wa Chama Cha Mapinduzi ambao tukienda tunapiga magoti na kugaragara kwao kuwaambia Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni Sikivu basi tuwape kitu ambacho kinafanana na uelewa wao ambao ni Benki ya Kilimo na inatoa riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ukisikia mchele mzuri ambao unalimwa Kamsamba unalimwa ndani ya Jimbo la Momba achilia tu kwamba tunalima na kusambaza kwenye mikoa mingine ambayo iko hapa Tanzania lakini mchele ambao tunalima ndani ya Jimbo la Momba tunasambaza mpaka nchi ambazo ziko SADC. Lakini cha kushangaza ndani ya Jimbo la Momba ikiwa kama lilivyo jimbo lenyewe tuna bonde kubwa kabisa ambalo linabeba na mto wa Momba lakini cha kusikitisha tuna skimu moja tu ya umwagiliaji na ambayo na yenyewe haifanyi kama ambavyo inatakikana. Skimu ya umwagiliaji ya Naming’ong’o.

Mheshimiwa Spika, lakini Pamoja na hayo Serikali imeshawahi kutoa kwenye skimu nyingine ya umwagiliaji ambayo iko Iyendo, Kata ya Kapele Zaidi ya pesa milioni 800 na Wizara ya Kilimo wakaunda Tume kwa ajili ya kwenda kukagua skimu hii lakini mpaka sasa tunavyoongea hatujawahi kupewa hata majibu na hatujui nini kinaendelea kuanzia niko Form four na mpaka sasa ni Mbunge, jamani Serikali tunaomba wananchi hawa na wapiga kura hawa ni waadilifu na ni wachapakazi tunaomba tuwawezeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini skimu ya umwagiliaji Naming’ong’o kaka angu Bashe nimekufuata mara kadhaa hii skimu Serikali imetoa hela nyingi Zaidi ya bilioni 4.7 ina matatizo kadhaa farm layout kuna shida designing na drawings zina changamoto leveling farm roads mwenyewe nimeitembelea ile skimu mara kadhaa mara nyingi nimeitembelea hakuna mifereji ambayo inaonyesha inatoa maji na inaingiza maji, zile njia zote za kupitishia maji kwenye skimu zimejaa matope basi tunaomba mtupe excavator ili hata wataalamu ambao wako kule tuweze kukwangua wenyewe ile mifereji tunaomba sana.

Mheshimiwa Spika, lakini bonde hili lina zaidi karibu hekta 100,000 za kulima mpunga pamoja na mazao mengine ya umwagiliaji na mbogamboga. Lakini cha kushangaza ndiyo skimu hizo ambayo hata iliyopo yenyewe ni mbovu tunaomba kabisa tupate skimu ya umwagiliaji Kamsamba tupate skimu ya umwagiliaji Msangano, tupate skimu ya umwagiliaji Kasinde, tupate skimu ya umwagiliaji kubwa zaidi kwenye Mto Tesa tunaomba mtuongezee. Kwa sababu mazao yote ambayo tunayazalisha pale kwenye Jimbo la Momba ni tija kwa Mkoa ni tija kwa mikoa mingine lakini Taifa linakusanya mapato ya kutosha kwenye zile nchi za Jirani ambazo tunazitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuwepo Zambia muda mrefu wanatumia mchele wa kutoka Tanzania tu na kama Jimbo la Momba ndiyo tuko pale mpakani Kongo wanatumia mchele wa Tanzania tu lakini hata nchi zingine ambazo ziko huko Kusini wanatumia mchele wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini siyo hayo tu kama ambavyo ameongea Mheshimiwa Deus Sangu tunalima pia mahindi yamkini tungeweza kulima hata mara tatu kwa mwaka lakini tutafanyaje mkopo hatupewi tumepewa matapeli AMCOS. Umwagiliaji hakuna sasa huyu mkulima huyu tunamtazamaje aliyepo vijijini? Tunamtazamaje.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho tunaishukuru sana Serikali kwa kutupa soko la mifugo na mazao pale Kakozi lakini tuna vijiji 72 na jiografia jamani ni ngumu. Jiografia ya Jimbo la Momba ni changamoto wapo Waheshimiwa Wabunge ambao wamefika hapo wanaijua ile vijiji 72 ghala moja tu. Mtu aliyoko kule Kamsamba Usoche ili atoe mazao yake kabla yajafikisha kule juu Kakozi hayo maghala hakuna tuna maghala mawili tu na lingine hili halijakamilika liko toka kipindi hicho. Tunaiomba Serikali tunaomba kuongezewa maghala hata kama hayatafika 72 kwenye kila Kijiji lakini angalau basi yafike hata 26 kwa kuanzia tunaiomba sana Serikali ili tuweze kupandisha mazao yetu kufika pale Kakozi.

Mheshimiwa Spika, na jambo lingine la kumalizia tunaomba Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi tuwekewe mkakati mzuri namna gani hawa wakulima hawa wapimiwe ardhi zao ili wawe wanakopesheka na kwenye benki wenyewe wakienda peke yake ardhi ni potential tuko mpakani tunaishia tu kugawa ardhi kwa wazambia na Watanzania kwa sababu hakuna muundombinu mzuri ambao Serikali imeweka kwa wapiga kura hawa, naunga mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali yetu na kuishukuru kwamba tunashukuru kwa kutusaidia kutujengea soko la Kimataifa la mifugo na mazao ambalo lipo pale Kakozi ambalo lipo mpakani kabisa kati ya nchi ya Tanzania na Zambia ni kilometa moja tu kutoka Tanzania kuingia Zambia. Soko hili liligharimu karibu, Serikali iliidhinisha pesa karibu bilioni 8.645 na mpaka sasa hivi tumepewa kiasi cha pesa bilioni 3.09. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa kusema hivi kutokana kuwepo kwa soko hili la mifugo na mazao pale ni soko kubwa sana ambalo ninaamini kwamba Serikali wakati inaidhinisha kiwango hiki cha pesa na kutafuta mpango huu mzuri kwamba soko likajengwe pale ni mahsusi kabisa walizingatia kwamba ni kwa sababu tupo mpakani ina maana kwamba tutawahudumia Watanzania wa mikoa yote lakini pamoja na nchi zote ambazo zinatupaka kwenye lile eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ombi langu kwa Serikali, iko sababu kubwa sana Wizara hii iweze kufika kwenye lile soko ambapo tunaendelea na ujenzi japokuwa tunashukuru limeshakamilika kwa kiasi fulani na tumeshaanza kufanyia kazi. Ifike ili tuweze kushauriana muweze kuona miundombinu namna gani tumejipanga katika kuboresha kwenye hilo eneo la ufugaji na eneo lingine ambalo litakuwa linahusu Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa kuwa soko hili ni kubwa kwa kiwango hiki, naiomba Serikali ipo haja na sababu ambayo tunaweza tutakapoweka kiwanda cha kusindika nyama mahali pale inaweza ikatunufaisha sana. Itatunufaisha sana kwa sababu karibu mikoa yote ya Katavi, Rukwa na mikoa mingine iliyoko karibu nasi ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa mingine itaenda kwenda kutumia soko hili kwa sababu kua mnada kabisa wa kisasa ambao unatarajiwa kujengwa mahali pale, machinjio ya kisasa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wasiwasi wangu tunaweza, wakati tutakuwa tunafanya shughuli hizi za ufugaji tukawa tunawanufaisha wenzetu wa nchi za jirani. Sasa twende kuongeza thamani kwenye haya mazao ambayo yatatokana na ufugaji. Kwa hiyo, tukipata kiwanda cha kusindika nyama mahali pale, kuna soko kubwa sana la nyama kwenye nchi ya Kongo, Zambia na nchi zote ambazo ziko kwenye zile nchi za SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo liko andiko ambalo nimeziandikia baadhi ya Wizara hapa kuona kwamba kama tuko mpakani na soko lile liko pale mpakani kuna hati hati ya kwamba chochote tutakachokuwa tunazalisha pale kinaweza kikawa kinaenda nchi ya Zambia kinyume na utaratibu. Kwa hiyo, nimeiandikia andiko Wizara ya Fedha, Kilimo, Viwanda na Biashara, Uwekezaji, Mifugo yenyewe na Wizara ya Ulinzi na Usalama kwamba ninaiomba Serikali yangu Sikivu wkae wajadiliane waone kuna umuhimu wa sisi kutupatia geti pale ili tuweze kulinda mapato yote ambayo hayatapaswa kutoka pale kwa sababu soko litakapoanza kufanya vizuri na muingiliano wa watu utakuwa mwingi. Kwa sababu kuna njia zaidi ya 10 ambazo zinaizunguka lile soko ambazo zinatoka pale sokoni kuingia nchi ya Zambia na wakati mwingine huwa tuanzitumia hizo njia kupita ambapo wakati mwingine inakuwa ni kipindi cha Masika, barabara hazipitiki. Kwa hiyo, sitatamani kuona tunaenda kuzinufaisha nchi za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwa kuwasemea watu wa Momba kwenye suala la mifugo. Kwenye sensa ambayo ilikuwa imefanyika mwaka 2012 tulionekana tulikuwa na ng’ombe 128,218, mbuzi 78,522, kondoo 10,071 na kuku 155,233 na kwa ajili ya muda pamoja na mifugo mingine. Kwa miaka ya karibuni ambayo imeongezeka sasa tumeonekana kuwa na ongezeko la mifugo hii karibu mara tano kwa sababu tumepokea wenzetu wengi wa Jamii ya wafugaji, Wasukuma na Wamaasai ambao wamekuwepo maeneo yale. Sasa, kutokana na ongezeko hilo, kumeonekana uhitaji mkubwa sana wa kuhitaji malambo pamoja na majosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na lambo ambalo lilikuwa limeanza kujengwa kwenye Kata ya Mkomba ambapo Shirika hili la Debit kwenye mwaka 2016/2017 liliweza kutupatia kiwango cha pesa milioni 150 ambapo lambo hili lilikuwa linapaswa kukamilika kwa thamani ya milioni 800. Ombi langu kwa Serikali, kama mnaweza kufika, kupitia na kuliona lambo hili ili tuweze kuwasaidia wafugaji hawa wasiendelee kunung’unika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo yapo baadhi ya malambo ambayo yalikuwa yanatumika, lakini hayana ubora na yanahitaji kurekebishwa kwa sababu ongezeko la wafugaji limekuwa kubwa mara tano kama ambavyo nimesema. Naomba ukarabati wa malambo yafauatayo; lambo ambalo liko Kata ya Ivuna, Mkomba, Mpapa, Chitete, Msangano. Pia ombi langu kwamba kama tunaweza tukapata majosho kwenye Tarafa ya Ndalambo ambayo pia kwenye Bonde la Mto wa Kasinde pamoja na Tesa kuna ongezeko kubwa sana la watu hawa ambao ni wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kwenye suala la ufugaji tunaomba kuboreshewa vifaa vya uimarishaji ili kwa ajili ya kuboresha koo za mifugo ambazo ziko pale. Hii imeonekana ni changamoto lakini na vifaa vya hawa Maafisa Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la uvuvi naomba niende tu moja kwa moja niziongelee changamoto ambazo zinawapata wavuvi ambao wako ndani ya Jiji la Momba. Wavuvi ambao wako ndani ya Jimbo la Momba wanaomba jambo moja kama sio matatu au manne. Tunaomba tupate engine za boti kwa sababu mpaka sasa tunaendelea kuvua kwa kutumia uvuvi wa kienyeji kwa kutumia tu mitumbwi. Kwa hiyo, tukipata engine hizi tutaweza kutengeneza maboti ambayo angalau yanaweza yakawa ni ya kisasa.

Mheshimiwea Mwenyekiti, pia tunaomba kupata mikopo kwa wavuvi. Pia tunaomba kupata soko zuri ambalo liweze kutusaidia kuweza kukusanya mapato ndani ya halmashauri pia kukusanya mapato kwenye Serikali Kuu. Kwa sababu, pamoja na kwamba tunavua kienyeji, tunaweza kuvua kuanzia tani 7,000 mpaka tani 100,000 na pamoja na kuvua huku, tunalitosheleza soko la Mbeya Mjini, Tunduma, Vwawa na Mlowo. Kwa hiyo, tutakapokuwa tumepata hivi vifaa tunaweza kuzalisha tani kubwa na kwa wingi lakini pia tutaongeza mapato ndani ya halmashauri yetu pamoja na mapato kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa na mimi kwanza nianze kwa kupongeza wasilisho kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Na mimi naomba kutoa mchango wangu katika maeneo matatu kama muda utakuwa rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza kabisa nataka kutoa mchango wangu kwa kuishauri Serikali ni kwa namna gani iweze kutusaidia wananchi wa Tanzania kuendesha biashara zake, lakini kwa kuangalia na kasi halisi ya teknolojia ambayo iko duniani ili iweze kutusaidia kuendana na mataifa mengine na kukimbizana sawasawa na wenzetu ambavyo wanakimbizana huko kwenye mataifa ambayo yameendelea ambayo yanatumia teknolojia katika kufanya vizuri kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuomba ni kwa namna gani Serikali inaweza kuwekeza nguvu kubwa kwenye maeneo ya mipaka maana kuna fursa nyingi sana ikiwa ni pamoja na kufungua viwanda kwenye maeneo ya mipaka, lakini pia hata kuboresha mazingira mazuri ya biashara kwa sababu panapatikana ajira nyingi, kuanzia vijana, wazee, watu waliosoma na ambao hawajasoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na eneo la tatu, nitataka kuchangia na kuishauri Serikali kwamba vijijini akina mama wengi wameonekana ndio ambao wanatengeneza pombe za kienyeji na pombe hizi za kienyeji kwa kule vijijini zimeonekana zikipendwa sana. Basi kwa nini Serikali isitafute namna nzuri ya kuwasaidia akina mama hawa kuboresha ujuzi wao ili itusaidie kutoku-import pombe nyingi kutoka mataifa ya nje, tutumie ujuzi wa akina mama hawa ili kuendelea kutengeneza pombe zetu hapahapa kwa watu ambao ni watumiaji wa pombe waendelee kutumia vitu vyetu halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye teknolojia za biashara ambazo ziko duniani, naomba kuanza na namna gani ambavyo toka dunia ilivyokuwa imeanza kuna mifumo mbalimbali ambayo ilikuwepo ya biashara. Mfumo wa kwanza wa biashara uliokuwepo ni mfumo wa barter trade. Barter trade ilikuwa inafanyika katika mfumo kwamba kulikuwa hakuna means of exchange, kwa hiyo, biashara zilikuwa zinafanyika kwa kubadilishana bidhaa na bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya hapo, mfumo huo ulikuja ukapita baada ya dunia kuendelea tukaja kwenye metal au coin ambapo vito au dhahabu vilitumika kama means of exchange. Baada ya hapo dunia ikaondoka tukaingia kwenye paper (cash) ch currency, maana yake hapa tunaangalia Tanzanian Shilling, Kenyan Shilling, Zambian Kwacha, Nigerian Naira, Pula na pesa mbalimbali kutoka kwenye mataifa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo tunaendelea tuko kwenye huu mfumo, lakini tukaja kwenye mfumo mwingine ambao tunaita credit card ambao hata sasa hivi bado tunatumia, kwamba watu hawataki kubebeshana pesa nyingi, lakini mtu unapokuwa na kadi unaweza ukafanya transaction mahali popote pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa nne uliofuata ambao sasa dunia ipo na ndipo mahali ambapo dunia inatengeneza pesa nyingi sana, ndipo mahali ambapo hata matajiri wengi ambao wamepata kutokea katika kipindi cha miaka 15, ninapowaongelea Bill Gates, Alibaba, wametokana na mfumo huu wa teknolojia ambao umegawanyika katika phases mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naongelea fourth industrial revolution ambayo ndani yake kuna block chain technology. Kwenye block chain technology kuna teknolojia nyingi; watu wa sheria wanaweza wakaitumia block chain technology, watu wa ardhi wanaweza wakaitumia block chain technology, lakini hapa nataka niongelee kwenye mambo ya fedha namna gani block chain technology inatumika, na zaidi ya hapo nataka kuongelea kwenye digital currency.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye digital currency, hii ni teknolojia ambayo ni kubwa sana lakini kwa bahati mbaya tafsiri ambazo tunazipata sanasana kwenye Nchi kama Tanzania na nyingine za Afrika, tunashindwa kuitafsiri vizuri teknolojia hii. Na hakuna namna tunaweza tukaizuia teknolojia hii isije kufanya kazi, na tayari huko duniani kuna watu ambao wametokea matajiri wengi sana kwa kupitia block chain technology ambayo ndani kuna digital currency.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye digital currency nataka kuziongelea baadhi ya currencies. Mfano naziongelea bitcoin, ethereum, theta, bitcoin cash, litecoin na ripple, na zipo coin mbalimbali. Lakini hapa nataka kuiongelea zaidi coin ya bitcoin. Coin hii mpaka sasa Tanzania hatufahamu kwa upana namna bitcoin inavyofanya kazi, na Watanzania wengi wamekuwa wakiendelea kupoteza fedha zao kwa sababu wanadanganywa, hawajui. Lakini kama Serikali ingekuwa imeamua kulivalia njuga jambo hili wakaamua kuwekeza kwenye elimu kuna vijana wengi wa Kitanzania ambao wanaulewa mkubwa na wimbi kubwa sana la vijana ambao wapo wengine wanafanya na wanatengeneza hela, lakini pia Serikali inapoteza mapato yake kwa kiasi kikubwa sana kupitia hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano leo nikiongelea, jana bei ya bitcoin ilikuwa milioni 92 za Kitanzania, nachukulia mfano mtu kwa mfano South Africa kuna ATM ya bitcoin, Kenya kuna ATM ya bitcoin lakini sasa hivi tuchukulie mtu anatuma hela kutoka South Africa anamtumia Mtanzania aliopo hapa, hakuna namna yoyote ambayo BOT wanafuatilia transactions hizi kwa sababu mambo yote yanafanyika online, mambo yote yanafanyika kwenye internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata ilipotokea wakati ambapo Serikali iliamua kuzifunga zile bureau nyingi ambazo zilikuwa zipo Arusha na sehemu zingine, bureau nyingi ziliamua kuhamia kwenye online kwa mfano Serikali haijui kuna kitu kinaitwa remitano, Serikali haijui local bitcoin, Serikali haijui kuna kitu kinaitwa e-wallet huko kwote Watanzania wapo ambao wanatengeneza hela na wanatengeneza hela wakati mwingine naweza kusema hata hela zinaingia nchini kinyume na taratibu kwa sababu hakuna connection kati ya teknolojia, Serikali na taasisi za fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu kwa sababu ya ku-serve muda, Serikali tuamue kujifunza hata kwa nchi za wenzetu, tunaweza kujiuliza South Africa wanafanyaje mpaka wana ATM ya bitcoin, Kenya wanafanyaje mpaka wana ATM ya bitcoin? Kwa nini wanaweka zile ATM, wananufaika na nini.

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako ya mwisho.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa hiyo kwa kumalizia ni kwamba tunaiomba Serikali iwekeze sana mahali hapa kwa sababu wimbi kubwa la vijana ambao wanatumia teknolojia wanaweza wakapata ajira kwa kupitia mahali hapa na Watanzania wengi wasiendelee kupotoshwa na kuibiwa kama ambavyo lilikuja hata wimbi la D9 watu wengi wakaibiwa ni kwa sababu Serikali ilikuwa haijaweka mikono yake namna gani ikusanye mapato na namna gani iwalinde Watanzania hawa. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza nianze kusema tunaipongeza sana Serikali kwa vile ambavyo wameandaa bajeti yao kwa kuzingatia maoni mengi ya Wabunge na wamewatendea haki kwa sababu kazi za Mbunge ni pamoja na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana mama kwa namna ambavyo anaendelea kusikiliza na kupokea michango ya vijana wa Tanzania. Tarehe 22 mwezi wa Tano nilisimama kwenye Bunge hili Tukufu na kuchangia kuhusiana na mambo ya blockchain technology, cryptocurrency na digital currency na tarehe 13 mwezi huu mama aliweza kutoa kauli na kuwaomba BOT waweze kuendelea kufuatilia teknolojia hii kujifunza ili nasi tusiweze kupitwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito huu wa mama umepelekea kufanya aingie kwenye orodha ya marais wachache ambao wameonyesha kuongea kitu kikubwa sana duniani na kuunga teknolojia mpya ambayo inaweza ikaleta uchumi mkubwa lakini kuongeza ajira kwa vijana lakini na kuchochea uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya kufupisha muda naomba niendelee kuiomba Serikali na kuishauri kwamba, BOT whether taasisi zozote za kifedha kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango, watakapokuwa wanaunda Kamati zao tunaomba ushirikishi kwa vijana wa Kitanzania ambao wanauelewa ili waweze kuwasaidia, lakini elimu iendelee kutolewa kwa sababu elimu ni bure itawafanya Watanzania hawa waweze kuelewa na wasiendelee kudanganywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo naomba, wakati tunaendela kusubiri BOT waendelee kuamua na kujifunza kwamba uko mfumo ambao unatumika kwenye hizi online business, unaitwa PayPal. Ikiwa kama BOT imekubali kwamba Watanzania hawa waweze kulipa kwa kutumia PayPal, lakini wao hawawezi kupokea malipo kwa kutumia PayPal, tunaomba basi BOT tena waone namna gani watawasaidia hawa vijana wa Kitanzania ambao wanalazimika kutoa hela nje ya nchi, lakini wao hawawezi kupokea na wanalazimika kutumia nchi za jirani kulipwa na hivyo kupoteza mapato yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri wangu mwingine kwa Serikali kuhusiana na teknolojia ya miundombinu. Hapa nataka kuongelea nanofiber technology, kwa ajili ya muda nitafupisha tu, kwamba, teknolojia hii ina faida nyingi sana na ina faida nyingi sana especially kwa barabara ambazo zinatusumbua vijijini sisi Wabunge ambao tunatokea vijijini. Hata hivyo, teknolojia hii inaweza ikatumika hata mjini nanofiber technology wataalam wanasema kwanza ina PSI 11,000, kwa hiyo ina maana kwamba ina uwezo wa kuhimili kiwango ambacho lami haiwezi kuhimili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lami jua linapowaka magari makubwa yanapopita inatengeneza vitu kama mbonyeo. Kwa hiyo inapelekea Serikali kupoteza hela nyingi inapokuwa ina-maintain zile barabara, lakini nanofiber technology, Serikali itakapoamua kuitumia inaendana na mazingira yote hata kwenye zile mbuga zetu za wanyama ambako hatuwezi kuweka lami kwa sababu tunaogopa teknolojia ambayo tunatumia sasa ina emission, lakini teknolojia hii iko vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nanofiber technology ina uwezo wa ku-save gharama ambazo zinatumika kujengea lami za sasa kuanzia asilimia 25 mpaka asilimia 50. Kwa hiyo unaweza ukaona ni kwa kiasi gani Serikali itakapoamua kutumia teknolojia inaweza ika-save mapato yake, sitaweza kuendelea nitaandika andiko kwa ajili ya muda ili niseme vitu vingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba kuchangia kwenye suala la miradi hii ya kimkakati na nifupishe. Kwenye hii miradi ya kimkakati naomba niongelee mradi wa kimkakati ambao uko ndani ya Jimbo la Mwomba mradi wa chumvi. Kwenye soko letu la Tanzania inaonyesha kwamba kiwango cha chumvi ambacho Tanzania inahitaji ni tani milioni moja na laki tatu na kuendelea, lakini viwanda vyetu vya ndani kwa mfano Uvinza; viwanda vilivyoko Pwani au viwanda viliko huko Lindi vina uwezo wa kutengeneza tani za chumvi 270,000 tu. Kwa hiyo Serikali inapelekea Serikali kuangiza chumvi nyingi kutoka Nchi za Kenya na zingine ili tuweze kutosheleza soko la ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ikiwa miradi hii ya kimkakati tuliileta kwa lengo tu kwamba iweze kuzisaidia halmashauri kuongeza mapato yake, lakini iweze kutoa ajira kwa Watanzania na tuweze kuimarisha viwanda vyetu vya ndani, tunaomba Serikali irudi na kupitia tena kuangalia miradi hii ya kimkakati ikiwa ni pamoja na hiki Kiwanda cha Chumvi ambacho kipo Ivuna kwenye Jimbo la Momba. Wakati kiwanda hiki kinaendeshwa na TRC kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani mpaka 25,000, lakini toka kiwanda hiki kimerudi kwenye mradi wa kimkakati kinazalisha chini ya tani 100. Kwa hiyo tunaomba Serikali ipitie tena ili tuweze kunufaika na miradi hii ya kimkakati, iweze kwenda kutimiza lengo ambalo lilikusudiwa kwa Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Niseme kwanza naunga mkono hoja za Kamati zote mbili ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu kwa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia kwa namna ambavyo ametupatia pesa nyingi kwenye Majimbo yetu na wananchi wamenufaika, wanashukuru sana. Pamoja na pongezi hizo naomba nami nitoe mchango wangu kwenye maeneo mawili kama siyo matatu kama muda utakuwa rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza kabisa nataka kuongelea kuhusiana na TASAF. Kwenye majimbo ambayo ni ya kijijini haifanyi vizuri sana kama ambavyo Serikali ina picha halisi. Wanufaika wengi wa TASAF kule Vijijini kiukweli siyo wale ambao walipaswa waingie kwenye Mfuko wa TASAF. Watu wengi ambao ni wazee na wengine ni walemavu hawana hata uwezo wa kukopeshwa kwenye ile asilimia mbili yao ambayo inapatika asilimia kumi kwenye Halmashauri wameachwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine niwaombe sana Viongozi wa Serikali, Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri wakubali tufanye ziara za kushtukiza twende kule ili wajionee uhalisia namna gani ambavyo wananchi wanalalamika. Tumeona wakati mwingine wakitembelea kwenye maeneo yetu wanapata ule msururu wanazongwazongwa hawapati picha halisi. Wakati mwingine wanapewa taarifa ambazo siyo sahihi kulingana na uhalisia ambao upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TASAF wananchi wengi ambao wanapaswa kunufaika ambao kweli hawapati mlo na wengine hawawezi kujiendeleza kabisa hawajapata na wengine ambao ni watendaji hawafiki kwenye yale maeneo ili kuchukua takwimu halisi, wanawaachia Wenyeviti wa Vijiji, wanawaachia Wenyeviti wa Mitaa na wengine pia ni binadamu wanaingia kwenye tamaa wanawaingiza ndugu zao ilihali hawakuwa wanufaika na TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia kwenye TASAF, sehemu nyingine nyingi ambazo tumeona kwenye TASAF, ile miradi ya maendeleo ambayo imeubuliwa imeisaidia jamii kwa ujumla hata ambao hawakupaswa kunufaika na TASAF. Zipo baadhi ya halmashauri za vijijini watalaam wake hawana utalaam wa namna gani ya kuandaa haya maandiko ili wayalete TASAF Makao Makuu waweze kunufaika na miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusiana na TARURA. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu tena kwa namna ambavyo alimpatia kila Mbunge wa Jimbo bilioni 1.5 ili ziweze kwenda kumsaidia kwenye miundombinu. Kwa upande wangu kwenye Jimbo langu tumeanza kuona mwanga kutoka kwenye bilioni 1.5 hii. Ombi langu na ushauri kwa Serikali, wakati natoa ombi nisisahau kumpongeza Chief wa TARURA Injinia Seif kwa kweli amekuwa ni mtu mwema sana anawasaidia Wabunge wengi na nimesikia watu wengine wakimsemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TARURA tunaiomba Serikali kupitia Wizara yenye dhamana wawapunguzie TARURA mambo mengi wanapokuwa wamepata hela, kuwawekea vitu vingi mara sijui zabuni, vitu gani, inafika wakati wanaanza kutekeleza miradi hii wakati mvua zimekuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi kuna mafuriko, mkandarasi ameanza kulima barabara mwezi wa Pili, tarehe Mosi, leo tunavyoongea tarehe 14 Februari, barabara zote zimekwishasombwa na maji. Kwa hiyo, tunaomba pesa zinapotoka immediately watu wa TARURA waanze kufanya kazi mapema iwezekanavyo ili wafanye kipindi ambacho ni cha kiangazi, itatusaidia barabara zile zinapopitiwa na magari, zinapopitiwa na watu zinajishindilia lakini sasa hivi barabara zinaanza kutengenezwa mwezi wa Kumi na Mbili unapowauliza ni corrugations nyingi ambapo taratibu nyingi zinafanya hata zile pesa ambazo tumepewa na Mheshimiwa Rais zimepoteza thamani yake kwa sababu pale walipolima maji yamechukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, tunashukuru Serikali kwa kutujengea madarasa mengi lakini pia na watoto wakapata madawati. Walimu walisahaulika kwenye eneo hili, Walimu hawajapata fenicha, wamepata ofisi lakini hawana mahali pa kukaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na upungufu wa Walimu kwenye madarasa ambayo tumeyapata, naiomba Serikali, kama Serikali Kuu imekubali kwamba itawalipa Madiwani posho zao, tunaomba zile halmashauri ambazo hazina uwezo kwa sababu sisi wengine tunatoka kwenye halmashauri ambazo hazina uwezo, kwa hiyo hawataweza kuwaajiri watoto wao kupitia mapato yao ya ndani, tuombe hii iwe replaced na Madiwani kama watapata posho kutoka Serikali Kuu, kile ambacho walikuwa wanapata Madiwani basi wale vijana wenzetu ambao wako mtaani wamekaa zaidi ya miaka minne hadi mitano na watoto wamekaa bila kusoma basi tunawaomba vija hao wakachukue hizo nafasi hata wakilipwa shilingi laki nne ninaamini zitawasaidia sana. Ahsante sana. (Makofi)
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuunga hoja iliyopo mezani. Wakati naanza kuchangia mchango wangu naomba nirejee maneno ya Baba wa Taifa, Taifa la Afrika ya Kusini, ambaye ameshawahi kusema hapo, “Education is a most powerful weapon which, you can use to change the world.” Akimaanisha kwamba, elimu ndio silaha peke yake ambayo unaweza ukaitumia kuibadilisha dunia. Kwa muktadha wake huu ni nini?

Mheshimiwa Spika, sisi pia Watanzania pamoja na vizazi vyetu na hawa watoto ambao tunatarajia kuwasomesha, tunatarajia ya kwamba elimu ndio silaha mojawapo ambayo wao wanaweza wakaitumia kuibadilisha jamii yetu, lakini pia kuwa washindani kwenye soko la dunia huko tuliko. Tukiangalia hapa kwenye takwimu za sensa ambazo tumepewa jana pale na Mheshimiwa Rais, Milioni 61 ya Watanzania na hiyo Laki Saba, ukiangalia kwa uhalisia utagundua idadi kubwa ya Watanzania ni Watanzania ambao wana kipato cha kawaida kabisa. Maana yake asilimia kubwa ni wakulima, asilimia kubwa wanafanya shughuli ndogondogo kwa ajili ya kuendesha maisha yao ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ikiwa Watanzania hawa ni wa kawaida kabisa ambapo mtoto huyu hapati mkopo kabisa wa Chuo Kikuu, anapata mkopo chini ya kiwango au anaenda inafika hatua ameshadahiliwa kuanza masomo mpaka sasa hivi vyuo vimefunguliwa ni wiki ya pili, watoto bado hawajapata mikopo. Unajiuliza mzazi huyu ambae alikuwa akimsomesha mtoto wake kwa kuungaunga kwenye shule hizi za Kata kwa maisha magumu, sasa hivi ni wiki ya pili, mtoto labda amechaguliwa Dar-es-Salaam anatoka Mwanza Vijijini, mtoto amechaguliwa kwenda kusoma vyuo vilivyoko Mwanza ametoka huko Momba Vijijini, amefika na nini? Atalipia malazi nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamemtaka atoe hela ya udahili ili aanze masomo. Mtoto huyu ambae Serikali imefuta ada kutoka O-Level mpaka sasa hivi A-Level, mzazi anapata wapi hela ya kumsaidia mtoto huyu kumdahili? Ada ni zaidi ya Milioni Mbili, mzazi ni mkulima wa kawaida ambaye analima magunia mawili au anachoma mahindi barabarani, anafanya usafi Mama ni house girl, Baba anaranda, anapata wapi ameachwa kwenye mkopo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninao ushauri katika jambo hili. Kwanza tunaomba Bodi ya Mikopo (HESLB) ivunjwe na ipitiwe tena. Ipo haja ya HESLB inapaswa kuchunguzwa kwanza, yapo malalamishi mengi sana ambayo wanufaika wa mikopo huko nyuma bado wanayalalamikia.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili Tukufu naomba niseme wazi ninaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, mimi ni mnufaika ambaye nilikopeshwa mkopo na kupitia Bunge hili mwezi wa Kumi uliopita nimemaliza mkopo wangu. Kwa hiyo, tafsiri yake kile changu ambacho mimi Serikali iliniwezesha, mtoto wa mkulima wa kawaida kutoka Momba, nikasoma na niko hapa na inawezekana isingekuwa mkopo ningekuwa nimeshaolewa saa hizi nina wajukuu hata Wanne kwa hiyo, tafsiri yake inawezekana hata watoto wengine sasa hivi wakikosa mkopo wataingia kwenye mazingira magumu, wataendelea kuteseka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, HESLB ivunjwe, ichunguzwe, ipitiwe upya tena, lakini yale marejesho ambayo watu wengine ambao wanarejesha wanaonekana wanabambikiziwa yapitiwe tena pia, tuweze kuangalia Je, yale marejesho yanayorejeshwa hayawezi kuwasaidia watoto wapya ambao wanaingia? Je, hiki kiwango ambacho tulikipitisha hapa Bungeni hakiwasaidii watoto wapya ambao wanatakiwa kunufaika na mkopo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine ni kuwa, wako watoto wengi ambao wanafika chuo mwaka wa pili na wa tatu, wanashindwa kufanya mitihani yao kwa kukosa ada. Ninaomba Wizara ifungue dirisha, Wabunge tukiwaletea watoto hawa na sisi wakati mwingine ni binadamu, tunasaidia misiba, tunasaidia wagonjwa, inafika wakati tunashindwa. Mtoto yuko mwaka wa tatu, ameshindwa kufanya mtihani, ameomba mkopo zaidi ya mara tatu ameshindwa, mwaka wa tatu mtoto anaacha masomo?

Mheshimiwa Spika, tu-assume labda wewe mwaka wa tatu ungeachishwa masomo sasa hivi tungekuwa hatuna Spika hapo ulipokaa. Mwaka wa tatu ungeachishwa masomo tungekuwa hatuna Waziri Mkuu hapa ndani. Tunawaomba Bodi ya Mikopo mfungue dirisha, mtoto anapokuwa mwaka wa tatu ameshindwa kufanya mtihani wake kwa ajili ya kukosa ada laki nne, laki tano, tunaomba jamani watoto hawa muwape nafasi waweze kumaliza mitihani yao, waweze kufanya mitihani waende wakahangaike huko barabarani. Tuje hapa tujadili mambo mengine kwamba ajira ni changamoto, lakini kama tunasema education is the best weapon in the world, let us give them the weapon, acha tuwape silaha wakapambane huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawaomba sana watoto wasiache kufanya mitihani eti kwa sababu amekosa Laki Tano, amekosa Laki Sita. Hata sisi ni Wabunge wakati mwingine tunashindwa, siwezi mtoto afanye…

SPIKA: Ahsante sana dakika zako zimeisha Mheshimiwa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Naunga mkono hoja iliyoko mezani.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii adhimu ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa, nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu kama sitampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Nchi hii Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Tuseme ukweli, mama wa watu; mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, anajitahidi. Ombi langu tu kwa wale ambao amewaamini, wasiendelee kumwangusha, wamsaidie ili aweze kutimiza kusudi lake la kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia mambo mawili tu, kwa kuwa muda siyo rafiki. Jambo la kwanza kabisa, nataka kuwaongelea wananchi wa nchi hii, wale ambao ni wa kawaida, wanyonge, masikini, wakulima na wote ambao wanafanya shughuli zao ndogo ndogo, wanazalisha mambo ambayo yako ndani ya nchi yetu, ni pamoja pia na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa nchi hii wanajitahidi sana na wanajituma sana katika kuzalisha mazao yao ambayo Mwenyezi Mungu amewasaidia wazalishe, na wengine wanatumia mpaka jembe la mkono katika kuzalisha, lakini ambacho nakiona, tunapaswa tuwekeze nguvu kubwa sana kwenye masoko. Kwenye uchumi wanasema, demand inapokuwa high, supply ikawa low au constant inapelelea price kuwa high. Tafsiri yake ni nini? Kama supply itakuwa constant au itakuwa low, demand ikawa high, maana yake wananchi hawa chochote watakachokuwa wanakizalisha kwa sababu wanazalisha katika supply hiyo hiyo, lakini demand inapokuwa kubwa kwenye masoko, itakuwa inaleta motisha ya wao kuendelea kuzalisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya mpango, nimesoma ukurasa wa 125 ambao unasema kuhusu huduma za biashara na masoko. Waziri wa Fedha na Mipango anasema, kuimarisha miundo mbinu ya masoko, lakini kipengele cha pili anasema, kuimarisha mfumo wa kilimo cha mikataba na upatikanaji wa mikopo ya kilimo yenye riba nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kipo kipengele ambacho kinazisisitiza balozi zetu kuhakikisha zinatutafutia masoko huko nje. Je, balozi zetu zimesimamaje kuhakikisha zinawatafutia wakulima wa nchi hii masoko ya kutosha ili hata kama supply yetu itakuwa limited, demand iwe high ili wananchi hawa waendelee kupata kwa kiwango kikubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zipo baadhi ya balozi ambazo tukiwasiliananazo, wanasema changamoto kubwa ambayo wanaipata ni wakulima wetu kushindwa ku-supply kuanzia mwezi wa Kwanza mpaka wa Kumi na Mbili (continuously). Wanashindwa kwa sababu gani? Wanazalisha kwa kiwango cha chini. Kama wanazalisha kwa kiwango cha chini, tafsiri yake ni nini? Hawajawezeshwa. Hapa tunaposema kwenye mikopo yenye riba nafuu, ndipo tunaposema Benki ya Kilimo ihusike na pia Wizara ambazo zimepewa dhamana kwa ajili ya kuziomba benki ambazo zinaweza zikatoa mikopo ya riba nafuu iweze kuwasaidia wakulima wa nchi hii pamoja na wafugaji ambao pia watataka kuwezeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka kusoma kidogo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 15(xv) kinachoongelea miradi ya maji. Mheshimiwa Waziri anasema hivi, “hadi kufikia Juni, 2022 miradi ya maji kwa vijijini ilifikia asilimia 74.5 ukilinganisha na mwaka ya nyuma Juni, 2021 ilikuwa ni asilimia 72.3; na mijini asilimia 86.5 mwaka wa nyuma asilimia 86.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyosoma hapa kwa kweli asilimia 74 ya miradi ya maji ambayo anasema hivi: “kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji ambapo hadi kufikia Juni, 2022 imefikia wastani wa asilimia 74 kutoka mwaka wa nyuma asilimia 72.3.” Tafsiri yake nini? Maana yake ukitembea katika vijiji 100, vijiji 70 vina huduma ya maji. Nilipoona hii ripoti nikajiuliza, kwa hiyo, ni sisi Momba tu ndio tumesahaulika ama! Nikaanza kuuliza baadhi ya Wabunge wenzangu ambao na wenyewe wanatoka kwenye majimbo ya vijijini kama jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza Wabunge zaidi ya 20 hapa, hakuna Mbunge hata mmoja ambaye ameniambia yeye kwenye jimbo lake amefikisha hata asilimia 50 ya upatikanaji wa maji. Swali langu, sisi tunajenga nyumba moja, tuko hapa kuwatumikia Watanzania, hata Mama Samia sera yake anasema anataka kumtua mwanamke ndoo kichwani, nia yake ni ya dhati na nzuri zaidi kwa ajili ya kutaka kuwasaidia akina mama wa nchi hii pamoja watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia huu siyo wa kweli. Nitolee tu mfano wa jimbo langu, mimi nina vijiji 72. Katika vijiji 72, yaani leo nimeona niwasiliane na Madiwani wote waseme; katika vijiji 72 ziko baadhi ya Kata hazina mradi wa maji kabisa. Sasa nikajiuliza, hiyo asilimia 74 inatoka wapi? Wako pia Wabunge wengine hizo asilimia hazijafika? Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye ukurasa wa saba…

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ni mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, nataka kumpa tu taarifa hayo anayoyasema ni ya kweli kabisa kwamba takwimu hizo zinashangaza na mimi kama Mbunge ninayetokea Dar es salaam upande wa Jimbo la Kibamba, maji ni changamoto, katika kata nyingi hakuna, kwa hiyo ni mchango mzuri na ni kweli kabisa anachokisema. (Makofi)

MWENYEKITI: Nyie wa Dar es Salaam huwa mkisimama na mkaungana na wa vijijini kuna muda hatuwaelewi sana. Hivi na nyie wa Dar es Salaam mna changamoto kweli kama za Momba? (Makofi)

Mheshimiwa malizia sekunde 30.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika vijiji 72 ni vijiji 16 tu ambavyo vina maji na vijiji 56 havina maji. Sasa najiuliza hii takwimu inatoka wapi? Sisi tunajenga nyumba moja, tuwatendee Watanzania haki. Tulienda kuomba kura kwa kutumia ilani hii na kwenye ilani hii ukurasa wa saba, samahani kidogo tu nisome mama yangu. Katika miongoni mwa vitu ambavyo ni vipaumbele ambavyo sisi tulipewa ilani tukanadi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi inasema hivi; “Kuongeza kasi ya usambazaji wa maji safi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya 85% vijijini na zaidi ya 95% mijini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naamini kwa sababu wanaona tumeshafika mwaka wa pili na ilani inasema 85%, wameamua waseme 74% hii ili ionekane wametekeleza, hapana sio kweli. Kupitia Bunge hili, namwomba Mheshimiwa Aweso, nataka nikafanye naye ziara kwenye jimbo langu, vijiji 10 ili kweli na vyombo vya habari vimchukue nione kama kweli atakuja na hiyo takwimu ya 76%, kwamba kweli kuna maji. Hapana sio kweli. Ahsante sana. (Makofi)